HOTUBA YA RAIS
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWA
BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 12 FEBRUARI 2004
Mheshimiwa Spika,
Awali
ya yote, napenda sote tuungane kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai tangu
nilipohutubia Bunge hili Tukufu mara ya mwisho, tarehe 30 Januari 2002, hadi
leo hii. Namshukuru pia kwa afya yangu inayoimarika siku hadi siku. Nanyi,
Waheshimiwa Wabunge, nakushukuruni sana kwa salamu zenu za pole na dua kwa
ajili ya afya yangu zilizowasilishwa kwangu na Mheshimiwa Spika wakati nikiwa
nimelazwa hospitalini kule Uswisi.
Mheshimiwa Spika,
Nilipohutubia
wananchi, tarehe 31 Desemba 2003, niliwaambia kuwa ningependa katika kipindi
cha uongozi wangu kilichobaki nielekeze nguvu zangu kwenye kuimarisha uendelevu
wa mageuzi na mafanikio yetu, na unyumbulifu wa taifa letu kisiasa, kiuchumi na
kijamii, pamoja na kuweka mkazo mpya kwenye kujenga uwezo wa Watanzania kutumia
fursa za kujiendeleza ambazo mafanikio ya mageuzi yetu yanaziweka mbele
yao. Niliahidi pia kuwa, Inshallah,
ningetafuta fursa ya kufafanua nini hasa nilichokuwa nazungumzia.
Hakuna
fursa iliyo bora kwa lengo hilo kuliko hii ya kuzungumza na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Bunge hili si tu
mahali ambapo Watanzania wote wanawakilishwa, bali pia ni mshirika wangu mkuu
katika kutekeleza yote ninayokusudia kuyafanya. Na kwa vile nchi hii ni yetu sote, kiasi kwamba hata viongozi na
wafuasi wa vyama vya upinzani nao hufaidi matunda ya kazi za Chama Tawala, na
huhasirika tusipopiga hatua mbele, nimeomba viongozi hao wawe hapa
kunisikiliza. Kwa heshima naomba sasa
niwatambulishe, na kuwaomba wasimame ili Waheshimiwa Wabunge nao wawatambue.
Mheshimiwa Spika,
Napenda
nianze kwa kurejea kwenye muhtasari nilioutoa kuhusu sura kuu za mwelekeo wa
miezi 20 ijayo:
·
Kwanza, kuongeza
kasi ya kubadili mtazamo wa watumishi wa umma—kwenye Serikali Kuu na Serikali
za Mitaa—ili wajue kuwa kazi yao ya msingi sasa ni kuwasaidia na kuwawezesha
wananchi kujiendeleza.
·
Pili, kujenga na
kuimarisha uwezo kitaifa wa udhibiti, uratibu na usimamizi wa uchumi
wa soko.
·
Tatu, kufikiria
upya haki za wanyonge wakiwemo wananchi walio katika sekta isiyo rasmi;
hasa zile haki za kumiliki raslimali na mitaji, ikiwemo nguvu zao, na ardhi,
kama mbinu ya kuwawezesha kuingia katika mfumo rasmi wa uchumi wa kitaifa.
·
Nne, kuweka
kipaumbele kinachostahili kwenye mauzo nje ya nchi, ikiwemo kuongeza
thamani yake kwa kuyasindika, na kukaribisha uwekezaji kwenye viwanda
vitakavyotupatia haraka uwezo wa kufanya hivyo.
·
Tano, kuendelea
kubainisha kero za wananchi, na kuondosha vikwazo vilivyo katika njia ya
Watanzania walio tayari kujiendeleza.
Mheshimiwa Spika,
Ningependa Waheshimiwa Wabunge
waniunge mkono katika kuweka kipaumbele kwenye maeneo haya, na wawe wabia wa
Serikali katika utekelezaji wake wa dhati. Nawaomba mambo mawili ya msingi
kabisa:
·
Kwanza, nawaomba
wazingatie wakati wote ukweli kuwa nchi yetu ni maskini, na kama alivyotuasa
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tunapaswa kukimbia wakati
wengine wakitembea. Kwa kweli mimi
nimechoka kila mara kusikia Tanzania inaitwa “moja ya nchi maskini kuliko
zote”. Inawezekana kuachana na sifa
hiyo ya umaskini, lakini si kwa kasi yetu ya sasa. Nchi nzima, ikiongozwa na Bunge hili, inapaswa kubadili gia, na
tuonyeshe dunia kuwa baada ya kubuni sera na mwelekeo sahihi, sasa tunachochea
mwendo kweli. Sijengi hoja ya kugeuza
Bunge hili kuwa muhuri wa Serikali.
Wala sithubutu. Lakini najenga
hoja ya mazingira ya kibunge yanayoiwezesha Tanzania kukimbia badala ya
kutembea. Najenga hoja ya “a sense
of urgency”.
·
Pili, naomba
katika kuzungumza na wananchi, na pamoja na Uchaguzi Mkuu ujao mwakani, sisi
sote tusiwape matumaini kuwa ipo Serikali yenye majibu yote na uwezo wote. Serikali ya aina hiyo haipo popote
duniani. Serikali haina muujiza wa peke
yake. Lakini inawezekana kupata muujiza
wa kitaifa, kwa kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa matatizo, kwa kujituma na
kukubali wajibu wa kujiendeleza kama mtu binafsi, na kama jamii. Dhana ya kwamba wajibu wa Serikali ni kutoa,
na wajibu wa wananchi ni kushukuru, ni sawa na mbio za sakafuni, mwisho wake ni
ukingoni. Dhana hiyo inaweza kumpatia mgombea kura, lakini haitotufikisha mbali
kama taifa.
Hali ya Siasa
Mheshimiwa Spika,
Baada
ya miaka arobaini na mbili ya Uhuru wa Tanzania Bara, na miaka arobaini ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Tanzania imeuzatiti uhuru wake wa kisiasa, na kujenga
umoja wa kitaifa usio na shaka, ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia kuhakikisha
Tanzania inakuwa nchi ya amani na utulivu.
Katika
bara hili lenye historia ya vurugu za kisiasa na ghasia, Tanzania, iliyozaliwa
mwaka 1964 kwa kuunganisha nchi mbili huru— Tanganyika na Zanzibar—hadi leo hii
ndiyo Muungano pekee wa aina hiyo unaoendelea na kuweka hai matumaini ya umoja
wa bara la Afrika.
Serikali
zetu zinabadilishwa kupitia sanduku la kura, kwa kuheshimu Katiba ya
Taifa. Hakuna Rais—Bara na
Zanzibar—aliyeachia madaraka na kisha kulazimika kuikimbia nchi yake. Wote wanaishi nasi, na wanaheshimiwa.
Tanzania
ni nchi ya kidemokrasia. Serikali ya
Awamu ya Tatu Tanzania Bara, na Awamu ya Sita Tanzania Zanzibar, zimefanya kazi
kubwa kuimarisha misingi ya uhuru wa raia, demokrasia, haki na usawa, kwa
mujibu wa Katiba.
Siwezi
kusema Tanzania sasa ni peponi. Kote
duniani vyama vya upinzani vinakuwa na malalamiko ya aina fulani dhidi ya Chama
Tawala na Serikali yake. Ni mambo ya
kawaida kwenye ushindani wa kisiasa.
