HOTUBA YA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI NA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI, DODOMA, 15 FEBRUARI 2005

 

Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM;

Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM;

Mabibi na Mabwana:

 

            Baada ya Kamati Kuu ya CCM jana kuamua kuleta Taarifa mliyoizungumza, niliamua kuwa nifunge mjadala wake kwa maelezo ya maandishi.

Waheshimiwa Wajumbe:

Chama chetu Tawala, CCM, lazima kiendelee kutawala kwa sababu ya usahihi wa sera zake, kwa ubora wa uongozi wake na kwa vile, kwa sifa hizo, hakina mbadala!

            Leo tena, kama ilivyokuwa kwenye Mkutano wetu wa tarehe 25 Agosti mwaka jana, nimeamua kufunga mjadala huu kwa hotuba inayoendeleza hoja ya msingi niliyoijenga wakati ule ya “Ushupavu wa Uongozi”.  Maana ushupavu huo ndio utahakikisha kuwa Taifa letu haliyumbi, kwamba Taifa letu litapata uongozi bora linalostahili, na kwamba CCM itabakia kwenye usukani wa merikebu ya Taifa letu la Tanzania, na kuivusha salama kwenye mawimbi yote.

            Mwezi Agosti mwaka jana nilizungumzia hofu ya wananchi, hofu ya wahisani na hofu ya wawekezaji tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.  Nikataka tujiulize kwa nini wawe na hofu wakati wanao uhakika kuwa CCM itashinda.  Nikasema hofu hiyo inatokana na wao kuwa na wasiwasi kuwa pengine sisi wenye jukumu muhimu la kuteua wagombea wa CCM hatutakuwa makini vya kutosha, na hivyo kuweka wagombea wasiofaa lakini watakaoshinda kwa nguvu tu ya CCM.

            Leo nataka nizungumzie hofu nyingine, nayo ni hofu ya baadhi ya viongozi wenyewe ambayo nayo ningependa niitulize.  Maana haifai kufanya maamuzi mazito kama haya katika hali ya hofu.  Tujiandae kufanya maamuzi katika hali ya kujiamini, tukiwa na uhakika wa umakini wetu, busara zetu, uadilifu wetu na uwezo wetu wote.

            Kipindi hiki tunapoelekea kwenye uteuzi wa wagombea Urais, wapo viongozi wenzetu wenye hofu.  Wapo wanaohofia Chama chetu, hasa wanapoona bidii isiyo ya kawaida ya wanaowania kuteuliwa.  Wanaona kuwa bidii hiyo isipodhibitiwa mapema inaweza kukigawa Chama kwa misingi mbalimbali, ikiwemo misingi ya ukabila, kanda, na dini.

            Hofu na hatari hiyo ni jambo la msingi kabisa, na wala si jambo la kupuuzwa. Halmashauri Kuu hii itapata nafasi ya kuchuja wagombea wakati wa kufanya hivyo ukifika.  Kwa sababu hiyo, naamini tunao wajibu wa sisi wenyewe kujikumbusha na kuwakumbusha wanaokusudia kuwania nafasi hizi za juu kabisa katika uongozi wa taifa letu, kuwa kutumia rushwa, na kutumia mambo yanayotugawa kama vile ukabila, udini na ukanda katika kutafuta kuteuliwa, si mojawapo ya sifa za kuteuliwa; badala yake ni sababu ya kutosha ya kukataliwa.

Narudia.  Halmashauri Kuu hii ina wajibu wa kujikumbusha yenyewe, na kuwakumbusha wanaokusudia kuwania kuteuliwa kuwa wagombea kupitia CCM, kuwa kwetu sisi wana-CCM, rushwa, ukabila, udini na ukanda si sifa hata kidogo ya kuteuliwa; na badala yake ni sababu ya kutosha kukataliwa.  Nikiwa Mwenyekiti wa CCM, ninao wajibu wa kukumbusheni jambo hili mara kwa mara mpaka dakika ya mwisho.

Aidha, nikiwa Mwenyekiti, nitahakikisha haki inatendeka kwenye jambo hili la msingi kabisa.  Na haki hiyo ina pande mbili.  Upande wa kwanza ni kuwa kila anayethibitika kuvunja maadili ya CCM kwa kutumia, au kuendekeza, rushwa, maovu, ukabila, ukanda, na udini hapenyi hata kidogo kwenye mchujo wetu.  Upande wa pili ni kuwa asiyethibitika kuvunja maadili hayo naye haonewi wala kusingiziwa.

