|
|
CHAMA CHA MAPINDUZI
OFISI NDOGO YA
MAKAO MAKUU S.L.P. 9151 DAR ES SALAAM F2180108
Barua zote zipelekwe kwa Katibu Mkuu Fax: 255-022-2185245; 022-2184580; 022-2183275
KIKAO CHA KAMATI KUU YA HALMASHAURI KUU YA
TAIFA YA CCM CHA TAREHE 19-20 MACHI, 2004,
DAR ES SALAAM
1. Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi ilifanya kikao chake cha kawaida cha siku
mbili tarehe 19-20 Machi, 2004 mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake,
Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa.
Kama kawaida, Kamati Kuu ilijadili mambo mbali mbali yaliyokuwamo katika
agenda iliyowasilishwa kwake na Sekretarieti ya Chama na kuyatolea maamuzi na
maelekezo.
2. Awali ya yote, Kamati Kuu
iliwapongeza na kuwapokea wajumbe wake wawili wapya wanaoingia kwa nyadhifa zao
za Uwenyekiti wa Jumuiya za CCM walizozipata kwa kuchaguliwa hivi
karibuni. Wajumbe hao wapya ni Ndugu
Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa UVCCM na Ndugu Abioud Maregesi, Mwenyekiti wa
Jumuiya ya WAZAZI. Ilimpongeza pia
Mheshimiwa Getrude Mongella (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Bunge
la Afrika.
3. Kamati Kuu pia ilitoa
Tamko la kulaani vitendo vya vitisho vinavyofanywa huko Zanzibar dhidi ya
Watanzania wenye asili ya Bara wanaoishi huko.
4.
Ililaani pia vitendo vya uvunjaji wa amani vinavyofanywa huko huko
Zanzibar kwa kutumia kisingizio cha dini.
Kamati Kuu imezitaka Serikali zote mbili zividhibiti vitendo hivyo kwa
manufaa ya amani na utulivu wa nchi.
5. Aidha, katika kikao chake
hicho, Kamati Kuu imeamua kushiriki kikamilifu katika chaguzi ndogo za:-
(a) Ubunge - Jimbo la Bariadi Mashariki, na
(b)
Udiwani - katika jumla ya Kata zote 20
zitakazogombewa katika mikoa ya Lindi (Kata 1), Mbeya (Kata 2), Tabora (Kata
1), Tanga (Kata 1), Mwanza (Kata 1), Shinyanga (Kata 8), Kilimanjaro (Kata 5)
na Kagera (Kata 1).
CCM imepania na ina
uhakika wa kupata ushindi mkubwa katika chaguzi zote hizo zinazotarajiwa
kufanyika tarehe 30 Mei, 2004. Kamati
Kuu imetoa wito kwa wananchi wote wanaotimiza masharti, wa Jimbo la Bariadi
Mashariki na wa Kata zote zitakazofanya uchaguzi, wajitokeze kwa wingi kuanzia
tarehe 21 Machi hadi 10 Aprili 2004 kujiandikisha kupiga kura.
6. Kamati Kuu pia imethibitisha uamuzi
uliofanywa na uongozi wa Chama wa Mkoa wa Kagera wa kumvua uanachama wa CCM,
Ndugu Hassan Milanga, aliyekuwa Diwani na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya
ya Muleba, baada ya kuridhika kwamba amepungukiwa na sifa za uanachama.
7. Aidha, Kamati Kuu imeelekeza kwamba
uandaliwe utaratibu wa kuieneza dhana ya utandawazi ndani ya mfumo mzima wa
Chama Cha Mapinduzi. Hii inafuatia
hatua ya Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Kimataifa kuhusu Masuala ya Kijamii
katika Utandawazi, Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa kukikabidhi Chama Cha
Mapinduzi nakala za Ripoti ya Tume hiyo kama alivyofanya kwa vyama vingine vya
Siasa mara tu baada ya kuizindua hapa nchini tarehe 16 Machi, 2004, katika
Hoteli ya Royal Palm, Mjini Dar es Salaam.
Omar
R. Mapuri (Mb.),
KATIBU MWENEZI WA CCM TAIFA
21/03/2004