RAI YA KATIBU MKUU KWA JUMUIYA YA KIMATAIFA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Philip Mangula ametoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono jitihada za kuimarisha demokrasia pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali za kudumisha utulivu na utangamano nchini.
Ndugu Mangula ametoa rai hiyo leo Mjini Dar es Salaam wakati akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Nchi za Jumuiya ya Madola (FCO) Kitengo cha Afrika katika Serikali ya Uingereza, Bw. James Bevan.
Amesema pamoja na kuwa kimsingi masuala ya kuendesha demokrasi, kudumisha amani, utulivu na utangamano ni jukumu la nchi yenyewe lakini yapo mambo ambayo yanahitaji msaada wa marafiki mathalani kugharimia miundo mbinu.
Katibu Mkuu wa CCM ameutaja mpango wa Serikali wa kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kama moja ya mambo yanayohitaji msaada ili kuimarisha demokrasia nchini.
Amesema pamoja na shabaha ya kudumisha demokrasia, mpango huo utakapokamilika utasaidia kujenga utangamano zaidi nchini kwa vile ni mpango uliokubaliwa kama sehemu ya utekelezaji wa MUAFAKA baina ya CCM na Chama cha Wananchi (CUF).
Ndugu Mangula amesema kwa vile CCM wakati wote inapenda nchi iwe na amani na utulivu, itahakikisha Daftari hilo linaanzishwa na mambo mengine yaliyokubaliwa katika MUAFAKA yanatekelezwa. Pia amesema CCM itawakemea wote watakaodiriki kukwamisha utekelezaji kwa namna yoyote ile.
Bw. BEVAN pamoja na mambo mengine alitaka kujua kuhusu matarajio ya CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu mwakani ambapo Ndugu mangula alisema CCM ina uhakika wa kupata ushindi mkubwa.
Alizitaja sababu za matarajio hayo kuwa ni hali ya kisiasa ilivyo nchini ambapo CCM inaendelea kukubalika kila kukicha.
Alitoa mfano wa ushindi katika chaguzi ndogo za Ubunge na Udiwani na Uchaguzi mdogo wa Mitaaa kuwa moja ya vielelezo vya ongezeko la kukubalika kwa CCM.
Katika safari yake kuonana na Katibu Mkuu wa CCM, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Bw. Bevan alifuatana na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Bw. Andrew Pocock.
Imetolewa na:
Ofisi ya Katibu Mkuu
Makao Makuu, Ofisi Ndogo
DAR ES SALAAM
3/2/2004