| |
Katika
kikao chake cha siku mbili kilichofanyika mjini Dar
es Salaam hivi karibuni chini ya Mwenyekiti wa CCM,
Rais Benjamin William Mkapa, Kamati Kuu ilizingatia
ujasiri wa Afro-Shiraz Party wa kuikomboa Zanzibar kutoka
katika makucha ya wakoloni wa Kiingereza na utawala
wa Masultani walowezi tarehe 12 Januari, 1964.
Wajumbe wa Kamati Kuu waliuthamini na kuuenzi mchango
mkubwa wa mashujaa wa Mapinduzi ya Zanzibar chini ya
uongozi thabiti wa Rais wa Chama cha Afro-Shiraz, Mzee
Abeid Amani Karume, ambao walijitoa mhanga wa maisha
yao kwa ajili ya uhuru wa kweli wa Wazanzibar na kuutokomeza
kabisa utawala mkongwe wa Kisultani.
Katika kikao chake hicho, Kamati Kuu ilitamka kwamba
Chama Cha Mapinduzi kina fahari kubwa kuona kwamba ASP
na hatimaye CCM baada ya kuungana na TANU imeweza kuyalinda,
kuyaendeleza na kuyadumisha Mapinduzi ya Zanzibar kwa
karibu miako 40 sasa na kuyawekea msingi imara wa kuyadumisha
milele.
Kutokana na ukweli huu, Kamati Kuu imesisitiza kwamba
kauli mbiu ya MAPINDUZI DAIMA iendelee kutumika kama
kielelezo cha dhamira ya kweli ya kuyadumisha mapinduzi
hayo na matunda yake ambayo kila Mzalendo wa kweli wa
Zanzibar na Tanzania nzima anapaswa kujivunia.
Aidha, Kamati Kuu ilitafakari pia ujasiri wa TANU na
ASP chini ya Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius
Nyerere na Jemedali Mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar wa
kuziunganisha nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar na
kuwa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Karibu miaka 40
sasa, Muungano wa Tanzania ndio mfano pekee Barani Afrika
wa mafanikio ya utekelezaji wa dhamira ya Waafrika kuungana
kikweli.
Kamati Kuu ina fahari kubwa kwamba vyama vya TANU na
ASP na hatimaye CCM vimeweza kudumisha Muungano wetu
kwa kipindi chote cha miaka 40 na kuujengea msingi imara
wa kudumu milele, licha ya juhudi zinazofanywa na maadui
wa Muungano za kutaka kuudhoofisha na kuusambaratisha
ambazo zimegonga ukuta.
Kwa kuzingatia na kuthamini mafanikio hayo makubwa na
kuwapa heshima wanayostahili waasisi wa Mapinduzi na
Muungano, Kamati Kuu ya CCM imezitaka Serikali zote
mbili za CCM ziandae sherehe kubwa za kuadhimisha miaka
40 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo tarehe 12 Januari,
2004 na miaka 40 ya Muungano wa Tanzania hapo tarehe
26 Aprili, 2004.
Kamati Kuu ya CCM inawataka wananchi wote bila kujali
tofauti zao za kisiasa kushiriki katika sherehe hizo
muhimu na kamwe wasikubali kurubuniwa na wezi wa fadhila
wanaotaka tarehe hizo muhimu katika historia ya nchi
yetu zisahaulike. |
|