TATHMINI YA HALI YA SIASA TANZANIA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2005  

Na Philip J. Mangula, Katibu Mkuu wa CCM

 

 

1.0            UTANGULIZI

Itakapofika Novemba mwaka 2005 Watanzania watapiga kura kwa mara ya tatu katika uchaguzi utakaohusisha vyama vingi vya siasa.  Kwa mara nyingine tunategemea kubadilishana madaraka kwa amani kutoka awamu moja kwenda nyingine.  Uchaguzi wa mwaka 2005 una mvuto na msisimko wa aina yake kwa sababu Rais aliyepo atatakiwa kuachia madaraka kwa mujibu wa marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Hali hii inaleta ushindani si tu ndani chama tawala bali pia hata ndani ya vyama vya upinzani. Tukirudi nyuma kidogo ni muda mfupi tu tokea watanzania walipopiga kura mwaka 2000. Hiki ni kipindi kizuri kwa wachunguzi wa masuala ya kisiasa kwa sababu mambo mengi yanatokea au kufanywa ambayo huweza kutumika kama kigezo cha kupima demokrasia nchini. Katika makala hii tutajitahidi kutathmini hali ya siasa za Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Tutachambua ahadi zilizotolewa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2000 na kuona ni jinsi gani zilitekelezwa au hazikutekelezwa na athari zake kwa demokrasia, kwa kulinganisha na hali halisi ya sasa. Pamoja na kuwa matukio muhimu ya kila siku yatachukuliwa katika kuelezea baadhi ya mada tutakazojadili, si nia ya makala hii kujikita katika matukio ya kila siku.  Wakati tukielekea kipindi cha uchaguzi mkuu wa 2005 ni muhimu tukafanya tafakuri za kina za nini kimefanyika na maeneo ambayo bado kuna mapungufu.  Ni muhimu tukaeleza tokea awali kwamba tathmini itazingatia zaidi hali ya siasa ilivyobadilika kuanzia mwaka 2000.  Lengo la tathmini ni kutoa mwanga wa mwelekeo wa kisiasa baada ya mwaka 2005. 

 

 

 

Ili kutuwezesha kuweka bayana tafakuri hii makala hii imegawanywa katika vipengele vikuu vitatu:

 

          (a) HALI YA SIASA BAADA YA UCHAGUZI WA MWAKA 2000:  MATARAJIO, MAZURI NA MAPUNGUFU

 

·        Hali iliyojitokeza Zanzibar

·        Hatua za Kukabiliana na Rushwa ndani ya CCM na ndani ya Serikali

·        Magomvi/Migogoro ndani ya vyama vya siasa na athari zake katika ukuzaji wa demokrasia

·        Tathmini ya Imani ya Wananchi kwa Serikali

 

          (b) NAFASI YA VYOMBO VYA HABARI NA VYAMA VYA WANANCHI KATIKA KUKUZA DEMOKRASIA

 

·        Kushamiri kwa vyombo vya habari

·        Nafasi ya vyama vya wananchi kwenye ujenzi wa demokrasia

 

 (c) KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA 2005 NA MUSTAKABALI WA TAIFA

  Umoja wa Kitaifa

  Mwelekeo wa wananchi Kisiasa 

 

2.       HALI YA SIASA BAADA YA 2000

Uchaguzi Mkuu wa Novemba 2000 ulijenga taswira mbili zinazokinzana Tanzania.  Upande wa Tanzania Bara kwa ujumla uchaguzi uliendeshwa kwa amani na utulivu na uvumilivu.  Hadithi, hata hivyo, ilikuwa tofauti kabisa upande wa Tanzania visiwani.  Uchaguzi ulileta utata mkubwa na hata wasiwasi wa kutokea mgogoro wa kisiasa.  Isingalikuwa ukomavu wa kisiasa uliokuja kuonyeshwa na wote waliohusika, Tanzania ingaliwezaweza kuingia kwenye janga kama tunavyoshuhudia nchi nyingine za Afrika.  Kwa hakika hali ya siasa ya Zanzibar na hofu ya siasa za vurugu ilikwishaainishwa na Tume ya Nyalali[1] ambayo iliona uwezekano wa chama kitakachoshindwa katika uchaguzi kuyakataa matokeo.

 

Inatosha kusema hapa kwamba haja ya muafaka ilionekana kuanzia awali kama ambavyo makala zilizoandikwa na Prof. H. Othman, Bw. P. Mangula na Bw. S. S. Hamad[2] zinaonyesha kwa namna tofauti umuhimu wa kukaa pamoja na kuzungumza. Muafaka II wa mwaka 2001 ni kitu cha kujivunia na rekodi nzuri ya utatuzi wa migogoro katika nchi za kiafrika.  Matokeo ya muafaka ni kama ifuatavyo:

 

(1)     Kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika majimbo 16 ambayo awali Civic United Front (CUF) ilisusia matokeo yake hivyo kuwawezesha kurejea tena kwenye siasa za ushindani bila kupigana.

 

(2)     Kuimarika kwa amani na utulivu ambavyo vimeiwezesha nchi kupiga hatua za kimaendeleo. Kwa mara ya kwanza CUF walishiriki kwenye sherehe za mapinduzi za mwaka 2003 kuonyesha kuwa wanaitambua serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

(3)     Kuridhishwa kwa wahisani na hali ilivyo Zanzibar na kuanza kutoa misaada kwa serikali iliyokuwa imesitishwa. Hii imesaidia kuboresha hali ya uchumi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

 

(4)     Kuundwa upya kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambayo itahusisha vyama vya siasa katika uundaji wake.

 

2.1            Magomvi/migogoro ndani ya vyama vya siasa

Kwa bahati nzuri, Tanzania ina vyama 16 vya siasa vyenye usajili wa kudumu.  Mojawapo ya mihimili ya siasa za kiliberali ni kushindanisha sera za vyama vingi ili wananchi wapate fursa ya kuchagua chama wanachoona kinafaa.  Kwa vyovyote vile mfumo wa siasa wa vyama vingi unahuishwa na uimara na uthabiti wa vyama ambavyo vinakuwa tayari kuchukua fursa za kuongoza nchi kama chama tawala kikidorora.  Hali hii hukinyima usingizi chama kinachotawala na hivyo kukifanya siku zote kitafute njia za kuboresha utendaji wake – matokeo yake wananchi wanafaidika zaidi.  Hali ni tofauti Tanzania, hasa Tanzania bara kwa sababu bado haijafikia hatua chama tawala kikakosa usingizi kwa kuhofia kupoteza madaraka kwa upinzani. Kama ripoti ya Profesa Mukandala[3] ilivyoonyesha vyama vingi bado vinalegalega kwenye uchaguzi, havijajikita mizizi vijijini, na bado havijajulikana sana ukiachilia mbali sifa za waanzilishi. Kuna migogoro baina ya vyama na ndani ya vyama vyenyewe. Nitaelezea kidogo.

