HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA,
KWENYE UFUNGUZI WA SEMINA YA VIONGOZI WA KITAIFA WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU
KUENDELEZA DHAMIRA YA MUAFAKA, HOTELI YA BWAWANI, ZANZIBAR, 19 FEBRUARI, 2005
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la
Mapinduzi;
Mheshimiwa Waziri Kiongozi;
Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Waheshimiwa Wenyeviti Wenza, Tume ya Rais ya
Usimamizi;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Washiriki wa Semina;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Nilipolihutubia taifa na kuwapa wananchi salamu za mwaka mpya, tarehe 31
Desemba 2004, nilizungumzia nia yangu isiyo na shaka ya kuhakikisha mwaka huu
tunafanya Uchaguzi Mkuu wenye heri, wa haki na uhuru kamili, katika mazingira ya
amani na utulivu, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Semina hii ni maandalizi mazuri ya kufikia lengo hilo lenye maslahi
makubwa kwa kila raia mwema. Hivyo ninawashukuru sana walioandaa semina hii, na
ninawapongeza kwa wazo la kuwa na semina hii. Na ninashukuru sana kwa mwaliko wao
kwangu kuja kuifungua semina hii; na hivyo kunipa fursa ya kurudia na kufafanua
kauli hiyo niliyoitoa tulipokuwa tunaukaribisha mwaka mpya wa 2005, mwaka wa
Uchaguzi Mkuu katika taifa letu.
Ipo asasi moja isiyokuwa ya kiserikali ambayo mwaka 2000, tulipokuwa
tunajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu, ilifanya semina mbalimbali na kuendesha elimu ya
uraia kuhusiana na uchaguzi.
Hatimaye, katika kujumuisha matokeo ya semina hizo, waliorodhesha kile
walichokiita wao Maadili Kumi ya
Uchaguzi Huru na wa Haki. Hayo
ni:
(1)
Kushiriki
(2)
Mwafaka
(3)
Uwazi
(4)
Utawala wa
Sheria
(5)
Haki za
Binadamu
(6)
Ukweli
(7)
Utamaduni wa
Ushindani
(8)
Elimu ya Uraia na Mpiga
Kura
(9)
Uadilifu, na
(10)
Nafasi Sawa.
Ndugu Wana-Semina:
Najua hapa Tanzania tunapozungumzia MUAFAKA, kinachokuja kichwani haraka
ni Muafaka baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF) hapa
Zanzibar. Nami nitazungumzia
Muafaka huo, lakini napenda nianze kwa kujenga hoja kuwa Tanzania nzima
inahitaji muafaka mpana zaidi, muafaka unaojumuisha jamii nzima ya
Watanzania.
Mageuzi ya kisiasa na kiuchumi tuliyoyafanya katika miaka karibu 20
iliyopita yamelegeza baadhi ya kamba zilizokuwa zimetufunga pamoja kama taifa
moja, watu wamoja, ndugu wa familia moja.
Ninahofu kuwa bila kukubaliana na kuwa na muafaka juu ya aina ya jamii
tunayotaka kuijenga, tutapoteza hata zile sifa ambazo kwa miaka mingi
zilitutofautisha sisi na nchi nyingine za Kiafrika, ikiwemo baadhi ya majirani
zetu. Mimi naomba sana kuwa uchumi
wa soko, au kwa jina jingine uchumi huru, pamoja na uhuru wa kisiasa na vyombo
vya habari, usiwe mwanzo wa kudhoofisha umoja wetu, kulegeza mshikamano wetu, au
kupunguza utaifa wetu, muungano wetu na udugu wetu.
Najua ninyi nyote ni Waheshimiwa, lakini muafaka wa kwanza ninaoutaka
katika nchi yetu ni wa kukubaliana kuwa sisi sote ni ndugu. Uchumi wa soko
utawafanya baadhi yetu watajirike kuliko wengine. Uhuru wa kisiasa umetuletea
vyama vingi na Waheshimiwa viongozi wake wengi. Lakini hii isiwe sababu ya
kujiona wengine ni bora kuliko
wenzao. Lazima Watanzania
tubakie ndugu. Udugu wetu ndio unatufanya tujione sisi sote ni binadamu sawa,
wenye utu sawa, haki sawa na mahitaji ya msingi sawa. Hivyo japo wengine wetu tunaitwa
Waheshimiwa, naomba mkubali na
tuafikiane kuwa katika nchi yetu sisi sote bado ni ndugu, na wala “ndugu” hii si
ya itikadi, ni ya utamaduni wetu wa Kiafrika. Kwa kusisitiza jambo hilo,
mtaniwia radhi leo nitakuiteni nyote, “Ndugu-Wanasemina”.
