HOTUBA YA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM),
MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA CCM,
DODOMA, 25 AGOSTI 2004
Makamu
Mwenyekiti wa CCM (Bara),
Mhe. John Samwel Malecela, Mb.;
Rais
na Mwenyekiti wa CCM Mstaafu,
Mhe. Mzee Ali Hassan Mwinyi;
Makamu
Mwenyekiti wa CCM Mstaafu,
Mhe. Dkt. Salmin Amour;
Katibu
Mkuu wa CCM,
Mhe. Philip Mangula;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Kamati Kuu;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Halmashauri Kuu;
Mabibi
na Mabwana:
Karibuni nyote tena kwenye Mkutano
wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi.
Leo nimeamua kutoa hotuba, tena
iliyoandikwa, maana jambo nitakalo kulizungumza ni zito na nimelitafakari kwa
muda sasa. Napenda kuzungumza nanyi
kuhusu Ushupavu wa Uongozi, kwa Kiingereza: “The Courage of
Leadership.”
Nafanya hivyo kwa vile tunaelekea
kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani, uchaguzi ambao tuna kila sababu ya kuamini kuwa
utaendeleza Awamu ya Sita ya Uongozi Zanzibar, na utaanzisha Awamu ya Nne ya
Uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Chama Cha Mapinduzi. Na ningependa tujiandae vizuri kifikra,
kimaadili, kiutawala, na kwa kujikumbusha kanuni na taratibu zetu zote.
Napenda leo tujiulize swali la msingi kabisa: Sisi Chama Cha Mapinduzi tunataka uongozi;
vema, lakini je Chama chetu kinao ushupavu wa uongozi unaohitajika katika
mazingira ya Karne ya 21? Wagombea wetu
watarajiwa nao je?
Waheshimiwa
Wajumbe:
Katiba ya Chama Cha Mapinduzi
imeorodhesha malengo na madhumuni ya CCM, na mwanzo kabisa kwenye orodha hiyo
ni:
“Kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania
Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.”
Na zipo njia mbili kubwa za mtu kushinda
uchaguzi. Moja ni kuhakikisha unakuwa
mgombea wa chama chenye nguvu na mvuto, kama ilivyo CCM hivi sasa. Maana yake ni kuwa hata wewe mgombea ungekuwa
hovyo kiasi gani, utabebwa na chama, na utachaguliwa kuwa diwani, mbunge au
rais, kwa sababu tu ya chama. Njia
nyingine na ya pili ni mgombea mwenyewe kuwa na sifa ambazo zinatosha kuvutia
wananchi wampigie kura, sio chini ya kivuli cha chama chake. Napenda leo tujikumbushe kuwa yote haya
mawili ni muhimu: Chama imara, chenye ushupavu wa uongozi; na wagombea imara,
wenye sifa, uwezo na ushupavu. Na kuhakikisha kabisa, yote mawili ni muhimu na
ni vema yaambatane.
Napenda tujikumbushe maana upo
uwezekano wa wana-CCM kubweteka. Kwa vile tunajua chama chetu kina nguvu na
mvuto, hatuweki mkazo mkubwa kwenye kujinoa binafsi. Badala yake tunapigana
vikumbo kutafuta kuteuliwa, kwa kuamini ukishateuliwa ndio “umeula”. Na
tukishaelekea huko, hakutakuwa na kingine kinachotusukuma ila ubinafsi—ubinafsi
wa kusema mimi lazima niendelee, na anayenisogelea ni adui; au ubinafsi wa
kusema wewe sasa imetosha, sasa ni zamu yangu.
Upo uwezekano pia kuwa
tusipokuwa waangalifu, ajenda yetu kuhusu mwakani haitaandaliwa na sisi, katika
CCM, bali na wapinzani wetu na vyombo vya habari. Wapinzani wanataka kutuvuruga
na kutugonganisha, na wenye magazeti wanataka kuuza na kupata faida. Lakini wajibu wa hatma ya nchi yetu umo
mikononi mwa CCM, si mikononi mwa wapinzani wala waandishi wa habari na
wamiliki wa vyombo vya habari. Lazima tuuchukulie wajibu huo kwa uzito
unaostahili, na tujenge ushupavu wa uongozi wa kuutimiza.
Hivi sasa waandishi wa habari na
vyama vya upinzani wanatuchokoza tujielekeze kwenye kuzungumzia wagombea wetu
kwa uchaguzi wa mwakani.
Tusikubali. Tukiwaendekeza,
tutajikuta tunatafuta au kuunga mkono wagombea kabla ya wakati, na hivyo kuanza
kugawanyika na kudhoofika, badala ya
kushirikiana kubuni malengo na dira kwa miaka 5 ijayo. Vyama vya upinzani na vyombo vya habari
wanataka tuzungumzie watu, badala ya kuzungumzia kazi muhimu ya chama iliyo
mbele yetu. Kama ilivyo mtego wowote,
huu pia unavutia, hasa kwa wanaokusudia kugombea uongozi. Tuwe shupavu kuukwepa mtego huu.
Waheshimiwa
Wajumbe:
CCM ina nguvu. Lakini nguvu peke yake haitoshi. Nguvu hiyo
inapasa kudhihirisha na kuainisha mwelekeo wake. Huu ni wakati wa kujenga
ushupavu wa uongozi, ili CCM iandae ajenda na mwelekeo wa taifa, na iongoze
taifa—kwa maana ya watu na raslimali—katika karne ya 21 ya utandawazi. Ushupavu huo ndio utasaidia kuhakikisha
chipukizi wa CCM nao watakuja kuongoza nchi hii.
Mimi ni muwazi na mkweli: Naamini
hivi sasa wananchi wana wasiwasi mkubwa kuhusu hatma ya uongozi
wa taifa letu
baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani. Wasiwasi huo ni wa
kweli, na upo, ingawa wanajua CCM
itashinda. Tujiulize kwa nini wana wasiwasi. Wanaona mapungufu gani ambayo
sisi viongozi wao ama hatuyaoni, au hatuna ushupavu wa kuyashughulikia?