 

Migogoro imeshamiri ndani na baina ya vyama vya siasa hali inayowaacha wananchi njia panda.  Hapa tutazungumzia migogoro katika baadhi ya vyama vikubwa vyenye wabunge na madiwani.  Tumeshuhudia mgogoro mkubwa wa kugombea madaraka ndani ya UDP.  Ilianza kwa kamati kuu ya chama hicho kumtimua Mwenyekiti Bwana John Cheyo.  Baadaye msajili akabatilisha maamuzi ya kamati kuu na kumrudisha Mwenyekiti Cheyo.  Kilichofuata ni timua-timua.  Baadhi ya wabunge waliotuhumiwa kushirikiana na Bwana Amani Jidulamabambasi kumpindua Mwenyekiti wakawa wa kwanza kutimuliwa.  Matokeo: 

Aliyekuwa Mbunge wa UDP na Madiwani 9 walihamia CCM na wanachama 1,147 wa wilaya ya Bariadi walihamia CCM pia.

 

TLP sasa hivi kunafuka moshi na kuna kila dalili ya mlipuko hali ikiachwa iendelee ilivyo.  Madiwani matano wa wilaya ya Moshi Vijijini  walihamia CCM na hivi sasa kuna kampeni za uchaguzi mdogo zinaendelea.  Tarehe 24/4/2004 Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa Dar es Salaam ambaye alikwua pia mfadhili wa chama Bw.  Saab Ally na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho  wamehamia CCM.

 

Athari za migogoro katika vyama vya siasa ni nyingi, na kwa ujumla wake zinachangia kudorora kwa demokrasia.  Panapokosekana chama chenye upinzani wa kweli na nguvu ya siasa, hutokea chama kilichoshika dola kikalala usingizi na kujisahau kabisa.  Wananchi ndio waathirika wakubwa wa hali hii.

 

Ni jukumu la kila mmoja wetu na kila mdau kikiwemo chama tawala kuhakikisha  kuwa vyama vya upinzani vinaimarika Tanzania.  Hali ya vyama vya siasa Tanzania kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali lifuatalo inaonyesha kupungua nguvu kwa vyama vya upinzani ukilinganisha na CCM.

 

Idadi ya kura ambazo vyama vilipata katika uchaguzi wa Bunge 2000

 

CHAMA

 

IDADI YA KURA

 

ASILIMIA

 

ONGEZEKO TOKA 1995

 

1.

2.

3.

4.

5.

6.

7.

8.

9.

10

11.

12.

13.

 

CCM

NCCR-MAGEUZI

CHADEMA

CUF

UDP

TADEA

NRA

UMD

TLP

NLP

UPDP

PONA

TPP

 

4,634,047

  258,591

   99,461

  792,378

  315,357

     9,647

        70

    7,550

 652,535

    2,507

  14,818

  11,789

10,206

 

65.3

3.6

4.2

11.2

4.4

0.1

0.001

0.1

9.2

0.04

0.2

0.2

0.1

 

+6

  -18

 - 2

 - 6

     +1.1

     + 1

             0.

0.

          + 9

               0

0

0

0

 

JUMLA

 

100

 

Chanzo: Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC): Uchaguzi Mkuu wa 2000

NB:  Taarifa hii haihusu uchaguzi katika majimbo 25 ambamo CCM ilipita bila kupingwa.

 

Tunaona katika jedwali hapo juu kuporomoka kwa vyama vikubwa kama NCCR-Mageuzi ambacho kilitawaliwa na migogoro iliyoishia kukigawa chama.   Hapa nigusie tu kwamba CCM  kutokana na ukomavu wake kisiasa kimeweza kudhibiti migogoro kila ilipojitokeza.  Kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu kitatawaliwa na migogoro ndani ya vyama na ni vyema vyama viweke mikakati ya kukabiliana nayo.

 

2.2            Tathmini ya kukubalika kwa serikali na chama

Uchaguzi mkuu kwa kawaida ni tathmini ya kukubalika kwa chama kwa wananchi wapiga kura (na hivyo serikali kitakayoiunda).  Hutokea umaarufu wa chama ukaporomoka ghafla mara baada ya uchaguzi mkuu kwa sababu kadha wa kadha.  Katika utafiti uliofanyika hivi karibuni[4] asilimia 63 ya wasailiwa wanakataa mfumo wa siasa wa chama kimoja.  Asilimia 73 wanakataa utawala wa mtu mmoja (personalized rule) hasa machifu au wazee (wa makabila).   Asilimia 87 wanakataa kabisa utawala wa kijeshi.  Asilimia 86 wanapinga mawazo ya kufuta bunge na kumpa rais madaraka yote.  Tafsiri mojawapo ya matokeo haya ni kwamba watanzania wanahitaji sana mfumo wa demokrasia wa vyama vingi (yaani uliopo).

 

  Kukataa udikteta (Asilimia)

 

Nakubali Kabisa/Sana

Nakubali

Yote sawa

Sikubali

Sikubali Kabisa

Sijui

Chama kimoja tu kiruhusiwe kusimama kwenye uchaguzi

 

12.0

 

17.0

 

7.0

 

25.0

 

38.0

 

1.0

Maamuzi yote yafanywe na Mchifu au Baraza la Wazee

 

4.0

 

9.0

 

10.0

 

33.0

 

40.0

 

4

 

Jeshi litawale nchi

 

2.0

 

4.0

 

5.0

 

28.0

 

59.0

 

2.0

Chaguzi zisiwepo ili Rais aamue kila kitu

 

 

2.0

 

4.0

 

6.0

 

28.0

 

58.0

 

2.0

Chanzo:  “Results from Round II OF Afrobarometer Survey”

 

 

 

 

2.2.1 Ukuaji wa Demokrasia

 

Katika jamii nyingi demokrasia imehusishwa na maendeleo ya nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.  Kadri nchi inavyokuwa ya kidemokrasia zaidi ndivyo inavyoongeza uwezekano wa kupata maendeleo.  Hivyo kuna ulazima wa kuifanya demokrasia kuwa sera ya taifa.   Wananchi lazima waridhishwe na kiwango cha demokrasia ili waunge mkono.  Katika utafiti uliofanyika mwaka 2003 wahojiwa waliulizwa ni kwa kiasi gani Tanzania inafuata demokrasia. Kwa ujumla asilimia 81 walisema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia.  Hata hivyo walisema demokrasia Tanzania bado ina matatizo madogo.  Asilimia 12 tu walisema Tanzania ina demokrasia kamili, ambapo asilimia 19 walisema demokrasia ya Tanzania ina matatizo makubwa.  Asilimia 8 walisema hakuna demokrasia kabisa Tanzania.

