DK. A. KIGODA AELEZEA MAFANIKIO MAKUBWA  YA UBINAFSISHAJI NCHINI TANZANIA

 

Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa – Rais Benjamin W. Mkapa,

Waheshimiwa Makamu wa Mwenyekiti, Tanzania Bara na

Tanzania Zanzibar,

Waheshimiwa Viongozi wetu Wakuu wa Halmashauri Kuu ya Taifa,

Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

 

Assalam Alheikum.

 

          Nashukuru sana kupewa heshima na fursa hii ya kuzungumza mbele ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ili nitoe Maelezo juu ya Sera ya CCM ya Ubinafsishaji.  Mimi kama Waziri ninaesimamia masuala ya Ubinafsishaji nafarijika kuwa maelezo nitakayoyatoa hapa yatasambaa Tanzania nzima bila ya wasi wasi wowote, kwa vile ni ukweli usiopingika kuwa hadhara hii inawakilisha uongozi wa juu kabisa wa nchi yetu katika Chama na vile vile ni uongozi unaowakilisha Taifa zima.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ni Uamuzi.  Katika dunia, kila uamuzi una maana yake na unaweza ukawa na matokeo ambayo yanaweza yasimfurahishe kila mwananchi.  La muhimu ni mizania ya matokeo hayo yatathminiwe na kubaini athari na mafanikio yake.  KWA MAANA KUPANGA NI KUCHAGUA kama alivyotuasa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.  Iwapo mafanikio ndiyo mazito zaidi lazima Chama kiwe jasiri kukubali kuendelea na utekelezaji endelevu.  Na hivi ndivyo Serikali inavyofanya.

 

          Kwanza nikumbushie mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka 2000 hadi 2010.  Mwelekeo huu ulibuniwa mwanzoni wakati ambapo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa bado yu hai.  Nakumbushia hivyo kwa maksudi, maana wako wanaohoji Sera zetu za CCM tena kwa kupotosha tu, au kupinga Sera za CCM na mikakati yake, na wanatafuta uhalali huo kwa kutaja jina la Baba wa Taifa.  Wanalitumia jina vibaya.  Mwalimu, alitufundisha wazi kuwa mkakati wa kujenga uchumi imara kwa kutumia mashirika ya umma ulikuwa umefikia ukomo.  Wala hatukubadili mkakati na kukaribisha Sekta Binafsi kwa vile tuna TATIZO la KIITIKADI na Sekta ya Umma au kwa vile tuna mapenzi na Sekta Binafsi. UKWELI ni kwamba Mashirika ya Umma yametushinda, hayangeweza kuhimili uendeshaji wa uchumi.  Hadi sasa kama tungeendelea na utaratibu ule robo tatu ya uchumi wetu hivi sasa ungezimia au kufa na matatizo tele ambayo yangehatarisha maisha na utawala wa Chama Chetu na Tanzania kudhalilika.

 

          NJIA sahihi na ya uhakika iliyobaki ni mkakati wa kutanguliza mbele SEKTA BINAFSI kuwa mhimili wa uchumi.  Nguvu zetu zote tuzimalizie hapo.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 14 cha Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2000 hadi 2010 kinasema: nanukuu “Uchambuzi yakinifu wa hali ya Uchumi wa Tanzania ni kuwa Uchumi wetu una sifa kuu mbili.

 

·        Ni uchumi ulio nyuma.

·        Ni uchumi ulio tegemezi.

 

Sifa hizi mbili za uchumi wetu tusipoangalia tunaweza kuzilea kama vile tumepata watoto mapacha.  Katika hali ya sasa ya Uchumi wa dunia nchi haiwezi kujitegemea kiuchumi wakati uchumi wake uko nyuma, na pia uchumi wake hauwezi kuwa ulioendelea kama haujitegemei.   Kadri uchumi unavyozidi kuwa wa kisasa (kama tufanyavyo sasa) ndiyo nchi inavyoingia katika mkondo wa kujitegemea kiuchumi.  TUSIDANGANYIKE Uchumi vile vile ni siasa.

 

          Ilani ya  CCM ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2000 nayo inaongezea Ibara ya 2 …. Hivyo katika kipindi hiki cha mwaka 2000 hadi 2005, CCM itahakikisha kuwa Serikali zetu 2 zinazingatia mkakati wa modenaizesheni katika Sekta zote za Uchumi wa Taifa kama mkakati wa pekee wa kujenga msingi wa Uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea.

 

          Uchumi wa kisasa utajengwa kwa kuhakikisha kuwa Sayansi na teknolojia ya Kisasa inapenyezwa katika sekta zote ili hatimaye kutokomeza umaskini nchini.

 

          Ninachosema ni kwamba katika hali ya sasa ya Uchumi, na mazingira ya utandawazi hatuwezi kuendesha uchumi wetu kama tulivyokuwa tunafanya zamani.  Lazima tubadilike.  Tunahitaji, mitambo ujuzi, teknolojia mpya ili tuongeze uzalishaji na tija.  Lazima tuwe jasiri na kubadilika, kwa maana tusipobadilika uchumi wetu utabaki nyuma na utabaki kuwa tegemezi.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa jumla wa kuondoa uchumi wetu katika uduni na utegemezi wake nao upo wazi ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM.  Kifungu cha 4. Nanukuu “Sera ya CCM ya urekebishaji wa uchumi ulioanza tangu zama za awamu ya pili na kuendelezwa katika kipindi cha 1995 na 2000 itaendelea kutekelezwa kwa nguvu na kasi mpya katika miaka 2000 na 2005.”