            Na nitahakikisha pia kuwa tunao uwezo wa kuthibitisha penye hatia, au tuhuma nzito, na wa kuthibitisha pasipo na hatia au tuhuma nzito.  Uwezo huo unatokana na mfumo na mtandao wa Chama Cha Mapinduzi, ikiwemo kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya hadi tarafa, kata na kijiji.  Kazi ya kuhakiki usafi au uchafu wa mgombea si yangu peke yangu; ni ya kila mwana-CCM na kila kiongozi wa CCM ambaye yeye mwenyewe kwanza ni msafi, na pili ambaye hataki kanuni na maadili ya chama chetu yapuuzwe au kuchezewa.

Uvunjaji wowote wa maadili, taratibu na kanuni haufanyiki hewani; unafanywa ndani ya jamii zetu.  Na ninyi Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ndiyo wasimamizi wakuu wa maadili ya uongozi ndani ya Chama chetu.  Mkijituma, mkitambua uzito wa nafasi na wajibu wenu, na mkiwa wenyewe ni waadilifu, mtasaidia sana kuhakikisha CCM inaendelea kuwa imara, na kuongoza taifa imara.

Narudia.  Kwanza, ninyi wenyewe wote mnapaswa muwe waadilifu, msiokubali kununuliwa kwa fedha, kwa ahadi za vyeo, au kwa jambo lolote lile.  Pili, mtambue umuhimu wa kupata wagombea safi – safi kwa tabia na mienendo, na safi kwa upeo na uwezo wa kutekeleza Ilani ya CCM kwa uaminifu.  Na tatu, mjue na kuzingatia uzito wa dhamana mliyonayo.  Nyote mkitekeleza wajibu wenu, haki itatendeka ndani ya Chama, na Chama kitalitendea taifa haki kwa kulipatia viongozi bora. Tukiazimia kufanya hivyo hatuna sababu ya kuwa na hofu juu ya Chama chetu. Ni rahisi mkiwa kwenye makundi ya fitina kupuuza ushauri wangu, lakini siku moja kila mtu atakuwa peke yake, na ndipo umuhimu wa ushauri huu utakapobainika kwa kila mtu.

Waheshimiwa Wajumbe:

            Lakini najua pia kuwa wapo miongoni mwetu wenye hofu— si hofu ya Chama—bali hofu binafsi. Nataka nao niwatulize. Uongozi wenye heshima, uongozi ambao unapewa na wenzako kwa vile umechomoza kwa usafi, upeo na uwezo, si uongozi wa kuhuzunika usipoupata.  Maana uongozi wa aina hiyo, unaoweka Chama na Taifa mbele, ni mzigo mzito.  Nimekuwa Rais, huu ni mwaka wa 10 sasa.  Najua ninachosema, naelewa alichosema Baba wa Taifa, na bila shaka Mzee Mwinyi atakubaliana nami.  Uongozi wa juu wa taifa ni heshima kubwa sana, na dhamana kubwa mno.  Lakini ni mzigo mzito. Mwalimu hakuukimbilia. Mzee Mwinyi hakuukimbilia.  Na mimi mwenyewe sikuukimbilia kwa wepesi kama mwelekeo wa mwaka huu unavyoashiria.  Kulikoni?

            Hivyo, nawaomba sana wanaowania kugombea uongozi mwaka huu, tangu ngazi ya Rais, mpaka Wabunge, Wawakilishi na Madiwani, wasiwe na hofu binafsi ya kusema, “Itakuwaje nisipoteuliwa na Chama?” Wengi mtashindana. Nafasi za Rais, Wabunge, Wawakilishi, na Madiwani zitakuwa zote wazi, na kila mwenye sifa anayo ruhusa kugombea. Na mimi nitafanya kila lililo ndani ya uwezo wangu kuhakikisha taratibu, kanuni na Katiba ya CCM vinazingatiwa kwa ukamilifu, ili demokrasia ndani ya Chama itimie, haki itendeke, na ushindani uwe huru na wa haki. Na pale vigezo vya kuteuliwa vinapokuwa wazi, jambo la msingi si uhodari wa kujenga makundi ya fitina, bali kufikia vigezo hivyo kwa namna ambayo kila mtu atakiri kuwa huyu ndiye anayestahili kuteuliwa.