Kushiriki na Nafasi
Sawa
Ndugu Wana-Semina:
Naomba mnikubalie tuwe na muafaka wa kitaifa kuwa kila raia anayo haki
sawa kushiriki siasa, na kupata fursa sawa za kijamii, kiuchumi na kitamaduni
katika nchi yetu. Na leo napenda
nizungumzie haki sawa ya kisiasa.
Si kila raia anatamani uongozi wa kisiasa. Lakini ninaamini kuwa kila raia anapenda
ashiriki kuchagua viongozi wake, pamoja na kuchagua chama cha siasa
kitakachokabidhiwa uongozi wa taifa. Hivi sasa tunaendelea kuandikisha wananchi,
wenye sifa zinazotakiwa, kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Kazi hiyo inakwenda vizuri, na
ninawapongeza sana wanaoifanya kazi hiyo.
Lakini inaonekana kama vile bado hatuna muafaka wa kitaifa, miongoni mwa
baadhi ya vyama vya siasa, kuhusu haki sawa ya raia wetu kujiandikisha, na hivyo
kushiriki Uchaguzi ukifika.
Naomba sana kwenye semina hii tukubaliane sote, na tutoke na kauli moja,
kuwa kila raia, mwenye sifa zilizobainishwa wazi kisheria, anayo haki sawa ya
kujiandikisha na hatimaye kupiga kura.
Nasema hivyo maana ninasikia kuwa wapo wanaofanya jitihada kubwa kuzua
kila aina ya vikwazo kuwazuia wenzao wasijiandikishe, na kwa maana hiyo,
kuwazuia wasishiriki. Jambo hilo si sahihi, na ni vema tulirekebishe kama sehemu
ya muafaka mpana zaidi wa kitaifa.
Vipo vizuizi vya haki. Hivyo
tuendelee navyo. Lakini visivyo vya
haki tuachane navyo.
MUAFAKA
Ndugu Wana-Semina:
Nimekwisha kuzungumzia dhana ya muafaka katika jamii. Lakini kabla sijazungumzia Muafaka wa
Zanzibar, napenda kusema kuwa muafaka wowote ni maridhiano baina ya watu au
makundi ya watu katika jamii. Mambo
manne ni muhimu kabisa katika muafaka wa kweli. Kwanza ni dhamira. Muafaka wa kweli hauwezi kupatikana na
kuwa endelevu kama wahusika na wadau wote hawana dhamira ya kweli ya kufikia,
kufanikisha na kuendeleza muafaka. Naomba semina hii ifafanue vizuri jambo hili.
Muafaka usionekane kama vile ni jambo la kushurutishwa, ambapo kwa kisingizio
chochote kile, mhusika anajivua wajibu ndani ya muafaka. Muafaka hauwezi kufanikiwa ikiwa badala
ya kushirikiana kurekebisha kasoro zinazojitokeza, tunatafuta visingizio vya
kukwepa majukumu, au kulaumiana. Nasema, lazima tukiri na kudumisha dhamira ya
kweli ya kutaka muafaka wa kisiasa, kijamii na kiuchumi katika nchi
yetu.
Jambo la pili ni umuhimu wa kuvumiliana, kustahimiliana na kusahau yaliyopita. Muafaka wa kweli
unaanza na methali: “Yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo.” Muafaka wowote wa kijamii hauwezi kudumu iwapo kila
siku mtakuwa mnakumbushana au kutishana kwa mambo ambayo yamepita. Kiini cha muafaka ni ujasiri na kuachana
na yaliyopita; ni kuacha kutonesha vidonda, maana vidonda vinavyotoneshwa kila
mara kamwe haviwezi kupona.