Nizungukapo mikoani wazee wa CCM hunijia, pamoja na viongozi wengine wa
CCM, na hata wananchi wa kawaida, wakinisihi nihakikishe CCM inachagua vizuri
wagombea wake katika ngazi zote za uongozi.
Wanahofu kuwa pengine hatutakuwa makini vya kutosha, na kwamba pengine
CCM italewa nguvu yake na kubweteka. Wangejua tutakuwa makini wasingehofu. Huo
ndio ukweli. Na hofu yao inatokana na
kujua, kama alivyobainisha Baba wa Taifa, kuwa: “Bila CCM madhubuti nchi
yetu itayumba.”
Pamoja na kelele zote za wapinzani na magazeti, mwananchi wa kawaida
anajua kuwa CCM ndiyo mhimili wa taifa hili, na ndiyo bima yake dhidi ya
matatizo yanayozikumba nchi nyingine, ikiwemo baadhi ya nchi jirani. Ndio maana
hata wapinzani wenyewe wanafuatilia sana afya ya Chama Cha Mapinduzi. Tukipiga
chafya sisi, kila mtu anapata homa. Sisi tuna dhamana ya uongozi wa nchi hii,
dhamana ya amani, usalama na utulivu wa nchi, na dhamana ya kuongoza vita dhidi
ya umaskini. Tujikumbushe kila mara
uzito wa dhamana hiyo. Na wale miongoni mwetu tulio Serikalini, tuliokula viapo
vya utumishi wetu, tutafakari tena uzito wa viapo hivyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakula viapo vitatu:
·
Kiapo cha kwanza ni cha utii,
ambapo anaapa kuwa atakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kuitumikia kwa moyo wake wote, na kwamba ataihifadhi, kuilinda na kuitetea
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
·
Kiapo cha pili ni cha Rais, ambapo
anaapa kwamba atatenda kazi zake za Urais kwa uaminifu na kutimiza wajibu wa
kazi hizo kwa bidii na moyo mkunjufu, na kwamba atawatendea haki watu wote kwa
mujibu wa Sheria, mila na desturi za Tanzania bila woga, upendeleo, huba wala
chuki; na,
·
Kiapo cha tatu ni cha kudumisha
Muungano, ambapo anaapa kwamba ataitetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wao, Mawaziri wanakula viapo viwili. Kiapo cha utii kinachofanana na kile cha
Rais, na kiapo cha Waziri ambapo wanaapa kuwa wataitumikia vema na kwa moyo
thabiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kazi za Uwaziri na kuwa kwa
wakati wote watamshauri kwa hekima na uaminifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kuwa kwa vyovyote vile hawatatoa siri za Baraza la Mawaziri.
Waheshimiwa
Wajumbe:
Hivi ni viapo vizito. Tunaapa sisi tulio Serikalini, lakini
tumetumwa na Chama. Hivyo viapo hivi
vinakipa Chama wajibu kuhakikisha waliomo Serikalini wanaishi na kutumikia nchi
yetu kwa utimilifu wa viapo hivyo. Wapinzani hawali viapo kama hivi, hivyo
wanaweza kupayuka hovyo na kukosa umakini.
Hawana wajibu tulionao sisi.
Lakini sisi tunaokula viapo hatupaswi kwa vitendo vyetu na kauli zetu
kuonekana na sisi ni wapayukaji hovyo na watu wasio makini. Tukionekana au kufikiriwa hivyo, hatutoshi
kuongoza!!
Lazima, kwa ushupavu, tuwatoe wananchi hofu, waishi na kufanya kazi zao
wakiwa na uhakika kuwa nchi yao imo, na itaendelea kuwa, mikononi mwa viongozi
waadilifu, na Chama makini. Tupende
tusipende, hofu miongoni mwa raia ni hisia, na hata kielelezo, cha mapungufu ya
uongozi. Na hofu hiyo huzidi waonapo
watu wanataka kuingia Serikalini kwa uhodari wa ujanja, hila au rushwa, badala
ya kutaka kuingia kwa uhodari wa ushupavu wa kutumikia nchi.
Siku moja walikutana marafiki wawili waliokuwa wamepoteana kwa muda
mrefu. Mmoja akamuuliza mwenziwe, “Hivi
yule kaka yako aliyekuwa anatafuta kazi Serikalini anafanya nini siku hizi?
Rafiki yake akajibu, “Ah, yule
hafanyi kitu siku hizi. Alipata ile kazi
ya Serikali aliyokuwa anaitafuta!”
Waheshimiwa
Wajumbe:
Iwapo wananchi watapata hisia hizi,
au iwapo kwa vitendo vyetu tutawadhihirishia, kuwa tunatafuta uongozi
Serikalini ili tusifanye kazi zao, lakini tushibe, watakuwa na hofu kila
tunapoelekea kwenye uchaguzi.
Tunahitaji ushupavu wa uongozi.
Nikiwaulizeni hapa mmojammoja, nina uhakika wengi watasema kuwa zimeanza
kampeni za chinichini huko mikoani na wilayani.
Wengine wameniambia wapo wenye mkakati wa kununua wajumbe wa Mikutano
Mikuu ya Wilaya, Mikoa na hata Taifa.
Kama ni kweli, ujasiri wa viongozi huko mliko wa kusimamia maadili uko
wapi? Kwa nini sisikii viongozi wa CCM
wanaokerwa na hali hiyo wakiikemea katika vikao vya ndani? Kwa nini taarifa za namna hiyo haziji rasmi,
kwa taratibu zetu, lakini zinakuja kwa njia ya tuhuma, minong’ono na kupakana
matope? Waasisi wetu wasingekuwa jasiri
na shupavu tusingepata uhuru, wala kufanikisha Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Ujasiri na ushupavu wetu sisi, tunaodai haki ya urithi wa waasisi wetu, uko
wapi?