 

2.2.2 Ushiriki katika siasa

Demokrasia inaweza tu kushamiri pale ambapo watu wanashiriki katika siasa.  Watanzania wanapenda sana siasa na hii inajidhihirisha kwamba asilimia 67 ya wahojiwa walisema hujadili masuala mbali mbali ya kisiasa, asilimia 36 walisema hujadili sana siasa.  Asilimia 83 ya wahojiwa wanasema wanahudhuria mara nyingi mikutano ya kijamii.  Hata hivyo asilimia 34 ya wahojiwa wanaona mambo ya siasa na serikali kuwa ya utatanishi (complicated).  Hii inapunguza nguvu ya ushiriki katika siasa.  Lakini hata hivyo, inashangaza kidogo kwamba asilimia 76 wanasema wanaweza kuwafanya viongozi wao wawasikilize.  Tabia hii ni muhimu kwa demokrasia kwa sababu inaonyesha wananchi wanaweza kuwawajibisha viongozi wao.

 

Ushiriki mkubwa wa kisiasa huwasaidia Watanzania kujiunga katika kupigania haki zao.  Hivyo kiasi kikubwa cha wahojiwa (karibu asilimia 69) walionyesha kwamba hujiunga na wenzao kudai haki zao.  Hata hivyo asilimia kubwa hawajishirikishi na siasa za kupinga (protest politics) na hawashiriki kwenye maandamano. Hata hivyo wanaunga mkono demokrasia.  Asilimia 81 wanasema hawawezi kamwe kutumia nguvu kwa madai yoyote ya kisiasa.  Hii inaonyesha kuwa watanzania walio wengi ni wapenda amani na hawawezi kutumia nguvu kwa ajili ya madai ya kisiasa.

 

Njia nyingine ya ushiriki katika siasa ni kuonana na viongozi wao.  Ni muhimu wananchi kuwaona na kushauriana na viongozi wao wa serikali kama watataka kuwa karibu na serikali yao na kuunga mkono maamuzi yake.  Hivyo utafiti ulitaka kujua ni kiasi gani wananchi wanashauriana na viongozi wao.  Waliulizwa; “Katika mwaka uliopita, ni mara ngapi uliwaona hawa wafuatao ili wakusaidie kutatua matatizo yako?  Jedwali hapa chini linaonyesha watanzania wengi wanawaona viongozi wa ngazi za chini kuliko wa ngazi za juu (asilimia 33).  Hii ni ongezeko la asilimia 4 ukilinganisha na mwaka 2001.  Hata hivyo watanzania wengi (asilimia 56) wako radhi kuwaona viongozi wa dini kuliko kuwaona viongozi wa kisiasa (Asilimia 34 tu ndiyo waliowaona viongozi wa vyama vya siasa).

 

Ni Kiasi gani unawaona wafuatao kwenye matatizo?

 

2001

2003

Viongozi wa serikali za mitaa/madiwani

29

42

Watu wengine mashuhuri

26

32

Viongozi wa dini

49

56

Mbunge

12

19

Kiongozi wa jadi

12

27

Kiongozi wa chama

13

34

Kiongozi wa serikali kuu

 9

34

 

Chanzo:  “Results from Round II of Afrobarometer Survey”


2.2.3 Uhuru wa Kisiasa

 

Uhuru wa kisiasa ni kipimo cha kiwango cha ukomavu wa demokrasia katika jamii.  Uhuru finyu unamaanisha demokrasia finyu pia.  Hapa ni tathmini ya uhuru wa kisiasa kwa kuangalia uhuru wa kujieleza, uhuru wa kujiunga kwenye vikundi na kutokushtakiwa ovyo, na usawa mbele ya sheria.

 

Uhuru wa Kisiasa (Asilimia)

 

Mzuri

Mzuri sana

Sawa tu

Mbaya

Mbaya sana

Sijui

Uhuru wa kuongea unachofikiri

53

23

11

8

3

4

Uhuru wa kujiunga na chama chochote

52

29

11

3

1

4

Hofu ya kufungwa kwa kuonewa

42

16

19

13

3

7

Uhuru wa kupiga kura

46

31

13

6

2

2

Uwezo wa kuishawishi serikali

35

13

19

19

8

6

Usalama kutokana na uhalifu na fujo

34

 9

18

26

10

3

Usawa kwa wote

37

10

23

18

8

4

 

2.2.4 Kiwango cha kukubalika/uhalali kwa sherikali/chama

 

Serikali ambayo inatimiza ahadi zake za demokrasia na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma muhimu kwa kawaida huungwa mkono na wananchi.  Uhalali wa serikali ni ishara ya uzuri wa utendaji kazi wake.  Watu lazima waone kuwa serikali inawakilisha mawazo na ndoto zao.  Serikali ya namna hii inaweza kufanya maamuzi ambayo wananchi wote watayaheshimu.[5] Utafiti ulitaka kupima kiwango cha uhalali wa serikali kwa kuangalia vyombo vya serikali kama katiba, polisi, mahakama na idara ya kodi.  Hivi ni vyombo vya serikali ambavyo vinahitaji imani ya wananchi ili serikali iweze kufanya kazi sawasawa.