Jambo la tatu ni kuaminiana. Muafaka wowote hauwezi kudumu iwapo
wahusika watakuwa kila mara hawaaminiani, na kila mara wanatafuta sababu ya
kutupiana lawama na kutoana kasoro.
Jambo la nne ni kukubaliana juu ya mgawanyo wa majukumu ndani ya muafaka,
vigezo vya utekelezaji wa majukumu
hayo, na namna bora ya kusuluhisha
matatizo yanayojitokeza, bila kuvunja muafaka wala kuzua
magomvi.
Mambo haya manne ni muhimu katika kufikia muafaka, na ni ya lazima iwapo
tunataka tuwe na utulivu na uvumilivu wa kisiasa, ambalo ni sharti muhimu la
maendeleo ya nchi, na ya wenye nchi.
Ndio maana ni muhimu sana tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tukubaliane
kuwa kwa vyovyote vile lazima Muafaka wa CCM na CUF hapa Zanzibar ulindwe,
utetewe, uenziwe, na uheshimiwe.
Nimesikia wenzetu wa CUF wakisema kuwa hakutakuwa na Muafaka
mwingine. Nakubaliana nao, iwapo
nia yao ni kuhakikisha muafaka uliopo hauvunjiki. Lakini kama wanachosema
kinaashiria vurugu na fujo, sikubaliani nao hata kidogo, maana hapo sasa ni
kuchezea moto. Lakini kwa dhati
kabisa nasema lazima tuhakikishe kuwa muafaka uliopo unadumu. Hatuna ruhusa ya
kurudi nyuma.
Napenda kuamini kuwa Muafaka huu baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
Chama Cha Wananchi (CUF) ni kielelezo cha dhamira ya kweli ya kuondoa dosari
mbalimbali zilizojitokeza wakati na mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.
Na kila mwenye nia njema atakiri kuwa zimefanyika juhudi kubwa za kutekeleza
Muafaka huu katika mazingira magumu kisiasa na kiuchumi.
Katika Muafaka ule, sehemu kubwa ya utekelezaji tuliibebesha Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ambayo sote tunajua ilipata ugumu wa kisiasa katika
kuwashawishi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM kupitisha Marekebisho ya
Nane na ya Tisa ya Katiba ya Zanzibar na Sheria nyingine. Itakumbukwa kuwa
marekebisho hayo yalipitishwa na Baraza la Wawakilishi wakati huo likiwa na
Wajumbe wa CCM peke yao.
Sisi kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi majuzi
tulishindwa kupitisha Bungeni baadhi ya mapendekezo yetu ya Marekebisho ya 14 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini Marekebisho ya Nane na Tisa ya Katiba ya Zanzibar yalifanywa na
kuwezesha utekelezaji wa mambo mengi mengine makubwa na ya msingi yaliyotakiwa
na Muafaka. Hayo ni pamoja na
Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kuundwa upya kwa Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar, kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, kufanyika—kwa
mafanikio makubwa—Uchaguzi Mdogo kule Pemba mwaka juzi, kuanzishwa kwa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura, na mengine mengi. Haya ndiyo mambo ya msingi kabisa
yanayohakikisha uchaguzi huru na wa haki.
Mimi, kwa dhati kabisa, mbele yenu nampongeza Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Ndugu yetu Amani Abeid Karume, na Serikali
yake, kwa kazi kubwa waliyoifanya kuwezesha mambo haya
kutekelezwa.
Mimi nimeshiriki katika juhudi nyingi za usuluhishi katika nchi zetu za
Kiafrika. Ni nadra sana kwa
Serikali kukaribia, wacha kufikia, kiwango cha utekelezaji wa makubaliano
kilichofikiwa na SMZ. Hivyo,
ninashangaa sana ninaposikia kauli za kubeza utekelezaji huu, kana kwamba
wakosoaji hao hawafurahii hatua hii kubwa ya utekelezaji iliyofikiwa. Wengine wanathubutu hata kutoa picha ya
kama vile hakuna lililofanywa kutekeleza Muafaka. Najiuliza. Lengo la kauli kama
hizo ni nini? Kuikatisha tamaa
SMZ? Kampeni ya kuichafulia
jina? Au kuendelea kujenga
mazingira ya kuja kukataa matokeo ya uchaguzi na kujikosha? Kwa hakika
utekelezaji wa Muafaka uliofanywa hadi sasa unatoa fursa nzuri kwa vyama vyote
vya siasa kuzitumia ipasavyo taasisi na sheria zilizowekwa sasa kuendesha siasa
za kistaarabu badala ya kulalamika tu, na wakati mwingine hata kupotosha
ukweli. Narudia. Muafaka wa kweli unahitaji dhamira ya
kweli ya pande zote. Bila hivyo
tunajisumbua bure.
