KATIBU MKUU WA CCM, NDUGU PHILIP J. MANGULA AELEZEA MAAMUZI YA KIKAO CHA HALMASHAURI KUU YA TAIFA (NEC) YA CHAMA CHA MAPINDUZI
KWA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 31/01/2004
1.0 UTANGULIZI:
Kama mnavyofahamu, Halmashauri Kuu ya
Taifa ya Chama Cha Mapinduzi ilikutana mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti
wa CCM, Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa kuanzia tarehe 27-29/01/2004.
Kikao cha NEC kilijadili masuala mbali
mbali yaliyowasilishwa kwake na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo
nayo ilikutana mapema mjini Dar es Salaam kuanzia tarehe 20-22/01/2004.
Mkutano ulianza na Semina kuhusu
Ubinafsishaji ambayo ilihudhuriwa na Wajumbe wa NEC na nyinyi Wanahabari
mlikaribishwa kuhudhuria wakati wa ufunguzi na ufungaji wa Semina hiyo ambayo
ilikuwa ya mafanikio sana.
2.0
AGENDA ZA NEC:
Dondoo za agenda ambazo miongoni mwa
mengine, zilihusiana na mambo yafuatayo:-
(a) Hali ya Siasa nchini,
(b) Uteuzi wa wagombea nafasi za uongozi katika
Jumuiya za CCM za WAZAZI na VIJANA,
(c) Kuweka utaratibu bora zaidi wa kuwapata
wagombea wa CCM katika vyombo vya Dola,
(d) Uhuishaji wa Muundo wa Chama Cha Mapinduzi.
3.0
HALI YA KISIASA:
Halmashauri Kuu ya Taifa ilipokea taarifa
ya uchaguzi mdogo wa Madiwani uliofanyika tarehe 11/01/2004 katika Kata 41
Tanzania Bara.
Tume ya Uchaguzi (NEC) imekwisha tangaza
rasmi kwamba katika chaguzi hizo, CCM imeshinda katika Kata 39 kati ya Kata
41. Maana ya matokeo haya ni kwamba CCM
tumeweza kushinda tena katika Kata zote 37 zilizokuwa zikishikiliwa na Madiwani
wetu ambao walifariki dunia na kuziacha wazi.
Aidha, CCM tumefanikiwa kuzinyakua Kata
mbili kati ya nne zilizokuwa zikishikiliwa na upinzani kabla ya uchaguzi mdogo
huo uliofanyika tarehe 11/01/2004. Kata
tulizowapokonya wapinzani ni za Nkome, Wilaya ya Bariadi Mkoani Shinyanga na
ile ya Masama Rundugai iliyopo katika Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
Matokeo haya ni kielelezo dhahiri cha
jinsi CCM inavyokubalika kwa Watanzania kutokana na sera zake sahihi na
zinazotekelezeka.
Ushindi huu wa asilimia 95% ni ushahidi
tosha kwamba CCM inaendelea kuwa NAMBARI WANI nchini. Aidha, ni ushindi wa wazi wa jinsi sera za
wapinzani za vitisho, matusi na upotoshaji zinavyokataliwa na wananchi
wanaoitakia mema nchi yetu.
Hivyo basi, Halmashauri Kuu ya Taifa
imetoa pongezi kwa Madiwani wote wa CCM walioshinda katika uchaguzi huo, na
viongozi wa ngazi zote za uongozi walioongoza mapambano hayo. Aidha, imewapongeza na kuwashukuru wana-CCM
na wananchi waliokiunga mkono Chama Cha Mapinduzi na kutuwezesha kupata ushindi
huo mkubwa na wa kishindo. ALUTA
CONTINUA.
4.0
UTEUZI WA WAGOMBEA WA NAFASI ZA
UONGOZI KATIKA JUMUIYA ZA WAZAZI NA VIJANA
Kama tulivyokwisha watangazieni hapo
awali Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake hiki ilifanya uteuzi wa
mwisho wa wanachama walioomba kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika
Jumuiya za WAZAZI na VIJANA, ngazi ya Mkoa na Taifa.
Kwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Jumuiya za CCM
hufanyika kila baada ya miaka mitano kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa,
Halmashauri Kuu ya Taifa imezipongeza Jumuiya za WAZAZI na VIJANA kwa
kukamilisha uchaguzi hadi kufikia ngazi ya Wilaya, na imezihimiza Jumuiya hizo
kuendelea kukamilisha chaguzi hizo katika ngazi zilizobaki za Mkoa na Taifa.
Aidha, Halmashauri Kuu ya Taifa imetoa
pongezi maalum kwa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) kwa
kukamilisha uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa. Imewapongeza pia viongozi wote
waliochaguliwa katika ngazi mbali mbali za Jumuiya hiyo.