 

 

 

Maoni ya wananchi kuhusu uhalali wa serikali

 

Nakubali Sana

Nakubali

Yote Sawa

Sikubali

Sikubali Kabisa

Sijui

Katiba yetu inaeleza matarajio na ndoto za watanzania

 

14

43

10

10

5

18

Mahakama zina haki ya kufanya maamuzi yatakayoheshimiwa na watu wote

 

19

49

14

10

4

 4

Polisi wana haki siku zote ya kufanya watu waheshimu sheria

 

20

46

15

11

6

 3

Idara ya kodi ina haki ya kutoza kodi na kuhakikisha watu wanalipa

 

16

41

15

14

9

 5

 

Tukiangalia jedwali hapo juu, kiasi kikubwa cha wahojiwa (asilimia 57) wanaona katiba inaelezea mawazo na ndoto zao.  Hata hivyo idadi hii bado ni kidogo.  Wasomi na wanasiasa hapa Tanzania wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na mjadala wa kitaifa wa katiba.  Serikali inaonekana inalifanyia kazi hili kwa sababu karibu itapeleka muswada wa mabadiliko ya katiba bungeni.  Mahakama zinaonekana kupata uungwaji mkubwa wa mkono (uhalali) kwa kuwa na theluthi mbili (asilimia 68) ya wananchi wanaokubali kuwa mahakama zinatoa maamuzi yenye kufuatwa/kutekelezwa.  Watu wengi kiasi (asilimia 66) wanaona polisi wana haki ya kuhakikisha wananchi wanafuata sheria.  Kwa ujumla wananchi wanaipa uhalali serikali iliyopo lakini wanaona umuhimu wa mabadiliko kwenye nyanja fulani za uongozi.

 

  1. NAFASI YA VYOMBO VYA HABARI NA VYAMA VYA WANANCHI KATIKA KUJENGA DEMOKRASIA

 

3.1 Hali ya Vyama vya Habari

 

Katika mfumo wa siasa ambao Tanzania inaujenga, uhuru wa kuzungumza ni mhimili mmojawapo wa siasa.  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 18(1) na (2) inazungumzia uhuru wa mawazo na inasomeka:

 

(i)                Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yupo huru kuwa na maoni yoyote au kutoa vyema mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kwa chombo chochote bila kujali mipaka ya nchi; na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

 

(ii)              Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na juu ya masuala muhimu kwa jamii.[6] 

 

Umuhimu wa vyombo vya habari kama nyenzo muhimu katika kuimarisha uhuru wa kujieleza/kuzungumza hauwezi kusisitizwa zaidi hapa.  Ni vigumu kuifikiria hata hiyo demokrasia yenyewe kama uhuru wa vyombo vya habari utakuwa umefinyangwa.  Hapa Tanzania uhuru wa vyombo vya habari na nafasi yake katika ukuzaji wa demokrasia umekuwa ukiimarika na wakati mwingine umetumika vibaya.

 

 Bado kuna madai kwamba sheria nyingi kandamizi zimeendelea kubaki katika    vitabu vya sheria licha ya Tume ya Jaji Nyalali kupendekeza zifutwe.  Sheria zinazodaiwa kukwaza uhuru wa habari ni kama zifuatazo: Sheria ya Usalama wa Taifa (National Security Act, N. 3); Sheria ya Magazeti (Newspaper Act, No. 3) ya 1976; na Kanuni za Utumishi wa serikalini (Civil Service Regulations and Standing Orders).  Inadaiwa kwamba sheria hizi ni kama zinachukua kwa mkono wa kushoto haki ambayo ilikwishatolewa kwa mkono wa kulia na katiba ya nchi.

 

Hatua ambayo imechukuliwa hivi karibuni na serikali ya kurekebisha sheria ya utangazaji wa mwaka 1993 ya kuruhusu Radio na Television binafsi zitangaze nchi nzima inahitaji kuungwa mkono na wapenzi wa uhuru wa habari na demokrasia nchini.  Sheria zingine ambazo inadaiwa ni kandamizi zinafanyiwa kazi.[7]

 

3.2 Hali ya Vyama vya Wananchi Tanzania

Vyama vya wananchi (Civil Society Organizations – CSOs) ni mhimili muhimu katika kujenga demokrasia na kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla.[8]  Vyama vya wananchi viliendelea kukua na kujiongezea uwezo tangu uchaguzi mkuu uliopita.  Mpaka mwaka 2000 takwimu za utafiti zinatoa mwelekeo ufuatao wa idadi ya vyama vya wananchi.

 

3        Jumla ya vyama vyote vya wananchi vilivyoandikishwa ni 2,700 kati ya hivyo 93 viko Zanzibar na Pemba

 

4        Mikoa inayoongoza ni Dar es Salaam (808), Arusha (158), Morogoro (113), Kagera (87), na Kilimanjaro (86).

 

5        Mikoa ya kati ni pamoja na Mbeya (56), Mwanza (54), Dodoma (53), Songea (52), Tanga (51) na Iringa (48).

 

6        Mikoa ya chini ni pamoja na Mtwara (32), Kigoma (29), Rukwa (26), Shinyanga (17), Singida (15) na Lindi (10).

 

Hili ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.  Tafsiri ya haraka ya ongezeko hili ni kuwepo kwa mazingira rafiki kwa vyama vya wananchi pamoja na mwamko wa kisiasa  wa wananchi.

 

Idadi ya NGOs kwa mkoa, jinsia na kaz zake (Baadhi ya Mikoa)

 

MIKOA

KAZI ZA NGO

DSM

MWANZA

ARUSHA

 

WOTE

WAKE

JUMLA

WOTE

WAKE

JUMLA

WOTE WAKE JUMLA

Starehe na Utawala

5

-

5

-

-

-

1         -             1

Elimu na Utafiti

87

2

89

7

1

8

16       -            16

Afya

35

2

37

1

-

1

7          1           8

Huduma za Jamii

22

-

22

-

-

-

 3          -         3

Mazingira

48

1

49

16

-

16

11         1        12

Maendeleo ya jamii

460

63

528

23

10

33

95         6      101

Uhamasishaji

7

-

7

-

-

-

2           1          3

Kimataifa

34

-

34

3

1

4

4            -          4

Dini

3

-

-

-

-

-

1            -          1

Jumla

701

68

769

50

12

62

140         9       149

 

Chanzo:      Mchanganuo wa “Directory of Tanzania Non-Governmental Organizations – 2000”

 

Pamoja na idadi ya vyama vya wananchi kuongezeka tunapaswa kujiuliza kama ufanisi wake pia umeongezeka.  Kwa ujumla vyama vingi vya wananchi vinakabiliwa na matatizo mengi, mengine ya kiutendaji, na mengine ya miundo mibovu na ukosefu wa utaalam na uzoefu.  Ni vigumu kupitia kazi na michango ya vyama vyote lakini tutaangalia tu baadhi.

