| |
Katika
mkutano wake wa mwezi uliopita wa Septemba, Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM miongoni mwa mengine ilipokea taarifa
ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu maamuzi
iliyofanya baada ya kusikiliza na kuyajadili malalamiko
yaliyotolewa na baadhi ya wagombea wa nafasi mbali mbali
za uongozi katika ngazi ya Mkoa katika Uchaguzi Mkuu
wa CCM uliofanyika mwaka jana (2002).
Kamati Kuu haikupata lalamiko hata moja kuhusiana na
uchaguzi wa Ngazi ya Taifa uliofanyika Chimwaga mwezi
Oktoba, 2002.
Kuhusiana na chaguzi za Ngazi ya Mkoa, Kamati Kuu ilipokea
malalamiko kutoka Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa,
Kagera, Mara, Mbeya, Mwanza, Rukwa na Singida.
Kwa jumla, malalamiko mengi yalijikita juu ya tuhuma
za rushwa. Walalamikaji na walalamikiwa wote walipewa
fursa ya kutosha ya kujieleza katika vikao husika na
Kamati Kuu yenyewe kupitia Kamati ya Maadili ya CCM
ilifanya uchunguzi wa kina wa kila tuhuma katika kipindi
cha karibu mwaka mzima. Lakini hakuna hata tuhuma moja
iliyothibitika.
Kilichobainika kwa malalamiko yote ni uchungu tu wa
kushindwa ulioambatana na ugumu wa kukubali kushindwa.
Lakini hayo ndiyo maisha katika ushindani wowote; kuna
kushinda na kushindwa.
Kwa hiyo, uamuzi wa Kamati Kuu ni kwamba matokeo ya
uchaguzi yaliyotangazwa katika mikoa yote iliyolalamikiwa
ni halali na yanabaki yalivyo. Kwa mujibu wa Ibara ya
29 ya Kanuni za Uchaguzi wa CCM, uamuzi huo ni wa mwisho.
Halmashauri Kuu ya Taifa imeridhika kwamba si uchaguzi
wa ngazi ya Taifa tu ambao haukuathiriwa na rushwa,
bali pia hata chaguzi za ngazi ya Mkoa. Kwa hivyo, Halmashauri
Kuu ya Taifa imeungana na kauli ya Mwenyekiti wa CCM,
Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa aliyoitoa katika hotuba
yake ya ufungaji wa Mkutano Mkuu pale Chimwaga ambapo
aliutangaza uchaguzi mkuu wa Chama kuwa na mafanikio
makubwa. Kwa maneno yake Mwenyekiti, “mafanikio
hayo makubwa yameonyesha pia kuwa CCM si mali ya mtu,
ni mali ya watu, ambao ni wanachama.”
Halmashauri Kuu ya Taifa imeridhika pia kwamba mjadala
kuhusu rushwa ndani ya Chama ambao umekuwa ukikuzwa
sana na magazeti na vyombo vingine vya habari kwa kiasi
kikubwa ni mkakati tu wa wapinzani wa CCM kukichafulia
jina Chama wakati wakijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2005.
CCM inawataka wanachama wake na wananchi wote kwa jumla
wasimame kidete kufichua vitendo vya kweli vya rushwa
(siyo dhana tu), lakini wasikubali kuingizwa katika
mtego wa mikakati ya uchaguzi ya wapinzani.
Buriani
Mzee Ibrahim Raha Jongo
CCM
itakukumbuka daima
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mzee Ibrahim Raha
Jongo (66) amefariki dunia tarehe 29/8/2003 usiku mjini
Dar es Salaam.
|
|
|
Mzee
Jongo ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya Tumaini
ambako alikuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na afya
yake alizikwa tarehe 31/8/2003 kijijini kwake Chamazi,
katika Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Philip Mangula aliongoza maelfu
ya viongozi wa CCM, Serikali na wanachi kwenye mazishi
ya Mzee Jongo ambaye alizikwa kwa heshima zote za Chama.
Katika salaam zake za rambirambi kwa niaba ya Halmashauri
Kuu ya Taifa, wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla,
Ndugu Mangula aliusifu mchango wa marehemu kwa kutumia
kipaji chake cha usanii katika kukitetea na kukiimarisha
Chama.
Aidha, Katibu Mkuu wa CCM alimueleza marehemu kuwa alikuwa
mtu wa watu na ni mtu aliyetoa mchango mkubwa sana wakati
wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Serikali wa mwaka 1995
na 2000.
Marehemu alishika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya
CCM na katika Jumuiya ya CCM ya Wazazi.
Mzee Jongo alikuwa Mjumbe wa NEC tangu mwaka 1997 hadi
umauti wake ulipomfika.
|
|