Matatizo
ya kisiasa Zanzibar, kufuatia Uchaguzi Mkuu uliopita, yametatuliwa kwa amani na
majadiliano. Matukio ya Januari 26 –
27, mwaka 2001, ambapo wenzetu walipoteza maisha yao, yamebaki kama kasoro na
si hulka ya Watanzania. Na kasoro ni
kasoro—haifai kutukuzwa. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Tunaandaa mfumo endelevu wa ushindani wa
kisiasa ambao ni wa kistaarabu, huru na wa amani Zanzibar na Tanzania
nzima. Kwetu sisi, majadiliano ndiyo
njia muafaka zaidi na ya uhakika ya kuendesha siasa huko tuendako. Kama
alivyosema mshairi maarufu, Kahlil Gibran, “Tunapogeukiana na kushauriana
tunapunguza idadi ya maadui zetu.” Mimi binafsi na Chama Cha Mapinduzi hatutaki
uadui kwenye siasa. Tuko tayari kushauriana na kuelewana na wote wenye nia
njema.
Utayari
wetu umedhihirika kwenye MWAFAKA baina ya vyama viwili vikuu, CCM na CUF,
uliowekwa saini tarehe 10 Oktoba 2001 ambao umeendelea kuimarika, na umechangia
kwa kiasi kikubwa utulivu wa kisiasa uliopo sasa Zanzibar, kielelezo kimojawapo
kikiwa uchaguzi mdogo Mei 2003.
Naipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutekeleza wajibu wake
chini ya Mwafaka, na kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanayoonekana
wazi.
Katika
miezi ijayo tutapendekeza mabadiliko ya Katiba ambayo kwa maoni yetu yatasaidia
kuimarisha demokrasia katika nchi yetu.
Tutatimiza pia ahadi yetu ya kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao. Na
tutazidi kuongeza nafasi na uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.
Kwa upande wa Bunge, ninakusudia idadi yao isipungue asilimia 30 ya Wabunge
kabla sijaondoka madarakani.
Lakini,
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mawili katika siasa nchini mwetu
yasiyoniridhisha. La kwanza, ni udhaifu
wa vyama vya upinzani. Miaka michache
iliyopita nilielezea hofu hiyo kwa kofia yangu ya Urais. Lakini nikajibiwa kuwa si kazi yangu
kufikiria udhaifu wa vyama vya upinzani.
Mimi ninaamini wako Watanzania wengine walio na wasiwasi kama wangu,
maana ama tunao ushindani wa kweli, wa timu zinazokaribiana kwa nguvu, au
tunafanya mzaha. Ni nia yangu CCM
iendelee kutawala daima, lakini naelewa pia faida kwa taifa ya vyama vya
upinzani makini vinavyoweza kutuamsha tusilale usingizi. Na CCM ikiwa macho, ni
kwa faida ya wananchi na taifa.
Mheshimiwa Spika,
Jambo
la pili linalonifadhaisha ni kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa na
wanachama wao ambazo zinaonyesha kutojali thamani ya amani na utulivu nchini.
Wapo hata wanaothubutu kuzungumzia damu kumwagika, japo sijasikia wakijitolea
damu yao wenyewe, hata kwa jambo jema kama vile kutunisha akiba ya damu kwenye
hospitali zetu!
Pengine
hakuna sifa muhimu kwa nchi yoyote kama sifa ya amani na utulivu. Kiongozi, au mtu anayewania uongozi, lazima
ajifunze kuheshimu thamani ya uhai wa raia.
Inachukua muda mrefu kwa nchi kujijengea sifa ya amani na utulivu,
lakini ni rahisi sana kuibomoa, hasa ukipata viongozi wasiothamini uhai wa
raia, walio tayari kuutumia kama ngazi ya kuingia madarakani. Katika nchi huru
ya kidemokrasia hakuna uhalali wowote wa kutumia fujo na vurugu kutafuta
madaraka.
Naomba
sana kuwa tunapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu,
na Uchaguzi Mkuu mwakani, tusithubutu hata kuwazia matumizi ya fujo na
vurugu. Na sisi Serikalini, wenye
dhamana ya utulivu na usalama nchini, hatuwezi kuruhusu siasa za fujo na
vurugu. Ni wajibu wetu kikatiba
kudumisha amani na usalama nchini kote.
Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Spika,
Tunataka
kuhakikisha kuwa vikwazo dhidi ya ushiriki wa wananchi kwenye utawala na
maendeleo ya nchi yao vinaondolewa.
Maana demokrasia si siasa tu, demokrasia ni uchumi vile vile. Kwa asiye na chakula, demokrasia ni anasa.
Kwa wananchi walio wengi demokrasia inayowagusa moja kwa moja, na inayohusu
maisha yao ya kila siku na mustakabali wao, ni Serikali za Mitaa. Demokrasia ni madaraka kwa wananchi. Na ibara ya 146(1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuwa “Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa
ni kupeleka madaraka kwa wananchi.” Kwa
sababu hiyo, Serikali ilibuni na inaendelea kutekeleza Mpango wa Uboreshaji wa
Mfumo wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kuwa Halmashauri za Wilaya na Miji
zinawajibika kwa wananchi, pamoja na kutoa huduma bora zaidi kwao na
kurahisisha jitihada zao za kujiendeleza.
Mheshimiwa Spika,
Kielelezo
cha utashi wa kisiasa kuimarisha Serikali za Mitaa ni kiasi cha fedha
kinachokabidhiwa kwa Halmashauri.
Kumekuwa na ongezeko kubwa sana—mara 24—la ruzuku ya Serikali Kuu kwa
Serikali za Mitaa kutoka Sh.12.3 bilioni mwaka 1995/96 hadi Sh. 292 bilioni
mwaka huu wa fedha. Huu ni uwezeshaji
kimapato, utokanao na mafanikio ya mageuzi yetu ya uchumi.
Upo
pia uwezeshaji kielimu. Mafunzo ya kuimarisha
utendaji yametolewa kwa Wakuu wa Mikoa wote, na baadhi ya Wakuu wa Wilaya na
Makatibu Tawala wa Mikoa. Mpango wa
mafunzo ya Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Maafisa Watendaji wa Vijiji
umeandaliwa. Hadi sasa viongozi 72,000
wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji wamepatiwa mafunzo ya kuimarisha utawala bora.
Madiwani 3,447 na Maafisa Watendaji wa Kata 2,303 nao wamepatiwa mafunzo. Aidha, Wakurugenzi wa Halmashauri zote
wamepatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa mabadiliko. Na yote hayo yanawezekana kutokana na mafanikio ya mageuzi yetu
ya kiuchumi.
Mafanikio
hayo pia yamesaidia uwezeshaji kiutendaji.
Kwa mfano, Makatibu Tarafa wote wamepewa pikipiki ili kuwawezesha
kusimamia vizuri shughuli za maendeleo.
Pikipiki hizo zisingepatikana kama si mageuzi ya uchumi tuliyoyafanya.
Sera
zetu na mageuzi yetu vimetujengea mahusiano mazuri na wahisani wanaotusaidia
kutekeleza Mpango huu wa Uboreshaji Serikali za Mitaa. Aidha, mapato ya Serikali ambayo
yameongezeka sana baada ya mageuzi hayo ndiyo yamewezesha Serikali Kuu
kugharamia uwezeshaji wa Halmashauri nilioutaja hapa. Ni mafanikio ya mageuzi
hayo ndiyo vile vile yaliyoipa Serikali uwezo wa kufuta kodi mbalimbali
zilizokuwa kero kwa wananchi kwa miaka mingi. Wanaokebehi mageuzi waulizwe,
ingewezekanaje?
