TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Philip Mangula, amesema sababu kubwa ya CCM kuendelea kukubalika nchini licha ya kuwepo utitiri wa vyama vingine vya siasa ni uwezo kilionao katika kuoanisha nadharia na vitendo vinavyoendana na mahitaji ya wakati husika.

 

Ndugu Mangula amesema hayo leo mjini Dar es Salaam alipokutana ofisini kwake na ujumbe wa wabunge  Saba kutoka Bunge la Marekani.

 

Amesema mara kwa mara Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikifanya mapitio ya sera zake na wakati fulani kimediriki hata kutoa tafsiri mpya kuhusu falsafa inayohimidi itikadi yake ili kuona kama bado inaendana na matarajio ya umma.

 

Kwa mfano amesema katika nyanja ya uchumi CCM  ilitafsiri upya dhana ya uchumi wa nchi kumilikiwa na umma ambapo ulazima wa serikali pekee kuwa ndio imiliki njia kuu za uchumi wa Taifa lkwa niaba ya wananchi uliondolewa.

 

Amesema hivi sasa wananchi mmoja mmoja , vikundi, vyama vya ushirika na hata mashirika yasiyo ya kiserikali wanaruhusiwa kushiriki katika kuendesha na kumiliki uchumi wa nchi yao.

 

Hata hivyo amesema pamoja na kuitafsiri upya dhana hiyo ya uendehsaji  uchumi, itikadi ya CCM bado ni ile ile ya Ujamaa na Kujitegemea na  kwamba serikali zote mbili zinatekeleza sera zenye mwelekeo wa itikadi hiyo.

 

Katibu Mkuu wa CCM alitoa maelezo hayo baada ya wabunge hao kutaka kuelewa mazingira yanayoifanya CCM iendelee kukubalika nchini licha ya kuwepo changamoto anuwai  za dunia ya utandawazi ambazo zimeyalazimisha baadhi ya mataifa kuzitelekeza hata itikadi zao.

 

Akitaja sababu nyingine ya CCM kuendelea kukubalika, Ndugu Mangula amesema ni ile tabia ya chama na viongozi wake kupenda kusikiliza maoni ya umma.

 

Ndugu Mangula amesema hata msimamo wa sasa wa CCM na serikali yake kuendelea kusisitiza muundo wa muungano wa serikali mbili umetokana na kubaini kuwa hayo ndiyo matakwa ya Watanzania walio wengi. 

 

Amesema kwa maongozi ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali iliunda kamati ya jaji Kisanga ili kukusanya maoni ya wananchi kuhusu jambo hilo.  Amesema ripoti ya Kamati ilionyesha kuwa Watanzania walio wengi wanapendelea  Muungano wa Taifa la Tanzania uwe wa serikali mbili na wala siyo muungano wa shirikisho lenye serikali tatu.

 

Katibu Mkuu wa CCM amewaambia Wabunge hao kwamba hakuna muujiza kwa mtu au chama kukubalika na umma isipokuwa siri pekee ni kufanya mambo yanayowapendeza na kutarajiwa na watu.

 

Wabunge hao kutoka majimbo saba wanaowakilisha vyama tofauti vya siasa nchini Marekani wakiwa wamefuatana na maofisa toka serikali za majimbo na serikali ya Marekani walikuwepo nchini kwa ziara ya siku kumi inayomalizika leo na walikuja kwa mwaliko wa Taasisi ya Bunge (Bunge Foundation).

 

Imetolewa na:

 

 

Ofisi ya Katibu Mkuu CCM

Ofisi Ndogo Makao makuu DSM

18/5/2004