Ilani ya CCM Habari Mpya Historia ya TANU na ASP Kutoka Magazetini Hotuba

 

 

 

 

 

 

 

 

 

JARIDA LA MKEREKETWA

Tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu Palestina
  • NEC yaunga mkono Wapalestina katika harakati zao za kujikomboa
  • Yataka Israel isimuhamishe Arafat nchini mwake
  • Na Jumuiya ya Kimataifa yatakiwa kusimamia utekelezaji wa Road-Map
 

Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi imesema kwamba imepokea kwa mshangao na masikitiko makubwa, uamuzi wa Serikali ya Israel wa kutaka kumuondoa kutoka nchini mwake Rais wa Palestina, Mheshimiwa Yassir Arafat.

Katika tamko lililotolewa hivi karibuni Mjiji Dodoma, NEC ambayo ilikutana chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin Mkapa imesema kwamba uamuzi huo wa fedheha una shabaha ya kuvuruga jitihada zinazoendelea sasa za kuleta amani kati ya Israel na Palestina na katika Mashariki ya Kati kwa jumla.
“Hii inathibitisha kwa mara nyingine tena jinsi ambavyo Serikali ya Israel isivyokuwa na dhamira ya dhati wala utashi wa kisiasa wa kupata ufumbuzi muafaka na wa kudumu wa mgogoro baina yao na Wapalestina”, tamko la NEC lilisema.
Aidha, uamuzi huo na matendo kadhaa ya kikatili yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina vinadhihirisha wazi nia mbaya ya Serikali ya Israel ya kutaka kukwamisha Mpango wa sasa wa amani Mashariki ya Kati, maarufu kwa jina la Road Map, Mpango ambao hatimaye ungewezesha kuzaliwa kwa Taifa la Wapalestina lililo huru, na linaloishi bega kwa bega na kwa amani na Taifa la Israel.

       
   
       
Kiongozi wa Palestine, Yasser Arafat akiongoza mkutano wa Kamati Kuu ya Chama cha PLO
(Palestine Liberation Organization)
 
   
Katika tamko lake NEC imeazimia kuwa: “Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi inapenda kuelezea kutokufurahishwa kwake na uamuzi huo, na kuulaani vikali. Kutekelezwa kwa uamuzi huo hakutaongeza usalama kwa Israel bali kutazidisha chuki na kuchochea ghasia zaidi. Hivyo basi, Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi inaitaka Serikali ya Israel kubadili uamuzi wake huo. Kimsingi Halmashauri Kuu ya Taifa inaisihi Serikali ya Israel kurudi kwenye mstari wa utekelezaji wa Mpango wa Amani wa sasa na Mkataba wa Oslo”.
“Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi inatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa na nchi za Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa zilizotayarisha Road Map kufanya kila linalowezekana kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wake”.
“Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi inapenda kukariri msimamo wake wa kuwaunga mkono watu wa Palestina katika harakati zao za kujikomboa na kupata Taifa lao lililo huru wanaloliendesha wenyewe”.