Mabadiliko ya Fikra na Usimamizi wa Uchumi wa
Soko
Mheshimiwa Spika,
Jambo
jingine ambalo nitalitilia mkazo katika kipindi changu kilichobaki ni
mabadiliko ya fikra ya viongozi na watendaji wa Serikali, pamoja na Serikali za
Mitaa, kuhusu nafasi ya sekta binafsi.
Kila kiongozi na mtumishi wa Halmashauri anapaswa kujua kuwa maslahi
yake binafsi, na maendeleo ya wilaya au mji unaohusika, vinategemea sana
mafanikio ya uwekezaji, uzalishaji, huduma na biashara. Wakati umefika sasa kwa Halmashauri kushindana
kwa dhati miongoni mwao katika kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara. Watumishi
wa umma waelewe kuwa nyakati zimebadilika, na tunahitaji mbinu mpya kukabiliana
na changamoto za leo na zijazo.
Ipo
hadithi ya bwana mmoja aliyekuwa anatembea barabarani. Akamsimamisha mtu mmoja
na kumuuliza wakati. Mtu yule akaangalia saa yake na kumjibu, “Hivi sasa ni saa
10:00.” Yule bwana aliyeuliza akakuna kichwa na kusema, “Unajua, ninyi wenye
saa mnanichanganya kweli. Siku nzima ya leo nimekuwa nauliza watu wakati, na
kila mara ninapewa jibu tofauti!”
Na
mimi nawaambia watumishi wa umma kuwa wasiwalaumu wenye saa, wala
wasichanganyikiwe. Ukweli ni kuwa nyakati zinabadilika haraka, na majibu lazima
yabadilike.
Mheshimiwa Spika,
Hivi
sasa ni kama vile kila mmoja anakubali kwa wepesi kuwa uwekezaji mkubwa na
biashara mahali pake ni Dar es Salaam.
Hivi leo Mkoa wa Dar es Salaam, na hususan Jiji la Dar es Salaam,
huchangia karibu asilimia 82 ya mapato yote ya Serikali. Hali hii si nzuri hata kidogo. Chanzo cha maendeleo ni uwekezaji,
uzalishaji, huduma na biashara. Kwa
kadri mambo hayo yanavyofanyika Dar es Salaam, ndivyo maendeleo yatakavyoelekea
Dar es Salaam, na kuzidi kuwavuta vijana toka pande zote za nchi kuja Dar es Salaam
kwa matumaini kuwa huko ndiko kwenye uwekezaji, na hivyo kwenye ajira; na
kwamba huko ndiko kwenye maendeleo na hivyo maisha bora. Bila Halmashauri kwenye mikoa mingine
kufanya bidii kuvutia uwekezaji huko waliko, tatizo hili haliwezi kwisha na hakutakuwa
na usawa wa kijiografia kwenye maendeleo ya taifa.
Ndio
maana nachukua fursa hii kuupongeza Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa mstari wa
mbele kujiandaa kuvutia wawekezaji, na kuitisha Kongamano la Uwekezaji
Kilimanjaro lililofanyika tarehe 14-15 Agosti 2003.
Lakini, Mheshimiwa Spika, uchumi wa soko
lazima udhibitiwe kwa maslahi ya taifa na walaji. Ili kuwalinda wateja na
kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki kwenye biashara, Serikali imeanzisha
mashirika manne ya usimamizi ambayo ni: Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Maji
na Nishati (Energy and Water Utilities Regulatory Authority -EWURA),
Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Surface and
Marine Transport Regulatory Authority- SUMATRA), Mamlaka ya Usimamizi wa
Huduma za Mawasiliano (Tanzania Communication Regulatory Authority-TCRA),
na Mamlaka ya Serikali ya Tanzania ya Usimamizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga (Tanzania
Government Aviation Regulatory Authority-TGARA). Mamlaka hizi na nyingine
zote zitahitaji kuimarishwa sana katika siku zijazo.
Hali ya Uchumi
Mheshimiwa Spika,
Kwa
ujumla, uchumi wa Tanzania umeendelea kuboreka katika miaka ya hivi karibuni,
kufuatia utekelezaji wa kina uliofikiwa katika marekebisho mbalimbali ya uchumi
na sekta ya fedha. Viashiria vya
mafanikio ya hivi karibuni, yaliyoleta kutengamaa kwa uchumi mpana, ni pamoja
na kuongezeka kwa mitaji katika sekta za umma na sekta binafsi, na kuongezeka
kwa akiba ya fedha za kigeni na kujenga uwezo wa kutosha kuagiza bidhaa na
huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi 7 – 8 hivi sasa ukilinganisha na miezi 6.3
katika mwaka 2001.
Kuanzia
mwaka 1990 hadi Desemba 2003, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimeidhinisha jumla ya
miradi 2,527, inayokadiriwa kutoa nafasi za ajira 497,539. Kati ya miradi hiyo, miradi 1,809 ilikuwa
mipya, na miradi 718 ni ya upanuzi na ukarabati. Miradi 1,113 (asilimia 44)
inamilikiwa na wawekezaji wa ndani ya nchi, miradi 609 (asilimia 24) ni ya
wawekezaji wa nje, na miradi 805 (asilimia 32) ni ya ubia kati ya wawekezaji wa
ndani na wa nje.
Katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita, kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa imeendelea
kuongezeka, kutoka asilimia 3.3 katika mwaka 1997 hadi kufikia asilimia 6.2
mwaka 2002. Wastani wa ukuaji huu wa
kiuchumi wa asilimia 5.6 kwa mwaka kwa miaka mitatu mfululizo unatia moyo, hasa
ukilinganishwa na wastani wa ukuaji wa uchumi barani Afrika wa asilimia 3.4
katika kipindi hicho.
Kwa
sababu ya ukame uliotupata, inakadiriwa kuwa mwaka 2003 uchumi umekua kwa
asilimia 5.7, na mfumuko wa bei umeongezeka kidogo kutoka wastani wa asilimia
4.5 mwaka 2002 hadi asilimia 4.6 mwezi Desemba 2003. Kwamba ukame huu
haukuathiri sana utulivu wa uchumi mkuu ni ishara ya mafanikio makubwa ya
mageuzi yetu ya uchumi. Tutaendeleza
mageuzi hayo, na tutayaimarisha ili kamwe tusirudi nyuma tulikotoka.
Mheshimiwa Spika,
Sababu
kubwa ya Azimio la Arusha kusema “Fedha si msingi wa maendeleo”, ni kwa vile
tulikuwa hatuna fedha. Likasisitiza
kuwa huwezi kupanga maendeleo kwa kutegemea kitu ambacho huna. Ni hoja nzito, na ya haki kabisa.
Lakini
dunia inabadilika, na mahitaji ya maendeleo nayo hubadilika. Kwenye orodha ya mambo ambayo Azimio
lilituambia ni muhimu kwa maendeleo—yaani ardhi, watu, siasa safi, na uongozi
bora—napenda niongeze jingine, nalo ni mitaji. Ipo mitaji ya aina nyingi.
