Ilani ya CCM Habari Mpya Historia ya TANU na ASP Kutoka Magazetini Hotuba

 

 

 

 

 

 

 

 

 

JARIDA LA MKEREKETWA

Uhusiano kati ya Chama Cha Mapinduzi na Vyama vya Nje vya kidugu na rafiki
 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na vyama rafiki. Miongoni mwa vyama hivyo ni ZANU-PF (Zimbabwe), SWAPO (Namibia), FRELIMO (Msumbiji), ANC (Afrika Kusini), UNIP (Zambia) na MPLA (Angola).
 
   
   
   
Katibu Mkuu wa FRELIMO, Komredi Armando Emilio Guebuza akisalimiana na Mweka Hazina wa CCM Taifa, Mama Salome Mbatia katika ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam.
   
 
Aidha, CCM imeendeleza uhusiano na ushirikiano wa karibu na Chama cha Kikomunisti cha China, Chama cha Kikomunisti cha Cuba, Chama cha Wafanyakazi cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea na vyama vingine rafiki ndani na nje ya Bara la Afrika.
Viongozi Wakuu wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin Mkapa wamekuwa wakitumia fursa ya ziara za nchi za nje kukutana na viongozi wa vyama rafiki kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano na CCM.
Vile vile, Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Philip Mangula alifanya mazungumzo na Mabalozi na Wawakilishi kutoka nchi za vyama rafiki kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano na CCM.
Baadhi ya vyama rafiki vilivyo-tembelea Tanzania hivi karibuni kwa mwaliko wa CCM ni pamoja na ANC, SWAPO, Labour Party ya Uingereza na FRELIMO.
Aidha, CCM ilialikwa na kushiriki katika mikutano kadhaa ya siasa pamoja na kutembelea vyama vya ANC - Afrika Kusini, NRM ya Uganda, Botswana Democratic Party (BDP), UDF ya Malawi na Labour Party ya Uingereza.
 
         
       
Mjumbe wa NEC, Capt. John Komba ambaye pia ni Mkurugenzi wa TOT akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu wa UDF, Ndugu Kennedy Makwangaza Makao Makuu ya CCM, Dodoma
     
Wajumbe wapya wa NEC wateuliwa
   
  • Mwasamale awa Katibu
    wa CCM wa Mkoa
 

Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) ilimaliza kikao chake cha siku mbili mjini Dodoma tarehe 14/9/2003 kwa kuwateua wanachama wa CCM sita kuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Walioteuliwa ni Ndugu Asha Abeid Faraji, Ndugu Mohammed Mohammed Jecha, Ndugu Abdallah Said Natepe, Ndugu Cleopa David Msuya, Ndugu Grace Soka na Ndugu Jumanne Mangara.
Wajumbe hao wameteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwa mujibu wa Katiba ya CCM ambayo imetenga nafasi kumi kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin W. Mkapa kupendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM majina ya wanachama kuingia kwenye NEC.
Katika nafasi kumi alizotengewa Kikatiba Mwenyekiti wa CCM, ni nafasi saba sasa zilizokwisha jazwa ikiwemo na ile ya uteuzi wa Ndugu Saleh R. Ferouz ambae kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.
Aidha, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilithibitisha uteuzi wa Ndugu Aron T. Mwasamale kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa.

SEMINA

Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kinaendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa programu ya kujenga uwezo wa viongozi wake kwa ngazi zote kupitia mafunzo kwa mujibu wa maagizo ya Mkutano Mkuu wa Sita wa Oktoba 2002.
Mpaka sasa zimekwishafanywa semina ngazi za Kamati Kuu ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na Halmashauri Kuu za CCM za Mikoa. Mafunzo pia yametolewa kwa Wakufunzi (Makada) wa Kitaifa na Makada wa Mikoa. Baadaye mafunzo yatafika Wilayani na kuhuka hadi ngazi ya Kata na Tawi. Lengo kuu ni kujenga itikadi moja ndani ya Chama.