 

Vyama vya wananchi vilivyoonekana kutoa hamasa kubwa ni vile vya uhamasishaji.  Tumeshuhudia kwa mfano TAMWA (Tanzania Media Women’s Association) ikifanya kazi kubwa ya uhamasishaji dhidi ya ukandamizaji wa haki za wanawake na watoto.  Tafiti zao mbali mbali zinaleta upeo mpya wa kuyaendea matatizo haya ambayo yalianza kuonekana kama sehemu ya kawaida ya jamii. TAMWA kwa kushirikiana na TGNP ilishinikiza kupitishwa kwa muswada wa sheria uliotoa adhabu kali kwa wanaonyanyasa watoto na akina mama.[9]   Katika hali isiyo ya kawaida, katika Mkoa wa DSM UONGHOZI  wa TAMWA ulikwenda POLISI  na kufanikiwa kuzuia Msichana wa umri  mdogo kuolewa. Kulitokea tafrani na mjadala mkali lakini iliwezekana.

 

4.0     KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA 2005 NA MUSTAKABALI WA TAIFA

Tunapoelekea uchaguzi, mkuu na sasa ikiwa imebaki chini ya miezi kumi na minane kabla ya uchaguzi homa ya uchaguzi imeanza kupanda. Vichwa vya habari vya magazeti vinapambwa na picha za wale ambao wanatarajiwa kushika wadhifa mkuu wa seriakali (yaani urais).  Vichwa vya habari vya aina hiyo vinafanya magazeti yauzike. Katika mijadala inayoendelea sasa hivi ni ule wa wale wanaosema mgombea urais lazima ajulikane mapema kwa wapiga kura ili waweze kupata nafasi ya kutosha ya kumtafakari kama kweli anafaa kuwa rais wa nchi.  Hoja ni kwamba rais hana chama cha siasa, akishachaguliwa anakuwa rais wa wote na hakuna wanaosema iwe mapema kwa kiasi gani.  Hata hivyo utaratibu wa kumpata  mgombea urais kutoka CCM utaanza 2005 mwezi Machi kwa kuchukua fomu na kutafuta Wadhamini wasiopungua 250 kutoka Mikoa isyopungua 10 ikiwemo miwili

 ya Zanzibar (Unguja 1/Pemba 1).  Hapa chini nitazungumzia nyanja chache zinazogusa uchaguzi na mambo yanayopaswa kufanyika ili kuondoa uwezekano wa kuwa na uchaguzi usioleta muafaka wa kitaifa

 

4.1 Mfumo wa uchaguzi

Mfumo wa uchaguzi wa Tanzania ni ule wa kiti kwenda kwa aliyepata kura nyingi (first past the post). Mfumo huu una mapungufu yake kwa kuwa unavifungia nje ya uongozi vyama vidogo na hivyo kuvifanya vikate tamaa.[10] Mfumo wa sasa unavifanya vyama vidogo pamoja na wale wanaovipigia kura kukata tamaa na hasa baada ya kujaribu kupata viti kwa muda mrefu na kushindwa.  Mfumo wa uchaguzi ambao unampa kiti aliyepata kura nyingi hautoi nafasi ya kustawi kwa vyama vidogo na unajenga mazingira ya nchi kuwa na vyama vikubwa viwili na vingine hubaki havina nguvu wala uwezo wa kubadilisha chochote katika siasa za nchi. Mfumo huu una mapungufu.   Kunakosekana uwiano wa kura na idadi ya viti ambavyo chama kinapata. Kwa mfano, mwaka 1995 CCM ilipata asilimia 59.2 ya kura zote lakini ilipata asailimia 80.2 ya viti vyote bungreni. CUF ilipata asilimia 5 ya kura lakini ikapata viti asilimia 10.3 na NCCR Mageuzi ilipata kura aslilimia 21.8 lakini ikapata asilimia 6.9 tu ya viti vyote. Kwa jinsi hali ilivyo hapa Tanzania mfumo wa uchaguzi unampa kiti yule mwenye kura nyingi na unaonekana kama utoaji zawadi kutokana na ushindi kwa mgombea wa chama tawala. Sasa hivi ukishashinda kura za maoni na ndani ya CCM unakuwa umeshashinda kiti cha ubunge kwa sababu hakuna upinzani wenye nguvu.   Hata hivyo zipo faida nyingi tu za kuwa na mfumo unaompa kiti yule aliyepata kura nyingi. Moja kubwa ni kwamba ni rahisi kuutekeleza na huwezesha kuundwa kwa serikali iliyo imara. Ili kujaribu kupunguza athari za mfumo huu Halmashauri Kuu ya taifa imependekeza Serikalini kwamba kuwe na kura za uwiano kwa wabunge wanawake ambao hawatapungua 30% ya Wabunge wote 247 waliomo Bungeni.  Uwiano huo tayari unatekelezwa Baraza la Uwakilishi Zanzibar.  Aidha kutakuwa na kundi la pili la Wabunge watakaopatikana kwa uwiano wa kura.  Kundi hili ni la jinsia zote.  Jumla ya Wabunge watakaopatikana kwa utaratibu huu watakuwa 103 ambayo ni asilimia 29.4 ya Wabunge wote (350).  Kama muswada huu utapitishwa utaboresha kwa kiwango kikubwa mfumo wa sasa wa uchaguzi.

 

4.2     Asasi za kusimamia uchaguzi

Asasi muhimu za kusimamia na kuamua katika ushindani zimekwishaundwa na kusimikwa katika uwanja wa ushindani.  Asasi kuu tatu ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Uchaguzi (NEC na ZEC) na Mahakama.  Asasi hizi zinakubalika na wadau walio wengi kwa kiasi kikubwa, lakini bado kuna matatizo madogo madogo.

 

Kwanza, imekuwepo migongano kati ya vyama vya upinzani na Msajili wa Vyama vya Siasa tangu mwanzo wa mpito.   Vyama vya upinzani vinaona kama Msajili anaweka mkazo mkubwa zaidi juu ya wajibu wa kukosoa na kuadhibu kuliko wajibu wa kulea na kuvikuza vyama.