Mtaji wa maskini ni nguvu zake. Lakini
wakati umefika pia kutumia siasa safi na uongozi bora kuongeza upatikanaji wa
mitaji ya fedha.
Sote
tutakumbuka hali ya uchumi ilivyokuwa mwaka 1995. Na wala sisemi hivyo kwa kulaumu. Nimlaumu nani wakati mimi pia nilikuwa sehemu kamili ya Serikali
zilizopita nikiwa Waziri kwa miaka mingi?
Lakini ukweli ni kuwa
wakati ule ukuaji wa Pato la Taifa ulikuwa chini ya asilimia 3 kwa mwaka,
mfumuko wa bei ulikuwa karibu asilimia 30, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa
ndogo isiyotosha hata miezi minne ya thamani ya bidhaa na huduma kutoka nje,
Serikali ilikuwa inakusanya mapato yasiyozidi wastani wa Sh. 25 bilioni kwa
mwezi, nidhamu ya matumizi ya Serikali na usimamizi wa fedha za umma ilikuwa
ndogo sana, uwajibikaji Serikalini na katika Sekta ya Umma kwa ujumla ulikuwa
mdogo, na Serikali ilikuwa inadaiwa kulia na kushoto, nje na ndani ya
nchi. Aidha, ushirikiano kati ya
Serikali na Sekta Binafsi ulikuwa wa kiwango cha chini, na uwekezaji ulikuwa
unasuasua. Misaada ya nje ilikuwa
michache na ilipatikana kwa masharti magumu. Kweli yupo anayetaka turudi huko?
Kiongozi, msomi au mwandishi habari aliye makini atakosaje kulinganisha
tulikotoka na tulipo leo? Ni kweli bado
kuna kazi kubwa ya kufanya. Lakini hiyo si sababu ya kupuuza yaliyofanyika.
Mheshimiwa Spika,
Mojawapo ya mambo ya mwanzo
yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu ilikuwa kubuni sera na mikakati
itakayoongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili Serikali iweze kuboresha huduma
za uchumi na za jamii na hivyo kusaidia jitihada za kupunguza umaskini. Tuliimarisha Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na kuipa madaraka kamili ya kukusanya mapato bila kuingiliwa na
Serikali. Aidha, Serikali ilianzisha
utaratibu thabiti wa majadiliano na wadau, hasa walipa kodi wakubwa, kuhusu
sera za kodi na utawala wa ukusanyaji wa kodi. Matokeo yake leo TRA inakusanya
wastani wa Sh. 108 bilioni kwa mwezi, ikilinganishwa na Sh. 25 bilioni mwaka
1995. Hadi mwisho wa mwezi uliopita,
pamoja na matatizo ya ukame, TRA ilikuwa imeshavuka lengo lake la miezi 7 ya
kwanza ya mwaka huu wa fedha kwa kukusanya Sh. 788.3 bilioni ikilinganishwa na
lengo la Sh. 757.4 bilioni. Yaani wamevuka lengo kwa karibu Sh. 30.9 bilioni.
Naomba Bunge hili liungane nami kuwapongeza kwa dhati kabisa viongozi na
watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kazi nzuri, na kuwataka waendelee
mbele. Tuna kazi ya kupiga vita umaskini.
Jambo la pili lilikuwa kurejesha mahusiano mazuri na
nchi wafadhili na mashirika ya fedha ya kimataifa. Leo tunapata misaada yenye thamani zaidi ya mara nne ya ile
tuliyokuwa tunapata kabla ya 1996.
Aidha, Tanzania ilikuwa moja ya nchi nne za kwanza kufuzu mtihani wa
kufutiwa madeni chini ya mpango wa HIPC, jambo ambalo limetuongezea uwezo wa
kutoa huduma za uchumi na za jamii.
Fedha zinazotolewa kwa sekta za kipaumbele kwenye vita dhidi ya
umaskini, ikiwemo elimu, afya, barabara, maji, vita dhidi ya UKIMWI na kilimo,
sasa ni mara nne zaidi ya kiwango cha mwaka 1996.
Tumeimarisha nidhamu katika matumizi ya fedha za
Serikali, kwa kuamua kutumia kile tu tulichonacho. Nalishukuru Bunge hili Tukufu kwa kupitisha sheria mbili muhimu
kwa nidhamu na usimamizi bora wa fedha za Serikali: Sheria ya Fedha za Umma (Public
Finance Act 2001), na ile ya Ununuzi wa Umma (Public Procurement Act
2001). Sheria hizi mbili
zimeimarisha nidhamu na utawala bora kiasi kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi
maskini zinazosifiwa sana kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika,
Uchumi mpana tulivu ni nyenzo muhimu sana ya
kuvutia uwekezaji, kuchochea ukuaji wa uchumi, kupanua nafasi za ajira,
kuongeza mauzo ya nje, kuongeza mapato ya Serikali na kuongeza misaada ya nje
pamoja na mikopo yenye masharti nafuu.
Uwezeshaji wananchi kimitaji nao unahitaji ushindani kwenye sekta ya
fedha. Tumepiga hatua kubwa ukizingatia
tulikotoka. Benki za biashara sasa ziko 26, taasisi nyingine za fedha ziko 6,
kuna kampuni za bima zaidi ya 10, tumeanzisha Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi
wa Umma (PSPF) unaoongezea kwenye huduma inayotolewa na mifuko iliyopo ya PPF,
NSSF na LAPF, soko la mitaji limeanzishwa na linakua, ipo sera mpya ya mikopo
midogo midogo, umeanzishwa mfuko wa kudhamini mikopo kwa sekta za kipaumbele
ambazo ni pamoja na vyama vya ushirika na kampuni zinazozalisha bidhaa maalum
kwa ajili ya kuuza nje, na umebuniwa mfuko wa hisa za pamoja (Unit Trust of
Tanzania). Maeneo haya yote yana mchango mkubwa katika kukua kwa uchumi, na
kuwawezesha Watanzania kimitaji.
Nitakazania sana eneo hili katika siku zijazo.
Mheshimiwa Spika,
Tusisahau
tulikotoka, na wala tusione haya kujivunia mafanikio yetu. Lakini kamwe tusiridhike, maana ukweli ni
kuwa bado ipo kazi kubwa mbele yetu, na matatizo bado ni mengi. Lakini tumeweka msingi mzuri, na hakuna
sababu ya kukosa ujasiri na kuanza kuangalia nyuma. Katika miaka michache ijayo, tutaweka mkazo katika maeneo
yafuatayo:-
1.
Kuchochea
uwekezaji na ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa zaidi. Asilimia 6 haitoshi. Tunataka kufika asilimia 8 na kuzidi. Huduma za benki na vyombo vya fedha
zitatakiwa kurahisisha upatikanaji mitaji na kushiriki kuvutia wawekezaji wa
ndani na nje. Marekebisho ya Sheria ya Ardhi yatasaidia. Bajeti ya Serikali
nayo itatumika kuboresha miundombinu na kuondosha vikwazo vingine vya uwekezaji
na biashara.
2.
Tutatumia bajeti
ya Serikali kuchochea upatikanaji wa ajira kwa kutumia sera za mapato na
matumizi, hasa kupitia mifuko ya udhamini wa mikopo kwa wawekezaji wadogo na wa
kati.
