HOTUBA YA MHESHIMIWA
JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE MKUTANO
NA VIONGOZI NA WANACHAMA WA CCM NA JUMUIYA ZAKE, DIAMOND JUBELEE
02 APRILI, 2008
Ndugu Wana-CCM Wenzangu;
Viongozi na Wanachama Jumuiya za CCM;
Ndugu Wananchi;
Kama
mjuavyo tumejiwekea utaratibu wa Rais kuzungumza na taifa kila mwisho wa
mwezi. Lakini, kwa mwisho wa mwezi wa
Machi nilishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya kulazimika kwenda Mererani,
Mkoani Manyara ambako kumetokea maafa makubwa kwa wachimbaji wa madini. Maafa hayo yalisababishwa na mafuriko
yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha katika eneo hilo usiku wa tarehe 28
kuamkia tarehe 29. Nilikwenda kuwafariji
wenye migodi, wachimbaji na familia zao kwa maafa yaliyowakuta. Pia nilikwenda kuona shughuli za uokoaji na
uopoaji wa miili ya wale waliofariki.
Kwenye
hotuba yangu ya mwezi Machi, nilikuwa nimepanga kuongea na Watanzania kuhusu
mambo mawili. Mambo hayo ni Ushiriki wa
Majeshi ya Tanzania kama sehemu ya Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Comoro na
tatizo la mauaji ya ndugu zetu Maalbino kwa imani za kishirikina. Awali
nilikuwa na wazo kuwa maadam tarehe 31 Machi imeshapita basi niache na hotuba
ipite. Lakini, baada ya kusikia
kueleweka vibaya kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM kuhusu Mazungumzo ya Muafaka
baina ya CCM na CUF nikaona ipo haja ya kuzungumza. Niitumie fursa hii kuzungumzia yale mambo
mawili niliyoyakusudia, na pia nizungumzie maafa ya Mererani na uamuzi wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu mazungumzo ya Muafaka baina ya CCM na
CUF.
Tanzania Kupeleka Majeshi Comoro
Ndugu Wananchi;
Tanzania
imepeleka wanajeshi wake 924 kuungana na wanajeshi wa Sudan, Senegal na Libya
katika Jeshi la Umoja wa Afrika lililoundwa kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya
Shirikisho la Visiwa vya Comoro kurejesha mamlaka yake katika Kisiwa cha Nzuani. Jamhuri ya Shirikisho la Visiwa vya Comoro
inaundwa na visiwa vitatu, yaani Ngazija (Grand Comoro), Nzuani (Anjouan) na
Mwali (Moeli). Kwa mujibu wa mfumo wao
wa utawala, kila kisiwa kina Serikali yake ya ndani inayoongozwa na Rais, na
kuna Rais wa Shirikisho anayekaa na kufanyia kazi mjini Moroni, kwenye Makao
Makuu ya Taifa la Comoro.
Urais
wa Shirikisho unashikiliwa kwa mzunguko baina ya raia wa visiwa hivyo
vitatu. Rais wa sasa ni Mheshimiwa Abdallah
Sambi ambaye anatokea Kisiwa cha Nzuani.
Uchaguzi ujao wa Urais unaenda kwa mtu wa kisiwa kingine. Kipindi cha Urais wa Shirikisho na wa Visiwa
vinavyounda Shirikisho ni miaka mitano.
Mwezi
Aprili, 2002 uchaguzi wa Marais wa Visiwa vya Ngazija, Mwali na Anzuan
ulifanyika. Kipindi cha miaka mitano cha
Marais hao kiliisha rasmi tarehe 13 Aprili, 2007. Kwa mujibu wa utaratibu na Katiba ya Comoro
uchaguzi wa Rais hufanyika ndani ya siku 90 baada ya kipindi cha uongozi cha
Rais kumalizika. Katika kipindi hicho
cha siku 90, Spika wa Bunge huwa Kiongozi wa muda. Kwa mujibu huo wa Katiba, tarehe 14 Aprili,
2007, Marais wa visiwa vya Ngazija na Mwali waliachia madaraka kwa Maspika wa
Mabunge ya Visiwa vyao, lakini Bw. Mohamed Bakari, Rais wa Kisiwa cha Nzuan
akakataa na kudai kuwa ataendelea kuwepo mpaka baada ya uchaguzi. Akamfukuza Spika ili kutengeneza mazingira ya
kutokuwepo mtu anayestahili kuchukua nafasi yake. Rais wa Shirikisho alitumia mamlaka yake ya
Kikatiba kuteua mtu mwingine badala ya Spika aliyeondolewa kibabe na Bwana Mohamed
Bakari. Lakini naye huyo pia Bwana Bakari akamkataa.