 

Na Sehemu ya Mwisho ya Kifungu cha 5 Cha Ilani nayo inasema “Katika Kipindi kijacho, CCM itahakikisha kuwa Serikali itaendelea na zoezi la Urekebishaji na Ubinafsishaji wa mashirika na makampuni yaliyosalia”.  Tujiulize zoezi hili linaendelea au limesitishwa?  La bado linaendelea.

 

          Kwa hiyo basi Sera hii ni yetu lazima CCM tuilinde, na tuitetee bila ya aibu.  Hatuwezi kubabaika na kuangalia nyuma na tukakaa tu tukisikia ikipotoshwa.  Kujenga hisia kuwa Sera hizi na mikakati hii ni Shinikizo la Mashirika ya Fedha ya Kitaifa ni upotoshaji.  Sera hizi ni za CCM na ndizo zilizotupatia idhini ya Chama chetu kutawala kwa ushindi mkubwa na ridhaa isiyo na shaka.

 

          Ni kweli CCM imezungumza na kukubaliana na Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, ya Kikanda, nchi wahisani juu ya ratiba ya utekelezaji wa malengo yetu.  Hali hii imetujengea heshima dunia nzima.  Madeni tunasamehewa na nchi inakopesheka.  Hii ni Sera yetu, sisi sote Wana CCM na Watanzania.  Kwa mantiki hii Sera ya Ubinafsishaji si Sera ya Mwenyekiti wetu wa Taifa, au ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ya Waziri yeyote au mtu yeyote.  Hii ni Sera ya CCM iliyofafanuliwa vizuri katika Ilani zote za Uchaguzi za CCM za mwaka 2000 na 2005 pamoja na kusisitizwa katika mwelekeo wa CCM kuelekea mwaka 2005, kama nilivyoelezea hapo awali.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu na mwelekeo tunaousikia na kuuona hivi sasa katika kuelezea Sera ya Ubinafsishaji, unaofanywa hususan na baadhi ya Wanasiasa Wapinzani wanapoona mafanikio ya Sera za CCM, kwa vile hawapendi wanayakejeli na kuyakebehi bila ya sababu zozote zile, ila ile ya UPOTOSHAJI.  Upotoshaji huo unaofanywa umefikia kiwango cha wapotoshaji hao hata kushindwa kutofautisha kati ya Sera ya Ubinafsishaji na ile ya Uwekezaji.  Hali hii inasikitisha na ni bahati mbaya.  Hali hii vile vile inadhihirisha mtazamo finyu wa wale wapinzani kupinga jambo au fanikio lolote lile kwa sababu tu ni wapinzani.  Kwa wanasiasa hawa kufanya hivi wanafikiria kuwa watapata afueni za kisiasa.  Hili haliwezi kutokea kwa sababu popote pale ukweli unaposimama uongo hujitenga.  Kutokana na hali ya maendeleo ya uchumi duniani ilivyo hivi sasa, itakuwa ni vigumu sana kuwashawishi Wananchi kwa kutumia propaganda ya upotoshaji  wa kutoa habari ambazo si sahihi.

 

          Kwa upande mwingine inashangaza vile vile kusikia na kuona kuwa hata baadhi ya wasomi wetu nchini nao wanatumia taaluma na elimu zao walizozipata kuwapotosha Wananchi aidha kwa kukidhi dhana, matakwa na maslahi yao binafsi au kwa malengo ya kupaka matope siasa nzuri za CCM.  Sote tunafahamu kuwa mchakato wa kuleta maendeleo yawe ya kiuchumi au kijamii, pamoja na mambo mengine, unahitaji tujenge fikra zilizo sahihi na kubadilisha mtazamo wetu ili twende kwa wakati kwa kukubali kuwa dunia sasa hivi inapambana na mabadiliko makubwa ya kijamii na Uchumi.  Wanasiasa na wasomi hawa wamekuwa wakitumia baadhi ya vyombo vya habari kama vile Radio, TV, Magazeti kueneza propaganda hizo za upotoshaji mkubwa wa Sera nzuri za CCM, hususan hii ya Ubinafsishaji.  Nadhani hali hii ni kupoteza wakati mzuri tunaouhitaji katika kupambana na Umaskini.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningependa kusema wazi kuwa hata hivyo vyombo vya habari wanavyovitumia kwa upotoshaji huo, hivi sasa vimeshamiri sana nchini kutokana na Sera hii hii ya Ubinafsishaji.  Wito wangu kwa baadhi ya vyombo vya habari visaidie kuwaelimisha Wananchi na kuelezea ukweli wa mafanikio ya Sera za CCM na pale penye matatizo vikiri mbinu na ufumbuzi  unaofanywa na Serikali yetu inayoongozwa na Chama Tawala cha CCM.

 

           Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema sasa nielezee Sera ya Ubinafsishaji kwa mantiki ya kupima mafanikio yetu na matatizo yetu kulingana na dhamira ya Sera yenyewe kama ilivyoainishwa katika madhumuni ya Sera ya Urekebishaji wa Mashirika ya Umma.

