|
|
| JARIDA
LA MKEREKETWA
|
Tumeachana
na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea? La hasha |
| |
[Na
Omar R. Mapuri] |
|
|
| |
Tokea
mwanzoni mwa miaka ya tisini, Tanzania imo katika mageuzi
makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo yanakwenda
sambamba. Mageuzi ya kisiasa yametuingiza katika mfumo
wa vyama vingi vya siasa baada ya zaidi ya miaka 40
ya mfumo wa chama kimoja. Mageuzi ya kiuchumi yametutoa
katika uchumi hodhi uliokuwa ukimilikiwa na dola na
kutuingiza katika mfumo wa uchumi wa soko unaotoa nafasi
ya ushiriki wa sekta ya binafsi. Mageuzi ya kijamii
ni pamoja na kupanuka kwa uhuru wa vyombo vya habari
pamoja na mambo mengine mengi ambayo aghlabu ni matokeo
ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa.
Kama ilivyo kawaida ya mageuzi, mageuzi haya makubwa
na mengi yanayokwenda sambamba yamewa-fadhaisha na hata
kuwababaisha wananchi wengi wakiwemo
wana CCM. Ilivyokuwa mageuzi hayo yameletwa, yanaendeshwa
na kusimamiwa na CCM, wapo wana CCM wanaojiuliza kama
CCM imeachana na sera zake za msingi, hasa Siasa ya
Ujamaa na Kujitegemea na dira ya utekelezaji wake ambayo
ni Azimio la Arusha. Wapo pia wanachama wa CCM wachache,
wakiwemo hata viongozi, ambao hawajiulizi tena, bali
wanaamini hasa kwamba CCM imekwishaachana na sera zake.
Katika nyakati fulani wapo hata viongozi wa CCM waliosikika
wakitoa kauli kama vile: “tulipokuwa tukijenga
ujamaa ….” au “enzi zile za Azimio
la Arusha ….” kama vile ujenzi wa ujamaa
haupo tena au enzi za Azimio la Arusha zimekwisha. Yupo
hata kiongozi mkubwa wa CCM aliyewahi kutamka mwanzoni
mwa vuguvugu la mageuzi kwamba eti CCM haina dira. Aidha,
wapo wasomi wanaojaribu kuonyesha kwamba CCM imeachana
na ujamaa na kwamba sasa inaendesha sera wanazoziita
za kiliberali. Zaidi ya yote, vipo hata vyama vya upinzani
vilivyodiriki kujinasibu kwamba eti vyenyewe ndivyo
sasa vyenye sera za ujamaa eti kuziba pengo lililoachwa
na CCM iliyoutelekeza ujamaa.
|
|
| |
|
|
|
|
|
|
|
|
| |
|
|
|
“Siasa
ya Ujama na Kujitegemea ipo pale pale,” Katibu
Mwenezi wa CCM Taifa, Ndg. Omar R. Mapuri akiwaeleza
waandishi wa habari hivi karibuni |
|
|
|
|
|
Katika
makala haya tutajaribu kusahihisha dhana hizo ambazo
tunaamini kwa kiasi kikubwa ni matokeo tu ya ubabaikaji
uliosababishwa na mageuzi. Tutajitahidi kuonyesha
kwamba CCM haijaachana na siasa yake ya Ujamaa na
Kujitegemea, bali ambacho kimekuwa kikibadilika kulingana
na wakati na mazingira, ni mikakati tu ya kufikia
lengo hilo kuu la muda mrefu.
UCHANGANUZI WA MANENO
”FALSAFA”, “IMANI”, “SIASA”,
“SERA”, “ILANI” n.k.
Kabla ya kuitazama kwa undani siasa ya Ujamaa na Kujitegemea,
inafaa kwanza kuchanganua maneno ya “falsafa”,
“imani”, “siasa”, “itikadi”,
“sera”, “maamuzi” na “ilani”
ambayo yanatumika sana katika kuielezea dhana nzima
ya ujamaa na kujitegemea katika mikutadha mbali mbali.