Rais
Abdallah Sambi aliamua kwenda Nzuani kumuona na kuzungumza na Bw. Mohamed
Bakari na viongozi wengine ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo usiokuwa wa lazima. Bwana Mohamed Bakari akafunga kiwanja cha
ndege cha Ouani, Nzuani na kuweka magogo uwanjani hapo hivyo ndege ya Rais wa
Shirikisho ikashindwa kutua.
Aidha,
Bwana Mohamed Bakari akaamuru kuteremshwa bendera za Shirikisho na kukamatwa
kwa askari 30 wa Jeshi la Shirikisho.
Mmoja wakamuua, watatu wakawajeruhi, na 26 wakawanyang’anya silaha na kuwafukuza kisiwani humo.
Baada
ya hapo, Umoja wa Afrika ukaingilia kati na kufanya mazungumzo na Bwana Mohamed
Bakari kumtaka aheshimu Katiba aondoke madarakani na kuruhusu taratibu stahiki
zifanyike. Imefanyika mikutano tisa (9)
ya namna hiyo; miwili Pretoria, mwili Cape Town, mitatu Addis Ababa na miwili Nzuani. Mikutano yote hiyo haikufanikiwa.
Ndugu Wananchi;
Bwana
Mohamed Bakari alikaidi mara zote kuondoka na kufanya mambo kuwa magumu zaidi. Alikaidi uamuzi wa Rais wa Shirikisho
ulioungwa mkono na Umoja wa Afrika na kutaka uchaguzi Nzuani usifanyike tarehe
10 Juni, 2007. Sababu ya agizo hilo ni
kutaka uchaguzi huo ufanyike siku ambayo Serikali ya Shirikisho na Umoja wa
Afrika utakuwepo kusimamia. Bwana
Mohamed Bakari akakaidi na kuendelea kufanya uchaguzi huo chini ya usimamizi
wake yeye mwenyewe. Kwa kutumia
madaftari ya shule, akaendesha uchaguzi na kutangaza kuwa amepata ushindi wa
asilimia 85. Mahakama ya Katiba ya
Comoro ikakataa kuutambua uchaguzi huo, lakini yeye akaendelea kula kiapo na
kuendelea kuwa Rais wa Nzuani kwa kipindi cha pili cha miaka mitano.
Umoja
wa Afrika ukaendelea na juhudi za kumtaka aachie madaraka kuruhusu taratibu za
Kikatiba zifuatwe na uchaguzi halali ufanyike.
Kama nilivyosema hapo awali, mikutano tisa iliyofanywa (wa mwisho
ulikuwa mwezi Februari, 2008) haikuzaa matunda.
Kwa
sababu ya ukaidi wa dhahiri wa Bw. Mohamed Bakari, ndipo katika kikao
kilichopita, Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika walikubali ombi la Rais Abdallah
Sambi la kuunda Jeshi la Umoja wa Afrika kusaidia Jeshi la Comoro kurejesha
mamlaka ya Serikali ya Shirikisho katika kisiwa cha Nzuani. Iliamuliwa kuwa, Baraza la Amani na Usalama
la AU lishirikiane na Kamisheni ya Afrika kutafuta nchi zitakazotoa majeshi ya
kufanya kazi hiyo. Kwa kushirikiana na
Serikali ya Comoro ndipo zikaombwa nchi nne yaani Libya, Senegal, Sudan na
Tanzania kuchangia wanajeshi kwenye Jeshi la UA.
Baada
ya kupokea uamuzi huo wa Baraza la Amani na Usalama la UA, tulijadiliana na
kufanya mashauriano na wahusika mbalimbali na hatimaye tukakubaliana kuwa
tuyakubali maombi hayo. Tumefanya hivyo
kwa kutambua wajibu wetu kwa UA na
wajibu wetu kwa nchi jirani ya Comoro ambayo wetu wake na wetu wana mahusiano
makubwa hata ya kinasaba. Lakini pia
kwetu sisi kama Mwenyekiti wa AU tunao wajibu wa kuhakikisha maamuzi muhimu
kama haya ya kuhakikisha kuwa nchi ya Comoro haimeguliwi tena kama ilivyofanywa
huko nyuma.
