Ilani ya CCM Habari Mpya Historia ya TANU na ASP Kutoka Magazetini Hotuba

 

 

 

 

 

 

 

 

 

JARIDA LA MKEREKETWA

“CCM ni Chama kinachotawala kwa uhakika, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar; kwa nini hatusijisifu na tunawaachia ukumbi wapinzani kutubeza?” - Mkapa
        Alipokuwa akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM uliofanyika Dodoma Septemba 13,2003, Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliwataka wanachama wa CCM kujisifu na kutembea kifua mbele kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2003, badala ya kuwaachia ukumbi wapinzani kutubeza.          
 

Kwa niaba ya Kamati Kuu, na wananchi wa Dodoma, nawakaribisheni nyote, Waheshimiwa Wajumbe, kwenye mkutano wetu huu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi – Chama kinachotawala kwa uhakika, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar!
Matarajio yangu ni kuwa nyote mmepokewa vizuri, mmepumzika vya kutosha, na sasa mko tayari kwa kazi kubwa na muhimu iliyo mbele yetu.
Sisi, kwenye Chama Cha Mapinduzi, tunao utaratibu mzuri wa kidemokrasia wa kuchambua matatizo na Sera, wa kuchuja wanaowania uongozi na uwezo wao wa kutekeleza Sera na maamuzi ya Chama. Ni heshima kubwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Tawala; lakini heshima hiyo tunaipata kwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi huru na wa haki. Pili, tunafanya vikao vyetu kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.
Vikao hivi, pamoja na mambo mengine, vinatoa fursa nzuri ya kufanya tathmini ya hali ilivyo ndani ya Chama, na nje ya Chama, kwa uwazi na ukweli. Tunafanya pia tathmini ya utendaji ndani ya Chama, na utendaji wa Serikali nje ya Chama. Kisha tunaeleweshana na kukubaliana ni kazi gani iliyo mbele yetu, na mipango ya kwenda kuitekeleza kazi hiyo ndani na nje ya Chama.
Mkutano huu unafanyika wakati ambapo tupo katikati ya kipindi tulichokabidhiwa kuongoza nchi kabla ya taifa kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwingine. Hivyo, tathmini yake lazima izingatie ukweli huo. Tunao wajibu wa kufanya tathmini ya kina zaidi, kwa lengo la kuanza kujiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani, na Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.
Hiki ni kipindi cha kubadili gia katika utendaji wetu, katika Chama na katika Serikali; ni kipindi cha kuchaji betri zetu kwa kazi kubwa inayokuja.
Sisi ni Chama makini, tena tumekabidhiwa na Watanzania wenzetu wajibu na dhamana kuongoza nchi. Hivyo, hatupaswi, na hatuwezi, kufanya mambo yetu kwa kubahatisha. Tunafanya kwa mipango, kwa ratiba, na kwa kuzingatia vipaumbele.
Na hapa tulipo, katikati ya kalenda yetu ya miaka 5 iliyopo kutoka uchaguzi mmoja hadi mwingine, ni wakati wa kurejea kwenye Ilani yetu, tuone tuliwaahidi nini wananchi mwaka 2000; tuone tumefika wapi katika utekelezaji wa ahadi hizo; tuone tumekwama wapi, kwa sababu gani; na tuone tunajiandaa vipi kukamilisha kazi hiyo kabla ya kurudi kwa wananchi.

       
         
       
       
“Swali langu ni lile lile: Kwa nini hatujisifu zaidi na tunawaachia ukumbi wapinzani kutubeza?” Mwenyekiti wa CCM, Rais Mkapa
awauliza Wajumbe wa NEC.
     