 

 

 

          UKUZAJI WA PATO LA TAIFA

(a)              Dhumuni la kwanza ni kuongeza ufanisi wa uzalishaji katika sekta zetu mbalimbali ili ziweze kuchangia zaidi katika Pato la Taifa na kupunguzia Serikali na walipa kodi mzigo wa ruzuku na mikopo kwa mashirika ya umma.  TUJIULIZE dhumuni hili tumelifikia au la?  Hivi sasa uchumi wetu unakua kwa asilimia takribani kati ya 6.2 na 7 na kuifanya Tanzania nchi ya 3 kwa Kukuza uchumi wake katika nchi 14 za SADC mwaka 2003.  Mfumko wa bei umepungua na mapato ya Serikali sasa yameongezeka kuanzia sh. 25 bilioni hadi kufikia zaidi ya sh. 100 bilioni kwa mwezi hivi sasa.  Kabla ya Ubinafsishaji Serikali ilikuwa ikitoa ruzuku kuyabeba Mashirika ya Umma kwa kiasi cha dola 100 milioni kila mwaka na mashirika haya yalikwisha ingizia Serikali hasara ya dola 300 milioni.  Hivi sasa kwa eneo la KODI Serikali inalipwa kodi badala ya kutoa ruzuku.  Mifano ni viwanda vya sukari Mtibwa, Kilombero; Mbeya Cement, Tanga Cement, Tanzania Portland Cement, NBC, CRDB, Canvass Mill, Handico, Blankets na Textile Manufacturers Ltd., TBL, TCC, DAHACO, Sabuni Detergents Ltd, nk.  Mtibwa ililipa VAT ya zaidi ya Tsh. 800/= mwaka 2001.  Ilipobinafsishwa mwaka 1998 ililipa malimbikizo ya kodi ya Tshs. 400 mil.  Kabla ya hapo malipo ya kodi hayakuwa ya kuaminika.  TBL mwaka 2002 ililipa kodi ya sh. Bilioni 43.5 na gawio kwa wanahisa sh. Bilioni 34.5.  Kabla ya kubinafsishwa mwaka 1993, TBL haikuwahi kupata mapato (total revenue) zaidi ya Tsh. 15 bilioni na hivyo kodi ilikuwa ndogo sana.  Handico haikuwa ikilipa kodi kabla ya kubinafsishwa mwaka 1996 kwa sababu ilikuwa ikiendeshwa kwa hasara.  Hivi sasa inalipa wastani wa Sh. 2 milioni kwa mwaka kama kodi mbalimbali.  Blankets and Textile Manufactures Ltd. inalipa wastani wa kodi ya sh. 200 milioni kwa mwaka.  Wakati kinabinafsishwa mwaka 1997, kiwanda kilikuwa kimefungwa kwa miaka kadhaa na hivyo kilikuwa hakilipi kodi.  TTL (Zamani Kibo Paper) ililipa kodi ya Tsh. 460 milion mwaka 1999 na Tsh. 662 mwaka 2000.  Kabla ya kubinafsishwa mwaka 1977 kiwanda kilikuwa kikiendeshwa kwa hasara.  Canvass Mill ilifungwa kwa muda wa miaka minne kabla ya hakijabinafsishwa mwaka 1998.  Mwaka 2002 ililipa Tsh. 109.7 milioni kama kodi mbalimbali.  Sigara (TCC) inalipa Serikalini wastani wa kodi Tsh. 40.9 bilioni kwa mwaka.  Mwaka 1999 ililipa Tsh. 34 bilioni kama kodi mbalimbali.  Kabla ya ubinafsishaji kiwango cha kodi kilikuwa kidogo kwa sababu ya uzalishaji mdogo uliombatana na biashara ya magendo ya sigara.  Tanzania Portaland Cement ililipa Serikalini kodi ya Tsh. 3.4 bilioni mwaka 2002.  Tanga Cement ililipa Serikalini kodi ya Tsh. 1.9 bilioni mwaka 2002.  Kiwanda kinaongoza katika kulipa kodi mkoani Tanga.  Mbeya Cement ililipa Serikalini kodi ya Tsh. 847.5 milioni mwaka 2002.  Kabla ya ubinafsishaji mwaka 1997 Kampuni iliendeshwa kwa hasara.  NBC ililipa kodi Tsh. 3.2 bilioni mwaka 2002.  Kabla ya ubinafsishaji mwaka 1999 Benki ilikuwa inapata hasara ya wastani wa Tsh. 1.5 bilioni kila mwezi.  NBC pia ilikuwa na mtaji hasi (negative capital) wa Tsh. 39,517 bilioni hapo Desemba 1999.