Falsafa:
Falsafa inayosarifu dhana na nadharia za Chama Cha
Mapinduzi, na nchi nzima kwa jumla ni usawa wa binadamu
na mtu kuthaminiwa kwa utu wake. Falsafa hii inabeba
dhana za uhuru, demokrasia, haki, udugu na amani.
Falsafa hii inaashiriwa katika Ahadi ya Kwanza ya
Mwanachama wa CCM isemayo: “Binadamu wote ni
ndugu zangu na Afrika ni moja”. Falsafa hii
ndiyo pia iliyoweka misingi ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar. Katika Utangulizi
wa Katiba zote mbili unapata maneno yafuatayo: “…
tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu
jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu
na amani.” Pia Katiba hizo zinaendelea: “….
Misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye
demokrasia …” Ibara ya 12 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikuvunga vunga maneno
katika kuibainisha falsafa hii ya msingi. Ibara hiyo
inasomeka kama ifuatavyo:-
“12. - (1) Binadamu wote huzaliwa huru, na wote
ni sawa.
(2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake.
Ibara ya 11 ya Katiba ya Zanzibar ina maneno hayo
hayo.
Inathibitika kwa hivyo kwamba falsafa hii si ya CCM
peke yake, bali ni ya nchi nzima. Hatujapata kusikia
chama hata kimoja cha siasa kinachoipinga falsafa
hii.
Imani/Siasa/Itikadi:
Ni imani ya CCM kwamba ujamaa na kujitegemea ndiyo
njia pekee ya kujenga nchi ya watu walio sawa, huru
na wanaoheshimiana. Kwa hivyo, hiyo ndiyo siasa au
itikadi ya msingi ya CCM. Ibara ya 4 ya Katiba ya
CCM inaweka bayana imani ya CCM kama ifuatavyo:-
4. CCM kinaamini kwamba:
(1) Binadamu wote ni sawa
(2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake.
(3) Ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga
jamii ya watu walio sawa na huru
Kwa upande wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
sehemu ya Utangulizi imeelezea madhumuni ya kutungwa
kwa Katiba hiyo kuwa ni kujenga jamii yenye demokrasia
na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa
na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na
ujamaa. Maneno kama hayo yamerejewa pia katika Katiba
ya Zanzibar.
Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inaitangaza rasmi Tanzania kuwa ni nchi ya
kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Ibara ya 8(1) ya Katiba ya
Zanzibar nayo imeitangaza hivyo hivyo Zanzibar isipokuwa
tu imetumia maneno “haki za kijamii” badala
ya neno “ujamaa”. Hata hivyo madhumuni
ni yale yale.
Tukizilinganisha Katiba za nchi na ile ya CCM katika
muktadha wa siasa ya ujamaa na kujitegemea, inadhihirika
kwamba neno “kujitegemea” halikutumika
katika Katiba za nchi. Tafsiri yetu ya tofauti hiyo
ni kwamba katika siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ncha
ya ujamaa ni ya nchi nzima lakini ncha ya kujitegemea
inatoa fursa kwa vyama vya siasa kutofautiana kwa
sera. Ingawa kuna vyama vya upinzani ambavyo husikika
vikitaka kipengele cha Ujamaa kiondoshwe katika Katiba
ya nchi, lakini ukizitazama kwa undani sera za vyama
hivyo, utagundua kwamba zimejengwa juu ya msingi huo
huo wa ujamaa. Na vipo vyama ambavyo hujinasibu kwa
wananchi kwamba eti ndivyo vyenye uwezo mkubwa zaidi
wa kuzitekeleza sera za CCM kuliko CCM yenyewe. Vyama
kama hivyo vinakiri usahihi wa siasa ya Ujamaa lakini
vinadai kuwa eti CCM haina uwezo wa kuitekeleza. Lakini
zaidi ya yote, hatujapata kusikia chama cho chote
cha siasa nchini Tanzania kinachojitambulisha na ubepari.