 

Pili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekwishaonyesha uwezo wa kusimamia uchaguzi kwa ufanisi na ushirikiano na vyama huku Tanzania Bara, lakini wajibu wake na mahusiano yake na ZEC huko Zanzibar bado vina utata.  ZEC ilikuwa moja ya asasi zilizotakiwa kurekebishwa na Muafaka wa 2001.

 

Tatu, tangu mwanzo wa mpito mahakama zimejihusisha na kesi za uchaguzi, kwa mfano, kesi ya Mchungaji Mtikila kuhusu wagombea binafsi, kesi ya Mtei/Marando kuhusu matumizi ya vyombo vya habari vya umma (hasa RTD) wakati wa kampeni za uchaguzi, kesi ya Mkuu wa Wilaya (DC) kutoa vibali vya mikutano ya vyama vya siasa, malalamiko mbalimbali dhidi ya uchaguzi, kesi kuhusu kuweka shilingi milioni tano kwa ajili ya kufungua kesi ya uchaguzi, n.k.  

 

Nne, kuna mjadala miongoni mwa vyama vya upinzani pia  kama wakuu wa mikoa (RCs) na wakuu wa wilaya (DCs) waendelee kuwa waamuzi  na wachezaji wa “mchezo wa siasa”.  Viongozi hawa ni wanasiasa na huteuliwa na Rais kwa msingi wa uanachama wa chama tawala.  

 

Tano,  kiwango cha kujivua ushabiki wa chama tawala (delinking) kwa watumishi wa serikali (wanaotumiwa na tume za uchaguzi wakati wa uchaguzi na katika makao makuu yake), na vyombo vya dola vinavyosimamia usalama katika mikutano ya vyama  ya kawaida na ya kampeni za uchaguzi unatiliwa mashaka na vyama vya upinzani.  Kwa mujibu wa ripoti za ufuatiliaji uchaguzi, ushabiki wa chama tawala ulikuwa mkubwa katika uchaguzi wa 1995 na kisha kupungua kiasi katika uchaguzi wa 2000 (isipokuwa Zanzibar).[11]  Ushabiki huu utaendelea kupungua kadri ambavyo utamaduni mpya wa kisiasa wa vyama vingi unavyozoeleka miongoni mwa wadau mabalimbali.

 

Kumekuwapo vuguvugu kwenye duru za vyama vya kisiasa na jamii kwa ujumla kutaka suala la mgombea binafsi liruhurisiwe. Hili linaendena na upeo wa siasa za kiliberali ambazo hutoa vikwazo vyote katika kushiriki siasa. Hali ilivyo sasa hivi mtu asiyekuwa na ushabiki wa vyama vya siasa hawezi kabisa kuchaguliwa kuwa kiongozi katika ngazi yoyote ile.   Tume ya Jaji Kisanga ilionyesha matokeo yafuatayo:  Kati ya washiriki 17,891 waliohojiwa Zanzibar 17,577   (98.24%) walitaka wagombea binafsi wasiruhusiwe na 309 (1.73%) walitaka waruhusiwe.  Kwa Tanzania Bara washiriki 31,574  kati ya 35,459 (89.4%)  waliotoa maoni walikataa wagombea binafsi na 3,743 (10.6%)  walitaka wagombea binafsi waruhusiwe.

 

4.3     MUAFAKA WA KITAIFA

 

Uchaguzi katika nchi yoyote ile ni njia nzuri ya kuleta muafaka wa kitaifa. Wananchi wanapopiga kura wanaonyesha imani yao kwa vyama na watu wanaowachagua. Wanaochaguliwa wanakuwa na jukumu zito la kuwatumikia wananchi na kuhakikisha kuwa wanatimiza ahadi walizotoa wakati wa uchaguzi.

 

Baada ya uchaguzi 1995 na ule wa 2000 tulishuhudia vurugu kule Zanzibar kutokana na kukosekana Muafaka wa Kitaifa.  Hapo palikuwa hakuna kuelewana.  Sera za chama Tawala zilikuwa hazitekelezeki kwa sababu ya upinzani kutoka kwa wasiokubaliana na matokeo.  Nchi ilishindwa kutawalika.  Wahisani waliamua kusitisha misaada yote na hivyo kuifanya hali ya  uchumi kuwa mbaya na maendeleo kudorora.  Kimsingi shughuli za utalii zilipungua na kwa hiyo kupunguza pato la serikali.  Hali hii tunaweza kuiita kulikuwa na mzunguko wa siasa za chuki katika nchi.

 

Kijamii watu waligawanyika makundi makundi. Tulishuhudia watu wa familia moja kugawanyika mara mbili kwa sababu ya tofauti za kisiasa. Watu waliacha hata kuzikana kama wanapishana mitazamo ya kisiasa! Shule na zahanati zilisusiwa. Vurugu na wingu zito likatanda na kila mmoja akashindwa kuelewa mustakabali wa taifa.

 

Mwisho ni  vitendo vya hujuma dhidi ya serikali. Hali iliyofuatia uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka 2000 ilikuwa ya kutatanisha. Ususiaji wa uchaguzi uliendana na vitendo vya hujuma vikihusisha kulipua mabomu mali za serikali. Hatuna haja ya kurudia kwamba kwa mara ya kwanza Tanzania ilizalisha wakimbizi mwaka 2001.

 

Tunapoelekea uchaguzi wa 2005 kuna vitu viwili ambavyo lazima tuvitilie mkazo ili mustakabali wa taifa letu uwe ni wa kutabirika. Kwanza ni kuendelea kupambana na  rushwa ambayo ilijitokeza kwa nguvu mwaka 2000 na pili haja ya kukamilisha uamuzi wa  kuwa na daftari la kudumu la wapiga kura. Nitaelezea kwa kifupi.

 

Tumeongelea katika makala hii kwamba rushwa ilikuwa ni kero namba moja ambayo serikali ya CCM chini ya Rais Mkapa imedhamiria kupambana nayo. Juhudi hizi zinaungwa mkono na kila anayelitakia mema Taifa hili. Bahati mbaya baadhi ya wagombea waliingiza  mchezo mchafu katika siasa. Watu ambao hawana sifa za kutosha za kugombea na kushinda hujiingiza katika njia za makato za kutafuta ushindi – walijaribu kuwarubuni wapiga kura kwa kuwapa rushwa. Athari yake ni kuwa mtu anayepata uongozi kwa rushwa ataiendeleza rushwa mara baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa wake hivyo kuendeleza mzunguko wa rushwa. Lakini mbaya zaidi ni kwamba hata kama kutakuwa na kiongozi mzuri maadam tu hawezi kutoa rushwa basi hawezi kuchaguliwa. Mwishowe ni kuwa na taifa linaloongozwa na matajiri watoa rushwa. Hawa asilani hawawezi kutekeleza matakwa ya wananchi na wanawafanya wananchi kukata tamaa na mfumo uliopo wa uongozi. Wananchi wakikata tamaa watatafuta mbinu zozote hata kama ni za vurugu kuiondoa madarakani serikali.