3.
Bajeti ya
Serikali pia itatumika kama kichocheo cha kuinua uzalishaji wa kilimo kwa njia
za udhamini na uwezeshaji, hasa kuhusu upatikanaji wa pembejeo na mbegu.
4.
Tutaendelea
kuboresha usimamizi wa fedha za Serikali ili mapato yanayoongezeka kutokana na
mafanikio ya mageuzi yetu yatumike kwa ufanisi katika vita dhidi ya umaskini na
kuwezesha wananchi kujiendeleza.
5.
Kwa kadri uchumi
unavyokua, na ukusanyaji kodi unavyoboreshwa, tuna lengo la kuongeza mapato ya
Serikali kutoka asilimia 12 ya Pato la Taifa hivi sasa hadi asilimia 15 ifikapo
mwaka 2006, na asilimia 18 ifikapo 2008.
6.
Tutaanzisha
mpango wa kubainisha na kutambua kisheria mitaji na raslimali za watu walio
katika sekta isiyo rasmi, pamoja na kubaini na kuondoa vikwazo vinavyofanya iwe
vigumu kwao kuingia kwenye sekta rasmi, inayotambuliwa kisheria.
Vita Dhidi ya Umaskini
Mheshimiwa Spika,
Umaskini
una sura nyingi—upo umaskini wa kukosa kauli katika masuala yanayomhusu mtu; na
upo umaskini wa kipato, miongoni mwa sura nyingine za umaskini.
Nimekuwa
Rais kwa zaidi ya miaka 8 sasa. Na
mambo mawili kuhusu umaskini yananitatiza sana kinadharia.
La
kwanza, ni namna ya kupima umaskini.
Wengi wanapenda kutumia kigezo cha mapato, tena kwa dola za marekani,
kwa siku. Lakini hicho ni kigezo finyu
sana, na kisicho sahihi hata kidogo. Ni
kipimo kinachokazania umaskini wa kipato tu, wakati umaskini hauna sura ya
mapato peke yake. Isitoshe, kwa uchumi
uliojikita kwenye sekta isiyo rasmi, kuna uhakika gani kuwa takwimu zetu
zinabeba ujumla wa mali na raslimali za jamii zetu? Mfugaji wa Kitanzania
anaweza kuwa anahama kila baada ya miezi michache, nyumba yake wala haistahili
kuitwa nyumba, na mfukoni hana pesa.
Lakini anao ng’ombe 500. Halafu
anaambiwa anaishi kwa chini ya dola moja kwa siku!
Mimi
nafikiri wakati umefika tuwe na tafsiri ya umaskini inayozingatia mazingira
yetu.
Jambo
la pili linalonitatiza linahusu swali la msingi kabisa. Hivi hasa vita dhidi ya umaskini
inapiganwaje? Na, ni nani hasa mwenye
wajibu wa msingi kupigana na umaskini?
Maana huishi kusikia au kusoma kwenye vyombo vya habari kuwa Serikali
haipigi vita umaskini, au mageuzi hayasaidii kupiga vita umaskini.
Ninyi,
Waheshimiwa Wabunge, ni wawakilishi halali wa wananchi. Naomba mnisikilize vizuri. Umaskini wa kauli unapigwa vita kwa
kuwapa watu kauli. Lakini umaskini wa
kipato haupigwi vita kwa kuwagawia watu pesa!
Mtaniwia
radhi, lakini lazima niweke jambo hili wazi, maana utakuta mtu mzima, mwenye
akili timamu, anauliza: “Kama mageuzi
yamefanikiwa mbona sina pesa mfukoni?
Serikali ina mpango gani?
Serikali hii haipigi vita umaskini.”
Ukweli
ni kuwa anayekuahidi kuwa Serikali inaweza kukuondolea umaskini wa kipato
anakudanganya. Nchi hii haiwezi kushinda
umaskini wa kipato kwa hadaa kama hizo, hadaa zinazowafanya wananchi wabweteke,
wasijitume vya kutosha wakingojea msaada.
Serikali makini haifanyi hivyo.
Yapo
mambo makuu manne niliyoyaahidi kwa nyakati mbalimbali kama mkakati wa vita
dhidi ya umaskini:
·
Kwanza, ni
kuwapa watu kauli juu ya mambo yanayowagusa, ikiwemo ushirikishwaji wa
kidemokrasia katika kupanga, kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo,
hususan ile ya kuondoa kero zao. Miradi
mikubwa kama TASAF na MMEM imejengwa imara juu ya dhana hii, kama ulivyo mpango
wa kuboresha Serikali za Mitaa.
·
Pili, ni kuweka
mazingira bora ya uchumi kukua na ajira kupatikana, ikiwemo mazingira
yanayovutia uwekezaji na kurahisisha biashara.
·
Tatu, ni
kupeleka kiasi kikubwa zaidi cha bajeti ya Serikali kwenye maeneo muhimu kwa
vita dhidi ya umaskini, ambayo tumekubaliana kitaifa kuwa ni elimu, afya, maji,
barabara za vijijini, na UKIMWI.
·
Nne, ni kuweka
mazingira mazuri kwa wananchi kujiendeleza, ikiwemo kwa kubaini na kisha
kuondosha vikwazo vyote kwa wananchi wanaotaka, na walio tayari, kujiendeleza.
Mheshimiwa Spika,
Nafurahi
wanapojitokeza wananchi kutathmini vita dhidi ya umaskini niliyoahidi
kuiongoza. Lakini wafanye tathmini ya
haki, kwa yale niliyoahidi.
Niliyoyataja hapa niliyaahidi, na niko tayari kupimwa nayo. Lakini
sikuahidi, wala Chama changu hakikuahidi,
kuweka fedha mifukoni mwa watu.
Tuliahidi fursa, na fursa zinawafaa wanaozitumia. Haziwezi kuwafaa wasiozitumia.
Ushirika
Mheshimiwa Spika,
Idadi
kubwa ya Watanzania ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Kwa hawa, na kwa hali halisi ya nchi yetu, ipo njia moja tu ya
uhakika ya kuwawezesha kutumia fursa za kujiendeleza katika mazingira ya uchumi
wa soko. Njia hiyo ni ushirika. Pamoja na matatizo yote yaliyovisibu vyama
vya ushirika bado ukombozi wa uhakika wa wakulima, wafugaji, wavuvi na
wafanyabiashara ndogondogo ni umoja kupitia ushirika. Nguvu ya mnyonge ni umoja.
Mwaka
2000 niliitisha kongamano kuhusu ushirika kule Mwanza kuchambua matatizo ya
ushirika, na kuyatafutia ufumbuzi ili ushirika ukidhi matarajio yetu ya
kuimarisha umoja wa wanyonge, umoja ambao ndio uwezeshaji wao.
Ninalishukuru
Bunge hili Tukufu kwa kupitisha Sheria mpya ya Ushirika mwezi Novemba 2003
ambayo inaweka mazingira mazuri ya kuimarisha ushirika, na kuwapa wanachama
kauli kubwa zaidi ya kidemokrasia katika uendeshaji wa vyama vyao. Sheria hii pia itasaidia kudhibiti wizi na
ubadhirifu, mambo ambayo huko nyuma yalihujumu ushirika kwa kuwavunja moyo
wanachama.