Ninyi ndiyo wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa. Na mojawapo ya kazi za
Halmashauri hii ni “Kudumisha uangalizi juu ya vitendo vya Wanachama na
Viongozi wa CCM na endapo itadhihirika kwamba tabia na mwenendo wa Mwanachama
fulani vinamwondolea sifa za uanachama au uongozi itakuwa na uwezo wa
kumwachisha au kumfukuza uanachama au uongozi alio nao…” (Katiba ya CCM, 77(8)). Haya ni madaraka makubwa, lakini sioni
ushupavu wa kuyatumia katika ngazi zote za uongozi wa Chama. Badala yake ni malalamiko ya chini kwa
chini. Hiyo ni hatari kubwa kwa Chama,
na kwa Taifa.
Nasema ninyi ndio Halmashauri Kuu ya
Taifa ya Chama Cha Mapinduzi. Hatma ya
CCM na Taifa letu imo mikononi mwenu.
Jiulizeni: Kama kweli hiyo
minong’ono ni ya kweli, hivyo ndivyo mnavyotaka iwe? Ndio mustakabali wa Chama chetu
mnaoutaka—kwamba maslahi binafsi yawe na nguvu kuliko maslahi ya CCM na
Taifa? Kama sivyo, ujasiri wenu wa
kusimamia maadili na haki uko wapi? Nitauliza maswali mengi leo.
Kwa asili yetu, huko tulikotoka, kulikuwa
hakuna fedheha kama ile ya mwanachama kujulikana kuwa eti amenunuliwa. Tuliona
kununuliwa ni sawa na utumwa, ni sawa na kuuza utu wako. Maana, huamui tena kwa akili aliyokupa
Mwenyezi Mungu, bali kwa kutumwa na aliyekununua. Utakuta mtu na akili yake
anatetea ambacho hakiwezekani kutetea. Tutastahilije kuongoza nchi katika
mazingira hayo? Mtu mzima una macho,
lakini unakuwa huoni kwa kupofushwa na fedha; una masikio lakini husikii kwa
vile masikio yako yamezibwa na ahadi za vyeo. Kisha unapojiangalia kwenye kioo,
unamwona nani: unaona kiongozi, au unaona kibaraka?
Nasema sisi katika Halmashauri Kuu
ya Taifa, wenye jukumu la kusimamia maadili, lazima tuwe mfano wa kufuata
maadili, mfano wa kuheshimu Katiba; mfano wa kuheshimu haki za kila mwanachama. Agombeaye nafasi si adui. Na tusisahau kuwa sifa moja ya kiongozi iliyo
ndani ya Katiba ni kuwa, “Awe ni mtu aliyetosheka, na asiwe mtu aliyetawaliwa
na tamaa.” (Katiba ya CCM, (17(1)).
Aliyetawaliwa na tamaa yuko radhi kuhujumu haki za wengine kugombea,
yuko radhi kuwazulia kashfa anaowaona ni washindani wake, na yuko radhi hata
kuhujumu maslahi ya Chama, ili mradi tu apate anachokitamani. Hatujengi Chama
namna hiyo!
Ipo hadithi ya mgombea mmoja kwenye
uchaguzi aliyetaka ushauri wa kiongozi wake wa chama kabla ya kampeni kuanza.
Mgombea: “Nadhani jambo muhimu kwenye
kampeni hii ni mimi kuelezea na kusimama kwenye rekodi yangu.”
Kiongozi wa chama: “Hapana. Jambo muhimu ni wewe kukanyaga na
kupondaponda rekodi ya mpinzani wako.”
Sasa, pengine mbinu hiyo inafaa kwa
wapinzani kutoka vyama tofauti. Lakini inawapa wananchi mashaka pale
inapotumika miongoni mwa wagombea kutoka chama kimoja. Wana-CCM tuiepuke!
Tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tahadhari ni kwamba adui wa CCM anaweza kuwa
yupo miongoni mwetu. Kikulacho kinguoni
mwako. Hakuna wapinzani wenye nguvu ya
kutudhoofisha. Tukidhoofu, tumejidhoofisha wenyewe, na hasa kwa kuendekeza
ubinafsi.
Hivi Mbunge au Diwani ambaye
haoni lolote jema lililofanywa na Serikali ya CCM anafanya nini ndani ya CCM? Na atajinadi vipi kwa rekodi ya utekelezaji
wa sera za CCM? Nchi hii imepata sifa
kubwa kwa kazi zilizofanywa na Serikali ya CCM, halafu Diwani au Mbunge wa CCM
anasema hakuna kilichofanyika. Nauliza tena. Anafanya nini ndani ya CCM? Ana tofauti gani na wapinzani? Mwalimu Nyerere alituonya tuhakikishe CCM
haiwi dodoki linalonyonya maji masafi na maji machafu sawia. Ushupavu wa NEC uko wapi?
Waheshimiwa
Wajumbe:
Sitaki ieleweke kwamba Wabunge na
Madiwani wa CCM hawana haki ya kuikosoa Serikali. Wanayo haki hiyo. Lakini, kuna
tofauti ya kukosoa utekelezaji wa sera, ambao ni wajibu wa Wabunge na Madiwani
wa Chama Tawala; na kukosoa sera yenyewe, ambao ni wajibu wa Wabunge na
Madiwani wa Upinzani. Katiba na
busara zinataka tupambanue wapi na lini tukosoe sera na utekelezaji wake.
Mbunge na Diwani lazima aamue yuko upande gani.
