TAMKO LA KAMATI KUU YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA ZANZIBAR ULIOFANYIKA TAREHE 30 OKTOBA, 2005

 

  1. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi imekutana katika kikao cha dharura tarehe 7 Novemba, 2005 mjini Dar es Salaam kuzingatia miongoni mwa mengine, Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 30 Oktoba, 2005.

 

  1. Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa, Kamati Kuu imempongeza kwa dhati Ndugu Amani Abeid Karume kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuendelea kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kipindi cha pili. Ushindi wa asilimia 53.2 alioupata Ndugu Karume katika uchaguzi huo ni mkubwa na wa kujivunia hasa ukizingatia mazingira ya kisiasa ya Zanzibar.

 

  1. Ushindi huo wa Ndugu Karume ni kielelezo stahiki cha kukubalika kwake na jinsi wananchi wanavyotambua na kuthamini mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake. Aidha, ni uthibitisho wa kukubalika kwa Chama Cha Mapinduzi na sera zake za amani, umoja, utulivu na maendeleo. Ni ukweli ulio wazi kwamba, chini ya uongozi thabiti na shupavu wa Rais Amani Abeid Karume, wananchi wa Zanzibar na Zanzibar kwa ujumla imepata utulivu wa kuridhisha na maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii. Katika pembe zote za Visiwa vya Unguja na Pemba upo ushahidi wa kutosha wa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuendeleza miundo mbinu na kuboreshwa kwa huduma za jamii kama vile Elimu, Afya, Umeme, Maji, n.k. Uchumi umekuwa unakua vizuri na kusababisha kuongezeka kwa ajira na kukua kwa pato la watu.

 

  1. Aidha, Kamati Kuu imewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Unguja na Pemba kwa imani yao kwa Chama Cha Mapinduzi na kukipa ridhaa ya kuongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Pamoja na kumchagua Ndugu Amani Abeid Karume, wananchi wa Zanzibar wamewachagua wana-CCM 30 katika majimbo 50 kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Imani huzaa imani, CCM inawaahidi wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla kwamba itahakikisha Serikali yake inafanya vizuri zaidi ya ilivyokuwa miaka mitano iliyopita. Wakati huo huo, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa inatoa pongezi kwa wana-CCM 30 waliochaguliwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wanawake 9 walioteuliwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Viti Maalum.

 

  1. Kamati Kuu imeipongeza pia Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kutoa uongozi sahihi na Kamati ya Kampeni ya CCM Zanzibar kwa kuendesha kampeni kwa ustaarabu, umahiri mkubwa na ufanisi wa hali ya juu. Mambo hayo ndiyo ambayo yameleta ushindi. Katika mtiririko huo huo, Kamati Kuu imewapongeza viongozi wa CCM wa ngazi zote na wanachama wote wa CCM wa Zanzibar kwa uvumilivu wao, mshikamano na bidii kubwa, mambo ambayo yamekuwa chachu ya ushindi huo.

 

  1. Kamati Kuu imeridhika na kufurahishwa na jinsi zoezi zima la Uchaguzi Mkuu Zanzibar lilivyoendeshwa. Hivyo basi, CCM inaungana na Waangalizi wa uchaguzi wa kutoka ndani ya nchi na wenzao wa kimataifa kuipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kuendesha vizuri zoezi zima la Uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani huko Zanzibar. Safari hii, maandalizi, uendeshaji, utawala na mwenendo mzima wa uchaguzi vilikuwa bora zaidi kuliko wakati wa chaguzi zilizopita. Kamati Kuu ya CCM imeridhika kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.

 

  1. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefurahi kwamba Wapiga kura wengi sana walijitokeza vituoni kupiga kura (zaidi ya asilimia 90) na upigaji kura ulikuwa wa amani na utulivu. Watu walipiga kura kwa uhuru bila vitisho wala shinikizo. Haki yao ya kupiga kura ya siri iliheshimiwa na kutimizwa kwa ukamilivu. Mawakala wa vyama walikuwepo katika kila kituo cha kupigia kura, jambo lililohakikisha kuwa maslahi ya vyama yanalindwa na wasiostahili kupiga kura hawakuruhusiwa kupiga kura. Kila aliyepiga kura alipakwa wino usiofutika kumzuia asipige kura tena. Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kwa wakati na vifaa husika vilipatikana kama ilivyopasa. Majina ya wapiga kura wa kila kituo yalibandikwa ukutani pembeni mwa kituo wazi kwa kila mmoja kuona. Kura zilihesabiwa vituoni baada ya kukamilika upigaji kura na vituo kufungwa. Zoezi la kuhesabu kura lilifanywa kwa uwazi na kushuhudiwa na mawakala wa vyama vya siasa pale kituoni. Kwa baadhi ya vituo, hata waangalizi wa uchaguzi waliokuwepo waliweza kushuhudia. Kwa ajili hiyo, kila wakala aliondoka kituoni na matokeo kamili. Isitoshe, matokeo ya kila kituo yalibandikwa ukutani nje ya kituo kwa yeyote anayependa kujua aweze kuona. Mambo yalifanywa kwa uwazi wa hali ya juu. Ni kutokana na ukweli huu CCM inaridhika kuwa uchaguzi ulikuwa huru, haki na wa amani.