 

Halamshauri Kuu ya Taifa ya CCM  ilifuta matokeo ya kura za maoni kwenye majimbo matatu kwa tuhuma na ushahidi wa mazingira ya rushwa.   Katika majimbo manne waliachwa waliiongoza katika kura za maoni akateuliwa mgombea aliyeshika namba tatu.  Katika majimbo matatu waliachwa walioongoza katika kura za maoni wakateuliwa walioshika nafasi ya pili.

 

Kwa hiyo katika uteuzi wa wagombea ndani ya CCM tulishuhudia  baadhi ya matokeo ya kura za maoni yakitenguliwa na kuteuliwa wengine walioonekana na sifa zinazofaa na ambao hawakukiuka maadili ya chama. CCM inaandaa utaratibu mpya wa kura za maoni ili, pamoja na mambo mengine, kupunguza uwezekano wa rushwa. Tuna uhakika kuwa elimu ya uraia pia itapunguza kiasi kikubwa cha matumizi ya rushwa kujipatia madaraka. Kadri wananchi wanvyokuwa na uelewa mkubwa wa mambo ya kisiasa ndivyo ambavyo wataepa kuwapa madaraka watoa rushwa. Mifano ipo mingi .

 

Kitu kingine ambacho kimeonekana kuwa muhimu  ni kuwepo kwa daftari la kudumu la wapiga kura.   Hivi sasa kila uchaguzi wapiga kura hujiandikisha na baada ya kupiga kura orodha hiyo haitunzwi kwa ajili ya uchaguzi mwingine.  Katika uchaguzi wa mwaka 2000 yalijitokeza malalamiko mengi ya watu kujiandikisha na kupiga kura mara mbili au zaidi. Watu wengine pia kwa kukosa muda huwa hawajiandikishi kupiga kura hivyo kuwanyima nafasi hii muhimu. Kule Zanzibar hii ilikuwa ni moja ya makubaliano ya Muafaka II. Kwa kutambua umuhimu wake serikali imeazimia kuwa mpaka ifikapo uchaguzi mkuu wa 2005 daftari la kudumu la wapiga kura liwe tayari. Tunaambiwa maandalizi yote muhimu yamekamilika na zoezi litaanza wakati wowote. Daftari la kudumu la wapiga kura lazima liaminiwe na wadau wote na liwe bora.

 

Pamoja na mambo mengine yanayohusu  daftari hilo kuna mjadala juu ya utaratibu   wa nani anastahili kuandikishwa na nani hastahili. Baada ya kuandikishwa panatakiwa kuwa na utaratibu mzuri wa kulifanyia marekebisho daftari hilo. Wananchi wana uwezo  wa kuweka pingamizi kwa mtu wanayedhani hastahili kuwemo kwenye daftari la kudumu. Kwa kawaida orodha hiyo huchapishwa na kuwekwa bayana kwa ajili ya kuikagua. Hata hivyo elimu bado inahitajika kwa ajili ya kuwafahamisha wapiga kura umuhimu wa daftari la kudumu. Pia lazima waelimishwe mapungufu yake ili wasije wakadhani daftari la kudumu la wapiga kura  ndio muarobaini wa matatizo yote ya uchaguzi.[12]

 

5.0     MATARAJIO BAADA YA 2005

 

5.1     Kujenga umoja wa kitaifa

Kama taifa lengo la kuingia katika uchaguzi mkuu ni kutaka kutafuta uhalali wa kuongoza kutoka kwa wananchi ambao ndio wenye uamuzi wa mwisho wa nani ashike hatamu za uongozi wa nchi. Sio lengo la makala hii kutabiri nini kitatokea mwaka 2005 baada ya uchaguzi. Katika sehemu hii ya mwisho tutajaribu kwenda mbele zaidi na kuangalia yanayoweza kutokea baada ya 2005.

 

Katika uchaguzi wa mwaka 2000 na chaguzi ndogo zilizofanyika Mei mwaka 2003 CCM iliendelea kupata ushindi na hivyo kuonyesha imani ya wananchi kwa chama na serilkaili yake. Kwa hali ilivyo sasa tunaweza kusema bado CCM ni chama chenye nguvu na kinachoweza kutoa ushindani mkali kwa vyama vingine. Ndiyo sababu lilipozuka suala la kupokezanan urais kati ya bara na visiwani, watu wote hata viongozi wa vyama vya siasa ya upinzani walitoa maoni yao ya nini kifanyike ndani ya CCM ili kufikia muafaka juu ya jambo hili. Kifupi tu hapa kinachoonekana dhahiri ni kwamba vyama vingine vinaona vina uwezekano finyu wa kuitoa CCM madarakani.

 

Lakini ni lazima tuseme kwamba siasa mara nyingi huwa hazitabiriki. Tukiangalia chaguzi zilizowahi kufanyika katika nchi jirani na yetu vyama tawala viliweza kutolewa madarakanai na vyama ambavyo awali havikuwa vikijulikana kabisa. Je hii inaweza kutokea Tanzania?  Kiashiria kimojawapo kikubwa ni mbio za urais ndani ya CCM.  Utaratibu wa CCM wa kumpata mgombea wake wa Urais ni wa kidemokrasia sana.  Aidha ushindi wa kishindo wa 1995 (61.7%) na wa 2000 (71.4%) ni tofauti na ushindi wa 30 – 35% wa mgombea Urais wa KANU ambaye utaratibu usio wa kidemokrasi wa kuteuliwa kwake ulisababisha baadhi ya watu maarufu kujitoa ndani ya chama hicho na kujiunga na kambi ya upinzani na hivyo kuimarisha safu ya upinzani.