Na hata ukosoaji wa utekelezaji sera
lazima nao uwe wa staha, wa kujenga heshima na kuimarisha umoja, si ukosoaji wa
kudhalilisha, kubomoa na kukomoa. Nitatoa mfano. Hivi Mbunge au Diwani
anaposema madarasa ya MMEM hayafai kabisa, maana yake ni nini. Kwanza, kauli hiyo si ya kweli kwa ujumla
wake. Maana mimi nimezunguka nchi hii
kuliko wengi wenu. Nimeona madarasa ya MMEM vijijini ambayo ni mazuri kuliko
baadhi ya yaliyopo mijini. Nimezungumza
na wahisani wetu ambao wamekiri hivyo. Nimepokea barua za pongezi kutoka kwao.
Ni kweli kuna maeneo machache ambapo ujenzi wa madarasa hayo haukuwa
mzuri. Lakini, tatizo si sera, wala MMEM yenyewe, wala Waziri mhusika. Tatizo ni uongozi wa eneo linalohusika; na
Mbunge au Diwani ni sehemu ya uongozi huo.
Kashfa ambayo Mbunge au Diwani anafikiri anaizua, anajizulia yeye mwenyewe
kwanza. Iweje maeneo ya Wabunge au
Madiwani wengine yawe na madarasa ya MMEM mazuri yanayosifiwa mpaka Washington,
na ya kwake yeye ndiyo yawe mabaya?
Kulalamika Bungeni au kwenye Halmashauri, badala ya kuongoza kusahihisha
makosa, ni mapungufu ya ujasiri wa uongozi.
Nasema, tunahitaji ushupavu wa
kuongoza. Ushupavu huo si hotuba nzuri Bungeni au kwenye Halmashauri; ni
ushupavu wa kukaa na wananchi na kuwaongoza.
Penye makosa ni kusaidia kusahihisha, si kugeuka mwangwi wa kuchafua
rekodi ya Serikali ya CCM. Fedha za
Serikali zinaliwa kwenye jimbo la Mbunge, lakini anakuja kupigia kelele
Bungeni. Anaogopa kusemea kwenye jimbo
lake kwa kukosa ujasiri. Hayo nayo ni mapungufu ya ushupavu wa uongozi.
Halmashauri au Bunge la watu wenye haraka ya maendeleo ni mahali pa
kubadilishana uzoefu wa uhamasishaji na uchangiaji maendeleo huko Wabunge na
Madiwani wanakotoka, kila mmoja akieleza aliyoyafanya yeye kwenye jimbo lake,
au kata yake, kusudi wengine wamuige. Tusigeuze Bunge, Baraza la Wawakilishi na
Halmashauri kuwa mahali pa kumlaumu kila mtu isipokuwa wewe mwenyewe. Narudia. Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa ina
wajibu kusimamia nidhamu ya Chama. Bila nidhamu, punde si punde hatutakuwa na
Chama.
Waheshimiwa
Wajumbe:
Nchi rafiki, wahisani na mashirika
ya kimataifa nao wamenieleza hofu yao. Wawekezaji wamenieleza hofu yao. Wanataka uhakika wa kitakachotokea baada ya
uchaguzi mwakani. Na kwa nchi maskini na
tegemezi kama yetu, ambapo asilimia 42 ya bajeti yetu bado inawategemea
wahisani, hatuwezi kupuuza hofu yao. Kwa nchi ambayo fursa za ajira na mapato
ya Serikali hutegemea zaidi na zaidi uwekezaji wa sekta binafsi, hatuwezi
kupuuza hofu ya wawekezaji.
Si kwamba wana husuda tu ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi yetu;
wengi wao ni watu makini wanaotaka uhakika kuwa yale ambayo sisi na wao
tumekubaliana kuwa ni mema na ya maslahi kwa nchi yetu yatadumishwa; na yale ambayo
si mema na hayana maslahi kwetu, ambayo tumeanza kuyashughulikia, kuyafuta au
kuyakomesha, yataendelea kushughulikiwa. Wao pia wanajua CCM itashinda mwakani,
lakini bado wana wasiwasi. Kwa nini? Kwa kazi kubwa ya mageuzi na kukuza uchumi
tuliyoshirikiana nao kuifanya, wangependa Tanzania ipige hatua mbele kwa kasi,
si kuanza kubabaika, kusuasua, au kurudi nyuma.
Kila mara ninarudia kuwaambia wahisani na wawekezaji kuwa mageuzi haya
si yangu mimi binafsi, na kwamba ninaongoza utekelezaji tu wa Mwelekeo, Sera na
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Lakini bado wana hofu. Najiuliza, kwa nini? Nanyi nataka mjiulize: Kwa nini, na kwamba mtazamo huo unaashiria
nini?
Waheshimiwa
Wajumbe:
Leo napenda, kwa unyenyekevu kabisa,
nikupeni tathmini yangu kwa nini wananchi wanahofu, kwa nini wanachama wenzetu
wanahofu, na kwa nini wahisani na wawekezaji wanahofu. Kwa tathmini yangu binafsi, hofu yao
inatokana na mambo mawili ya msingi yanayoashiria mapungufu ya ushupavu wa CCM katika
kuongoza nchi yetu kwa kuzingatia mahitaji, na mazingira halisi, ya dunia ya
leo na ijayo.
Kwanza, wanashuhudia utekelezaji wa baadhi ya mambo yaliyo katika Ilani
yetu, na Mwelekeo wa Sera za CCM, ukichelewa au kusuasua kwa upinzani wa baadhi
ya wenzetu katika CCM, au kwa kukosa umakini miongoni mwa baadhi ya wenzetu
tuliowakabidhi kazi ya kusimamia utekelezaji.