 

KUONGEZEKA KWA UZALISHAJI

          Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana Wanasiasa Wapinzani, wasomi hawa na wanapropaganda wanatatizo kubwa la USAHAULIFU au KUSAHAU.  Mara hii wamekwishasahau kuwa tulikuwa tukisimama mistari mirefu (foleni) kutafuta chumvi, sukari, mafuta, sabuni za kufulia, nguo nk.  Wanakumbuka kuwa wakati ule utawala bora ni kwa viongozi kugawa sabuni au mafuta?  Taifa lilitumbukia katika dimbwi la aibu, ulanguzi na rushwa na tulikata tamaa.  Hali hii tuizungumzeni kwa ukweli kabisa na tuwahamasishe Wananchi waelewe vyema kuwa baada ya Ubinafsishaji kupitia menejimenti bora, ujuzi mzuri na teknolojia ya kisasa, sekta zetu za kuzalisha uchumi moja kwa moja zilifufuka na kuongeza bidhaa, ajira na mapato kwa Serikali kwa faida ya kujenga uchumi wa Taifa letu.  Ngoja nitoe mifano michache ifuatavyo:  Viwanda/mashirika mengi yaliyobinafsishwa yameongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zenye ubora wa kimataifa.  Hii imewezekana kutokana na uwekezaji katika teknolojia ya kisasa na mbinu bora za uendeshaji (management/business skills).  Kilombero uzalishaji wa sukari umepanda kutoka tani 29,000 wakati wa ubinafsishaji mwaka 1997 hadi tani 98,000 mwaka 2002/2003.  Mtibwa tani 29,000 wakati wa ubinafsishaji mwaka 1998 hadi tani 49,700 sasa.  Katumba kilo 1,042,000 mwaka 2001 hadi kilo 2,194,000 za chai mwaka 2002.  kabla ya ubinafsishaji ukulima wa chai ulisimama na viwanda vya Katumba na Mwakaleli kufungwa.  Tanga Cement mwaka 1999 tani 340,000 hadi tani 400,000 mwaka 2002/2003.  Sabuni Detergent (FOMA); Kiwanda hiki kilibinafsishwa kwa utaratibu wa kufilisiwa kupitia LART mwaka 1995.  Baada ya ukarabati, uzalishaji wa sabuni ulianza upya mwezi Machi 1996 na sasa umeshamiri.  Sabuni zinazotengenezwa ni aina mbalimbali za Foma za unga na maji, Foma Limao, Foma Dazzle, nk.  Gombamwenga Sisal Estate uzalishaji umeongezeka kutoka tani 481 mwaka 1998 hadi tani 535 mwaka 2002.  Kabla ya ubinafsishaji shamba liliota majani na kusitisha uzalishaji mkonge. Viwanda vingi vya Nguo kama Mwatex, Mutex nk. sasa vimeendelea kuzalisha nguo nchini baada ya kusimama kwa muda mrefu.  Ajira imeongezeka sana na taarifa tulizonazo hivi sasa karibu asilimia 75 ya pamba yetu ghafi, inasindikwa na viwanda vyetu.

 

          SUALA LA AJIRA, MISHAHARA NA MENEJIMENTI.

          Dhumuni la pili ni kuongeza ajira na kuboresha menejimenti.  TUJIULIZE dhumuni hili tunalifikia au la?  Inafaa izingatiwe kwamba Ubinafsishaji si lazima usababishe upunguzaji wa ajira.  Wafanyakazi wengi walipoteza ajira zao hata kabla ya Sera ya Ubinafsishaji haijaanza kutekelezwa kwani mashirika yapatayo 78 yalikwishafunga shughuli zake na hivyo wafanyakazi husika kujikuta hawana kazi/ajira.  Baadhi ya mashirika haya sasa yamefufuliwa na yanafanya kazi vizuri.  Mifano ni Kiwanda cha Mablanketi, Kiwanda cha Viatu (Bora), Kiwanda cha Sabuni cha Tanga nk. na yameajiri upya wafanyakazi.  Mashirika mengine yalilazimika kupunguza wafanyakazi baada ya ubinafsishaji kwa vile yaliajiri wafanyakazi zaidi ya waliokuwa wanahitajika.  Kwa sasa ajira katika mashirika yaliyobinafsishwa ni yenye uhakika na endelevu.  Ajira zaidi zimeongezeka nje ya viwanda/mashirika ambayo sasa yanafanya kazi vizuri na kwa ufanisi mkubwa.  Kwa mfano viwanda vyote vya saruji sasa vimeongeza uzalishaji.  Hali hii imechangia kuongezeka kwa haraka shughuli za ujenzi na biashara ya kufyatua matofali; usafirishaji wa saruji pia umetoa ajira kwa wenye vyombo vya usafiri, n.k.  Viwanda vya sukari vimeongeza ajira ya wakata miwa, wakulima wadogo wadogo (outgrowers), watengezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumia sukari, nk.  Wakulima wa mazao mengine kama tumbaku, nao wameongeza uzalishaji baada ya kuhakikishiwa soko kutoka kwenye viwanda ambavyo vimefufuliwa baada ya ubinafsishaji.  Inakadiriwa kwamba mapato/maisha ya zaidi ya Watanzania 300,000 hutegemea sana usambazaji na ugawaji wa bidhaa za Kampuni ya bia (TBL) na Kampuni ya sigara (TCC).  Kabla ya ubinafsishaji Watanzania karibu 100,000 walikuwa wanapata ajira kutokana na usambazaji wa bidhaa za TBL na TCC.  Mishahara na maslahi ya wafanyakazi wa mashirika mengi yameongezeka na kuboreshwa.  Kwa mfano:  Kabla ya kubinafsishwa, kima cha chini pamoja na marupurupu Tanga Cement kilikuwa sh. 150,000/= kwa mwezi.  Sasa ni zaidi ya sh. 450,000/=.  TBL ilikuwa inalipa kima cha chini sh. 9,000/- kabla ya ubinafsishaji.  Sasa kiasi ni zaidi ya sh. 120,000/= mbali ya marupurupu yanayotolewa nk.  Aidha kiwanda cha Tanga Cement hutumia sh. 100 milioni kwa mwaka kugharamia elimu kwa wafanyakazi; TBL imetenga zaidi ya saa 100 za mafunzo ya kompyuta kwa kila mfanyakazi kwa mwaka nk.