Lakini,
sera na sheria zitakuwa na maana tu iwapo wanachama wenyewe watakuwa jasiri
kudhibiti viongozi wao na mwenendo wa ushirika wao. Hivyo, tumeanzisha Mpango
wa Elimu ya Ushirika Shirikishi ili kuwajasirisha wanachama, kuwapa mbinu za
ujasiriamali, na mbinu za kusimamia vizuri zaidi vyama vyao.
Mheshimiwa Spika,
Sera
ni muhimu. Sheria ni muhimu. Na uwezeshaji kielimu ni muhimu. Lakini mitaji nayo ni muhimu. Hali ya mitaji ya vyama vingi vya ushirika,
hasa vya mazao ya kilimo, ni mbaya sana.
Hivyo, Serikali imeamua kuvisaidia na kuviwezesha vyama hivyo kimitaji
kupitia utaratibu wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya Nje (Export Credit
Guarantee Scheme) unaoviwezesha kukopa fedha za kununulia mazao ya
wakulima, na kuyauza nje ya nchi. Kwa
utaratibu huu, vyama vya ushirika vilikopeshwa Sh.10.1 bilioni na CRDB mwaka
2002/03. Mwaka huu, 2003/04, vyama vimekopeshwa Sh.16.3 bilioni na CRDB na
Benki ya Ushirika Kilimanjaro (Kilimanjaro Cooperative Bank). Nazishukuru Benki hizi kwa kushirikiana
nasi, na navionya vyama vya ushirika visithubutu tena kutumia mikopo hii nje ya
makusudio yake, na wahakikishe wanailipa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika,
Huu
ni ufumbuzi wa muda mfupi wa matatizo ya mitaji. Ufumbuzi wa kudumu ni kujenga uwezo wa mitaji ndani ya vyama
vyenyewe. Huo ndio utakuwa uwezeshaji wa
kudumu. Vyama vya ushirika vya kuweka
na kukopa ni jibu la uhakika la tatizo la mitaji. Tumeweka mkazo mkubwa sana kwenye jambo hili, na mafanikio
yameanza kuonekana. Vyama vya Akiba na
Mikopo vimeongezeka kutoka 803 mwezi Juni 2000 hadi 1,264 mwishoni mwa 2003,
sawa na ongezeko la asilimia 57 katika kipindi cha miaka 2½ tu. Hisa na akiba kwenye vyama hivyo nazo
zimeongezeka kutoka Sh.14.0 bilioni hadi Sh.25.7 bilioni, ongezeko la asilimia
83. Mikopo nayo ikaongezeka kutoka
Sh.11.5 bilioni hadi Sh.28.5 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 117. Huu
ndio uwezeshaji wanyonge kimitaji, na utawanufaisha walio tayari kushirikiana
na wenzao. Wasiotaka kushirikiana watabaki kulalamika.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja
na kuviwezesha vyama vya ushirika kwa kuviwekea mazingira bora ya kisera na
kisheria, na pamoja na kuviwezesha kielimu na kimitaji, tutaweka mkazo pia
kwenye ukaguzi ili kuhakikisha kuwa mali na fedha za vyama zinatumika vizuri,
kwa ufanisi, kwa manufaa ya wanachama badala ya manufaa binafsi ya viongozi.
Mheshimiwa Spika,
Wapo
wanaouliza faida ya mageuzi yetu ya kiuchumi ni nini kwa wananchi wa
kawaida. Nasema, utashi wa wazi wa
kisiasa wa kuwasaidia wanyonge kupitia ushirika, mapato ya Serikali
yalioongezeka na kutuwezesha kugharamia uwezeshaji kwenye ushirika kama nilivyoelezea hapa, na mageuzi
kwenye sekta ya fedha yaliyowezesha vyama vya ushirika kukopeshwa, ni faida za
wazi kwa wanyonge na ni uwezeshaji wao katika uchumi wa soko, na utandawazi.
Lakini ili wafaidike, wanyonge lazima wajiunge kwenye ushirika, lazima
wausimamie vizuri ushirika wao, lazima wawe wajasiriamali, wabunifu na wenye
kuthubutu na kujiamini. Sifa hizo
zinatokana na wananchi wenyewe. Serikali haiwezi kuzishurutisha kwao. Waheshimiwa Wabunge mnayo nafasi nzuri, na
ni wajibu wenu, kujenga sifa hizo miongoni mwa wananchi kwenye kila jimbo la
uchaguzi, na ni vema muwaambie wananchi ukweli huu.
Unajua,
Mheshimiwa Spika, wasiotupenda wanadai kuwa sisi wanasiasa ni walaghai,
wasiosema ukweli wote. Si sifa nzuri hata kidogo na inaweza kuwa na madhara
baadaye. Siku moja basi lililojaa wanasiasa liliacha njia na kugonga mti kwenye
shamba la mkulima mmoja mzee. Mzee yule akaenda kuchunguza. Kisha akachimba
kaburi na kuwazika wanasiasa wote. Siku chache baadaye akaja askari polisi. Akamuuliza
yule mzee, “Je, wote walikufa?” Mzee akajibu, “Ah!, wengine walisema hawajafa,
lakini unajua tena jinsi wanasiasa walivyo hodari wa kudanganya!”
Mungu apishie mbali!
Mheshimiwa Spika,
Ulimwengu, kupitia
Umoja wa Mataifa, ulijiwekea malengo 8 ya kufikiwa ifikapo 2015 ili kupunguza
umaskini kwa nusu duniani. Yanaitwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Lengo la 2 kwenye orodha hiyo linahusu
elimu, kwamba ifikapo mwaka 2015 kila mtoto, wa kike na wa kiume, apate elimu
kamili ya msingi. Benki ya Dunia
inasema ifuatavyo kuhusu lengo hilo:
“Elimu ni maendeleo.
Inawapa watu uwezo wa kuchagua na inawapa fursa, inawapunguzia mizigo
miwili ya umaskini na maradhi, na inampa mwenye nayo kauli nzito zaidi kwenye
jamii. Inafanya nchi ziwe na nguvukazi
yenye elimumwendo (dynamic) na raia waelewa wanaoweza kushindana na
kushirikiana na wengine duniani—ikifungua milango ya mafanikio ya kiuchumi na
kisiasa.”
Mheshimiwa Spika,
Serikali inakubaliana
kabisa na kauli hiyo. Ndiyo maana
Serikali ya Awamu ya Tatu imeweka mkazo mkubwa sana kwenye elimu ya msingi; na
tukaona kuwa mwaka 2015 ni mbali mno kufikia lengo muhimu kama hili.
Tukabuni Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Msingi, (MMEM), 2002-2006, kuhakikisha lengo hili
linafikiwa ifikapo mwaka 2006. Yapo
mafanikio mengi ya mpango huu katika miaka yake miwili ya kwanza. Nitataja machache tu.
1.
Tumefikia usawa
wa kijinsia kwenye shule za msingi;
2.
Idadi ya
wanafunzi kwenye shule za msingi imeongezeka kwa asilimia 50;
3.
Tumeongeza
uwiano wa watoto wanaoandikishwa shule kwa rika ya wanaopaswa kuwepo shuleni
(GER) kutoka 77.6% mpango ulipoanza hadi 105.2% hivi sasa;
4.