     
Wakati nikifunga Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, tarehe 31 Oktoba 2002, niliorodhesha mambo manne ambayo, kwa maoni yangu, tunapaswa kuyapa umuhimu wa pekee. Karibu mwaka umepita tangu wakati huo. Hivyo mniwie radhi niyarudie kwa ufupi, ili tuone tumefanya nini hadi leo kuyashughulikia.
La kwanza, ni kuwa sisi wenyewe, viongozi na wanachama wa CCM, tujitahidi kuelewa vizuri zaidi Sera zetu, Ilani yetu, na Mwelekeo wa Chama chetu. Kisha tujielimishe kuhusu kiwango cha mafanikio katika utekelezaji wake, na sababu za mapungufu pale yanapojitokeza, pamoja na mbinu za kushughulikia mapungufu hayo. Tukishaelewa, twende kwa wananchi kuwaeleza mambo haya, kwa uwazi na ukweli.
· La pili, ni kuwa lazima tukusanye nguvu za Chama na Serikali kusukuma utekelezaji wa Ilani. Kutimiza ahadi ni uungwana. Ni uungwana wetu ndio utawafanya wananchi waendelee kutuamini na kutukabidhi dola ya nchi hii. Na tuwakumbushe watumishi wa umma kuwa utekelezaji wa Ilaniya CCM si jambo la hiari, au la kuchagua; ni jambo la lazima na la haki.
· La tatu, ni kuwa tusionee haya ushindi wetu. CCM ilishinda, kwa uhakika na kwa haki, kwa hiyo haina sababu ya kusitasita kwenye kudai Ilani yake itekelezwe, na kwenye kuhamasisha umma wa Watanzania uliotuweka madarakani ushiriki kazi za maendeleo yao binafsi, na ya taifa lao.
· La nne, ni kuhakikisha tunaendelea kuwa wamoja ndani ya Chama. Migawanyiko, kwa sababu yoyote ile, au kisingizio chochote kile, ni sumu kubwa. Tusiiachie upenyo, na tusikubali wengine watengeneze ufa wa kupitishia sumu yao ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Nasema, mwaka karibu unakwisha tangu nitoe orodha hiyo. Je, tumefanya nini? Tufanye tathmini.
Lakini tathmini tutakayoifanya isiwe ya kulaumiana tu – Chama kuilaumu Serikali, wala Serikali kukilaumu Chama. Tunataka tathmini inayotambua, na kuzingatia, kuwa CCM na Serikali zake zote mbili, ni kitu kimoja. Tuelekeapo 2004 na 2005, nataka tuelewane kuhusu jambo hili. CCM na Serikali zake ni watu wamoja, wenye lengo moja, ila majukumbu mbalimbali.
Kama kweli sisi ni wamoja, tutashirikiana na tutaendelea kupendwa na wananchi kwa umoja wetu. Lakini tukishindwa kuonyesha umoja huo, tutadharauliwa na kupuuzwa kwa kushindwa kutimiza matarajio ya wananchi kwetu.