Ndugu Wananchi;
Kama
mnavyofahamu, operesheni maalum ya kumng’oa Bwana Mohamed Bakari na utawala
wake ilianza rasmi alfajiri ya tarehe 24 Machi, 2008 na siku iliyofuata, yaani
tarehe 25 Machi, 2008, majeshi ya Umoja wa Afrika yakiongozwa na Tanzania
yaliweza kukamilisha zoezi hilo bila umwagaji wa damu au uharibifu wa
mali. Hakuna mtu aliyeuawa wakati wa
operesheni hiyo. Bwana Mohamed Bakari
ametoroka na kiongozi wa muda Nzuani amepatikana kwa mujibu wa Katiba ya
Comoro. Ameanza kazi ya kuliongoza taifa
kwenye uchaguzi utakaofanyika mwezi Mei, 2008.
Majeshi
yetu yataondoka kwa awamu mbili: Awamu
ya kwanza yataondoka mwisho wa mwezi huu na ya pili mara baada ya
uchaguzi. Umoja wa Afrika una dhamana ya
kugharamia operesheni hii. Kiasi cha
fedha kimetolewa na UA unaendelea kutoa.
Pale ambapo tutalazimika kutumia fedha zetu tumeelewana kuwa UA
utatufidia.
Kwanini Tanzania Imeshiriki
Ndugu Wananchi;
Operesheni
hii imefanikiwa. Ni heshima kwa UA na ni
heshima kwa nchi yetu kuwa sehemu ya mafanikio haya. Kwa niaba yenu napenda kuitumia nafasi hii
kuwapongeza Wanajeshi wetu kwa kazi nzuri waliyoifanya. Imeliletea jeshi letu heshima kubwa na sifa
kwa nchi yetu. Kabla ya operesheni ile
kwanza kulikuwa na hofu kubwa hasa ya kutokea vifo na uharibifu wa mali. Mkuu wa Majeshi yetu Jenerali Davis
Mwamunyange alinihakikishia kuwa wameiandaa kisayansi kuepuka hayo yote. Na kweli ndivyo ilivyotokea. Nawashukuru na kumpongeza Mkuu wa Majeshi na
Maofisa Wakuu Wanadhimu Makao Makuu ya Jeshi katika operesheni hii huko Comoro
kwa kazi nzuri iliyotukuka. Nawapa pole
kwa magumu yote waliyokabiliana nayo.
Nawapa pole kwa msiba uliowapata wa kumpoteza mwenzao mmoja aliyezama
majini pale Kisiwani Mwali siku moja kabla ya majeshi yetu kuondoka kuelekea
Nzuani. Ajali haina kinga. Kila mtu ana siku yake na namna yake ya
kuondoka. Tuzidi kumuombea marehemu wetu
huyo kwa Mwenyezi Mungu aipokee roho yake na kuiweka mahala pema peponi,
Amin.
Tatizo la Mauaji Yanayotokana na Imani za Kishirikina
Ndugu Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kuliongelea ni kuhusu mauaji ya ndugu zetu wa jamii ya
albino yanayofanyika hapa nchini. Niseme
mapema tu kwamba jambo hili ni la aibu kubwa kwa jamii yetu. Ni jambo la hatari kwa amani na usalama wa
watu wetu.
Ndugu Wananchi,
Mauaji
yanayotokana na imani za kishirikina ni tatizo la muda mrefu kabla na wakati wa
ukoloni na imeendelea hata baada ya nchi yetu kupata uhuru.
Uzoefu
unaonyesha kwamba baadhi ya wahanga wanaoathirika ni akina mama vikongwe ambao
hutuhumiwa kuwa ni wachawi, kwamba wanawaroga watu wengine na kuwaua. Mauaji ya namna hii yamejikita sana katika
mikoa ya Kanda ya Ziwa mikoa ya Mara, Shinyanga, Mwanza na hata mkoa wa
Tabora. Mauaji haya hufanywa na magenge
ya watu wanaokodishwa na watu ambao wamepata maelezo potofu kutoka kwa waganga
wa jadi baada ya kuuguliwa au kufiwa na jamaa zao, na wao kuamua kulipiza
kisasi kwa watu waliotajwa kuwa ndio waliowaroga jamaa zao.
Vilevile,
mauaji mengi ya kishirikina hufanyika kutokana na imani potofu walizonazo
baadhi ya watu kwamba kwa kutumia viungo vya watu wengine wanaweza kufanikiwa
katika biashara wazifanyazo au katika shughuli zao za uchimbaji wa madini na
uvuvi.