Sasa nitamshangaa sana yule ambaye baada ya demokrasia kutumika, baada ya haki kutendeka, baada ya kanuni, taratibu na katiba kuzingatiwa, bado atasononeka na kununa asipoteuliwa.  Nitashangaa vilevile akitokea yule ambaye baada ya kuteuliwa na kushinda atajiona bora sana na kupuuza wenziwe.  Maana, wenye sifa na uwezo ni wengi. Hawawezi kuteuliwa wote. Watakaoteuliwa na wale ambao hawatateuliwa wote wana wajibu kwa Watanzania wenzetu kuendelea kushirikiana, kuimarisha umoja wa Chama, na kuwa mhimili mkuu wa umoja wa taifa.  Ikiwa hivyo ndivyo, hofu binafsi ni ya nini?  Hofu hiyo itaendelea kuwapo iwapo tu mhusika ni mbinafsi, aliye tayari kutoa kafara maslahi ya CCM na taifa ili kunusuru maslahi yake binafsi.

            Najua wapo pia wenye hofu binafsi kwa vile wameingia, kabla ya wakati, kwenye makundi ya kampeni zisizo rasmi na za fitina za wanaowania uongozi katika ngazi mbalimbali.  Wapo walioingia kwa kuamini usafi na uwezo wa wanaowaunga mkono.  Lakini najua kuwa wapo pia wanaojiunga na yeyote yule anayewaahidi vyeo na fadhila mbalimbali.  Sasa hiyo ni hatari kubwa; na kwa kweli hao wana kila sababu ya kuwa na hofu, na ninawaonea huruma.

Nyote mnajua.  Nilipowania kuteuliwa kugombea Urais mwaka 1995 sikumwahidi mtu yeyote fadhila wala cheo.  Kwa upande mwingine hiyo ilikuwa ndiyo salama yao. Maana ukishakuwa Rais unaweza kubadili mawazo kulingana na hali halisi utakayokabiliana nayo kwenye uongozi. Na leo pia nisingependa wana-CCM, na hasa viongozi, wawe watu wa kununuliwa kwa fedha au kwa ahadi za vyeo, ambavyo wala hawana uhakika wa kuvipata baada ya uchaguzi.

Na mambo hayo hayawezi kufichika daima. Tena najua wapo wanaowania kuteuliwa ambao kwa cheo kimoja wanawaahidi watu wengi.  Ndio maana nasema kuwa hao wanaokubali kununuliwa kwa ahadi hizo wana kila sababu ya kuwa na hofu:  hofu ya kujulikana, na hofu ya kutotimiziwa ahadi hizo.  Lakini dawa yake ni nyepesi.  Ni kujirekebisha.  Ni kuacha kuufanya uchaguzi uwe wa kutafuta maslahi binafsi, na badala yake kuweka mbele maslahi ya Chama na maslahi ya nchi yetu Tanzania, na wananchi wenzetu wanaokiamini Chama Cha Mapinduzi.  Ni kuwakataa wanaogawa fedha na ahadi za vyeo.

Waheshimiwa Wajumbe:

            Nimezungumza sana kuhusu kupiga vita rushwa, ukabila na ukanda.  Leo napenda nikemee, kwa nguvu zote, tabia inayoanza kuonekana ya wanaowania kuteuliwa kujipendekeza na kujinadi kwa viongozi wa dini; jambo hatari sana hilo!

            Ninaamini kuwa kila anayewania kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM anaijua vema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania—Katiba ambayo akichaguliwa ndiyo atakayoapa kuilinda, kuihifadhi na kuitetea kwa moyo wake wote na nguvu zake zote.  Katiba hiyo inatenganisha mambo ya kidini na mambo ya kiserikali.  Kila raia anao uhuru wa imani ya dini na ibada; lakini Serikali haina uhuru wa kuwa na dini wala ibada maalum.

            Sisi tumefanya kazi kubwa sana kuwataka viongozi wa dini wasitumie mimbari zao kuwashawishi waumini wao kuchagua chama fulani, au mgombea fulani.  Hili ni suala la msingi kabisa kabisa—la msingi kikatiba na la msingi kimaadili ndani ya Chama Cha Mapinduzi.  Sasa, baada ya kazi hiyo, viongozi hao wa dini watatushangaa sana iwapo wagombea wetu wataanza tena kuwafuatafuata, kwa kisingizio kimoja au kingine.  Viongozi wa dini si wajinga.  Ni wasomi na wanazuoni.  Wana busara.  Wanajua wale wanaowafuata wanataka kuwashawishi ili watumie nyadhifa zao za dini kuwasaidia kuungwa mkono na wafuasi wa dini zao.