Sera na Dira:
Baada ya kubainisha siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea
iliyojengwa juu ya msingi wa falsafa ya usawa wa binadamu
na mtu kuthaminiwa kwa utu wake, TANU mnamo mwaka
wa 1967 ilipitisha Azimio la Arusha lililoandaa mazingira
na kuweka dira ya utekelezaji wa siasa hiyo. Sera
ni mkakati wa utekelezaji wa siasa kwa kipindi fulani
kulingana na uchambuzi wa dira uliofanywa kwa ajili
ya kipindi hicho. Sera huweza kubadilika kulingana
na mahitaji ya wakati. Kwa hivyo, wakati siasa ya
Ujamaa na Kujitegemea ni ya kudumu na Azimio la Arusha
kama dira yake ya utekelezaji nalo ni la kudumu kwa
kiasi fulani, sera na mikakati ya utekelezaji huweza
kubadilika kila baada ya muda, kulingana na mabadiliko
ya mahitaji ya wakati. Na kweli uzoefu katika TANU
na ASP na baadaye CCM unaonyesha kwamba baada ya kila
kipindi cha wastani wa miaka 10, Chama kimekuwa kikitathmini
utekelezaji wa siasa ya Chama na kuzitazama upya sera
zake za msingi kwa lengo la kuzifanya zikidhi mahitaji
ya wakati. Baada ya kufanya mapitio hayo Chama huja
ama na mwongozo unaojikita katika ufafanuzi na kuyawekea
mkazo maeneo fulani au huja na sera mpya kabisa, lakini
lengo kuu likiwa ni lile lile la kutekeleza siasa
ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kuzingatia misingi ya
Azimio la Arusha. Ndiyo maana katika kipindi cha toka
1971 hadi sasa, CCM imetoa nyaraka nne zifuatazo za
kisera za msingi:-
(1) Mwongozo wa TANU wa 1971 ambao
ulijenga hamasa ya utekelezaji wa Azimio la Arusha.
(2) Mwongozo wa CCM wa 1981 ambao
ulijielekeza katika kukabiliana na mmong’onyoko
wa maadili uliokuwa unasababishwa na hali ngumu ya
uchumi iliyochangiwa na vita vya nduli Idi Amin.
(3) Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya
Tisini uliozingatia haja ya kujihami na taathira
za upepo wa mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa
uliokuwa ukivuma Duniani na kuziangusha dola kubwa
za kijamaa za Ulaya ya Mashariki likiwemo la Urusi
yenyewe ya Kisovieti.
(4) Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya
2000-2010 unaozingatia zaidi suala la matumizi
ya teknolojia (modenaizesheni) katika ujenzi wa uchumi
wa kisasa.
Kwa jumla, chimbuko
la sera zote za CCM ni Azimio la Arusha na zinapoandaliwa,
yanazingatiwa pia malengo na madhumuni ya CCM yaliyobainishwa
katika ibara ya 5 ya Katiba ya CCM.
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere katika “Kujitawala
ni Kujitegemea” aliyaelezea ifuatavyo mahusiano
baina ya Azimio la Arusha na Sera za Chama:-
Azimio la Arusha ndilo
linaloeleza itikadi ya chama chetu. Ndiyo kauli kuu
ya lengo letu na misingi yetu; ndilo msingi wa maamuzi
yote ya sera za Chama na Serikali.
Aidha Mwalimu alitambua haja ya kupitia upya sera kila
mara na kurekebisha Azimio. Alisema tena katika “Kujitawala
ni Kujitegemea:-
Kila miaka inavyopita,
kauli yo yote muhimu kupitiwa mara kwa mara kuona kama
misingi yake bado inahitajiwa katika mazingira mapya
… Hata mimi nakubali kwamba (Azimio la Arusha)
linahitaji marekebisho.
