HOTUBA YA MWENYEKITI WA  CHAMA CHA MAPINDUZI NDUGU BENJAMIN WILLIAM MKAPA, AKIFUNGUA MKUTANO MKUU MAALUM WA SABA WA CCM; CHIMWAGA, DODOMA, 24 JUNI 2006

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

            Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete;

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar na Mwenyekiti wa

            Baraza la Mapinduzi, Ndugu Amani Abeid Karume;

Makamu Mwenyekiti wa CCM,

Ndugu John Samwel Malecela, Mb;

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

            Dkt. Ali Mohamed Shein;

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

            Mzee Ali Hassan Mwinyi;

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi,

            Ndugu Philip Japhet Mangula;

Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Zanzibar na

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Salmin Amour

Muasisi Wetu Mzee Rashid Mfaume Kawawa;

Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi,

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa,

Wajumbe wa Mkutano Mkuu,

Wazee na Waasisi wa TANU, ASP na CCM,

Mabibi na Mabwana.

 

 

1.         Napenda kukukaribisheni wote katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa Saba wa Kawaida wa Chama Cha Mapinduzi.  Mkutano huu umekuwa wa kawaida baada ya Mkutano Mkuu wa Taifa kufanya marekebisho kwenye Katiba ya Chama hapo mwaka jana.  Kwa mujibu wa marekebisho hayo, Mkutano Mkuu wa Taifa sasa utakutana mara tatu katika kipindi cha miaka mitano badala ya mara moja tu kama ilivyokuwa huko nyuma.

 

2.         Mwaka mmoja uliopita tulikuwa hapa Chimwaga kuhitimisha kazi muhimu ya kuteua wagombea wa Chama chetu kwa uongozi wa Taifa letu kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005. Ushindi wa kihistoria tulioupata ni kielelezo kwa mara nyingine cha imani ya Watanzania kwa historia na uzoefu wetu; kwa ubora na usahihi wa sera zetu; kwa matumaini ya amani na maendeleo tunayoendelea kuwapa wananchi; na kwa ubora na uzoefu wa wagombea wetu.

Nauliza kama nilivyouliza tena na tena kwenye kampeni: Nani kama CCM? Nani kama CCM?

 

Ndugu Wajumbe,

 

3.         Katika mkutano wetu wa tarehe 4 Mei, mwaka jana tulifanya kazi kubwa ya kuteua Mgombe Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama chetu.  Kwa njia ya uchaguzi kama Katiba na Kanuni zetu zinavyotaka, tulimteua ndugu Jakaya Mrisho Kikwete kwa wingi mkubwa wa kura.  Tulipompeleka kwa wananchi, aliibuka na ushindi mkubwa wa kishindo wa asilimia 80.28, na hivi sasa ndiye Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne.  Ni wajibu wetu sote kutumia fursa ya Mkutano huu kumpongeza kwa dhati Ndugu Kikwete kwa ushindi huo mkubwa wa aina yake alioupata na kukipatia Chama Cha Mapinduzi.

 

4.         Tumpongeze pia Ndugu Amani Abeid Karume kwa kupata ushindi wa asilimia 53.18 ambao umemwezesha kuendelea kuwa Rais wa Zanzibar kwa kipindi chake cha pili na cha mwisho.  Kwa mazingira ya Zanzibar, ushindi huo nao ni wa kishindo.

 

5.         Pongezi zetu hazitokamilika bila ya kuzielekeza pia kwa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa CCM kwa kupata imani za wapiga kura.

 

 

Ndugu Wajumbe,

6.         Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Mlifanya kazi kubwa sana ya kutetea rekodi ya Chama chetu kwenye uongozi wa Taifa, na kujenga hoja ya kutosha kwa nini tuendelee kupewa dhamana ya uongozi wa Taifa. Sifa zenu zilikutangulieni. Maana ushindi kwenye uchaguzi unasimama kwa miguu miwili. Sifa za Chama kwa upande mmoja na sifa za wagombea kwa upande wa pili. Miguu yetu yote miwili katika CCM ilikuwa imara na ushindi ulikuwa stahili yetu.

 

7.         Wengi wenu hapa mlishiriki mchakato wa uteuzi wa wagombea katika ngazi zote. Nakupongezeni sana kwa kazi nzuri mliyoifanya. Nakushukuruni sana. Yapo maamuzi mengine magumu ilibidi tuyafanye. Kuna wakati na mahali tulijikuta tuna wagombea wawili au zaidi ambao wote wana sifa kubwa sana, na wote wanatosha na kustahili kubeba bendera ya CCM. Kwa moyo mzito ilibidi tuchague mmoja na kumwacha mwingine, si kwa vile hafai bali kwa vile hatuwezi kuwachukua wote.

 

Nafasi ya Wanawake

Ndugu Wajumbe:

8.         Tukiwa Chama kikubwa kuliko vyote, Chama Tawala, tulikuwa pia na wajibu wa kuhakikisha kuwa baada ya uchaguzi tunakuwa na Bunge na Mabaraza ya Halmashauri yenye uwiano wa kijinsia unaotimiza dhamira yetu na makubaliano ya nchi za SADC kuwa angalau asilimia thelathini ya Wabunge wawe wanawake. Ilibidi tufanye juu chini kupata wagombea wanawake wa kutosha kwenye majimbo. Iibidi wakati mwingine tuwasihi wagombea wakiume walioongoza kwenye kura za maoni waridhie uamuzi wetu wa kuwachukua wagombea wanawake. Nafurahi kuwa walielewa, wengi hawakununa sana, na waliwasaidia hao wagombea wanawake hadi wakashinda. Nauliza tena. Nani kama CCM? Nani kama CCM?

