| |
Nnachojivunia.
Ni kipi? Sio elimu. Sio utajiri. Sio dini. Sio kabila.
Kwangu mimi, vyote sio muhimu. Kwa nini? Twahibu!, vyote
ni pambo tu. Kama ni mali; mali yako. Wachache huipata.
Wengi ni mafukara. Wachache wao hupata kihalali. Wengi
wao chori chori! Ukiwa na elimu ni mali yako. Si yetu
sote. Kumpa mwingine ni kupenda tu. Ni wewe ujinga utakayeutoroka.
Naam! Nayo dini ni imani. Imani hutofautiana. Wapo wasioamini
cho chote. Wao, wapo wapo tu! Huko paradise hao watakaokwenda
hadi leo hawajijui! Kufika huko nako, sio kwa leo au
kesho. Safari ni ndefu! Kujivunia kabila, ni ubozi na
ubahaluli. Zinauzwa wapi kabila? Si unaikuta tu. Asokabila
sio mtu?
Nnachojivunia nini? Uwanachama wa chama
changu: Chama cha siasa chenye historia. Chama kilichofanya
matendo makubwa Afrika. Ni chama hiki kilichotoka ndani
ya mifupa na damu ya vyama vya ukombozi. Vipi hivyo,
ni ASP na TANU. Naam! Vyama vya Waafrika. Vyama vya
ukombozi. Vyama vilivyoona mbali. Vyama vya Nyerere
na Karume. Viongozi waanzilishi. Viongozi waasisi wa
taifa letu. Vyama vyao viliunganisha Waafrika. Viliwahamasisha.
Vikawaamsha katika maruirui ya kutawaliwa. Walilemazwa
ili kujiona sio watu kama watu. Waliamini kuwa wao ni
watwana na wajakazi tu. Utu wao ulidhalilishwa! ASP
na TANU, waasisi wa uanachama wangu, vikaweka mikakati
ya kudai haki za Waafrika. Vikakataa katu kutawaliwa.
Vikadai uhuru wa Tanganyika. Vikagombania uhuru wa Tanganyika.
Vikagombania uhuru wa Zanzibar. Vilimkataa mkoloni.
Vilimkataa Sultani. Mapambano yakapamba moto. Wakoloni
wakasalimu amri Tanganyika. Masultani wakatimuliwa huko
Zanzibar. Nchi zetu zikawa huru. Uhuru wa Mwafrika.
Uhuru wa mtu mweusi. Hiki nnajivunia.
Nnachojivunia. Ni uwanachama wangu. Chama hiki kilichorithi
historia hii ya ukombozi. Bila historia hii bado leo
tungekuwa watwana na wajakazi katika nchi yetu ya asili.
Naionea fahari historia hiyo. Nnachojivunia uwanachama
wangu wa Chama Cha Mapinduzi. Chama kilichorithi heshima
ya kuwa mkombozi. Hakuna chama kingine kinachoweza kujinasibisha
na hilo. Huo ni ukweli. Hiyo nayo ni hoja nzito. Nnachojivunia
kuwa mwanachama wa chama kikongwe. Sio ukongwe na kuishiwa
au kukongoroka! La hasha. Ukongwe wenye busara na hekima.
Chama kizoefu katika kuendesha nchi. Chama kiongozi.
Chama kinachoongoza na vingine vinajikongoja! Chama
kilichoonyesha na kubainisha umahiri wake. Kimeunganisha
umma wa Tanzania kuwa kitu kimoja. Hakuna ufa wala mpasuko
ndani ya Taifa. Kimefanikiwa kujenga umoja na utangamano
wa kweli. Macho yanachukia kuona damu inamwagika ya
binadamu! Tumezoea kununia mfarakano. Ni mfarakano wa
dini, kabila ama rangi. Amani na upendo ni chaguo la
watu wa nchi hii. Nnachojivunia mafanikio hayo yaloletwa
na chama changu.
Nnachojivunia kuwepo kwa umoja thabiti wa kitaifa. Umoja
wenye kukumbatisha makabila yote, dini zote, jinsia
zote na maeneo yote. Umoja wa Waafrika wa nchi zetu
mbili walioungana miaka arobaini iliyopita. Ni umoja
wa Waafrika wa Tanganyika na Zanzibar. Lakini budi ifahamike
umoja huo ulianza mwaka 1957. Ni pale African Association
ya Zanzibar na Shiraz Association zilipounda Afro-shirazi
Party. Mshikamano huo ukaimarika na kuongoza Mapinduzi
halali ya mwaka 1964. Umoja huo ni wa kidugu na kihistoria.
Kuuvunja itakuwa ni kosa kubwa. Nnajivunia kuwa chama
changu kimerithi na kuendeleza umoja huo! Chama kipi
kingine cha siasa nchini chenye historia ya kuunganisha
umma wa Tanzania na kusimamia kwa dhati umoja huu? Hakuna
zaidi ya chama changu. Hivyo budi nnajivunia hili.
Nnajivunia uhusiano mzuri uliojengwa na chama changu
kati ya vyombo vya usalama ikiwemo Jeshi, Polisi na
Usalama wa Taifa! Hili haliji wenyewe. Ni kazi ya busara
na hekima iliyojengwa. Raia wanaheshimiwa na vyombo
vinaheshimiwa. Utaifa unapewa umbele. Mipaka na majukumu
ya kazi hayaingiliani. Uadilifu unapewa kipaumbele.
Hakuna mfarakano. Hili katika nchi nyingine haliwezekani.
Nnajivunia ufanisi wa chama changu katika kujenga kuaminiana
huku katai ya vyombo vya usalama raia na vyombo vingine
vikiwemo Serikali, Bunge na Mahakama!
Nnachojivunia chama changu kwa sera sahihi zinazokubalika
na kutekelezeka! Sera zenye uhalisi wa mambo. Hazibuniwi
kuwalaghai watu, la hasha! Hazibuniwi kufurahisha watu
tu! Ila hilo. Zinabuniwa kuondolewa watu umasikini.
Zinabuniwa kuwaletea watu maendeleo. Ni sera zinazosimamiwa
vizuri na Serikali zetu. Zinawekewa mikakati ili zilete
tija na fanaka. Ufanisi wa utekelezaji huo katika ngazi
zote. Kila mwanachama miongoni mwetu aangalie kitongoji
na kijijini pake nini kimetekelezwa. Hakuna shule iliyojengwa
au kukarabatiwa? Nyumba za walimu, vyoo na kadhalika
zimejengwa? Hakuna zahanati mpya? Hakuna soko au gulio?
Hakuna kuboreka kwa huduma za madawa za mahospitali,
huduma za wakunga na watoto? Mwanachama wa CCM kama
mimi anayejivunia chama chake lazima atajivunia ufanisi
wa utekelezaji wa sera zake. Yapo ya kusemea kifua mbele
katika kitongoji au kijiji. Tena utayasemea kwa uhakika
na mifano. Ikiwezekana utoe takwimu na gharama zote.
Si hivyo tu ipo miradi katika kata, tarafa, wilaya na
hata mkoa. Lakini ukiweza unaweza kuisemea miradi ya
kitaifa kama ya barabara, madaraja, umeme, gesi, nyumba,
hospitali na kadha wa kadha. Lakini sio lazima kama
hauelewi.
Mimi Nnachojivunia, umahiri wa chama changu katika utendaji
wake na uongozaji wake. Taifa hili linajizolea sifa
kemkem duniani kote. Hilo wewe hujivunii? Mimi nnajivunia.
Tujivuniye. |
|
|