Tukiwa peke yetu, kama hivi leo, tuna wajibu wa kuulizana, kwa uwazi na ukweli, kwamba mbona wewe hujafanya hili, au wewe mbona hujasema lile. Lakini tutawapa wananchi matumaini zaidi tukionekana wazi mbele yao kuwa tu wamoja – Serikali ya CCM, na CCM yenye Serikali. Chama kina wajibu wa kufafanua na kutetea kazi za Serikali; na Serikali nayo ina wajibu wa kufafanua na kutetea nafasi na malengo ya Chama katika uongozi wa nchi yetu.
Kutoka kwenye Chama, Serikali imepewa Ilani na Mwelekeo. Hili nalo napenda nilisisitize. Serikali yetu haina dira nyingine nje ya dira tunayopewa na Chama Cha Mapinduzi. Nasema hivyo kwa maana, nikiwa nimevaa kofia yangu ya Urais, siwezi kukubali lawana kwa kazi ambayo Serikali inaifanya katika kutekeleza Ilani na Mwelekeo. Kama wapo miongoni mwetu, na kwenye uongozi wa Chama katika ngazi zake zote, ambaye amesahau kazi na malengo tuliyopewa na Chama, kupitia Ilani na Mwelekeo, basi namwomba akasome tena miongozo yetu hiyo ya kazi za Serikali.
Narudia. Serikali haina mwongo-zo wake au dira yake tofauti na Ilani na Mwelekeo. Kazi yetu ni moja tu: kutekeleza. Tukikwama tutakuja kusema hapa, na kueleza kwa nini. Lakini pale tunapotekeleza mliyotutuma msitu-funge kamba. Na kwa kweli tunatazamia kuwa mtakuwa mstari wa mbele kuwaelezea wananchi, na wana CCM wengine, kuwa hivyo ndivyo hasa mlivyoituma Serikali kwenda kufanya. Tunayo haki pia kutarajia Chama kiwe mwangwi wa kueneza pembe zote sifa nzuri, na utendaji mzuri, wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Kazi mliyotutuma ni yenu. Tukiifanya vizuri sifa ni kwa Chama.
Na sasa nikivaa kofia yangu ya Mwenyekiti wa Chama, ninamhimiza kila kiongozi wa CCM, kuanzia tuliomo humu ndani, na wengine wote, tuone ni wajibu wetu wa msingi kukumbuka kila mara Ilani inasema nini, na Mwelekeo unasema nini, na kisha kufuatilia kwa makini utendaji wa Serikali.
Tunahitaji kujituma zaidi ili kuelewa, kutetea na kutangaza mafanikio ya Serikali zetu mbili; ndani ya Chama na nje ya Chama. Kwenye Mkutano Mkuu uliopita Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kila moja ilitoa taarifa yake ya utendaji. Mkutano Mkuu ukakasimu kwetu kazi ya kuchambua na kujadili taarifa hizo, ili hatimaye zitumike kujenga hoja kwa wananchi kwa nini tunastahili kuendelea kukabidhiwa uongozi wa nchi hii.
Naomba mkazisome tena taarifa hizo ili mjiridhishe wenyewe na kazi tuliyoifanya. Mafanikio hayo, na mengine ambayo yametajwa kwenye Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichopita, sambamba na kwenye Kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar, yanatosha kabisa kutufanya tutembee kifua mbele tunapoelekea 2004 na 2005.
   