Kutokana na imani
hizo potofu, watu hao wanaowania utajiri wa haraka haraka huenda kwa waganga wa
jadi na kupata maelekezo ya viungo vinavyotakiwa kutoka kwenye mwili wa
binadamu. Katika mazingira haya,
tumeshuhudia baadhi ya watu wakiuawa na kukutwa wamenyofolewa baadhi ya sehemu
za miili yao kama vile sehemu za siri, ndimi, viganja, matiti na wengine
kuchunwa ngozi.
Katika
nyakati zingine, huvumishwa habari za watu wenye maumbile au mapungufu fulani
kwenye mwili kama vile watu wenye vipara au maalbino kwamba viungo vyao vina
mchango mkubwa katika kufanikisha utajiri wa haraka. Kwa sababu hiyo katika kipindi cha mwezi
Julai, 2007 hadi sasa tumeshuhudia ndugu zetu wa jamii ya maalbino wakivamiwa
na kuuawa na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa bado
hawajapatikana. Kuanzia mwezi Machi 2007 hadi 01 Aprili, 2008, jumla ya
maalbino 19 wameuawa na wengine wawili wametoweka na hadi sasa hawajapatikana,
lakini inasadikika kwamba nao wameuawa.
Tatizo
hili la mauaji yanayotokana na imani za ushirikina limekuzwa zaidi na baadhi ya
watu ambao hawana taaluma ya uganga (waganga pandikizi) kwa kujiingiza kwenye
shughuli za uganga wa jadi hivyo kuzidisha upotoshwaji wa watu kwa kupiga ramli
chonganishi au maelekezo yasiyosahihi kwa lengo la kujipatia kipato kwa njia ya
udanganyifu.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Kama
nilivyosema, mauaji haya ni ya kusikitisha na ni ukatili usio na mfano. Ni aibu kubwa kwa jamii yetu. Nawasihi wale
wanaojihusisha na vitendo hivi, waachane na dhana ya kwamba utajiri unaweza
kuja kwa njia ya miujiza bila ya kufanya kazi kwa bidii. Utajiri unakuja kwa kufanya kazi kwa juhudi
na maarifa. Pia unakuja kwa kuwa na
nidhamu ya kazi na matumizi ya fedha uzipatazo.
Tiba
ya asili na uganga wa jadi ni sehemu ya asili ya Mtanzania, na hiyo Serikali
inaitambua na wala haiikatazi. Hata hivyo, nawasihi Watanzania wenzangu
tujiepushe na matapeli na wahuni walioingilia fani hii na wao wakiwa na nia ya
kuwalaghai wananchi kwamba wanaweza kuwafanya wapate utajiri wa haraka haraka
kwa kutumia baadhi ya viungo vya wanadamu.
Hatua za Serikali Kukabiliana na
Tatizo Hili
Ndugu Wananchi,
Serikali
kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti mauaji haya kwa
kuwashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo wale waganga wa jadi waliosajiliwa
Serikali.
Kwa
kushirikiana na Chama vya Maalbino nchini, Serikali inaendelea na zoezi la
kupata orodha ya maalbino wote nchini na kutambua sehemu wanazoishi ili kwa
kushirikiana na Serikali za Mitaa, Manispaa, Kata na Vijiji kubuni kwa pamoja
namna ya kutengeneza mazingira ya ulinzi yanayoweza kuwahakikishia usalama
wao. Zoezi hili ni muhimu liambatane na
matumizi ya Ulinzi-Shirikishi ili kuwashirikisha wananchi katika kuyatambua
makundi ya waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi na makundi yanayoendesha
mauaji hayo na wale wanayoyakodisha.
Vilevile,
Serikali itaendelea kutoa elimu ya uhamasishaji kwa wananchi wetu ili wasaidie
kutoa taarifa kwa vyombo vya dola dhidi ya wahalifu wote wanaofahamika
kushiriki katika mauaji yanayotokana na imani za kishirikina.
Ningependa
Jeshi la Polisi nalo liharakishe zoezi la kuwaorodhesha waganga wote wa Tiba
Asili walioko nchini ili kudhibiti wale wanaotoa maelekezo ya kuua watu. Nina
imani waganga wa jadi wa kweli watatoa ushirikiano, kwani wanawajua wenzao
wanaotoa maelekezo kinyume na sheria za nchi.