Najua kuwa yapo mambo machache ambayo hayajatekelezwa na Serikali. Lakini, kila mwenye nia njema, ataona
kwamba mambo hayo aghalabu ni yale yanayohitaji fedha nyingi ambazo sote tunajua
Serikali hainazo. Kwa mfano, katika
eneo la fidia kwa waathirika wa matukio mbalimbali ya kisiasa, hata wahisani
wetu ambao hapo mwanzo walituahidi kwa hamasa kubwa kwamba wangesaidia,
hawajafanya hivyo, na sasa wengine wamebadili kauli.
Wapo waliosema kuwa hawana fedha.
Wapo pia waliosema kwamba hawawezi kufidia madhara yanayompata mtu baada
ya kuvunja Sheria za nchi. Hayo
ndiyo mazingira inayokabiliana nayo Serikali katika kutekeleza Muafaka. Hata hivyo, ni jambo la faraja kwamba
eneo hili la Muafaka, ambalo utekelezaji wake bado haujawezekana kwa ukamilifu,
linahusu kunufaika kwa mtu mmoja mmoja.
Yale yanayohusu manufaa kwa wote, karibu yote yametekelezwa. Naamini SMZ bado inatafuta njia nyingine
mbadala za kutafuta fedha kwa ajili ya fidia hizo. Lakini hilo litachukua muda. Muhimu ni kwamba dhamira ya utekelezaji
bado ipo. Tuwe waungwana basi, na tusikimbilie kuihukumu SMZ kwa umaskini wa
nchi yetu na utegemezi wetu.
Ndugu Wana-Semina:
Nasikitika kuwa zipo dalili kwamba dhamira na ari ya Muafaka inaonekana
kupungua. Hii inadhihirishwa na
kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa zinazoashiria kujenga chuki, kuleta
shari, na kueneza uchochezi. Tulikubaliana katika Muafaka kuachana na kauli kama
hizi. Tulikubaliana pia katika
Muafaka kuheshimu Sheria za nchi.
Tuliweka utaratibu wa mashauriano patokeapo kutoelewana au matatizo. Sasa kwa nini mwaka huu mambo haya
yamezidi?
Kuendelea kutolewa kwa kauli kama hizi na vitendo vya kuvunja Sheria ni
ukiukaji wa Muafaka na dhamira yake.
Jukumu la utekelezaji wa Muafaka si la Serikali peke yake, bali pia ni la
Vyama vya Siasa vinavyohusika. Viongozi wa Vyama vya Siasa wana nafasi kubwa kwa
sababu wana uwezo wa kuonana na kubadilishana mawazo na wanachama wao, na wana
ushawishi mkubwa kwao. Wakipenda,
viongozi hao wanaweza kuimarisha imani ya wafuasi wao juu ya Muafaka. Wakipenda
pia wanaweza kufifisha imani hiyo kutegemeana na ujumbe wanaoufikisha kwa
wanachama wao na wananchi. Kila
chama kijiulize kipo upande upi:
Upande wa kuimarisha dhamira na imani juu ya Muafaka au upande wa
kuidhoofisha na hivyo kuhujumu utekelezaji wake.
Kwa upande wa Serikali, ninaridhika na juhudi za dhati zinazofanywa
kuweka mazingira mazuri ya kufanikisha Muafaka. Mimi mwenyewe nimekuwa
nikisisitiza katika mikutano yangu mbalimbali, ndani na nje ya nchi, kwamba
nimekusudia katika kipindi changu cha uongozi kilichobaki kuhakikisha kwamba
juhudi zinachukuliwa kufanikisha Muafaka na kuiona Tanzania inaendesha siasa za
ushindani bila ya kugombana. Tukiwa
sote na dhamira ya kweli ya Muafaka, tofauti za mawazo tuliyonayo haziwezi kuwa
chanzo cha kugombana. Tuufanye
umoja wetu, na udugu wetu, kuwa jambo muhimu zaidi.