Mara kadhaa wamesikia kuwa imebidi mimi mwenyewe kukutana na Wabunge wa
CCM kuwakumbusha kwamba Serikali inachotaka kukifanya ni utekelezaji wa Sera za
CCM. Mara kadhaa inabidi tufanye semina
za Chama katika ngazi mbalimbali kuelimishana na kukumbushana sera hizo. Sera
zetu zinapopingwa kidogo na wapinzani wetu au vyombo vya habari, au Asasi
Zisizokuwa za Serikali, ambao wengi wao hawaitakii CCM mema, baadhi ya wenzetu
wanaanza kuyumba. Hofu ya wahisani na
wawekezaji inatokana na mapungufu ya ushupavu wa CCM kutetea sera zake yenyewe,
hata pale ambapo mafanikio yake yanaonekana wazi. Wanasikia kauli tofauti kutoka ndani ya
CCM. Njia pekee ya kuondoa hofu hiyo ni
kurejesha umoja, mshikamano na ushupavu wa uongozi wa taifa letu ndani ya CCM.
Chanzo cha pili cha hofu yao, kwa tathmini yangu, ni kuwa kwa miezi
kadhaa sasa wanaona sisi wenyewe kwenye Chama Cha Mapinduzi tukitaka kutoana
roho kwa kujiweka vizuri kwa Uchaguzi Mkuu mwakani. Kama nilivyosema, baadhi ya madiwani waliopo
wanafanya kila mbinu wasitokee wengine kuwania nafasi zao. Baadhi ya wabunge
waliopo wanafanya kila mkakati kulinda wanachokiona kama vile ni himaya yao. Sisemi wanaotarajiwa au kushabikiwa kujipanga
kuwania Urais!!
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM,
kugombea au kutetea nafasi za uongozi ni haki ya kila mwanachama. Tatizo langu si hilo. Tatizo langu ni kuwa
wakati bado. Kama nilivyosema awali, tatizo
langu ni pale tunapogombea nafasi kabla ya kukubaliana hao tutakaowapendekeza
kugombea watakwenda kufanya nini.
Hivyo naomba tuache kwanza kuzungumzia, na pengine hata kuchukiana na
kuhujumiana, juu ya majina ya wagombea.
Tusitangulize mkokoteni kabla ya farasi. Tusiwe kama wapinzani. Sisi tuzungumze kwanza
kuhusu programu na Ilani ya CCM kwa miaka 5 ijayo. Tuzungumze mambo ya maslahi kwa wananchi na
taifa badala ya yale ya maslahi ya wagombea na wapambe wao. Tuzungumze kukuza uchumi wa kisasa katika
mazingira ya utandawazi. Tutafakari
changamoto zilizopo na zijazo, na kisha ndipo tuone nani kati ya makada wetu
wanaweza, na wanatosha, kuaminiwa kukabidhiwa usimamizi wa utekelezaji wake.
Mambo hayo yatatutofautisha na wapinzani na ndiyo yatatupa vigezo vya
kisayansi vya kujua nani miongoni mwetu anafaa kwa uongozi, kwenye ngazi ipi,
kwa malengo gani. Tutapata pia vigezo
vya kupima utendaji wa tutakaowachagua.
Kama tunataka kujenga ushupavu wa uongozi lazima tuanze hivi. Kazi
ijulikane kwanza; majina ya watakaosimamia kazi hiyo yaje baadaye.
Maana CCM inayo hazina kubwa ya
wanaofaa kuwa madiwani, wabunge, na marais.
Chama kimoja cha siasa kiliitisha mkutano wa kura za maoni kupata
mgombea wa chama hicho. Mmoja kati ya ambao hawakushinda akalalamika,
“Mimi nilisikia kabisa sauti za wananchi wakinitaka nigombee!”
Rafiki yake akamfariji, “Usijali
rafiki yangu. Pengine sauti hiyo ilikuwa
yako mwenyewe ukiwaza kwa sauti.”
Waheshimiwa
Wajumbe:
Ipo tofauti kubwa kati ya Chama kuwa
na nguvu, na Chama kuwa shupavu. Nguvu
ya CCM leo ni ya kihistoria; ni ya huko tulikotoka kwa waasisi wetu, na
mazingira tofauti ya wakati huo. Na
nguvu hiyo imeegemea sana kwenye heshima ya waasisi hao. Tuelekeako, nguvu
ya CCM itategemea zaidi ushupavu wa uongozi wa leo na wa kesho, na hasa katika
kusimamia maadili ya utendaji katika mazingira tofauti kabisa kitaifa, kikanda
na kimataifa. Ushupavu wa uongozi una sifa nne kuu: Kwanza ni upeo mkubwa wa kubuni malengo na
dira; Pili, ni uongozi madhubuti wa watu
na raslimali kuelekea kwenye malengo hayo na kuzingatia dira hiyo; Tatu, baada
ya kuridhia malengo, ni ung’ang’anizi na kukataa kuyumbishwa bila sababu za
msingi; na Nne ni ujasiri wa kusimamia na kutetea maadili. Maana kwa hakika, asiye na maadili hawezi
kuwa shupavu.
Kuongoza ni kupanga kwanza. Mipango
mizuri huleta maamuzi mazuri kimkakati na kiutendaji. Chama Cha Mapinduzi
kinapaswa kuongoza kwa kupanga; ili iwe rahisi kwa Serikali yake
kutekeleza. Uzoefu wangu wa kuongoza
Chama hiki na Serikali yake ni kuwa Chama kimeiachia Serikali madaraka ya
kupanga, lakini wakati wa maamuzi ya mkakati na utendaji, kama nilivyosema,
wanatokea viongozi wa Chama, wakiwamo Wabunge na Madiwani wanaochelewesha
maamuzi, hata pale ambapo msingi wa maamuzi hayo ni sera za Chama.
Waheshimiwa
Wajumbe:
Chama Cha Mapinduzi ndicho hasa
kiongozi wa nchi hii. Au tuseme hivyo
ndivyo inavyopasa kuwa. Chama kwanza,
mtu baadaye. Ndiyo maana huko nyuma
tukasema, “Chama legelege huzaa Serikali legelege”. Nami leo naongeza: Chama shupavu, huzaa viongozi shupavu.
