| |
Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi
imeamua kuanzishwa kwa Jarida la CCM linaloitwa MKEREKETWA.
Lengo kuu la MKEREKETWA ni kufikisha kwa wanachama na
Jumuiya zilizo chini ya CCM za Wanawake, Vijana na Wazazi
maamuzi na maelekezo ya Chama.
Ni muhimu ikafahamika kwamba siyo viongozi wa Chama
katika ngazi fulani fulani tu ndio wanaostahili kupewa
taarifa na ripoti za Chama, bali ni lazima wanachama
wetu wa ngazi zote waelimishwe juu ya maendeleo ya Chama
na Serikali zote mbili za CCM za Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Jambo hili ni muhimu sana kwani "Bila ya kuwa na
taarifa kamili, hakuna mwanachama awezaye kuzitetea
Sera za CCM mbele ya umma".
Zaidi ya kutoa taarifa za maamuzi, maelekezo na maendeleo
ya Chama, Mkereketwa litakuwa pia likifanya uchambuzi
na kutoa ufafanuzi wa sera za CCM hasa pale zinapopotoshwa.
Litakuwa pia na makala za historia ya Chama na viongozi
wake pamoja na mashujaa mbali mbali waliojitoa muhanga
katika kupigania Uhuru wa Tanganyika na kufanikisha
Mapinduzi ya Zanzibar.
|
|
Mkereketwa
litaongozwa na ukweli na usahihi wa mambo katika makala
zake na halitokuwa na ushabiki. Lengo la Mkereketwa
zaidi ya kuwaarifu wanachama wa CCM, ni kuwa kimbilio
la Watanzania wote la kutafuta ukweli na usahihi wa
mambo.
Wanachama wa CCM, wasomi na wananchi wote kwa jumla
wanakaribishwa kuchangia makala katika jarida hili kwa
kuzingatia sera na malengo yake.
Tofauti na magazeti ya kawaida, MKEREKETWA litakuwa
linachapishwa kila baada ya vikao vya Halmashauri Kuu
ya Taifa au wakati wote wowote mwingine Chama kitapoona
kuna umuhimu wa kuchapisha Jarida hili ili kufikisha
ujumbe haraka kwa walengwa.
Ningependa kuchukua nafasi hii kuwataka Makatibu Wenezi
wa Chama chetu wa ngazi zote kuhakikisha kwamba Jarida
hili linawafikia wanachama wetu. Jitihada zote hizi
zitakuwa za bure endapo MKEREKETWA haliwafikii walengwa
na kwa haraka mara tu lichapishwapo.
|
|