 

          TEKNOLOJIA YA KISASA.

          Dhumuni la tatu ni lile la kupata teknolojia ya kisasa.  TUJIULIZE dhumuni hili tunalifikia au la?  Hivi sasa ni vigumu kupata nafasi muhimu viwandani na hata katika maeneo ya menejimenti bila ujuzi au elimu ikizingatiwa na pale zamani.  Teknolojia ya kisasa imeanzishwa katika uzalishaji mali na utoaji wa huduma muhimu kwa jamii.  Umwagiliaji mashamba ya miwa Kilombero hutumia mitambo ya kisasa.  TBL pia hutengeneza bia kutumia kompyuta nk.

 

          UPATIKANAJI WA MITAJI NA MASOKO.

          Dhumuni la nne lilikuwa ni lile la kupata mitaji ya ndani na nje na kupata masoko ya ndani na nje ya bidhaa zetu.  TUJIULIZE dhumuni hili linafikiwa au la?  Hivi sasa saruji yetu, huuzwa nchi jirani za Malawi, Zambia, Rwanda, Burundi nk.  Bia pia huuzwa Kenya, Uganda na nchi nyingine za jirani.  Maturubai ya Canvas Mill yanauzwa katika majeshi ya NATO nk.  Sabuni zetu zimepata soko DRC Kongo, Malawi, Msumbiji na hata Kenya.  Aidha Sigara, chai na Tumbaku tunayozalisha tunaziuza nje.  Hivi sasa, ubora wa bidhaa za viwanda vingi vilivyobinafsishwa umeongezeka na vingine vimeweza kuthibitishwa, kutambuliwa na kukubaliwa na asasi za kimataifa zinazodhibiti ubora wa bidhaa na usimamizi wa mzingira kama ISO, NOSA nk. na hivyo kukubalika katika masoko yetu ya ndani na nje.  Hii ni moja ya sababu ya kuongezeka kwa akiba yetu ya fedha za kigeni zinazoweza kuhimili miezi 7 hadi 8 badala ya wakati ule ambapo akiba yetu isingeweza kuhimili hata kipindi cha miezi 2.

 

          KUIPA NAFASI SEKTA BINAFSI.

          Dhumuni la tano ni lile la kuipa Sekta binafsi nafasi ya kuendesha uchumi ili Serikali ielekeze nguvu zake katika kuimarisha shughuli za jamii, miundombinu, ulinzi, usalama na utawala bora.  TUJIULIZE dhumuni hili linafikiwa au la?  Kuainishwa kwa Baraza la Wafanyabiashara, Taasisi ya kuendeleza Sekta binafsi nchini ni vigezo tosha kwa upande wa dhamira ya Serikali ya kubadilishana mawazo na Wawekezaji, wafanyabiashara binafsi ili kujenga mazingira bora ya utendaji kazi.  Aidha watanzania wengi wamepata fursa ya kuwa wawekezaji katika mashirika yapatayo 138 kwa asilimia 100 na wengine zaidi wameingia ubia na wageni katika kumiliki mashirika 123 yaliyobinafsishwa, kati ya Mashirika zaidi ya 266 yaliyobinafsishwa.  Vile vile zaidi ya Wananchi 98,000 wamenunua hisa katika mashirika yaliyobinafsishwa na wanapata gawio kila mwaka.  Katika hawa, wanawake wanaongoza (55%). 

 

          Aidha ili sasa kuendeleza zao la Korosho, Serikali imeamua kufuata utaratibu wa kubinafsisha viwanda vya kubangulia Korosho kwa misingi ya kuangalia Mpango wa Uwekezaji na Uendeshaji, badala ya kung’ang’ania fedha za kununulia viwanda hivi.  Utaratibu wa kutoa fedha umekwamisha kuendelea kwa viwanda hivi kwa vile baada ya kununua viwanda inabidi mwekezaji aingie gharama kubwa ya kubadilisha teknolojia iliyopitwa na wakati ili wazalishe kwa ufanisi na tija.  Umuhimu na kipaumbele katika kubinafsisha viwanda hivi utatolewa kwa Watanzania ili waendeleze viwanda hivi.  Hoja hii ya kusema nchi inauzwa kwa wageni inatoka wapi kama si upotoshaji tu?  Kwa upande wa kuboresha huduma za jamii hivi sasa tunashuhudia juhudi kubwa za Serikali katika kuboresha mashule, vituo vya afya, mabarabara nk.  Mikakati ya kupambana na rushwa inaendelezwa na vile vile mpango wa kurekebisha Serikali za Mitaa na Miji unaendelea kama njia mojawapo ya kuboresha utawala bora.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kuwa mikataba inayoingiwa na Serikali na Wawekezaji katika ubinafsishaji ni ya siri na ni vyema ikajadiliwa na umma.  Utaratibu huu utakiuka haki na Sheria za Kimataifa na vile vile utaondoa mantiki ya ushindani baina ya Wawekezaji pale ambapo wale wanaowania kununua kiwanda fulani, mipango yao ya Uwekezaji na Uendeshaji, pamoja na bei walizotoa zinapokuwa bayana kwa kila mtu.