Aidha, tuhakikishe kwamba vyombo na maadili yanayohusiana na demokrasia
ya uchaguzi hasa wakati wa kampeni na uchaguzi wenyewe vinaimarishwa. Tuwe na
muafaka miongoni mwa vyama vyote juu ya maadili ya kisiasa na namna ya
kuhakikisha yanafuatwa na kila chama cha siasa.
Uwazi na Ukweli, na Elimu
ya Uraia na Mpiga Kura
Ndugu Wana-Semina:
Ipo hisia iliyojengeka kwa wananchi kuwa siasa ina ulaghai kiasi fulani
ndani yake. Mimi naamini kuwa si
lazima iwe hivyo, lakini hiyo haiondoi wajibu wetu wanasiasa kuongeza uadilifu
wetu ili kufuta hisia hizo. Na
tusisahau kuwa wakati mwingine mbio za mwongo huwa fupi kweli kweli kwenye
siasa.
Mgombea mmoja wa Ubunge, tumwite Masanja, alikuwa anazungukazunguka
kwenye jimbo analowania akimchangamkia kila anayemkuta. Akakuta watoto kadhaa
wanacheza nje ya nyumba, na mama mmoja akiwaangalia. Akamwendea yule mama, akamsabahi, na
kisha akasema: “Watoto wazuri sana
hawa, mama. Naweza kuwabusu?” “Endelea tu,” akajibu yule
mama.
Baada ya kuwabusu, Mheshimiwa Masanja akarejea kwa yule mama, na kusema,
“Haki ya Mungu sijawahi kuona watoto wazuri kama hawa. Ni wako sio?” Kabla yule mama hajajibu,
Mheshimiwa Masanja akaendelea, “Lazima watoto hawa ni wako. Hebu ona macho yao mazuri, nyuso angavu,
na sauti kama tausi. Wanafanana na
wewe kwa kila hali.” Yule mama akabaki anamkodolea macho Mheshimiwa Masanja,
aliyeendelea kusema: “Tafadhali mama yangu. Nakuomba mume wako akirejea nyumbani
umwambie kwamba Bwana Masanja alipita hapa kumsabahi.” Yule mama akaamua kumtolea uvivu.
“Tazama Bwana Masanja. Sina muda na
ulaghai wenu wanasiasa. Kwa taarifa
yako mimi sina mume, na hapa ni kituo cha watoto yatima!”
Ndugu Wana-Semina:
Naomba pia tuwe na muafaka wa kitaifa wa kuendesha shughuli za kisiasa
kwa uwazi na ukweli. Tuache
udanganyifu. Kwa mfano nimeambiwa
kuwa kuna sehemu ya nchi yetu ambapo wazee walidanganywa na wanasiasa wa chama
fulani kuwa wao hawana haja tena ya kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura eti kwa vile tayari wamekamilisha mchango wao kwa taifa hili na
hivyo wanayo haki kupumzika!!
Huko nyuma katika mojawapo ya chaguzi kipo chama fulani kilichowadanganya
wananchi kuwa baada ya kufikia Muafaka mwaka 2001, basi vyama vyote vya siasa ni
sawa tu, na ukipigia kura mgombea wa upinzani ni sawa tu na kumpigia kura
mgombea wa Chama Tawala.
Na mifano ya namna hii ipo mingi.
Nasema, hatuwezi kuimarisha demokrasia ya vyama vingi kwa
udanganyifu. Na kwa hili naomba
sana vyombo vya habari vitusaidie kuwaumbua wanaowadanganya
wananchi.