Nafurahi sana kuwa tunazo kauli za wazi za viongozi wa dini zetu kuu zote kuwa hawatatumia ushawishi wao mkubwa kwenye jamii kupigia debe chama fulani, au mgombea fulani. Ninawaomba waendelee na msimamo huo, na wawafukuze wanaojipendekeza kwao kwa sababu hizi.  Lakini sisi tuonyane wenyewe pia.  Asitokee mtu tena kuwafuatafuata viongozi hao wa dini.  Tutagawa watu, tutagawa chama, na hatimaye tutagawa taifa, na kupoteza kabisa sifa za kukabidhiwa dhamana ya uongozi wa taifa hili.

Waheshimiwa Wajumbe,

            Namalizia kwa kumtaka kila kiongozi na kila mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi asiwe na hofu; awe jasiri na mkakamavu.  Kila mmoja wetu akiwa mwadilifu, awekaye mbele maslahi ya Chama na Taifa, hana sababu ya kuwa na hofu. Tuondoe hofu maana tunao, miongoni mwetu, uwezo na madaraka kuhakikisha tunapata mgombea bora wa Urais, wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.  Hofu pekee inayoweza kuwepo ni pale wagombea wanapokuwa wadaiwa wa fadhila na vyeo wanavyonadi wakitafuta fedha au kuungwa mkono. Hofu nyingine ni kwa wale wanaokubali kuahidiwa fadhila hizo na vyeo hivyo.  Lakini, kwa wote wanaoweka maslahi ya Chama na Taifa mbele, ambao ninaamini ndio wengi, hawana sababu ya kuhofu.

            Tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha haki inatendeka, demokrasia inaimarika ndani ya Chama, na taifa linapata viongozi bora kwa tabia njema, kwa maadili mema, na kwa uwezo mkubwa wa kusukuma taifa mbele kimaendeleo—sio kurudi nyuma, kupunguza kasi, au kubakia pale pale tulipo.  Kwa wasioweka mbele ubinafsi, hawataona taabu kujipanga nyuma ya wale tutakaowateua, na kuwasaidia, ili kweli sifa ya Tanzania nje ya nchi, na mafanikio ya maendeleo na vita dhidi ya umaskini, viendelee mbele chini ya uongozi wa CCM.  Mimi siamini kabisa kuwa Rais atakayepita kwenye mchujo thabiti wa CCM, atakuja kutaka kuangamiza watu, kulipiza visasi au kuwaandama wasiokubaliana naye. Sisi, Tanzania, na hasa Chama Cha Mapinduzi, tumeshavuka huko.  Hatutoi wala kulea viongozi wa aina hiyo.

            Kwa hiyo, narudia.  Tuondoe hofu.  Tujisafishe wenyewe, sisi Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi, ili tuwe na uhalali na ushupavu wa dhamira kusimamia maadili, haki na demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi tunapoelekea kufanya maamuzi mazito kwa maendeleo, utulivu, na hatma ya taifa letu. Natarajia kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka huu wa 2005 itatupa mwelekeo na kigezo muhimu cha kisayansi cha kubainisha nani miongoni mwetu – aliyetangaza kuwania au ambaye bado hajajitokeza – anazo sifa za kutufanya sisi sote tuseme huyu mwenzetu ndiye anastahili kuliko wengine kukabidhiwa utekelezaji wa Ilani yetu.

            Nakuhakikishieni, kwa wale wenye shaka, kuwa mimi Mwenyekiti wenu sina mgombea wangu, na wala sijamtuma mtu yeyote akawanie kuteuliwa kwa baraka zangu. Narudia.  Sina mgombea wangu.  Ninayo kura yangu wakati wa uteuzi ukifika.  Nitaitumia kwa makini sana, kwa kulinganisha sifa, uadilifu, na uwezo wa wagombea watakaojitokeza. Lakini hatimaye nitaheshimu ushindi wa atakayechaguliwa kwa haki, na kwa mujibu wa kanuni, taratibu, na Katiba ya CCM.  Na huyo ndiye nitakayemnadi kwa bidii zangu zote kwa Watanzania wenzangu, ili wamchague na kunipa mimi idhini isiyo na shaka ya kumkabidhi yeye usukani wa taifa letu.

            Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe busara na hekima tunapoelekea kilele cha mchakato huu mzito na adhimu.

 

            KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!

            MAPINDUZI DAIMA!

 

            Ahsanteni kwa kunisikiliza.