Maneno hayo yanatosha kuwasuta
wale wanaodai kwamba eti Mwalimu hakutaka mabadiliko
ya Azimio na Sera.
Maamuzi:
Ndani ya utekelezaji wa sera ya msingi, Chama huweza
kupitisha maamuzi yenye lengo la kutoa msukumo wa utekelezaji
wa jambo fulani mahsusi au kukabili tatizo fulani la
utekelezaji. Ni kwa msingi huo ndio TANU na baadaye
CCM ilipitisha maamuzi mengi yakiwemo yafuatayo:-
(1) Siasa ni kilimo (Azimio la Iringa) (1972) kwa lengo
la kutoa msukumo katika suala zima la kilimo.
(2) Mpango wa Elimu kwa Wote (UPE) (Azimio la Musoma),
(1974) uliotoa msukumo wa kuharakisha kufikisha elimu
kwa wote ikiwa ni pamoja na suala la elimu ya watu wazima.
(3) Mtu ni Afya (1976): Kutoa msukumo kwa sera ya kinga
kuliko tiba.
(4) Mpango wa Kujihami Kiuchumi (1980/81) ili kukabiliana
na hali ngumu ya uchumi wa nchi.
(5) Maamuzi ya Zanzibar (1991) ambayo yaliwaondolea
wanachama wa kawaida wa CCM masharti ya uongozi yaliyoainishwa
katika Azimio la Arusha. Maamuzi hayo yalikuwa na lengo
la kuwawezesha wanachama wa CCM kushiriki katika harakati
za kiuchumi katika mazingira mapya yaliyokuwa yanaingia
ya uchumi wa soko. Masharti ya uongozi yalibaki kwa
viongozi tu kama ilivyokuwa imekusudiwa katika Azimio
la Arusha.
Ilani:
Kama ilivyokwishabainishwa, sera za msingi huchukua
upeo wa muda mrefu kidogo, na kwa uzoefu wa CCM, ni
kama miaka 10 hivi. Ndani ya kipindi hicho, Chama huchambua
sera na kujipangia malengo ya utekelezaji kwa vipindi
vifupi vifupi, aghlabu vya miaka mitano mitano. Hapo
ndipo tunapopata ilani za uchaguzi ambazo huwasilishwa
kwa wananchi kwa ajili ya kuombea kura katika chaguzi
za dola ambazo hufanywa kila baada ya miaka mitano.
Baada ya uchanganuzi huo wa maneno “falsafa”,
“siasa”, “itikadi” “sera”,
“maamuzi” na “ilani” kama yanavyotumika
katika msamiati wa CCM, imedhihirika kwamba falsafa
na siasa ni vitu vya kudumu, au ni malengo ya muda mrefu,
lakini sera, maamuzi na ilani ni vitu vinavyobadilika
kila baada ya muda. Na hapa ndipo penye siri ya mafanikio
ya CCM. Ingawa CCM ni chama kikongwe, lakini kila baada
ya muda hujirekebisha kwa mujibu wa mazingira ya wakati,
lakini bila ya kupoteza lengo. Kwa ufupi, CCM inafuata
kanuni ya mwezi ambao katika mzunguko wake huanza na
uchanga (ukiwa na umbo la hilali), ukafikia upevu (ukiwa
na umbo la sahani) na kurejea tena uchanga ambapo unakuwa
tunu tena. Ni kutokana na kanuni hiyo ndiyo maana wananchi
hawaichoki CCM pamoja na ukongwe wake, kwani wakati
wote inawaletea matumaini mapya.
UJAMAA NA KUJITEGEMEA
KAMA SIASA YA CHAMA:
Kama siasa ya Chama, Ujamaa na Kujitegemea ni lengo
la kudumu. Ni kwa msingi huo ndiyo tunasema kwamba Chama
Cha Mapinduzi bado kabisa hakijaachana na siasa hiyo.