Na hili linanifikisha kwenye umuhimu wa elimu ya uraia, na elimu ya mpiga
kura. Ni dhahiri udanganyifu
unaofanywa na baadhi ya wanasiasa unachangiwa na kutoelewa kwa wananchi juu ya
haki zao katika siasa na katika demokrasia ya vyama vingi. Jambo hili ni muhimu, na ni la kutiliwa
mkazo. Na, kwa kadri
inavyowezekana, ni vizuri elimu hiyo itolewe na Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Lakini viongozi wa kisiasa, wa vyama vyote, nao wanayo nafasi nzuri ya
kutoa elimu ya uraia, lakini pale tu ambapo wamekuwa wawazi na wakweli, na
waadilifu, wasiotumia fursa hiyo kupigia kampeni vyama vyao au kuhujumu vyama
vya wenzao. Vivyo hivyo Asasi
Zisizokuwa za Serikali zina nafasi nzuri ya kutoa elimu ya uraia, na elimu kwa
wapiga kura. Na kwa kweli wengine
wamefanya kazi nzuri huko nyuma.
Lakini narudia. Elimu hiyo
isiwe fursa ya kupigia kampeni chama kimoja, na kuponda chama au vyama vingine,
au isitumike kama mbinu ya kuhujumu nchi yetu kutoka kwa watu wa
nje.
Viongozi wa vyombo vya habari pamoja na vyombo vyao wana nafasi kubwa
katika kutoa elimu ya uraia na kuendeleza dhamira ya Muafaka. Wana uwezo mkubwa pia wa kuvuruga
dhamira hiyo kama watataka kufanya hivyo. Lakini wajue wazi kuwa wanapotoa
taarifa za kuchonganisha wanasiasa, au za kushabikia kauli za uchochezi na za
kutishia amani zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa, au za kupotosha ukweli,
wanadhoofisha dhamira za Muafaka.
Mimi nawaomba wachague kuendeleza dhamira ya Muafaka na si kuidhoofisha,
wajenge udugu wa Watanzania badala ya kufarakanisha jamii. Watakuwa wanachangia
katika kuendeleza dhamira ya Muafaka ikiwa watatoa uzito na kipaumbele kwa
habari zinazoonyesha kukerwa na uchochezi, zinazoheshimu haki ya kuelezea
msimamo wa pande zote zenye mawazo yanayotofautiana, na pia habari zenye ukweli
uliothibitishwa na utafiti.
Nawaomba sana waandishi wa habari wasikubali kununuliwa na wanasiasa,
kwa madhumuni ya kuwapaka matope washindani wao, na kuwatukuza
waliowanunua. Hivi sasa yapo
magazeti nchini ambayo kila uchao, hawakosi baya la kuandika kuhusu wanasiasa
fulani. Na yapo magazeti ambayo
mabaya ya wanasiasa fulani kamwe hayaandikwi, na yakiandikwa wahusika
wataandamwa sana, na pengine kutishwa.
Sisemi mabaya ya wanasiasa yasiandikwe; nasema uwepo uwiano mzuri
isionekane kuwa wapo watakatifu daima na wapo waovu daima.
Mgombea Urais katika nchi moja tajiri alikasirishwa sana na yaliyoandikwa
kuhusu yeye na gazeti moja kubwa katika mji wake. Akaenda kwa hasiri kumwona mhariri wa
gazeti hilo. “Unaandika uwongo
kabisa kuhusu mimi kwenye gazeti lako, na unajua hivyo!” Yule mhariri
akatabasamu na kumjibu, “Mheshimiwa, unishukuru kwa kuandika uongo. Hebu fikiri kampeni yako ingeishia wapi
iwapo tungeandika ukweli kuhusu wewe?”
Ndugu Wana-Semina:
Nimefurahishwa pia na ushirikishwaji wa viongozi wa kijamii katika semina
hii. Viongozi wa kijamii, hasa wa
kidini wana nafasi ya pekee kabisa katika kuendeleza dhamira ya Muafaka. Katika
dini, madhehebu na taasisi zao wanazoziongoza wanakutana na wafuasi wa vyama
mbalimbali vya kisiasa. Nawaomba
wafikishe ujumbe wa upendo, amani, umoja na uungwana kwa waumini wa dini zao.
Aidha, wanapoendesha ibada, ningependa waendelee kuiombea nchi yetu na watu wake
ili tufaulu mtihani wa uchaguzi mkuu unaotukabili mwaka
huu.
Utawala wa Sheria na Haki
za Binadamu
Ndugu Wana-Semina:
Hakuna haki isiyokuwa na mipaka.
