CCM YASHINDA
KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA BUNGE NA VITI VYA MADIWANI
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda katika Uchaguzi Mdogo wa Bunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki, Shinyanga baada ya mgombea wake DANHI MAKANGA kumshinda Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha upinzani cha UDP, JOHN MOMOSE CHEYO.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo
hilo, ANDREW JOHN ametangaza tarehe 31/5/2004 kwamba katika uchaguzi huo
uliofanyika Mei 30, 2004, MAKANGA alipata kura
27,747 na cheyo aliambulia kura 26,708.
CHEYO ambaye aliwahi kugombea
mara mbili Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995 na 2000, pia
aliwahi kushindwa katika Uchaguzi Mdogo wa Bunge wa Jimbo la Busega, Mkoa wa
Mwanza mwaka 1995.
Kwa ushindi wa Jimbo la Bariadi
Mashariki kumekifanya Chama Tawala cha CCM kuwa na Wabunge 259 (87.79%) kutoka
idadi ya Wabunge wote 295 wanaotakiwa kuwepo kwa mujibu wa Katiba katika Bunge
la Muungano.
Kati ya Wabunge wa CCM 259 waliopo sasa, jumla ya Wabunge 204 wamechaguliwa kutoka katika jumla ya Majimbo yote 231 ya Uchaguzi yaliyopo nchini (Bara Majimbo 181 na Tanzania Zanzibar Majimbo 50) hivi sasa; Wabunge tisa (9) ni wa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge watano (5) ni kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Vyama vya upinzani vina jumla ya
Wabunge 34 (11.52%) katika Wabunge wote wa Kikatiba 295.
Navyo ni CUF Wabunge 22 (7.45%);
CHADEMA Wabunge 5 (1.69%); TLP viti 5 (1.69%) na UDP Wabunge 2 (0.67%).
Hii inafanya Wabunge wote wa CCM
259 na wa upinzani 34 waliopo sasa kufanya idadi yao kufikia 293 Bungeni.
Nafasi moja ya Bunge imejazwa na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (ex-official) na Jimbo la Kisesa, katika Mkoa wa
Shinyanga liko wazi. Nafasi hiyo
ikijazwa ndiyo itakamilisha idadi kamili ya Wabunge wote wanaotakiwa Kikatiba
kukomea 295.
Kwa upande wa uchaguzi mdogo wa
Madiwani, CCM imeshinda viti 16 vya Udiwani kati ya 19 vilivyokuwa vinagombewa
na vyama mbali mbali vya siasa.
Ushindi wa kujivunia ulipatikana
katika Wilaya ya Bariadi, Shinyanga ambapo CCM imeweza kushinda viti saba kati
ya vinane ambavyo katika uchaguzi wa 2000 Madiwani wote wanane walioshinda
walikuwa wa UDP. Kwa ushindi huu,
Halmashauri ya Bariadi Mashariki sasa ni ya CCM na siyo kama ulivyokuwa
ikiongozwa na UDP.
Katika Wilaya ya Moshi Vijijini,
CCM pia imefanikiwa kuwanyang’anya wapinzani viti vitatu kati ya vitano vya
Udiwani vilivyogombaniwa. Aidha CCM pia
ilishinda kiti kimoja kimoja cha Udiwani kilichokuwa wazi katika Wilaya za
Kyela (Lusungo), Ileje (Itale), Lindi (Mnolela); Tabora (Urambo), Muheza (Duga)
na Ukerewe (Irigwa).
Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani hufanyika kila baada ya miaka mitano. Uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka 2000 na ujao utafanyika Oktoba, 2005.