Vilevile,
Jeshi la Polisi lijipange upya kuyatambua na kuyakamata magenge ya watu wanaokodishwa
kufanya mauaji kwa wanawake vikongwe, au kwa watu wengine ili kunyofoa sehemu
zao za mwili au kuchuna ngozi
Ndugu
Wananchi,
Kila mtu ana imani yake. Na Serikali
haiwezi kuingilia imani za watu kwa mambo ya asili na jadi. Hata hivyo, pale
imani yako inapoingilia uhuru na haki ya msingi ya mtu mwingine, ikiwemo haki
yake ya kuishi, Serikali haiwezi kukaa kimya. Lazima ichukue hatua.
Nina
imani kabisa kwamba tukishirikiana kwa pamoja, wananchi, Serikali, asasi za
kiraia, vyombo vya habari, waganga wa jadi na wadau mbalimbali, tunaweza
kulimaliza kabisa tatizo hili ili lisije likaonekana
Muafaka Kati ya CUF na CCM
Sasa
napenda kulizungumzia suala la tatu nalo ni Mazungumzo ya Muafaka kati ya CCM
na CUF. Suala ambalo limetawala vichwa
vya habari vya vyombo vya habari nchini na duniani tangu Butiama mpaka
sasa. Na sasa, naona inaanza kujitokeza dhana
potofu hasa kuhusu nini kilichoamuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Ndugu Wananchi;
Moja
ya ajenda katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichokutana Butiama hivi
majuzi ilikuwa ni kujadili taarifa ya Kamati ya
Mazungumzo baina ya CCM na CUF ya kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa
kisiasa Zanzibar.
Kwa kweli haikuwa
nia yangu kulizungumzia suala hilo katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi. Lakini kutokana na yanayoendelea sasa,
nisipolisema sitaeleweka. Nitaongeza maswali
mengi yasiyokuwa na majibu na kuishia kuwafanya wanachama wa CCM, wananchi na
hata wenzangu wa CUF wachanganyikiwe zaidi.
Ndugu Wananchi,
Nianze kwa
kutamka moja kwa moja kwamba, tofauti na yanayosemwa na baadhi ya watu, sisi
katika CCM tunaamini kwamba maamuzi yaliyofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa ni
ya kujenga na wala siyo ya kubomoa. Kimsingi
ni maamuzi yanayotusogeza hatua kubwa sana mbele kwenye kufikia muafaka.
Labda
nirudi nyuma kidogo. Chimbuko la mazungumzo yanayoendelea sasa ni ahadi yangu,
wakati nikizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 30 Desemba
2005, kwamba nitaanzisha na kuwezesha mjadala wa kisiasa kwa lengo la kumaliza
mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Dhamira
yangu ilitokana na kusoneshwa na uhasama, chuki, kejeli, dharau na hata fujo na
vurugu, hasa nyakati za uchaguzi, na hata baada ya uchaguzi, baina ya wakazi wa
Zanzibar. Kwangu mimi, hali hii, ambayo imefanya hali ya kisiasa na kiusalama
kutokuwa ya utulivu, haiendani na
taswira ya Tanzania tunayotaka kuijenga na Tanzania tunayoijua sisi na
wanaoijua marafiki zetu wote duniani.
Kutokana
na uhasama wa kisiasa, ilifika mahali ambapo watu walikuwa hawaoleani, Bibi na
Bwana wanapeana talaka, wazazi na watoto wanatengana na hata ndugu
kufarakana. Watu wamekuwa wanasusiana
misiba, hawasalimiani, wanaachiana safu misikitini, na hawabebani kwenye vyombo
vya usafiri na hawauziani bidhaa hadi wawe wa Chama kimoja. Hiyo sio Tanzania
ninayoijua mimi, na wala siyo tunayoijua sote.
Hiyo sio Tanzania ambayo waasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume waliyokuwa nayo mioyoni mwao walipojitolea
muhanga kuongoza harakati za ukombozi wa nchi zetu mbili zilizokuja kuungana na
kuwa nchi moja.
Ndugu zangu,
Siku zote nimekuwa natambua kwamba
dhamira yangu pekee haitoshi kwenye kuifikia
Bahati
nzuri, nilipolipeleka suala hili kwenye vikao vyote vikubwa husika vya Chama
chetu (CCM), viongozi wenzangu wa Chama, kutoka Bara na Visiwani, waliunga
mkono hoja na haja ya kufanya mazungumzo na Chama cha CUF. Vilevile, sote
tulifarijika kwamba wenzetu wa CUF nao walikuwa tayari kufanya mazungumzo nasi.