Nasi wachanga kwenye demokrasia ya vyama vingi lazima tuwe tayari
kukubali mipaka ya haki zetu ndani ya mfumo huu wa siasa. Maana wapo ambao kwa vitendo na kauli
zao ni kama vile hawadhani ipo mipaka katika uhuru wao wa kisiasa na uhuru wa
maoni. Na zaidi sana tusisahau kuwa
sisi ni Waafrika, wenye utamaduni wetu, na maadili yetu.
Ukweli ni kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nao una maadili yake ambayo
lazima tuyazingatie. Mojawapo ni
hayo ya uwazi na ukweli niliyoyasema. Si ruhusa, kwa makusudi, kuwadanganya
wananchi na wapiga kura. Jingine ni
umuhimu, na kwa kweli ulazima, wa kufuata sheria.
Kwa mfano, sheria inasema kuwa kabla ya kufanya mkutano wa hadhara au
kufanya maandamano upate kibali cha Polisi. Lengo lake si kuzuia, bali ni kuratibu
na kuwapa Polisi muda na nafasi ya kusimamia mikutano na maandamano ili amani
idumishwe. Lakini utakuta mwanasiasa ambaye, akiulizwa, anasema anapenda siasa
za amani, huyo huyo anakerwa sana akiambiwa apate kwanza kibali cha Polisi. Hebu fikiri. Kitoke Chama “A” kifanye maandamano bila
kuiarifu Polisi, halafu njiani kikutane na maandamano ya Chama “B” ambacho nacho
hakitaki kupata kwanza kibali cha Polisi, unafikiri kutatokea nini kama si
mlipuko wa fujo, na pengine kuumizana au hata kutoana
roho?
Napenda vyama vya siasa vyote vielewe kuwa kazi ya Polisi ni kuratibu na
kuhakikisha usalama wakati wa shughuli za kisiasa. Hawako kupendelea chama chochote, na
wala hawana ruhusa kuzuia mkutano wa kisiasa au maandamano bila sababu ya
msingi, na siku zote wataeleza wazi sababu hiyo. Na ni wajibu wetu sote wanasiasa kufuata
sheria na kuheshimu utawala wa sheria.
Na pale unapoona umezuiwa kwa sababu ambazo si za msingi utaratibu wa
kukata rufaa upo. Ufuatwe huo,
maana siku zote tabia ya kuvunja sheria haina mwisho
mwema.
Na, kama nilivyosema, ni vizuri pia kuzingatia mila na desturi zetu. Uhuru wa kisiasa, na uhuru wa maoni,
usiwe uhuru wa matusi na lugha chafu, na usiwe uhuru wa uchochezi. Majukwaa ya siasa yawe ya kuuza sera na
mikakati, si ya kuchochea fujo na uvunjifu wa sheria.
Kila chama cha siasa kina vijana, wenye damu inayochemka. Unapochochea vijana wa chama chako ujue
wengine nao wanaweza kuchochea vijana wao.
Hapo itakuwa zahama kubwa.
Na mimi napenda kuweka wazi kuwa wakati mwingine nina kazi kubwa kuwazuia
vijana wa CCM, ambao ndio wengi, wasilipize visasi. Sasa nasema, tafadhali sana tuwe na
muafaka wa kitaifa kuhusu jambo hili.
Majukwaa ya siasa kamwe yasiwe fursa ya kutukana, au kuchochea fujo na
vurugu.
Na pia ni vema tujenge tabia ya kuheshimu vyombo vya dola. Hawa tumewafunza na kuwapa silaha
kihalali ili walinde amani na usalama katika nchi yetu. Na pamoja na semina zote tunazowapa
kuhusu haki za binadamu tujue kuwa na wao ni binadamu, wenye hisia. Ni vema sisi wanasiasa tuwatendee haki
kwa kuwachukulia kama binadamu wenzetu ambao nao hawapendi
kutukanwa.
Na pia, kama nilivyowahi kusema, utulivu wa kisiasa ni matokeo ya vyama
vyote kukubaliana kuwa tuwe na ushindani wa kisiasa wa kistaarabu. Na wala si kweli kuwa kila panapotokea
matatizo au fujo kwenye siasa, wa kulaumiwa ni Chama Tawala peke yake, na
Serikali. Wazungu wana msema: “It takes two to tango”.