Tumeongeza kiasi
cha wanafunzi wanaobakia shuleni mpaka mwisho (NER) kutoka 58.8% tulipoanza
hadi 88.5% hivi sasa.
5.
Tumejenga
madarasa 31,825, na nyumba za walimu 7,530 kwa kushirikiana na wananchi;
6.
Tumejenga shule
mpya za msingi 1,081;
7.
Walimu wapya
17,851 wameajiriwa, na 14,852 kupatiwa mafunzo ya kujenga uwezo wao na
kujiendeleza;
8.
Upatikanaji wa
vitabu umeongezeka kutoka uwiano wa kitabu 1 kwa wanafunzi 8 (1:8) katika
madarasa ya I-IV hadi kufikia 1:3, na kutoka 1:10 hadi 1:6 kwa madarasa ya
V-VII;
9.
Kiwango cha
kufaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kimeongezeka kutoka 22% mwaka 2000
hadi 40.1% mwaka 2003;
10.Kamati za shule 12,689 zimepatiwa mafunzo ya kujenga
uwezo wa kusimamia miradi ya shule na shule zenyewe.
Mheshimiwa Spika,
Mafanikio ya MMEM
yameonyesha usahihi wa mwelekeo ambao tunaamini ndiyo njia pekee ya kufikia
Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Mimi
ninaamini kuwa malengo hayo yatafikiwa iwapo tu kuna ushirikiano wa kimataifa
unaozingatia mambo matatu yafuatayo:
·
Kwanza, utashi
wa kisiasa na utawala bora katika nchi maskini.
·
Pili,
mipango-shirikishi kwenye kila jamii.
·
Tatu, mazingira
nje ya nchi yanayosaidia jitihada za nchi maskini kama vile kusamehe madeni,
kuongeza misaada badala ya mikopo, na kutoa fursa za uwekezaji na biashara.
Haya mambo matatu ndiyo yametuwezesha
kupata mafanikio yetu, na kutupa matumaini kuwa malengo ya elimu ambayo dunia
ilifikiri yatafikiwa mwaka 2015, sisi tutayafikia mwaka 2006, yaani miaka 9
kabla ya tarehe iliyowekwa na Umoja wa Mataifa!!
Lakini narudia
kibwagizo changu. Ni mageuzi yetu ya uchumi ndiyo yaliyosaidia kukua kwa uchumi
na kuongezeka kwa mapato ya Serikali, na hivyo kutuwezesha kufuta ada kwenye
shule za msingi. Ni mageuzi yetu ndiyo
yalitufanya tuwe na mahusiano mazuri na wahisani, na kusamehewa kiasi fulani
cha madeni ya nje na kuelekeza unafuu tulioupata kwenye sekta muhimu kwenye
vita dhidi ya umaskini kama ilivyo elimu.
Ni mageuzi yetu ndiyo yametufanya tuaminiwe na wahisani na kupewa
misaada zaidi na mikopo ya masharti nafuu.
Na ni utashi wa kisiasa uliotuwezesha kuongeza sehemu ya bajeti ya
Serikali iendayo kwenye sekta za kipaumbele kwenye vita dhidi ya umaskini.
Mheshimiwa Spika,
Mafanikio ya Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Msingi yametupa uzoefu na dhamira ya kuwa na Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Sekondari utakaoongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na
elimu ya sekondari kutoka asilimia 22 ya waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2003
hadi asilimia 50 ya watakaomaliza elimu hiyo mwaka 2009, tena kwa kuzingatia
jinsia na mtawanyiko kijiografia ndani ya nchi. Lengo pia ni kuongeza kiwango cha kufaulu mtihani wa kidato cha
IV ili wanaopata Daraja la I – III wafikie asilimia 70 ya wanafunzi wafanyao
mtihani ifikapo 2009.
Mheshimiwa Spika,
Yote haya
yamewezekana, na yataendelea kuwezekana kutokana na mafanikio ya mageuzi yetu,
ili mradi tusirudi nyuma wala kupunguza kasi. Mageuzi yanafungua milango na
fursa kwa wengi, ukianzia na hawa wapatao elimu. Baadhi yao wamefanya vizuri
sana katika shule zetu za Serikali na za binafsi, na kututia moyo.
Leo, mbele yenu,
Waheshimiwa Wabunge, napenda niwatambulishe vijana wetu wanafunzi, mmoja wa
kike na mwingine wa kiume, waliofanya vizuri kuliko wenzao wote Tanzania kwenye
mitihani iliyopita ya Darasa la VII, Kidato cha IV, na Kidato cha VI.
Katika mtihani
uliofanyika Septemba 2003 wa kumaliza elimu ya msingi, binti wa Kitanzania,
Mbuke Solomoka, aliyekuwa anasoma Shule ya Kanawa, Wilaya ya Shinyanga
Vijijini, alikuwa msichana wa kwanza; na kijana wa Kitanzania, Kesy Fulano,
kutoka Shule ya Bumanji, Wilaya ya Geita, naye alikuwa wa kwanza kwa upande wa
wavulana.
Katika mtihani wa
Kidato cha IV uliofanyika Oktoba 2003, binti mwingine wa Kitanzania, Sara A.
Cheche, aliibuka cheche kweli kweli na kuwa wa kwanza kwa upande wa wasichana
Tanzania nzima. Yeye alikuwa anasoma
St. Mary, Mazinde Juu. Kwa upande wa
wavulana, kijana wa Kitanzania, Mosses Mwizarubi aliyekuwa anasoma Ilboru
alikuwa wa kwanza.
Katika mtihani wa
kumaliza Kidato cha VI uliofanyika mwezi Mei 2003, binti wa Kitanzania, Alice
Edward, kutoka St. Mary, Mazinde Juu alikuwa msichana wa kwanza, na kijana Emil
Patrick aliyekuwa anasoma Mzumbe alikuwa wa kwanza.
Vijana wetu hawa wako
katika ukumbi huu, na naomba wasimame Bunge hili liwatambue ipasavyo. Naomba
tuwapigie makofi wanayostahili.
Mheshimiwa Spika,
Nataka Bunge
liwatambue maana hawa na wenzao wengi ndilo tumaini la Tanzania ya kesho. Uendelevu na ustawi wa Tanzania unawategemea
hawa. Lazima kama wazazi na kama taifa
tuwekeze sana kwenye vijana wetu kama hawa.
Dunia ijayo ni ya ushindani mkubwa sana. Walioelimika vizuri ndio wenye uhakika wa kuhimili ushindani huo,
iwe kwenye ajira au kwenye biashara.
Kupitia kwa vijana
hawa napeleka ujumbe kwa wenzao wote wa Kitanzania. Ujumbe wangu ni mfupi sana.
Tutafanya kila tuwezalo kuwapeni elimu.
Lakini uamuzi wa kutumia elimu hiyo ni wenu. Tambueni kuwa upo mzigo mkubwa wa kuendesha nchi hii ambao unawasubiri. Jiandaeni vizuri. Someni kwa makini.
Msituangushe. Na zaidi sana
msipate UKIMWI. Thamani yenu ni kubwa
sana na ni ya kudumu. Msiipoteze kwa
tamaa za mwili zipitazo.