 

          Hata mtu anaponunua baiskeli haitawezekana atangaze katika mitaa yote juu ya mkataba wake wa kununua baiskeli hiyo.  Utayarishaji wa Mikataba hii huhusisha Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Sheria na Katiba pamoja na Mnunuzi baada ya makubaliano ya uuzaji kufuata utaratibu niliokwisha uelezea.  Hi inatosha.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika yaliyobinafsishwa hayajauzwa kwa bei poa.  Yale yaliyonunuliwa na Watanzania yamegharimu takriban sh. 60 bilioni, yale ya wageni takriban sh. 23 bilioni na yale yaliyonunuliwa kwa ubia yamefikia takriban sh. 400 bilioni.  Hii hoja inayozungumzwa siku zote na wahusika kuwa mashirika haya yameuzwa bei poa imetoka wapi.  Misingi ya uuzaji inayozingatia aina ya teknolojia, madeni ya shirika kutokana na mikopo inaeleweka kabla ya kutoa hoja hizi.  Kiwanda maana yake si majengo tu.  Huu ni upotoshaji.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasiasa wapinzani, baadhi ya wasomi na watu wengine wamekuwa wakiuliza na kuhoji, kwa kujifanya kwa maksudi, eti hawajui Ubinafsishaji umemfaidishaje Mtanzania wa kawaida.  Nimeshaonyesha kuwa Serikali sasa haitoi ruzuku na kufidia madeni ya mashirika haya yaliyolimbikiza hasara ya dola takriban 400 milioni kabla ya Ubinafsishaji.  Badala yake Serikali sasa inapata mapato kupitia kodi na gawio kutoka viwandani ambazo zinaingia moja kwa moja katika mfuko wa Serikali.  Tunashuhudia sasa ujenzi wa mabarabara uboreshaji wa huduma za jamii: elimu, afya, maji n.k.  Haitawezekana na wala haiwezekani kiwanda kikiuzwa waitwe wananchi wote wagawiwe fedha mifukoni!  Swala la kupunguza umaskini lina mtazamo wa aina mbili: kupunguza umaskini usio wa kipato na kupunguza umaskini wa kipato.  Bila ya kuelewa dhana hii tutabaki kuoegelea kwenye propaganda ya upotoshaji kama vile inavyoshabikiwa na Wanasiasa Wapinzani na baadhi ya wasomi.  Hakuna njia ya panda katika ajenda hii na CCM iko katika mstari sahihi. 

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, sera hii ya Ubinafsishaji inayozungumziwa na Wanasiasa wapinzani kwa upotoshaji na kupakana matope, ni kama vile sera hii inatekelezwa Tanzania peke yake.  Hii siyo sahihi.  Nchi zile zilizoikataa sera hii pale awali sasa zinaitekeleza.  Afrika ya Kusini, Kenya n.k.  Aidha nchi nyingi za Afrika, Ulaya na Asia zinaendeleza kutekeleza sera hii hadi hivi sasa ili kuipa nguvu sekta binafsi.  Aidha Malawi, Rwanda na Burundi pamoja na Kenya na Uganda zimeshaleta wajumbe wao hapa nchini kujifunza taratibu za ubinafsishaji kutokana na mafanikio tuliyoyapata.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, si sahihi kusema kuwa ubinafsishaji haujali malipo ya mafao ya wafanyakazi.  Serikali imelipa mafao yote ya kisheria ya wafanyakazi walioachishwa kazi kutokana na viwanda vyao kufungwa kwa kushindwa kufanya kazi na hatimae kubinafsishwa.  Tatizo lipo katika malipo ya mafao chini ya utaratibu wa Mikataba ya Hiari.  Mikataba hii hutekelezeka wakati kiwanda au shirika husika likitengeneza faida.  Kama shirika limefilisiwa au limefungwa kwa kushindwa kufanya kazi, faida hiyo na hususan malipo hayo ya mkono wa kheri yatatoka wapi au yatatokana na nini?  Wanasiasa Wapinzani na baadhi ya Wasomi wanajifanya hili hawalijui au hawalielewi.  Mafao yanayotokana na mikataba ya hiari ni makubaliano kati ya menejimenti ya wafanyakazi, na wala Serikali haihusiki.