Mtaalamu mmoja wa menejimenti
alisema: “Wajibu wa kwanza wa kiongozi
ni kuwafafanulia anaowaongoza hali halisi.” Kama Chama Cha Mapinduzi kinataka
kuendeleza sifa zake za uongozi, na nguvu yake katika siku za usoni, lazima
kiwe chama shupavu, chama kisichoogopa kusimamia maadili yake, chama kisichoogopa
kusema ukweli, chama cha kuwafafanulia wananchi hali halisi ya tulipo, na
mahitaji na masharti ya mafanikio ya huko tuendako.
Waheshimiwa
Wajumbe:
Ninakusudia mwishoni mwa mkutano
wetu huu kutangaza timu ya kuandaa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005, na
kuwataka kuikamilisha kabla hatujafikia kipindi cha kuteua wagombea. Kama nilivyosema, hii ina faida mbili. Kwanza Ilani hiyo ndiyo itamwezesha anayetaka
kugombea aitafakari vizuri na kujishauri yeye mwenyewe iwapo anaona anazo sifa
na nia thabiti ya kutekeleza Ilani hiyo, akijua sisi wengine tutamtarajia
afanye hivyo kwa niaba ya Chama. Pili,
Ilani hiyo, na majukumu itakayokuwa imeyaainisha, itatuwezesha sisi kwenye
Chama kubaini ni kada gani miongoni mwetu anafaa kugombea wadhifa gani, kwa malengo
na sababu gani, na kwa kipindi gani.
Maana, hatimaye, katika kuamua nani awe mgombea wetu wa Udiwani, Ubunge
na Urais, kigezo cha msingi ni uwezo wa
kutekeleza sera na malengo ya Chama.
Uhodari binafsi wa kampeni si sifa ya msingi, maana jukumu la kampeni
kimsingi ni la Chama, si la mgombea binafsi.
Naomba sana tujifunze kwa marafiki
zetu wa siku nyingi, Wachina. Hapana
shaka kuwa kiongozi hasa wa China ni Chama cha Kikomunisti cha China. Chama hicho kina uwezo mkubwa na ushupavu wa
kupanga na kusimamia mwelekeo, si wa Chama tu, bali wa nchi nzima. Kila awamu ya uongozi nchini China inapangiwa
majukumu ya msingi (Central Tasks), tena
yanapangwa mapema kabisa, na yanapangwa na Chama, hayapangwi na Serikali. Kisha
kila awamu inapatiwa viongozi wanaolingana na kushabihiana na mahitaji ya
majukumu hayo ya msingi. Hivi leo,
tayari wanajua majukumu ya miaka 20 – 25 ijayo, na tayari wanaandaa viongozi wa
kuyasimamia majukumu hayo. Huo ndio
ushupavu wa uongozi ninaouzungumzia.
Uongozi shupavu hauogopi kubadili
mkakati iwapo ni lazima kufanya hivyo. Leo China ina uchumi wa soko
unaoshindana, na kwa kweli unaowatoa jasho, wakongwe wa uchumi wa soko kwenye
nchi za Magharibi. Leo China, kwa
uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, imeweka ndani ya Katiba yao haki ya
kumiliki mali na raslimali binafsi. Nani
angeamini, miaka 10 tu iliyopita, kuwa China ingefanya hivyo? Wameweza kwa vile hawaogopi kukubali ukweli
kuwa dunia imebadilika; hawaogopi kuwaeleza wananchi wao hivyo; hawaogopi
kubuni mipango na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko hayo; hawaogopi
kuwaonyesha wananchi wao njia sahihi ya kuinusuru nchi yao, na kuwaongoza
katika njia hiyo; na hawaogopi kusimamia
maadili ya Chama chao. Wakishakubaliana kwenye Chama wote wanazungumza
lugha moja. Ukimsikiliza mmoja ni sawa
na umewasikiliza wote.
Sisi hapa tunababaika kwa nini? Wakati mwingine, ungempeleka mgeni kutoka nje
ya nchi kwenye Bunge letu, kwenye Baraza la Wawakilishi, au kwenye Mabaraza ya
Madiwani, akisikiliza mijadala hawezi kujua anayezungumza ni wa Chama Tawala au
anatoka kwenye vyama vya upinzani.
Tunapimana uhodari wa ubishi, badala ya uhodari wa kuelezea sera na
kuongoza utekelezaji wake kwa makini na ushupavu. Maneno hayajengi nchi. Nchi gani imejengwa kwa uhodari wa
maneno? Nchi inajengwa kwa kazi. Tukishaamua sera tunahitaji ujasiri wa
kutenda, si wa maneno. Ukiwepo ubishi
uwe wa kasi na ubora wa utendaji, si wa sera tena.
Nchi pia haijengwi kwa madai.
Maana tunazoea kila mara kuuliza:
Serikali ina mpango gani?
Serikali inafanya lini jambo hili au lile? Serikali italipa lini mshahara wa
kutosha? Na hakuna anayekwambia fedha
zitatoka wapi. Hakuna anayejenga hoja kuwa uwezo utoke wapi, au utokane na
nani! Na sisi ndio viongozi, lakini hatuna ujasiri wa kulinganisha mapato na
matumizi, wala matokeo yake. Uwazi na
ukweli, ushupavu na ujasiri.
Haifai viongozi wa Chama hiki wakose ujasiri wa kueleza ukweli wa uwezo
mdogo, kama alivyokosa ujasiri bwana mmoja aliyeambiwa na mkewe waende kununua
vitu vya sherehe ya mwaka mpya. Alikuwa
hana fedha za kutosha, na alikuwa hana ujasiri wa kutosha. Alipofika kazini akamwendea mkubwa wake wa
kazi. Akamwambia, “Tafadhali bwana mkubwa, naomba ruhusa niende na mke wangu
kununua vitu vya sherehe ya mwaka mpya.”
“Haiwezekani”, akajibu mkubwa wake wa kazi. “Tuna kazi nyingi sana.”