Haya hayakuwa mazungumzo ya kwanza baina ya vyama vyetu lakini safari hii
tulikuwa na dhamira ya kutafuta suluhu ya kudumu.
Katika miezi yote kumi na minne,
tumeendesha mazungumzo haya katika mazingira ya udugu na kuheshimiana, wote
tukiwa na dhamira ya kupata suluhu mapema kadri inavyowezekana. Palipotokea
vizingiti vya hapa na pale, wote tulishirikiana kuvimaliza na kuendelea na
mazungumzo.
Ndugu
Wananchi,
Kama mnavyojua, tuliamua
kufanya mazungumzo haya kwa mfumo wa Kamati ya pamoja, kila Chama kikiwa na
Wajumbe walioongozwa na Katibu Mkuu wa Chama husika. Kila Chama kilitengeneza hadidu za rejea kwa
Wajumbe wake. Lakini, Kamati ya Pamoja
ilitengeneza agenda ya pamoja ya mazungumzo yao. Bahati nzuri vikao vya uamuzi vya vyama vyetu
kila kimoja kwa wakati wake viliridhia agenda hiyo.
Agenda
ya Mazungumzo ilikuwa na mambo matano:
(i)
Uchaguzi Mkuu wa 2005 na
athari zake.
(ii)
Usawa na haki kuendesha
siasa.
(iii)
Masuala ya Utawala wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
(iv)
Njia za kuimarisha maelewano
katika uendeshaji wa Uchaguzi Huru na Haki.
(v)
Utaratibu wa Utekelezaji na
Programu ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo
hayo.
Ndugu Wana-CCM;
Kwa
miezi kumi na minne, yaani tangu Februari, 2007 mazungumzo yamefanyika baina ya
Wajumbe wa vyama vyetu viwili kwenye Kamati hiyo. Pamoja na tofauti au migongano ya hapa na
pale, mazungumzo yalifanyika katika mazingira ya uwazi, ukweli na moyo wa
udugu. Mara kwa mara Wajumbe wa Vyama
vyetu walitoa taarifa kwa uongozi wa juu wa vyama na vikao vyake. Kwa upande wa CCM, Wajumbe wetu walitoa
taarifa kwangu na kwa Kamati Kuu, na kila Halmashauri Kuu ya Taifa ilipokutana,
taarifa ya maendeleo ya mazungumzo ilitolewa.
Maoni yalitolewa na Wajumbe walielekezwa ipasavyo kuhusu yale
yaliyofikiwa na yale ambayo walitakiwa kurudi kwa wenzao na kuzungumza
nao. Nao walifanya hivyo na kutoa
taarifa ipasavyo. Zipo nyakati Wajumbe wetu
walilazimika kurudi kwetu kutoa taarifa kuhusu baadhi ya maelekezo tuliyowapa
kutoafikiwa na upande wa wenzetu. Pale
ilipoonekana kuwa wenzetu wanayo hoja bora zaidi ilikubaliwa.
Ndugu Wananchi;
Nalisema hili kutaka kuwathibitishia kuwa
kilichofanywa Butiama na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM si jambo la ajabu,
ndiyo utaratibu wetu. Katika vikao vya
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM vilivyofanyika Musoma, hususan
Butiama, wajumbe wetu wa Kamati
waliwasilisha taarifa ya mwisho ya mazungumzo yao wa wenzao wa CUF. Hivyo walileta taarifa ya mazungumzo na
makubaliano kuhusu agenda zote tano.
Wajumbe walijadili agenda moja baada ya nyingine. Kwa jumla Wajumbe wamepokea kwa furaha
taarifa hiyo, wameridhika na kazi nzuri iliyofanywa na kuwapongeza wajumbe wake
na wenzi wao wa CUF kwa kazi nzuri waliyoifanya. Kazi ambayo waliitambua kuwa ni hatua kubwa
katika safari yetu ya pamoja kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa
uliopo Zanzibar.
Mjadala
ulikuwa wa kina, tena mrefu. Ilituchukua
saa 6 kwenye Kamati Kuu na karibu saa 8 kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa. Agenda hii siyo tu ilichukua muda mwingi wa
mkutano wetu wa Butiama bali ilipunguza hamu ya wajumbe kujadili kwa urefu
agenda nyingine. Hii ilikuwa ndiyo ilikuwa
ndiyo mama wa agenda zote.