Na mwisho, kwa kuzingatia maadili ya Kiafrika, ni vema heshima ya nafasi
kuu za uongozi katika nchi yetu ziheshimiwe. Leo mimi ni Rais. Mwaka kesho sitakuwa Rais. Heshima ya ofisi hii si yangu binafsi,
ni heshima ya ofisi. Hivyo hata
kama hunipendi binafsi, unao wajibu kuheshimu ofisi hii. Yapo mengi mema tunayoweza kuiga kutoka
nchi tajiri. Naomba tusiige dharau.
Tusiige kushusha heshima ya viongozi wetu katika jamii. Hili pia naomba tuwe na muafaka nalo
katika nchi yetu.
Utamaduni wa Ushindani na
Uadilifu
Ndugu Wana-Semina:
Nitashukuru pia iwapo semina hii itahimiza muafaka wa kitaifa kuhusu
uadilifu katika siasa na utamaduni wa ushindani. Wahenga walisema: “Asiyekubali kushindwa si
mshindani”. Hivyo kwenye siasa,
kwenye chaguzi ndani ya kila chama, na vile vile kwenye chaguzi
zinazoshindanisha chama na chama, lazima kuwe na uchaguzi huru na wa haki,
lakini baada ya hapo kila mgombea, awe mtu binafsi au chama, akubali kuwa kuna
kushinda, na kuna kushindwa.
Uchaguzi ukiisha tuendelee kujenga nchi badala ya kushinda mahakamani
kufungua kesi baada ya kesi kila baada ya uchaguzi. Pale ambapo ni lazima, sawa. Lakini ninaamini kesi nyingi
zinazofunguliwa zinatokana na kukataa kushindwa tu, badala ya
kuonewa.
Na kama nilivyosema uadilifu ni muhimu katika vyama vyote. Tusiwape wananchi hisia kuwa siasa ni
mahali pa ulaghai, rushwa, wizi na matumizi mabaya ya fedha. Kila chama cha siasa kiwe tayari kupimwa
uadilifu wake kwa vigezo vile vile ambavyo Chama Tawala na Serikali yake
inapimwa navyo. Maana wasipokuwa waadilifu, wawazi na wakweli wakati wakiwa
kwenye upinzani, kwa hakika wataendelea kuwa vivyo hivyo wakibahatika kuingia
madarakani.
Hitimisho
Ndugu Wana-Semina:
Kwa kumalizia naomba nikumbushe kidogo tu kwamba Tanzania imekuwa moja
miongoni mwa nchi chache Barani Afrika iliyo na utulivu mkubwa wa kisiasa na
yenye utamaduni wa kuvumiliana na kusaidiana. Tofauti zetu za kabila, dini na
itikadi hazikuruhusiwa kudhoofisha udugu, umoja, na mshikamano wetu. Utamaduni
huu hauna budi kuenziwa na kuimarishwa.
Naomba sote tukubaliane kuwa tofauti za kisiasa hazitaruhusiwa kuwa
chanzo cha kufarikiana na kuhasimiana.
Tukidumisha utulivu na ustahamilivu tutaondoa shaka ya kutoaminiana baina
yetu. Tukiimarisha dhamira ya muafaka tutaona mema zaidi kuliko mabaya. Ni
vizuri watu wakaishi kwa upendo na umoja na kukabili matukio yoyote ndani ya
Taifa letu kwa pamoja, tukijua sote ni wadau kamili wa hatma ya nchi yetu.
Wanasiasa tukumbuke kuwa watu wetu ni kama watu wengine duniani, wanaweza
kubadilika kwa mujibu wa mazingira yalivyo, hivyo tusiwafanye wakabadilika kwa
mivutano isiyokuwa na maana. Badala yake tuwawekee mazingira ya kimaendeleo na
ya kujenga upendo na umoja wa Kitaifa.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa Semina hii ya Viongozi wa
Kitaifa yenye Dhamira ya Kuendeleza Ari ya Muafaka wa CCM na CUF imefunguliwa
rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.