Bwana yule akashusha pumzi, “Nakushukuru sana, bwana mkubwa. Una huruma tele kwa kunikatalia.”
Waheshimiwa
Wajumbe:
Wakati wa kuandaa Ilani mpya ni
wakati pia wa kufanya tathmini yetu ya ndani ya utekelezaji wa Ilani ya mwaka
2000. Mimi nadhani tumefanya vizuri,
lakini kufanya vizuri kwa kipindi kilichopita si sifa pekee ya kuaminiwa
kuendelea kuongoza nchi. Utekelezaji
mzuri wa Ilani ya 2000 ni ushahidi wa usahihi wa sera kwa upande mmoja, na kwa
upande mwingine ni ushahidi kuwa sisi ni waungwana, na kwa kadri ya uwezo wa
Serikali tunatekeleza tunayoyaahidi.
Uungwana huo ni sifa nzuri,
lakini tutakachowaahidi wananchi kwa miaka 5 ijayo nacho ni muhimu, tena
pengine ni muhimu zaidi. Yaliyopita
yamepita; japo ni mema, wananchi watakuwa wanaangalia yajayo. Lazima tujiandae
vizuri kuelezea tuliyoyafanya, na yale tunayoahidi kuwa tutayafanya. Hata kama awamu ya sasa italala salama,
wananchi watatahayari: wataamka salama na awamu ya taswira gani?
Kwa heshima na unyenyekevu,
nathubutu kusema kuwa mwaka 2000, CCM ilipata ushindi mkubwa kuliko mwaka 1995,
si kwa sababu ya uhodari wetu wa maneno bali kwa vile wananchi walianza kuelewa
usahihi wa sera zetu kutokana na matunda ya utekelezaji yaliyoanza kuonekana. Matunda hayo yameongezeka tangu mwaka
2000. Wananchi wanaona wazi matunda hayo
kwenye elimu, afya, maji, miundombinu kama vile barabara, madaraja, vivuko,
bandari na simu, kushuka kwa mfumuko wa bei, nyongeza ya mapato ya Serikali,
mafao mazuri zaidi ya watendaji wa Serikali, heshima ya taifa na diplomasia
yake, misamaha ya madeni, nyongeza ya misaada na uwekezaji. Wanachotaka wananchi ni uhakika kuwa
hatutarudi nyuma.
Mambo mawili ni muhimu sana
yazingatiwe kwa makini. La kwanza ni
kuwa Ilani ijayo itahusu kipindi cha 2005-2010, ambacho ndicho kipindi cha
mwisho cha kutekeleza Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000-2010. Kwa hiyo Ilani lazima iandaliwe kwa
kuzingatia ukweli huo. Tupitie tena
mwelekeo huo, na kuona yapi yametekelezwa, na yapi yanapaswa kuzingatiwa kwenye
kipindi kijacho. Na kwa yale ambayo yametekelezwa tuone ni namna gani tutahakikisha
kwamba haturudi nyuma, kwamba tunayaimarisha, na kwamba tunajenga juu ya msingi
wa mafanikio ambayo tayari yamepatikana na kuongeza kasi ya maendeleo ya
jamii.
Tufanye hima kukubali pia kuwa dunia
yetu inabadilika haraka sana, na kila mabadiliko yanahitaji nasi tujipime
tulipo. Tuwe wepesi kutambua maslahi
yetu katika mabadiliko hayo, na tuwe wepesi kubuni mikakati ya kutetea maslahi
hayo. Tuwe shupavu kama Chama kuwaiga
rafiki zetu Wachina. Uchumi wa dunia ya leo ni uchumi wa soko. Ni kujidanganya
kufikiri tunaweza kuukwepa.
Ushupavu wa uongozi ni kuwaeleza wananchi ukweli huo, na kutekeleza kwa
dhati na makini yale tunayoamua ili kujenga uwezo wetu wa ushindani kibiashara
na kiuwekezaji. Leo tunasifiwa kuwa nchi yetu imedhibiti vizuri vigezo vya
uchumi mkuu, kama vile mfumuko wa bei na mapato na matumizi ya Serikali.
Tunasifiwa kwa kujenga uwezo wa ushindani kibiashara na kiuwekezaji. Tunao uwezo
wa kuamua na kuhakikisha haturudi nyuma, na tunalinda sifa hizo.
Waheshimiwa
Wajumbe:
Ni kweli Tanzania imepata mafanikio
mengi baada ya Serikali kujiondoa kwenye uwekezaji, biashara na huduma za
kiuchumi, na kwa kushirikisha zaidi sekta binafsi katika kukuza uchumi,
kuongeza nafasi za ajira, kuingiza nchini teknolojia ya kisasa, kutoa huduma za
kiuchumi na kijamii, na kuongeza mapato ya Serikali. Napenda niongeze jambo
muhimu sana. Tunaondoa mikono ya Serikali kwenye uchumi wa soko, lakini hatuondoi
macho ya Serikali. Uchumi wa soko
unahitaji sana usimamizi wa Serikali, kwa maana ya mwelekeo wa sera za kiuchumi
na kijamii, kuleta ushindani wa haki kwenye soko, na kulinda maslahi ya taifa
na wananchi. Aidha, yapo baadhi ya mambo
ambayo kwenye hatua yetu ya maendeleo hatuwezi kutegemea sekta binafsi
iyafanye, ikiwemo ulinzi na usalama, utawala wa sheria na haki za binadamu,
huduma za kijamii, na miundombinu.
Tumeanza katika Awamu ya Tatu, na
inabidi tuendelee katika Awamu ya Nne, kuimarisha dola na asasi zake za uongozi
na usimamizi wa uchumi wa soko.