 

          Mafao yanayotokana na makato ya Pensheni, mengi yalikuwa hayawasilishwi kwenye taasisi husika na mashirika mengi ya umma.  Fedha hizi zilipokatwa kutoka mishahara ya wafanyakazi hazikufikishwa kwenye taasisi husika; zilitumika.  Mzigo huu si wa Serikali.  Hata hivyo Serikali inajitahidi kulipa baadhi ya malipo haya ambayo hayakuwakilishwa hapo awali kwa sababu ya uzembe na ubadhirifu uliotokea.  Hivi sasa Serikali inatafuta sh. 18 bilioni ili kufidia uzembe huu.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, mada yangu haisemi kuwa Sera yeyote katika nchi inaweza kutekelezwa kikamilifu kwa asilimia moja.  Hili halijapata kutokea dunia nzima.  Kwa mantiki hii hata utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji haujaendelea bila ya matatizo.

 

Matatizo yaliyojitokeza:

·        Baadhi ya wananchi kutoelewa dhana nzima ya Sera ya Ubinafsishaji na kujenga hisia/imani kwamba mali yao inauzwa kwa wageni.

 

·        Mashirika mengi kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni na hivyo kuwa vigumu kuwavutia wawekezaji.

 

·        Baadhi ya mashirika/viwanda yalikuwa katika hali mbaya sana katika vitendea kazi muhimu, yaani mitambo na miundombinu yake ilikuwa imechakaa na teknolojia yake kupitwa na wakati.

 

·        Baadhi ya wawekezaji kushindwa au kuchelewa kufufua mashirika waliyokabidhiwa.  Mifano ni: Moshi Hotel, Kiwanda cha Ngozi Morogoro, Tegry Plastics, viwanda vya magunia, mashamba ya mkonge, nk.

 

·        Baadhi ya wawekezaji/wabia kutoa taarifa za uwekezaji zisizo sahihi na kutokuwa na uwezo wa kifedha wa kuendesha taasisi zilizobinafsishwa.

 

·        Watanzania wengi kukosa mitaji ya kumiliki na kuendeshea mashirika yanayobinafsishwa.

 

·        Mashirika mengi kuwa na kesi Mahakamani, nk.  Sasa hivi kuna kesi zaidi ya 170 Mahakamani dhidi ya mashirika ya umma.

 

·        Kukosekana kwa hati miliki karibu 700 za mashirika.  PSRC imeweza kuzipata hati 400.  Zilizobaki (300) zinafuatiliwa.

 

 

Hatua zilizochukuwa:

Serikali imechukua hatua zifuatazo ili kukabiliana na matatizo yaliyojitokeza:-

 

·        Kuimarisha ufuatiliaji wa utendaji wa mashirika yaliyobinafsishwa kwa kushirikiana na Wizara zinazohusika.

 

·        Kutumia wataalam kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa sugu.

 

·        Kuwafanyia tathmini wawekezaji wote wanokusudia kuwekeza kwenye mashirika ili kubaini uwezo wao kiutendaji, kibiashara na kifedha.

 

·        Kuendelea kuwaelimisha wadau mbalimbali kuhusu Sera ya ubinafsishaji na umuhimu wake katika jitihada za kufufua uchumi na kupiga vita umaskini.

 

·        Kuanzisha utaratibu wa dhamana za benki (bid bonds) kwa nia ya kuwaengua/kuwadhibiti madalali na wawekezaji wasio waaminifu.

 

·        Kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wawekezaji walioshindwa kutekeleza mikataba ya ubinafsishaji.  Mifano: Mikumi Wildlife Lodge na Katani Ltd., nk.

 

·        Kuajiri wanasheria kushughulikia kesi zilizo Mahakamani.

 

·        Kuajiri mtaalam wa masuala ya ardhi kufuatilia hati miliki zenye matatizo nk.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu wa upotoshaji na propaganda  unaoendelea hivi sasa juu ya Sera ya ubinafsishaji ni dhaifu.  Kutokuwaeleza ukweli na kuwapotosha Wananchi si mkakati ambao utazuia hata kidogo kuendelea na Sera ya Ubinafsishaji na sera nyingine za CCM zenye lengo la kuboresha uchumi na maisha yetu, hasa katika kipindi hiki tunachopambana na mabadiliko makubwa ya uchumi duniani pamoja na hili la sasa la utandawazi.  Nawasisitiza Wana CCM, Wakereketwa na Watanzania wenzangu tufanye kazi kwa bidii ili kuendeleza mafanikio haya tuliyokwishayapata sasa kupitia Sera ya ubinafsishaji ili tusije tukarudi katika zama zile za kukosa huduma muhimu za kibinadamu. Ndio maana hivi sasa Serikali ya CCM, Bunge la Jamhuri ya Muungano linalowakilisha Watanzania wote, tumefikia muafaka wa jinsi ya kubinafsisha Benki ya NMB ili ifanye kazi kwa tija na ufanisi zaidi kuliko inavyofanya kazi hivi sasa.  Aidha mikakati ya kubinafsisha mashirika makubwa yatoayo huduma za miundo mbinu kama vile TANESCO, TTCL, THA, TRC, NIC itaendelea kama vile tulivyokwisha binafsisha Shirika la Ndege na DAWASA.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapropaganda hawa wanapozungumzia Sera ya Ubinafsishaji wanatengeneza picha ya kuwafanya Wananchi kuona kuwa matatizo yote ya kiuchumi Tanzania yanaletwa na Ubinafsishaji.  Hii si kweli.  Uchumi hujengwa na utendaji bora wa sekta zote zinazozalisha moja kwa moja.  Aidha, ufumbuzi wa matatizo ya jamii kama Afya, Elimu, Maji husaidia sana kukua kwa uchumi.  Ni vyema tukaelewa kuwa Ubinafsishaji  ni moja ya mbinu za kurekebisha uchumi wa nchi ambao kwa Tanzania ni asilimia 2 tu ya mikakati yote ya urekebishaji inayofanyika.  Upo urekebishaji wa sekta ya fedha, sekta ya barabara, sekta ya uchukuzi, sekta ya sheria, sekta ya utumishi nk.  Ubinafsishaji unagusa  sekta nyingi za uzalishaji wa moja kwa moja.  Mimi naamini kwa dhati kuwa kama mafanikio ya uchumi na jamii tuliyokwisha kuyapata hivi sasa kutokana na matokeo ya utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji, kama tutajitahidi kuyafanya endelevu, tutapata ufumbuzi wa kimsingi wa matatizo yetu ya kujenga uchumi imara.  Kinachohitajika sasa ni kuendeleza uendeshaji wa mashirika yaliyobinafsishwa hasa kwa Watanzania kwa kuwajengea utamaduni na mazingira ya kuendesha mashirika hayo; na kuwajengea utamaduni wa kutayarisha vyema michanganuo ya kuombea mitaji kutoka taasisi na vyombo vyetu vya fedha.  Utaratibu wa sasa wa Serikali wa uwezeshaji wa wananchi, kuheshimu na kuthaminisha mali za wananchi ki haki, na sheria za ardhi zinazowezesha ardhi kuwa dhamana ya kuchukulia mikopo itasaidia sana katika kuimarisha shughuli za kiuchumi za Watanzania.