5.0 UTARATIBU WA KUWAPATA WAGOMBEA WA CCM
KATIKA CHAGUZI ZA VYOMBO VYA DOLA
A. Utaratibu
wa kumpata Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Halmashauri
Kuu ya Taifa baada ya kupokea na kutafakari juu ya Mapendekezo ya Kamati ya
Kupendekeza Namna Bora Zaidi ya Kuwapata Wagombea wa CCM Katika Chaguzi za
Vyombo vya Dola, imeamua katika maeneo mbali mbali kama ifuatavyo:-
·
Wanachama wote wanaopenda kuwania nafasi ya Urais na wanazo sifa
zinazotakiwa wajaze fomu na kuziwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM katika muda
utakaokuwa umewekwa, kupata wadhamini na kulipa ada kwa viwango vilivyowekwa
katika Kanuni za sasa. Utaratibu wa
sasa unasema kwamba kila mgombea wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya CCM anatakiwa
apate wadhamini 250 kutoka mikoa isiyopungua 10, angalao miwili kati ya hiyo
iwe ni mikoa ya Tanzania Zanzibar.
·
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itawachuja wagombea wote kwa
kupitia sifa zao na kutoa maoni na mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya
Taifa ya majina yasiyozidi matano.
·
Halmashauri Kuu ya Taifa itafikiria na hatimaye kupiga kura za siri
za kupendekeza majina yasiyozidi matatu na kuyawasilisha mbele ya
Mkutano Mkuu wa Taifa kwa uteuzi wa mwisho.
·
Mkutano Mkuu wa Taifa utapiga kura za siri kumchagua mgombea
Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM.
B. Utaratibu wa kumpata Mgombea Urais wa
Zanzibar
Kuhusiana
na namna ya kumpata Mgombea Urais wa Zanzibar, Halmashauri Kuu ya Taifa imeamua
utaratibu ufuatao:-
·
Wanachama wote wanaopenda kuwania nafasi hiyo na wanazo sifa
zinazotakiwa, wajaze fomu na kuziwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM katika muda
uliowekwa, pamoja na kupata wadhamini na kulipa ada kwa viwango vilivyowekwa
katika Kanuni za sasa.
·
Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa itawachuja wagombea wote kwa
kupitia sifa zao na kutoa maoni na mapendekezo yake mbele ya Kamati Kuu, bila
kuwapigia kura wagombea hao.
·
Kamati Kuu itafikiria na kupendekeza majina yasiyozidi matatu
na kuyawasilisha mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa uteuzi wa mwisho.
·
Halmashauri Kuu ya Taifa itapiga kura za siri za kuchagua jina
moja la mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
C. Suala la Wakati Muafaka wa Kuteua na
Kutangaza Wagombea wetu wa Urais wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Wagombea
Urais wa Zanzibar
Halmashauri Kuu ya Taifa ilikubali
kwamba utaratibu unaotumika katika kuteua wagombea wa Urais wa Jamhuri ya
Muungano na wa Zanzibar ufanyike ifuatavyo:-
(a)
Kwamba zoezi zima la uteuzi wa
wagombea wa ngazi hiyo lifanyike na kukamilika, angalau miezi sita kabla
ya siku ya Uchaguzi wenyewe.
(b)
Kwa kuwa Uchaguzi Mkuu hufanyika
mwishoni mwa mwezi Oktoba wa mwaka husika, zoezi la uteuzi wa wagombea wa ngazi
hiyo liwe limekamilika ifikapo tarehe 30 Aprili ya mwaka wa Uchaguzi Mkuu.
D. Utaratibu wa Kuwapata Wagombea
Ubunge/Uwakilishi:
Halmashauri
Kuu ya Taifa imeamua kuweka utaratibu mpya ufuatao wa kuwapata wagombea
Ubunge/Uwakilishi katika hatua ya kura za maoni:
Kura
za maoni zipigwe na Mkutano Mkuu wa Jimbo la Uchaguzi utakaowashirikisha
Viongozi wengi zaidi wa CCM kutoka katika Kata/Wadi, pamoja na Matawi.
E. Utaratibu wa Kuwapata Wagombea Udiwani:
Halmashauri
Kuu ya Taifa imeamua uendelee utaratibu wa sasa ambapo wagombea
wanapigiwa kura za maoni katika Mikutano ya Wanachama wote wa Matawi ya
Kata/Wadi inayohusika.
6.0
KUHUISHA MUUNDO WA CHAMA CHA MAPINDUZI
Halmashauri Kuu ya Taifa baada kupokea
taarifa ya Kamati ya Kuhuisha Muundo wa Chama Cha Mapinduzi na kuzingatia
mapendekezo ya Kamati Kuu, ilipitisha maamuzi yafuatayo ya msingi
kuhusiana na uhuishaji wa muundo wa Chama Cha Mapinduzi:
A. CCM Kuendelea kuwa Chama cha Umma (Mass
Party):
Chama
Cha Mapinduzi kiendelee kuwa Chama cha Umma kama ambavyo kimekuwa siku zote
tangu enzi za TANU na ASP.