 

Kazi kubwa kwa CCM ni kujitahidi kuzuia makundi ndani ya CCM yanayotokana na ushabiki kwa mgombea fulani kabla ya wakati. Tujiulize, NARC inawezekana Tanzania?  Mazingira ya siasa za Tanzania ni tofauti sana na siasa za Kenya ukiangalia hasa ufuasi wa vyama vya siasa, hivyo hapaonekani kuwepo  uwezekano wa kilichotokea Kenya kutokea pia Tanzania. Kama mgombea ataonekana dhahiri anapendwa na watu wengi atachaguliwa na  Mkutano Mkuu wa CCM.  Kama anayeshindwa kwenye Mkutano Mkuu ataamua kujitoa na timu yake na kujiunga na chama cha upinzani, anaweza kutoa upinzani mkali lakini hawezi kushinda.  Ndiyo sababu tunasema itahitajika busara na ukomavu wa hali ya juu ili kuweza kumpata mgombea wa uraisi wa mwaka 2005 ndani ya CCM bila kuitikisa CCM yenyewe wala misingi ya umoja wa kitaifa.

 

5.2 Utamaduni wa Kisiasa

Watanzania wanasifika kwa kuwa na sifa ya amani na utulivu. Lakini amani na utulivu vinaendana kwa karibu sana na uvumilivu wa kisiasa. Kwa kadri ambavyo wananchi wanakuwa na imani na serikali yao ndivyo wanavyokuwa wavumilivu zaidi wakitumaini kuwa serikali inafahamu matatizo yao na inayashughulikia. Kama wananchi wanakuja kugundua kuwa uvumulivu wao haokuonyesha dalili zozote za mafanikio wanaanza kukosa subira. Mtafuruku utafukuta ndani ya nchi. Hicho kitakuwa kiashiria cha mgogoro. Wakati wa uchaguzi mkuu ujao wananchi itabidi waoyeshe subira na ukomavu wa hali ya juu ikiendana na imani kwa taasisi za kusimamia uchaguzi. Tuna kila sababu za kusema uchaguzi ujao utafanyika kwa amani.

 

Ni dhahiri kwamba umaskini unaweza kutoa cheche za kisiasa.  Lakini utafiti unaonyesha pia kwamba wananchi wa Tanzania wanao uvumilivu mkubwa na kiwango cha juu cha kuaminiana kijamii na kisiasa.  Chapisho moja lina kichwa cha habari kinachowaelezea Watanzania kuwa “Raia Wasiolalalmika na Walengwa Wavumilivu.”

 

6.0 HITIMISHO

Tukirejea yale tuliyoyasema kwenye makala hii, Tanzania imekuwa na utamaduni wa kubadilishana madaraka kwa njia za amani na za kikataba. Hali haitakuwa tofauti mwaka 2005. Tumetoa viashiria vya migogoro kama sheria, taratibu na   miongozo ya uchaguzi haitafuatwa kama inavyotakiwa. Tumegusia mfumo wa uchaguzi na haja ya kuweka uwiano kati ya mifumo miwili ya uchaguzi ili kupunguza tofauti kubwa kati ya kura na idadi ya viti kwa chama. Pamoja na yote haya tunabakia kuwa Taifa moja. Kwa hiyo  wakati tukiwa katika ushindani wa kisiasa, tubaki na misingi yetu ya utaifa.  

 

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025  kwa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na 2020 kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni makubaliano ya mwelekeo uliopata ridhaa ya wananchi wote.  Katika dibaji Rais Benjamin William Mkapa anaandika,

 

“Amani, Utulivu na Usalama wa Raia na Mali zao ni mazingira ya lazima kabisa na ya msingi kwa maendeleo.  Bila mazingira hayo dira hii haitakuwa na maana na wala hatutapata maendeleo.  Hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuepuka kila linaloweza kuwagawa Watanzania kama vile kubaguana kwa msingi wa dini, kabila, rangi, jinsia au eneo analotoka mtu.  Ni wajibu wa kila mmoja wetu pia kumtenga na kumsuta ye yote anayeleta,  kushabikia, au kuleta dharau, mifarakano, chuki na kutoaminiana katika nchi yetu.”

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

REJEA



[1] Tazama Haroub Othman, (2002) “Hali ya Zanzibar Baada ya Uchaguzi Mkuu”, Katika Uimarishaji wa Demokrasia na Utawala wa Kidemokrasia Tanzania. Vitabu Vya Programu ya REDET. Uk. 184

 

[2] Makala hizi kwa pamoja zinapatikana katika kitbu cha REDET (2002) Uimarishaji wa Demokrasia na Utawala wa Kidemokrasia Tanzania. Uk 169 - 205

 

[3] Tazama Mukandala (2003) Hali ya Siasa Tanzania: Tathmini ya Miaka Kumi ya Vyama Vingi, 1992 – 2002. Makala iliyowasilishwa kwenye Semina ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Makda wa CCM, Dodoma 29/1 – 2/2/2003

 

[4] Tazama Amon Chaligha and Yul Derk Davis 2004 “Results from Round II Afrobarometer Survey. REPOA 9th Annual Research Workshop

 

[5] Chaligha, op.cit

 

[6] Kama ilivyonukuliwa kutoka Lawrence Kilimwiko na Gervas Moshiro (2000)“Nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza demokrasia, Utamaduni wa Siasa na Hatma ya Demokrasia Tanzania. REDET

 

[7] Tazama pia Makala ya Mukandala, op. cit na Anthony Ngaiza (2002) Hali ya vyombo vya habari nchini katika Uimarishaji wa Demokrasia na utawala wa Kidemokrasia Tanzania

 

[8] Andrew Kiondo (2002) “Hali ya vyama vya Wananchi” katika Uimarishwaji Demokrasia na Utawala wa Kidemokrasia Tanzania. Vitabu vya REDET

 

[9] Kiondo, A (2002) Hali ya Vyama vya Wananchi katika Madumulla, J.S Uimarishaji Demokrasia na Utawala wa Kidemokrasia Tanzania. REDET, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

 

 

[10] Sauti ya Demokrasia Na. 54 Machi, 2004

 

[11] Tazama, kwa mfano, Max Mmuya (2002) “Hali ya Taasisi na Wananchi: Hali za Vyama vya Siasa” katika Uimarishaji wa Demokrasia na Utawala wa Kidemokrasia Tanzania. REDET Publications 

 

[12] Tazama pia gazeti la Sauti ya Demokrasia, Na. 54 Machi, 2004