Usimamizi huo ni pamoja na kuendeleza na kudumisha mambo ya msingi kwa
utaifa na umoja wetu, usawa wa fursa za kuishi na kujiendeleza, na mshikamano
wa kitaifa na muungano wetu. Nchi hii
pia, chini ya uongozi wa CCM, lazima iendeleze dhana ya maendeleo ambayo
hayapishani sana. La msingi si kuwarudisha nyuma wanaotajirika kwa njia halali, bali
kuwasaidia wanaofukarika kwa kuwahimiza na kuwawezesha kutumia fursa
zinazoletwa na uchumi wa soko.
Uchumi wa soko hauwezi kushamiri iwapo wananchi walio wengi si
washiriki. Kwa hiyo kazi kubwa iliyo
mbele ya Chama chetu ni kubuni na kusimamia mikakati ya kuingiza wananchi wengi
iwezekanavyo kwenye uchumi rasmi wa soko.
Mkakati mmojawapo, ambao tayari tunaushughulikia, ni wa kutambua rasmi
raslimali na biashara za wanyonge ambazo bado ziko kwenye sekta isiyo rasmi ili
zitumike kuwafanya wawe washiriki kamili kwenye uchumi rasmi wa taifa.
Jambo la pili muhimu sana ni wajibu
wa dola kujenga miundombinu ya kiuchumi na kijamii ambayo bila kuwapo uchumi wa
soko hauwezi kushamiri. Tumeanza, na lazima tuendeleze, ujenzi na uimarishaji
wa barabara, madaraja, vivuko, reli, bandari, simu na umeme. Lazima tuendeleze maandalizi ya Watanzania
kuwa na elimu, ujuzi na afya ya kuwawezesha kushiriki uchumi wa soko. Hivyo miradi ya elimu, maji, afya na vita
dhidi ya UKIMWI na Malaria itabidi iendelezwe kwa kasi. Mapato ambayo Serikali inapata kutokana na shughuli
za sekta binafsi hayana budi kuelekezwa kwenye kuimarisha uwezo wa Serikali
kutimiza wajibu wake huu usiokwepeka.
Waheshimiwa
Wajumbe:
Napenda kumalizia kwa kuwakumbusha
mambo matatu tuliyoyabainisha kama ndiyo mambo makuu ya kuzingatiwa katika
kipindi cha 2000-2010:
·
Kwanza, kwamba CCM iwe mhimili wa
umoja wa taifa, na wa muungano wetu.
Mwelekeo unasema “Ili CCM iendelee kuwa na nguvu ya mhimili wa umoja wa
taifa, lazima ihakikishe kuwa sarakani ya udini, ukabila na ubaguzi wa aina
nyingine yoyote haijipenyezi ndani ya CCM yenyewe...Wana-CCM wanaoendekeza au
kupandikiza ubaguzi ndani ya Chama chetu lazima wafichuliwe au kuchukuliwa
hatua”;
·
Pili, kwamba CCM idumishe amani na
kutoa uongozi kwa taifa. Mwelekeo
unasema, “CCM lazima ionekane kuwa ndilo chimbuko la sera za kuwawezesha
wananchi kiuchumi.” Mwelekeo unaendelea kusema, “Kamati Kuu na Halmashauri Kuu
ya Taifa ziendeleze msimamo thabiti wa kulinda na kutetea maslahi ya chama
dhidi ya maslahi ya ubinafsi; na maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya vikundi
vya kibinafsi. Hivi ndivyo CCM
itajijengea uhalali wa kuwa chama kiongozi kwa taifa;” na
·
Tatu, kwamba CCM iongoze ujenzi wa
uchumi wa kisasa na kuutokomeza umaskini.
Leo dunia nzima inakiri kuwa vita dhidi ya umaskini haiwezi kufanikiwa
bila uchumi kukua. Kwa hiyo jukumu la
msingi ni kwanza kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi zaidi, na pili kwamba
uchumi ukuavyo maslahi ya wanyonge na ya taifa yanazingatiwa. Uwezeshaji wa wananchi, na usimamizi wa
uchumi wa soko, ni mambo ambayo yatahitaji mkazo maalum. Mwelekeo unasema, “Kazi hii ni nzito na
inahitaji uongozi thabiti wa vitendo wa Chama na Serikali zake. Serikali
zitabidi ziyaelewe na kuyaainisha majukumu yake na kuyatafsiri katika programu
mbalimbali.”
Waheshimiwa
Wajumbe:
Mimi ninaamini kuwa iwapo tutaandaa
programu yetu, na Ilani yetu, kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi,
tutaonekana wazi kustahili kuendelea kukabidhiwa uongozi wa nchi hii. Lakini narudia. Tukubaliane kwanza kuhusu programu na Ilani,
kabla ya kutafuta wagombea. Pili,
tuazimie kuwa na uongozi shupavu, uongozi usiosuasua, uongozi unaokiri hatua
tuliyopiga, usioogopa kubuni, kuongoza na kusimamia mabadiliko. Chama kisicho
tayari kubadili mikakati na mbinu kitapoteza uhalali wa uongozi katika dunia
inayobadilika, na Chama ambacho si shupavu, hakiwezi kubadilika.
Unaweza kuwa nahodha hodari wa merikebu, lakini huwezi kuwa nahodha wa
bahari. Watanzania, Chama Tawala cha CCM
na viongozi wake, tusifikiri tunaweza kuwa nahodha wa bahari ya utandawazi
inayotuzunguka kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.
Badala yake, tuboreshe unahodha wetu wa merikebu ya taifa katika bahari
iliyotibuka. CCM tuna wajibu kuwa
waaminifu, shupavu, kubadilika, na kuongoza na kusimamia mabadiliko, bila
kuathiri hata chembe imani yetu ya kisiasa na itikadi inayoambatana nayo. Tunahitaji ushupavu wa uongozi. Tukiamua tulio ndani ya ukumbi huu,
inawezekana kujenga ushupavu huo. Ombi
langu ni kuwa kila mmoja wetu asikilize dhamira yake na kisha atimize wajibu
wake.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.