KAMATI KUU YA CCM YAIPONGEZA SMZ NA RAIS KARUME KWA KUFANIKISHA SHEREHE ZA MIAKA 40 YA MAPINDUZI

 

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuandaa na kufanikisha sherehe kabambe za kuadhimisha miaka 40 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo zilifikia kilele chake Januari 12, mwaka huu.

 

Aidha, Kamati Kuu ya CCM imetoa pongezi maalum kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Amani Abeid Amani Karume kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa siku ya kilele cha sherehe hizo zilizofanyika katika Uwanja wa Amani, Zanzibar ambayo ilielezea kwa kina mafanikio ya Mapinduzi na juhudi zinazofanywa na Serikali kuijenga Zanzibar.

 

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam leo na Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Ndugu Omar R. Mapuri ilisema kwamba pongezi hizo zilitolewa katika siku ya kwanza ya kikao cha siku tatu cha Kamati Kuu ya CCM ambayo inakutana chini ya Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa.

 

Ndugu Mapuri alisema kwamba Kamati Kuu ya CCM pia iliwapongeza viongozi wa Chama na Serikali wa Tanzania Zanzibar kwa kuwahamasisha na kuwashirikisha wananchi, bila kujali tofauti zao za kisiasa kushiriki katika sherehe za Mapinduzi ambayo ndiyo yaliyoikomboa Zanzibar kutoka katika makucha ya wakoloni wa Kiingereza na utawala wa Masulani walowezi tarehe 12 Januari 1964.

 

Wanachama wa CCM, wakereketwa, wana-maskani, wapenzi wa CCM na wananchi kwa ujumla pia walipongezwa kwa wingi ambao haujawahi kuonekana kwa muda mrefu katika Uwanja wa Amani siku ya kilele cha sherehe.

 

Kamati Kuu ya CCM imesema kwamba itaendelea kuuthamini na kuuenzi mchango mkubwa wa mashujaa wa Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi thabiti wa Rais wa Chama cha Afro-Shirazi na Rais wa Kwanza wa Zanzibar huru, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, ambao walijitoa mhanga wa maisha yao kwa ajili ya uhuru wa kweli wa Wazanzibar.

 

Kamati Kuu ilisisitiza kwamba CCM ina fahari kubwa kuona kwamba ASP na hatimaye CCM baada ya kuungana na TANU imeweza kuyalinda, kuyaendeleza na kuyadumisha Mapinduzi ya Zanzibar hadi kutimiza miaka 40 sasa na kuyawekea msingi wa kuyadumisha milele.

 

Kutokana na hali hii, Kamati Kuu ya CCM imesisitiza tena kwamba kauli mbiu za MAPINDUZI DAIMA iendelee kutumika kama kielelezo cha dhamira ya kweli ya kuyadumisha Mapinduzi hayo na matunda yake ambayo kila mzalendo wa kweli wa Zanzibar na Tanzania nzima anapaswa kujivunia.