 

          Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Chama cha Mapinduzi kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kiwatahadharishe wale wapotoshaji wa maksudi wa Sera ya Ubinafsishaji kwa sababu zao tu za kisiasa.  Wananchi tuwahamasishe na tuwaelimishe.  Nami naamini penye ukweli wataelewa na nina hakika hivi sasa wameshagundua upotoshaji huu wenye malengo ya kisiasa hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.  Kama Mataifa mengine yanaiongelea na kupongeza ufanisi wa uchumi tuliokwisha upata kwa nini CCM tusijigambe na kuongeza juhudi zetu za kuimarisha uchumi.  Ubinafsishaji si suala tu la kuuza Mashirika ya umma, bali ni mfumo unaojenga mashirikiano ya kudumu baina ya wawekezaji wa nje, Serikali na Wawekezaji wa ndani kwa nia ya kuongeza ufanisi, kuboresha utendaji kupanua uwigo wa ajira, kuongeza ubora wa bidhaa na kuyapatia mitaji na utaalam mashirika yaliyobinafsishwa.

 

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tumekuwa tukijigamba Tanzania ni nchi ya amani na usalama, mazingira mazuri, hali nzuri ya hewa n.k.  Haya tunayo.  Tuongelee sasa yale ambayo hatuna, kama vile teknolojia, mitaji, ujuzi, menejimenti bora nk.  Haya yote tutayapata ikiwa mafanikio na matokeo ya Sera ya Ubinafsishaji kwa uchumi wetu tutayafanya endelevu.  Nina imani ya dhati kabisa Wanasiasa Wapinzani, wanapropaganda, baadhi ya wasomi na wale wanaowapotosha wananchi kwa maksudi juu ya Sera ya Ubinafsishaji, kwa mtazamo wa kisiasa, hususan Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005 watashindwa hivi karibuni tu.  Mhe. Mwenyekiti, kama nilivyosema, siasa hivi sasa ni Uchumi, na Mazingira ya Uchumi yanabadilika haraka haraka.  Huko tunakoelekea hatutaweza hata kidogo kuepukana na mabadiliko haya.  Tulianza na Uchumi funga; tukaingia Uchumi huria ulioandamana na mipango mingi ya kurekebisha muundo na mfumo wa uchumi, tunashuhudia zoezi la ubinafsishaji na uwekezaji; hivi sasa tumeingia katika kuimarisha Sekta Binafsi na Uwekezaji, na kama vile hili halitoshi tunapambana sasa na Sera ya Utandawazi.  Mabadiliko haya yanaweza kueleweka na wachache wetu sisi hapa ndani kama viongozi, lakini kwa wananchi haya mabadiliko ni ya kasi kubwa.  Inawezekana yasieleweke vizuri.  Hali hii sasa inatulazimisha kama Chama, kinachotegemea kutawala kwa muda mrefu ujao kuandaa mpango kabambe wa kuandaa Makada wa Uchumi wa CCM kufundishwa mabadiliko haya ya Uchumi yanayotokea hivi sasa kwa haraka ili waeneze hali hii kwa Wanachama, Wakereketwa na Wananchi wote kwa ujumla wanaokitakia mema Chama cha Mapinduzi ili nao waelewe tunakoelekea.  Nadhani kwa nguvu za Chama chetu hili linaweza kufanikishwa, sambamba na kuwakomesha wapotoshaji wa maksudi wa Sera zetu nzuri za Uchumi za CCM.

 

          Nawashukuru kwa kunisikiliza  Kidumu Chama cha Mapinduzi.

 

 

 

 Ahsanteni sana !