       
       
     
Lakini badala yake unasikia zaidi kelele za wapinzani, badala ya nyimbo za ushindi za Chama Cha Mapinduzi. Tunawaachia nafasi wapinzani kujaribu kupuuza, au kukebehi, rekodi ya usahihi wa Sera, na umakini wa utekelezaji. Hili si sahihi, na lazima tujirekebishe tuelekeapo kwenye uchaguzi. Tusikubali wapinzani wajipe nafasi wasiyostahili, nafasi kubwa kuliko yetu katika majukwaa ya kisiasa.
Maana, siasa ni mapambano ya kudumu ya kuvutia nyoyo na fikra za wananchi, wapiga kura. Kamwe tusisahau jambo hili. Kutetea rekodi yetu ni silaha katika uchaguzi ujao. Na kuelewa na kisha kueleza tunafanya nini, kwa namna gani, na mipango ijayo ikoje, nayo ni silaha. Kwenye siasa tusione haya kujisifu, na wala tusingoje tu kila mara wengine nje ya nchi ndio watusifu kama ilivyo sasa.
· Uchumi wa taifa umekua kutoka ongezeko la asilimia 3.3 kwa mwaka 1997 hadi asilimia 6.2 mwaka jana; kwa nini tusijisifu?
· Wastani wa kukua kwa uchumi barani Afrika katika miaka 3 iliyopita ni asilimia 3.4 kwa mwaka. Wastani wetu sisi Tanzania kwa miaka hiyo 3 ni asilimia 5.6; kwa nini tusijisifu?
· Mfumuko wa bei ulifika chini ya asilimia 10 mwaka 1999, na tangu wakati huo unaendelea kushuka kila mwaka, hadi kufikia chini ya asilimia 5 hivi sasa; kwa nini tusijisifu?
· Hivi leo tunayo akiba ya fedha za kigeni kuliko wakati wowote tangu tuwe taifa huru; kwa nini tusijisifu?
· Hivi leo washirika wetu katika maendeleo, yaani wahisani, wana imani na Serikali yetu pengine kuliko katika miaka mingi iliyopita. Wengi sasa wanaanza kupitishia misaada yao moja kwa moja kwenye bajeti ya Serikali wakiwa na uhakika kuwa hazitatumiwa isivyopaswa. Aidha, wengi wao wametuhakikishia fedha hadi 2005. Kwa nini tusijivune kwa kuaminiwa kiasi hicho?
· Hivi leo wawekezaji kutoka nje wanatuamini kuliko miaka iliyopita, na ndio maana wanaendelea kuwekeza katika nchi yetu ambayo ni miongoni mwa nchi zinazoongoza barani Afrika kwa kuvutia mitaji. Sasa kwa nini tusijisifu?
· Nchi chache sana hadi sasa zimepewa
msamaha wa madeni kwa nchi maskini sana. Tanzania ni mojajwapo, kwa vile tunaaminika kuwa tuko makini kupiga vita umaskini, na kuepuka madeni makubwa mno siku zijazo. Sasa kwa nini tusijisifu?
· Mapato ya Serikali yameongezeka mara nne katika miaka 7 iliyopita. Ndio maana tumeweza kufuta kodi za kezo kwa wananchi, ndio maana kasi ya kujenga barabara na madaraja imeongezeka, na ndio maana mishahara imeongezwa. Sasa kwa nini tunaogopa kujisifu?
· Mwaka jana sekta ya kilimo ilikuwa kwa asilimia 5; sekta ya madini kwa asilimia 15; sekta ya utalii kwa asilimia 9.3; sekta ya viwanda kwa asilimia 8; sekta ya ujenzi kwa asilimia 11; sekta ya mawasiliano na uchukuzi kwa asilimia 6.4; sekta ya fedha kwa asilimia 4.8; na nyingine nyingi zimeongezeka. Sasa kwa nini tusijisifu?
· Mauzo ya nje yameongezeka kutoka USD 543.3 mwaka 1999 hadi USD 902.5 mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 66 kwa miaka 3 tu. Sasa kwa nini hatujisifu?
· Tumeongeza bajeti ya elimu kwa asilimia 151.6 katika miaka 3 iliyopita. Uandikishaji watoto kwenye shule za awali umeongezeka kwa asilimia 87 kwa mwaka mmoja tu uliopita. Uandikishaji watoto darasa la kwanza umefikia asilimia 98.6 ya watoto wa rika la elimu ya msingi mwaka 2002, na walioko shuleni ni asilimia 80.7. Mwaka huu, 2003, kulikuwa na ongezeko la asilimia 23 katika kuandikisha watoto darasa la kwanza. Mwaka jana tumeongeza idadi ya shule za msingi za Serikali kwa asilimia 4.8, na walimu kwa asilimia 5.8. Wanafunzi wanaoingia katika Shule za Sekondari waliongezeka kwa asilimia 11.6 mwaka jana, na idadi ya walimu wa sekondari iliongezeka kwa asilimia 10. Kwa nini hatujisifu vya kutosha?
Ningeweza kuendelea, na kuendelea, na kuendelea, kutaja mafanikio, Bara na Visiwani. Lakini nawaachia Mawaziri wa Serikali zetu mbili ambao watatoa maelezo zaidi. Swali langu ni lile lile: kwa nini hatujisifu zaidi, na tunawaachia ukumbi wapinzani?
Sisemi vita dhidi ya umaskini imekwisha. Ninachosema ni kuwa takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa tuko katika njia sahihi; kilichobaki ni kuongeza kasi, maana tuna uhakika wa tuendako, na tuna uhakika wa njia ya kupita.
   