Kuna
nyakati mjadala ulikuwa mkali na kuwatisha baadhi, wakidhani kuwa huenda
tusifikie makubaliano. Lakini kama ilivyo kawaida ya Chama chetu, mwishowe
tulikubaliana na mapendekezo ya Kamati.
Kwangu mimi ukali wa baadhi ya wajumbe unaimarisha imani yangu kuhusu
umuhimu wa kuhakikisha kuwa juhudi za kupata muafaka zinafanikiwa. Kushindwa hakuna maslahi kwa Zanzibar na kwa
nchi yetu kwa jumla.
Pamoja
na kukubaliana na mapendekezo ya Kamati, Halmashauri Kuu iliona haja ya kufanya
marekebisho fulani fulani katika baadhi ya mapendekezo hasa kuhusu mapendekezo
ya muundo wa Serikali Shirikishi. Shabaha
ya mapendekezo hayo ni kuboresha na kuimarisha mfumo huo unaopendekezwa. Marekebisho yanapendekezwa kwenye utaratibu
wa uteuzi wa Wasaidizi Wakuu wawili wa Rais na Baraza la Mawaziri. Marekebisho mengine yanahusu pendekezo la
kuwepo Baraza la Usuluhishi. Mimi
naamini marekebisho yote ambayo Halmashauri Kuu imetaka yafanywe kwa nia ya
kuboresha mapendekezo ya Kamati yetu yasingekuwa mambo magumu. Naamini wenzetu na wao wangegundua hekima ya
Halmashauri Kuu kupendekeza inavyopendekeza.
Bahati mbaya wenzetu wanakataa jambo kabla ya kuliona. Hata kabla Katibu Mkuu wa CCM hajawaandikia
kuwasilisha kile kinachopendekezwa, wenzetu wamekaa na kukataa, sijui wamekataa
nini. Wamekataa Halmashauri Kuu kutoa
maoni ya kuboresha kitu ambacho inabidi sote tukubaliane ndipo
kitekelezwe. Je, ni sawa hivyo?
Ndugu Wananchi;
Pamoja
na marekebisho hayo yahusuyo mapendekezo ya Kamati kuhusu mfumo wa Serikali
Shirikishi, katika mjadala, Wajumbe ndani ya Kamati Kuu na baadaye Halmashauri
Kuu walikuja na mawazo mawili mapya. Nia
ya mawazo hayo ni kuimarisha na kuboresha huo mfumo mpya unaopendekezwa
uwepo. Jambo la kwanza linahusu kuwashirikisha
wananchi katika kufanya uamuzi huu mkubwa.
Halmashauri Kuu ya Taifa inaamini kuwa mabadiliko yanayopendekezwa ni
makubwa sana na ya msingi. Yanahusu
kuubadili kabisa mfumo wa sasa wa utawala na uendeshaji wa shughuli za Serikali
Zanzibar. Halmashauri Kuu ya Taifa
inaona kuwa ipo haja ya msingi ya kuwashirikisha wananchi wa Zanzibar kuamua.
Halmashauri
Kuu inaona kuwa sahihi za Maalim Seif na Mzee Makamba au za viongozi tu pekee
hazitoshi. Ridhaa ya wananchi ni muhimu
na hili ni jambo la msingi na la kawaida katika mifumo yote ya kidemokrasia. Kama suala ni muda, napenda kuwahakikishia
kuwa hata CCM inapenda mambo hayo yaishe mapema iwezekanavyo.
Jambo
la pili jipya lililojitokeza kwenye Halmashauri Kuu linahusu haja ya kujipa
muda wa kuufanyia mapitio mfumo huu mpya unapendekezwa hapo utakapokubaliwa na
kutumika. Tofauti na ilivyo sasa ambapo
mshindi anaunda Serikali hata kama ameshinda kwa tofauti ndogo (hata iwe chini
ya asilimia moja), mfumo mpya nao unaleta utaratibu ambapo hata kama mshindi
kapata ushindi mkubwa lazima awashirikishe wenzake. Halmashauri Kuu inaafiki hoja ya mfumo wa
sasa wa kutokidhi haja ya kuwepo utulivu wa kisasa na kiusalama hasa kwa
historia yetu tangu 1995 na hivyo kuafiki dhana ya kushirikiana katika Serikali
kama jawabu.