 

  1. Aidha, Kamati Kuu inatambua kujitokeza kwa matatizo ya hapa na pale katika baadhi ya vituo, hasa katika eneo la Mji Mkongwe. Tumeridhika kama walivyoridhika Waangalizi wa Uchaguzi kuwa kasoro hizo ndogo ndogo katika maeneo machache hazikuathiri mwenendo na matokeo ya uchaguzi mzima. Kamati Kuu inawasihi wale wanaoitakia mema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wasizichukulie kasoro zilizojitokeza katika vituo hivyo vichache vya eneo la Mji Mkongwe kama ni kielelezo cha hali ilivyokuwa katika uchaguzi mzima wa Zanzibar.

 

  1. Kamati Kuu imevipongeza vyombo vya dola kwa kusimamia vizuri hali ya usalama kiasi cha kuwapa wananchi wa Zanzibar, waliokuwa wamegubikwa na vitisho vingi vya viongozi na wafuasi wa CUF wakati wa kampeni, imani iliyowafanya kujitokeza kwa wingi na kupiga kura zao kwa uhuru siku ya uchaguzi.  Ukweli huu unathibitishwa na wingi wa wanawake waliojitokeza kupiga kura vituoni.

 

  1. Kamati Kuu imevipongeza vyombo vya habari, hasa vya ndani ya nchi, kwa jitihada kubwa vilivyofanya kutoa taarifa za uchaguzi huo kwa uwazi, usahihi na bila upendeleo.

 

  1. Kamati Kuu inatoa wito kwa Chama cha CUF kukubali matokeo ambayo ni kauli halali ya uamuzi wa wananchi wa Zanzibar. Vilevile, Kamati Kuu imesikitishwa na tabia ambayo sasa inaelekea kuwa hulka ya Bwana Seif Shariff Hamad na Chama cha CUF ya kukataa matakwa ya wananchi walio wengi. Hulka hii inadhoofisha jitihada za kujenga na kuendeleza demokrasia nchini. Aidha, Kamati Kuu imeelezea kufadhaishwa kwake na tabia na vitendo vya viongozi na wanachama wa CUF vya kuchochea ghasia na kuvunja amani. CCM inatoa wito kwa viongozi na wanachama wa CUF kuachana na muelekeo usiokuwa na maslahi kwa taifa letu changa na watu wake.

 

  1. Kamati Kuu imetoa wito kwa marafiki wa kweli wa Tanzania kuisadia nchi yetu iendelee kuwa na umoja, amani na utulivu. Rafiki wa kweli wa Tanzania atajiepusha kufanya vitendo au kuonekana anafanya vitendo au kutoa kauli zitakazochangia kuleta mgawanyiko badala ya umoja na mshikamano au itakayochochea ghasia katika jamii badala ya kuleta amani na utulivu. Tunawaomba marafiki zetu wa kweli wasifanye vitendo au kutoa kauli zitakazowatia moyo na kuwapa hamasa watu, vyama au vikundi vyenye nia mbaya ya kuchochea ghasia na tofauti na mifarakano miongoni mwa Watanzania. Marafiki wanaotaka kuiona Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika hali ya migogoro, hawawezi kujigamba kuwa ni marafiki wa kweli wa nchi yetu.

 

  1. Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi kinatambua kwamba upo umuhimu wa kuendeleza jitihada za kuleta umoja na kutafuta mustakabali wa kisiasa na kijamii Visiwani. CCM inatambua kuwa hakuna majawabu ya mkato katika kufikia azma hiyo. Kama vile ambavyo Muafaka umekuwa hatua muhimu katika kuwasogeza Wazanzibari kuelekea kwenye azma hiyo, Chama Cha Mapinduzi hakitachoka kuendelea na jitihada za kupata mustakabali endelevu kwa manufaa ya amani, utulivu na maendeleo ya Zanzibar na nchi yetu kwa ujumla.

 

  1. Kwa mara nyingine tena, Kamati Kuu imewashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kuipa tena ridhaa CCM kuendelea kuongoza. Kwa uamuzi wao huo, wamechagua sera za maendeleo na kuzikataa sera za chuki na visasi. Kamati Kuu inawaomba wananchi wa Zanzibar, bila kujali itikadi zao za kisiasa, watoe ushirikiano kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa manufaa yao. Uchaguzi umekwisha na uongozi umepatikana. Kilichobaki sasa kwa Wazanzibari ni kushikamana na kukusanya nguvu zao kujenga nchi na kupambana na umaskini.

 

  1. Mwisho, Kamati Kuu imeitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Ndugu Amani Abeid Karume iendeshe shughuli zake za kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar kwa kujiamini ikiwa na uhakika wa uhalali kamili unaotokana na ridhaa ya wananchi.

 

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

 

Philip J. Mangula

KATIBU MKUU