Katiba na sera za CCM zinabainisha wazi wazi msimamo
huo kama ilivyokwishaelezewa. Baada ya kuuelewa msimamo
huo, ni muhimu pia kuelewa tunapozungumzia Ujamaa na
Kujitegemea tunakusudia nini. Tutajaribu kwa kutumia
lugha nyepesi kabisa, kutoa ufafanuzi huo katika sehemu
hii ya makala haya. Kama inavyojieleza yenyewe, siasa
ya Ujamaa na Kujitegemea ina ncha mbili, yaani ya Ujamaa
na ile ya Kujitegemea. Katika Azimio la Arusha, umefanywa
uchanganuzi wa kina ambapo Sehemu ya Pili ya Azimio
hilo inachambua Siasa ya Ujamaa na Sehemu ya Tatu inachambua
Siasa ya Kujitegemea. Kwa maneno mengine siasa yetu
hii ni siasa mbili ndani ya moja. Nasi kwa ufupi kabisa
tutafanya uchanganuzi kama huo.
Siasa ya Ujamaa:
Siasa ya Ujamaa imechambuliwa na wanafalsafa wengi wakubwa
waDunia hii wakiongozwa na Karl Marx na Vladmir Lenin.
Pia imechambuliwa kwa kina na Mwalimu Julius K. Nyerere
kwa mazingira ya Tanzania katika vitabu vyake mbali
mbali, ambapo majumuisho yake yaliwekwa katika Azimio
la Arusha. Sisi katika makala haya hatukusudii kurejea
uchambuzi wa kifalsafa bali tu tunajaribu kumwelezea
mwananchi wa kawaida maana pana na nyepesi inayokusudiwa
katika Siasa ya Ujamaa. Kwetu sisi Ujamaa maana yake
ni kugawana utajiri wa nchi kwa usawa na kwa haki katika
misingi ya kuheshimiana. Jitihada zetu za kiutekelezaji
katika kufikia lengo hilo kama zinavyoongozwa na Azimio
la Arusha zimekuwa zikichukua sura za kusambaza huduma
za jamii (elimu, afya, maji n.k.) kwa wote, kujenga
misingi ya fursa sawa za kujiendeleza, kuondoa unyonyaji,
kupiga vita kila aina ya ubaguzi na dharau, kuwatetea
wanyonge na kuwasaidia kujikwamua na kadhalika. Uamuzi
wa kuanzisha vijiji vya ujamaa katika miaka ya sabini
ulikuwa na lengo la kurahisisha utekelezaji wa juhudi
hizi. Pamoja na matatizo ya hapa na pale ya utekelezaji,
tunaamini Watanzania walio wengi hasa wanyonge, bado
wanapenda kufikiwa kwa malengo hayo. Ndiyo maana tunasema
Siasa ya Ujamaa ni ya kudumu.
Kugawana au kusambaza kwa wote utajiri wa nchi (si kwa
kugawana fedha bali kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma
za kijamii kwa wote) ni sura moja tu ya Ujamaa. Lakini
pia kuna sura ya pili ambayo ni ya kuuchuma huo utajiri
wenyewe wa kugawana. Katika Azimio la Arusha, unafafanuliwa
utaratibu wa kuchuma utajiri bila ya kunyonyana. Mkakati
uliowekwa ni wa njia kuu za uchumi wa nchi kuwekwa chini
ya wakulima na wafanyakazi kupitia vyombo vya Serikali
Siasa ya Kujitegemea:
Siasa ya Kujitegemea imechambuliwa kwa kina katika Sehemu
ya Tatu ya Azimio la Arusha. Siasa hii inajikita katika
kuleta maendeleo ya kweli ya nchi na ya wananchi wenyewe
hasa wanyonge. Hoja inajengwa kwamba huwezi kuzungumzia
maendeleo ya kweli kama maendeleo hayo ni ya vitu tu
na si ya watu wenyewe na kama maendeleo hayo yamejengwa
juu ya msingi wa utegemezi wa fadhila za nje. Inasisitizwa
kwamba fedha si msingi wa maendeleo bali ni matokeo
ya maendeleo. Kwa hivyo mkakati unaotiliwa mkazo ni
wa kujituma katika kujiletea maendeleo bila ya kusubiri
fedha kwanza au misaada na mikopo kutoka nje. Vitu hivyo
kama vitapatikana vije tu kusaidia juhudi zetu za kujitegemea
na kamwe visiruhusiwe kuhatarisha uhuru wetu.