 

9.         Nawapongeza wagombea wetu wanawake kwa ujasiri wao mkubwa na kwa kuitikia wito wetu kuwa wajitokeze kwa wingi kugombea.  Binafsi wamestahimili mengi. Familia zao zimevumilia mengi. Wamefanya kazi kubwa kwa niaba ya Chama. Nawashukuru sana.

 

10.       Namshukuru pia Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar kwa uamuzi wao wa busara wa kuteua wanawake wengi kuliko zamani kushika nafasi muhimu katika uongozi wa nchi. Nionavyo mimi, kama ilivyokuwa kwa wale niliowateua mimi wakati wangu, kinamama hawa wameonyesha uelewa na uwezo wa uongozi. Wameonyesha wako tayari. Swali la msingi ni kiasi gani wanaume wako tayari kutoa nafasi zaidi kwa wanawake siku zijazo, si katika Serikali tu, bali pia katika familia, katika jamii, katika biashara na katika vyama vingine vya siasa. Kama mjuavyo uamuzi wa Umoja wa Afrika ni kuwa hatimaye, mapema iwezekanavyo, uwepo usawa wa kijinsia katika uongozi wa nchi zetu na Umoja wetu. Ni vema Tanzania ijiandae na ijiweke mahali pazuri kuwa miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kufikia lengo hilo.

 

11.       Ushindi mkubwa tulioupata katika uchaguzi Mkuu wa 2005 tulipewa na wananchi kwa imani yao.  Hatuna budi kuwashukuru kwa imani hiyo kubwa.  Ushindi huo mkubwa waliotupa umeambatana na matarajio makubwa kwa Serikali za CCM zilizoundwa mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu.  Kwa kujiamini kabisa, tunawahakikishia Watanzania kwamba matarajio yao yatakidhiwa.  Kujiamini kwetu huko kumeimarishwa na jinsi Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Awamu ya Sita inayoendelea kule Zanzibar zilivyoanza kazi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.

 

Ndugu Wajumbe

 

12.       Mkutano huu ni wa kazi.  Kazi ya kutathmini tulivyofanya huko nyuma katika kazi za Chama na za Serikali, hususan utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2000.  Lakini pia kazi ambayo ni ya msingi zaidi ni ya kutafakari majukumu yaliyo mbele yetu, hasa kuhusiana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005.  Nakuombeni kazi hizo tuzifanye kwa umakini mkubwa kama unavyotarajiwa Mkutano wa hadhi kubwa kama huu wetu.

 

 

Ndugu Wajumbe,

 

13.       Katika mkutano huu tutafanya pia Uchaguzi wa Mwenyekiti kwani kama wote mnavyofahamu, nitang’atuka baadaye katika Mkutano huu.  Nakuombeni kama kawaida yetu katika CCM wakati utakapofika tufanye uamuzi thabiti.

 

Ndugu Wajumbe,

 

14.       Mengi nakusudia kuyasema kesho wakati nitakapong’atuka.  Lakini siyo siri kwamba miongoni mwa mambo yaliyochangia ushindi wetu mkubwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, ni kutekelezwa kwa kiwango kikubwa yale tuliyoahidi katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2000.  Tuliwapa wananchi programu nzuri ya maendeleo kwa kipindi cha 2000 hadi 2005, na tukaitekeleza.  Na wao wakatuchagua tena.  Kama ambavyo Ndugu Rais amekuwa akisisitiza kwamba kumalizika kwa Uchaguzi wa 2005 ni kuanza kwa maandalizi ya Uchaguzi wa 2010.  Sasa tuna Ilani ya uchaguzi ya 2005.  Changamoto yetu kubwa ni kuitekeleza.  Na hakuna cha kusubiri kuanza kuikabili changamoto hiyo.

 

15.       Kwa hilo, napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kupitia ndugu Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuianza kazi hiyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.  Ni dhahiri kabisa bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejielekeza katika utekelezaji wa Ilani.  Na alipokuwa akiiwasilisha bajeti hiyo Bungeni, Waziri wa Fedha alisisitiza mara kwa mara na kuonyesha jinsi bajeti hiyo ilivyojikita katika utekelezaji wa Ilani.

 

16.       Pongezi zangu pia ziende kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi mahiri na makini wa Rais Karume.  Na wenzetu huko Zanzibar nao wameanza utekelezaji wa Ilani kwa ile ile ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.

 

17.       Utakelezaji wa Ilani si wa Serikali peke yake.  Nasi katika Chama ni jukumu letu pia.  Tuhamasishwe na fursa ya Mkutano Mkuu huu wa Taifa kujipangia mikakati ya utekelezaji wa jukumu hilo.  Lengo ni kuhakikisha kwamba mwaka 2010 utukute tukiwa tumetekeleza yote tuliyoahidi katika Ilani.  Nitafurahi sana kama majadiliano yetu katika Mkutano huu yatachukua mkondo huo kwa sehemu kubwa.

 

Ndugu Wajumbe,  Tuanze kazi.

 

Mkutano umefunguliwa.