Pamoja
na hayo, Halmashauri Kuu inasema mahali pote mfumo wa Serikali Shirikishi
ulipotumika ilifanyika hivyo kwa muda maalum.
Wakati wote lengo kuu likiwa kuivusha nchi katika mazingira magumu ya
wakati huo. Baada ya hapo, watu hurejea
kwenye mfumo wa kawaida wa mshindi kuunda Serikali akiwa na hiari ya
kuwashirikisha wenzake. Hivyo ndivyo
ilivyokuwa Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ndivyo ilivyo
hata sasa hapo Kenya. Halmashauri Kuu ya
Taifa ya CCM inataka hata kwenye huu mfumo wetu tuweke utaratibu wa kuutazama
upya kila baada ya wakati. Kwa jinsi
ilivyo sasa dhana hiyo haipo. Ni mfumo
utakaokuwepo daima dumu.
Ndugu Wananchi;
Kwa
kweli hayo ndiyo yanapendekezwa na CCM.
Na ndiyo mambo ambayo Halmashauri Kuu imeagiza Wajumbe wake waende
wakazungumze na wenzi wao wa CUF.
Tukubaliane ili tuendelee na hatua zinazofuatia. Kwa kweli sikutegemea yale mliyoyasikia ya
kusemwa na viongozi wa CUF kuhusu maamuzi hayo.
Upande mmoja siwalaumu kwa sababu walitoa matamko kabla ya kupata undani
wa kila kilichoamuliwa na CCM. Lakini,
upande mwingine nawalaumu kwa kutokusubiri taarifa rasmi kutoka kwa CCM juu ya
mapendekezo yetu. Mimi bado naamini kuwa
wangeyapata na kuyatafakari huenda wasingesema hayo wanayoyasema au kama
wangesema wangefanya hivyo kwa namna na lugha tofauti.
Kwetu
sisi katika CCM, tulichotegemea kutoka kwa wenzetu wa CUF, siyo tamko la
kujitoa kwenye mazungumzo na kutishia kuvurugika kwa amani. Tulichotegemea ni kwamba hata kama wangekuwa
na wazo la kujitoa kwenye mazungumzo, angalau wangetusikiliza ili kujua ni
marekebisho gani ambayo wana-CCM wanaona yangeimarisha na kuyapa uhalali zaidi
makubaliano ambayo Kamati zetu zilikuwa zinaelekea kuyapata.
Napenda
kuwahakikishia wana-CCM wenzangu, wenzetu wa CUF na wananchi kwa jumla kuwa CCM
haifanyi, wala haitafanya usanii wa kisiasa kwa jambo kubwa kama hili. CCM ina nia ya dhati ya kupata ufumbuzi wa
kudumu wa migogoro inayojirudia ya kisiasa na kiusalama Zanzibar. CCM inaamini kuwa mahali pa kuanzia ni kwenye
mazungumzo baina yake na CUF. Ni
kutokana na imani hiyo ndiyo maana tarehe 20 – 21 Desemba, 2006, Halmashauri
Kuu iliamua kuanzisha mazungumzo na CUF.
Baada
ya miezi 14 ya mazungumzo, CCM inaridhika kuwa tumefika mahali pazuri. Kilichobaki ni kukamilisha vizuri ili tupate
makubaliano ambayo yatakuwa endelevu
kama vile shabaha yetu ilivyo ya kupata suluhisho la kudumu. Kwa ajili hiyo pamoja na yote yaliyotokea na
kusemwa CCM itawasilisha mapendekezo yake kwa wabia wetu kwenye mazungumzo haya,
yaani CUF. Katibu Mkuu wa CCM, Lt.
Yusufu Makamba tayari ameshaandika barua hiyo kwenda kwa Maalim Seif Shariff
Hamadi, Katibu Mkuu wa CUF. Ni matumaini
yetu kuwa tutapata majibu mazuri na vyama vyetu vitakaa chini baada ya muda si
mrefu kukamilisha mazungumzo yetu.
Mimi
naamini ni kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar na wananchi wa Tanzania kwa vyama
vya CCM na CUF kukamilisha mazungumzo hayo.
Haya shime tufanye hivyo! Inawezekana sote hatuna budi kutimiza wajibu
wetu.
Ndugu Wana-CCM, Ndugu
Wananchi;
Nawashukuru
sana kwa kunisikiliza.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Kidumu Chama cha Mapinduzi