Kwa mnasaba huo, Siasa ya Kujitegemea inasisitiza kwamba:
Maendeleo ya nchi huletwa na watu, hayaletwi na fedha.
Fedha ni matokeo siyo msingi wa maendeleo. Ili tuendelee
twahitaji vitu vinne: (i) Watu; (ii) Ardhi; (iii) Siasa
safi na (iv) Uongozi bora. Kwa kuzingatia ukweli kwamba
nchi yetu ina watu wengi na eneo kubwa la ardhi, mkakati
wa siasa ya kujitegemea unabainisha kwamba maendeleo
yataletwa na kilimo na hivyo pia unamjali zaidi mkulima
vijijini.
Siasa ya Kujitegemea imebainisha masharti mawili ya
maendeleo. Masharti hayo ni Juhudi na Maarifa. Juhudi
inaashiria kufanya kazi kwa kujituma na Maarifa ni kiashirio
cha matumizi ya utaalamu na teknolojia kwa lengo la
kuziongezea tija juhudi.
Kwa jumla, mtu hahitaji utafiti wa kina kubaini kwamba
karibu yote yaliyoelezewa kuhusiana na Siasa ya Kujitegemea
yalikuwa na ukweli mwaka 1967 na bado yana ukweli hadi
leo. Aidha, yote hayo yanaendelea kupendwa na Watanzania
waliowengi ambao siyo tu wameyakubali, bali pia wanajitahidi
kuyatekeleza. Kwa mfano Watanzania pamoja na unyonge
wao, hawakubali kuonewa wala kunyanyaswa. Pia, Watanzania
wamejiletea maendeleo mengi (shule, zahanati, visima,
njia, maji n.k.) kwa kujitegemea bila ya kusubiri fedha.
Na zaidi ya yote, Watanzania wanajituma kwa bidii kubwa.
Kwa kuzingatia ukweli huo, mtu hapaswi kupata taabu
sana kuelewa kwa nini Siasa ya Kujitegemea inaendelea
kuwa siasa ya CCM.
Kama ilivyo katika siasa ya ujamaa, bila shaka yamejitokeza
hapa na pale matatizo ya kiutekelezaji. Yapo matatizo
yaliyo nje ya uwezo wetu kama vile matatizo ya kiuchumi
ya dunia ambayo yalipotukumba na sisi yaliathiri utekelezaji
wetu. Lakini pia yapo matatizo yaliyotokana na kasoro
zetu wenyewe kama vile kuweka mkazo mdogo katika maarifa
na badala yake kukazania tu juhudi ambapo matokeo yake
yamekuwa ni tija ndogo katika uzalishaji hasa katika
kilimo. Maeneo kama haya ya matatizo na kasoro ndiyo
yanayotoa fursa ya kuzipitia upya baadhi ya sera za
Chama kama tutakavyobainisha baadaye.
Mwandishi wa Makala hii ni Katibu Mwenezi wa CCM Taifa,
Ndugu Omar R. Mapuri ambaye katika toleo lijalo la jarida
hili atamalizia Makala yake kwa kueleza juu ya:-
Baadhi ya maeneo yaliyohitaji marekebisho ya Sera
Shabaha ya Ujamaa katika kipindi
hiki.
Masharti na miiko ya Uanachama
|
|
|
|
|