     
   
Daraja la Mto Rufiji ambalo sasa linaitwa la DARAJA LA MKAPA ni moja ya miradi mikubwa iliyokamilika ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
 
     
Ni muhimu pia katika kufanya tathmini ya utendaji wetu kuzingatia mazingira tunayofanyia kazi, ndani na nje ya nchi. Sisi wana-CCM, ambao ndio wenye Serikali, lazima tuelewe jambo hili, tulizingatie na kisha kuwaelimisha wengine. Bei ya kahawa au pamba inapoanguka kwenye soko la dunia si kwa sababu ya CCM. Kauli ya nchi maskini kama zetu ni ndogo sana, na ni kama vile haipo kabisa, katika kupanga bei ya mazao kwenye soko la dunia. Na siamini kipo chama kingine cha siasa nchini hapa chenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja ya mfumo wa haki zaidi wa biashara duniani kuliko CCM. Tutafanya hivyo pia kule Cancun, Mexico, ambako Mkutano wa Mawaziri wa Biashara Duniani unaendelea hivi sasa. Kwa kushirikiana na nchi nyingine zinazoendelea tutajenga hoja. Tatizo si kujenga hoja. Tatizo ni utashi wa kisiasa wa wakubwa waliobuni na wanaofaidi mfumo uliopo sasa.
Wapo watu wanaofanya mzaha na utandawazi. Wanasema huyu Mkapa naye kazidi na mambo yake ya utandawazi. Lakini hili si jambo la mzaha hata kidogo. Utandawazi umeweka mbele yetu fursa, na umeweka pia mbele yetu hatari kubwa. Kazi yetu ni kupanua uwanja wa fursa, na kuupunguza ule wa hatari. Si kazi rahisi; lakini lazima tuifanye. Tuendelee kulaani na kupinga mfumo wa utandawazi ambao si wa haki. Lakini, penye fursa, kama za AGOA zinazotuwezesha kuuza bidhaa zetu nchini Marekani kwa upendeleo maalum utolewao na nchi hiyo kwa nchi za Kiafrika, na EBA itoayo fursa kama hizo hizo za upendeleo tunapouza barani Ulaya, tuzitumie kwa ukamilifu fursa hizo. Ukweli ni kuwa hivi sasa hatuzitumii vya kutosha fursa hizo. Tunaona ni rahisi zaidi kulalamika tu. Lazima tubadilike.
Mwisho, napenda, kama nilivyofanya kwenye kufunga Mkutano Mkuu mwaka jana, nizungumzie umuhimu wa kupanga matumizi ya Chama kulingana na mapato yetu. Hii ni hekima ya kawaida tu. Tushone koti letu kulingana na kitambaa kilichopo. La sivyo tufanye bidii kupata kitambaa zaidi. Nilisema Oktoba mwaka jana, na leo narudia changamoto hizi mbili.
· Kwanza, tuhakikishe kwamba kinakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato yetu wenyewe ili kujinusuru na hatari ya kuishi kwa utegemezi, au kuwa Chama cha matajiri peke yao; na
· Pili, tupunguze matumizi, ikiwemo kwa kupitia tena muundo wa mfumo wa Chama chetu; lakini bila kuathiri ulazima wa kisiasa na kijamii wa kujenga utaifa, uzalendo, na umoja.
Nimezungumza vya kutosha. Inapasa tuendelee na kikao. Nimalizie kwa kuwakumbusha nilivyosema mwanzo: Tufanye tathmini na tusione haya kujisifu. Na kisha, tujue tumekuja kuchaji betri zetu kwa kazi kubwa iliyo mbele yetu.
Mwanafalsafa mmoja (Friedrich Nietzsche) aliwahi kusema, “Ukipoteza lengo, umepoteza njia.” Na bila shaka ukipotea njia huwezi kufika unakokusudia. Katika kuchaji betri zetu, tukumbushane lengo letu la msingi, nalo ni kushika dola. Lolote tufanyalo, mmoja mmoja na kwa ujumla wetu, tusisahau lengo kuu hilo: Kushika Dola!!