Mheshimiwa Spika,
Mafanikio ya mageuzi
ya uchumi yametuwezesha pia kupanua elimu ya juu, kwa kushirikiana na sekta
binafsi na mashirika ya dini. Matokeo
yake katika miaka 4 iliyopita (1998/99 – 2002/03) idadi ya wanafunzi katika
vyuo vya ufundi, vyuo vikuu binafsi na vyuo vikuu vya umma iliongezeka kutoka
18,829 hadi 30,602, sawa na ongezeko la asilimia 62.5. Cha kutia moyo zaidi ni kuwa ongezeko kubwa
lilikuwa la wanafunzi wa kike ambao wameongezeka kutoka 3,889 hadi 10,137, sawa
na ongezeko la asilimia 160.7. Miaka 4
tu iliyopita wanawake walikuwa asilimia 20.7 ya wanafunzi wote kwenye vyuo
hivi. Leo wapo asilimia 33.1. Nawapongeza sana wanawake waliojitokeza
kutafuta elimu ya juu. Maana Serikali
inaweza kutoa fursa, lakini uamuzi wa kutumia fursa hizo ni wa mtu binafsi.
Mheshimiwa Spika,
Uwezeshaji kwa njia ya
elimu ni sehemu muhimu ya mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na changamoto za
utandawazi. Bado tunayo kazi kubwa ya
kufanya. Lengo la Serikali ni kuwa
ifikapo mwaka 2008 wawepo wanafunzi 55,000 katika vyuo vya ufundi, vyuo vingine
vya elimu ya juu, na vyuo vikuu. Mambo
matatu ni muhimu sana ili tufike hapo.
Kwanza, Bunge hili liendeleze utashi wa kisiasa wa mkakati huu. Pili, uchumi ukue kwa kasi zaidi na kuipa
Serikali mapato ya kutekeleza mipango yetu, na Bunge hili lichochee ukuaji huo.
Tatu, elimu ya sekondari ipanuke na iboreke, kupitia mpango ambao
nimeuzungumzia, ili tupate wahitimu bora wa kutosha kudahiliwa kwenye vyuo
vyetu.
Napenda nilishukuru
Bunge hili Tukufu kwa kukubali kupitisha Sheria Na. 8 ya 2001 iliyoanzisha
Mfuko wa Elimu, ambao kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge watakumbuka una malengo
matatu makuu:
·
Kwanza,
kuhakikisha elimu yetu katika ngazi zote ni bora zaidi;
·
Pili,
kuhakikisha upo mfumo endelevu wa kugharamia elimu nchini; na
·
Tatu kuhakikisha
mfumo wa elimu unatoa fursa sawa kwa wote, bila ubaguzi wowote.
Mfuko umeanza kazi, na tayari Mamlaka
ya Elimu Tanzania inayousimamia imetoa Sh.3.4 bilioni kwa vyuo vya ufundi na
vyuo vikuu vya umma Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na vyuo vikuu binafsi na
vya mashirika ya dini. Narudia. Mfuko huu ni wa kuwezesha elimu kwa
Watanzania wote, bila ubaguzi. Popote
Mtanzania anapopata elimu, ujumla wake ni ongezeko la wasomi nchini ambayo ni
hazina ya taifa. Tutaendeleza
ushirikiano huu kati ya Serikali zetu mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, na
taasisi binafsi za elimu nchini kwa lengo moja la kuongeza idadi na ubora wa
nguvukazi ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
Sekta ya afya ni
muhimu sana katika vita dhidi ya umaskini.
Lakini ni wazi pia kuwa mafanikio yake hayategemei utashi na maamuzi ya
Serikali peke yake. Hatimaye afya ya
mtu ina gharama, ambayo mwenyewe lazima awe tayari kuibeba. Ipo gharama ya kuzuia usiumwe – kwa kula
chakula bora, kwa kuweka mazingira ya pale unapoishi na kufanya kazi kuwa safi,
kwa kufanya mazoezi, kwa kuzuia magonjwa kwa chanjo pale palipo na chanjo, au
kwa kuepuka kuambukizwa kwa magonjwa kama UKIMWI yasiyo na chanjo, na kwa kuchangia gharama za matibabu.
Mafanikio ya mageuzi
yetu, na mahusiano mazuri na wahisani na sekta binafsi, yote yametusaidia
kuleta mabadiliko makubwa ya mfumo wa huduma za afya, ukarabati wa taasisi za
afya na upatikanaji wa chanjo. Bajeti ya afya imekuwa ikiongezeka kwa miaka 3
mfululizo. Hili nalo limewezekana kwa
sababu ya mafanikio ya mageuzi yetu ya kiuchumi.
Hali ya chanjo
imeboreka na kufikia asilimia 83, kuzidi kiwango cha asilimia 80 ambacho
kimataifa kimekubalika kuwa ni kiwango kizuri.
Hivi sasa tumeanza kutoa chanjo ya Hepatitis ambayo imechanganywa
na chanjo iliyopo ya DPTT bila malipo ya ziada. Hii itasaidia kuokoa maisha kati ya 20,000 – 25,000 yanayopotea
kwa mwaka hivi sasa.
Tanzania ipo mstari wa
mbele duniani katika vita dhidi ya malaria.
Lakini tunaomba uelewa na ushirikiano wa wananchi. Tumefuta kodi kwenye vyandarua na bidhaa
zinazosaidia vita dhidi ya malaria.
Tumepata msaada wa Mfuko wa Kimataifa wa Kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu
na Malaria. Hivyo tumeweza kufidia
baadhi ya gharama za vyandarua vilivyotiwa dawa ambavyo imedhihirika vinasaidia
sana kupunguza maambukizo ya malaria hasa kwa kina mama waja wazito na watoto
wachanga. Lakini jitihada zetu hizo ni
bure iwapo wananchi hawatatumia utaratibu uliowekwa.
Mheshimiwa Spika,
Duniani kote bima ya
afya ndiyo kinga thabiti, hasa kwa wanyonge, ya kukabiliana na gharama za
tiba. Kwa wananchi wa kawaida
tumeanzisha Mifuko ya Afya ya Jamii.
Pale ambapo mifuko hii inafanya kazi yapo mafanikio makubwa ambayo siri
yake ni ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wananchi. Mifuko hiyo imewapunguzia mzigo na hofu
wananchi, na kuzipatia hospitali uwezo wa kujiendesha. Tunataka mifuko hii ianzishwe katika wilaya
zote zilizobaki katika miaka michache ijayo.
Kwa wafanyakazi wa
sekta ya umma, tumeanzisha bima ya afya ambayo huchangiwa kati ya mfanyakazi na
mwajiri. Matatizo mengi ya awali
kutokana na uchanga wa mfuko yamepatiwa ufumbuzi, na kazi iliyo mbele yetu ni
kuimarisha mfuko huo, na kuboresha taratibu zake.
Tumeendelea
pia na ukarabati mkubwa wa vituo vya huduma za afya, kuanzia Hospitali ya Taifa
Muhimbili ambapo kazi inaendelea, mpaka hospitali za wilaya. Kwa mfano, kwa kushirikiana na Serikali ya
Uholanzi, tayari tumefunga mashine za eksirei na mashine nyingine katika
hospitali za wilaya, mikoa na rufaa.
Kazi iliyo mbele yetu ni kuvitumia vifaa hivyo vizuri, na kuvitunza, ili
viendelee kutumika kwa miaka mingi ijayo na kuboresha uwezo wa madaktari kutibu
wagonjwa kwa usahihi na uhakika zaidi.
<