B. Marekebisho ya Idara za Makao Makuu
Yamefanywa
marekebisho ya Idara za Makao Makuu ya Chama ambapo sasa zitakuwapo Idara
zifuatazo:-
(a)
Organaizesheni (badala ya Mipango),
(b)
Itikadi na Uenezi (badala ya Uenezi),
(c)
Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Idara
mpya),
(d)
Uchumi na Fedha (badala ya Fedha),
(e)
Utawala na Uendeshaji.
Katika
ngazi za Mikoa hadi Tawi, Idara hizo zitakuwa na sura zifuatazo:-
(a)
Organaizesheni (itaongozwa moja kwa
moja na Katibu wa CCM wa ngazi husika),
(b)
Siasa na Uenezi,
(c)
Uchumi na Fedha.
7.0
PONGEZI MAALUMU:
Halmashauri Kuu ya Taifa ilitoa pongezi
zake kwa Kamati ya Kuhuisha Muundo wa Chama Cha Mapinduzi na Kamati ya
Kupendekeza Namna Bora zaidi ya kuwapata wagombea wa CCM katika chaguzi za
vyombo vya Dola kwa kukamilisha kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Kamati ya Kuhuisha Muundo wa Chama Cha
Mapinduzi iliyoteuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa na
Wajumbe wafuatao:-
(a)
Ndugu Kingunge Ngombale-Mwiru - Mwenyekiti
(b)
Ndugu Omar R. Mapuri - Mjumbe
(c)
Ndugu Jackson Msome - Mjumbe
(d)
Ndugu Anna Abdallah - Mjumbe
(e)
Ndugu Yussuf Mohamed Yussuf - Mjumbe
(f)
Ndugu Amina Salum Ali - Mjumbe
(g)
Ndugu Juma S. Nkumba - Mjumbe
(h) Ndugu Emmanuel John Nchimbi -
Mjumbe
Kamati ya Kupendekeza
namna bora zaidi ya kuwapata wagombea wa CCM katika chaguzi za vyombo vya Dola
ilikuwa na Wajumbe wafuatao:-
1.
Ndugu Pius Msekwa - Mwenyekiti
2.
Ndugu Abdulrahaman Kinana - Mjumbe
3.
Ndugu Omar R. Mapuri - Mjumbe
4.
Ndugu Jackson Msome - Mjumbe
5.
Ndugu Mohamed Seif Khatib - Mjumbe
6.
Dr. Maua Daftari - Mjumbe
7.
Ndugu Chrisant Mzindakaya - Mjumbe
8.
Dr. Mary Nagu - Mjumbe
9.
Ndugu Amina Salum Ali - Mjumbe
10.
Ndugu Pancras Ndejembi - Mjumbe
11.
Ndugu Haji Omar Kheri - Mjumbe
12.
Ndugu Juma S. Nh’unga - Mjumbe
NB: SIFA ZA MSINGI KUHUSU WAGOMBEA URAIS
ZILIZOWEKWA NA NEC MWAKA
1992
1.
Awe na uzoefu mkubwa wa kuongoza Taifa kwa
kuzingatia uzoefu wake katika uongozi wa shughuli za Serikali, umma na Taasisi.
2.
Awe Mwadilifu, mwenye Hekima na Busara.
3.
Awe na angalau kiwango cha Elimu ya Chuo Kikuu au
elimu inayolingana na hiyo.
4.
Awe mwenye upeo na uwezo mkubwa wa kudumisha,
kuimarisha na kuendeleza Muungano wetu, Umoja wetu, Amani na Utulivu wetu na
Mshikamano wa Kitaifa.
5.
Awe mtu mwepesi wa kuona mbali, asiyeyumbishwa na
mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara kuhusu masuala nyeti na muhimu ya
Taifa kwa wakati unaofaa.
6.
Awe na upeo mkubwa na usiotiliwa shaka kuhusu
masuala ya Kimataifa ili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi yetu na Dunia
yote kwa jumla.
7.
Asiwe mtu mwenye hulka ya udikteta au ufashisti bali
awe mtu anayeheshimu na kulinda Katiba ya Nchi, Sheria, Utawala Bora, Kanuni na
Taratibu za Nchi.
8.
Awe mtetezi wa wanyonge, wa Haki za Binadamu,
mzingatiaji makini wa maendeleo ya raia wote na asiwe na tamaa ya kujitafutia
umaarufu wa mtu binafsi.
9.
Awe mstari wa mbele katika kuzifahamu, kuzieleza,
kuzitetea na kuzitekeleza sera za CCM na Ilani ya CCM ya Uchaguzi.
10. Awe mpenda haki na awe mtu jasiri katika kupambana na
dhuluma
na maovu yote nchini.
11. Asiwe ni mtu ambaye anatumia nafasi yake ya uongozi
kujilimbikizia
mali.
12. Kwa ujumla awe ni mtu anayekubalika na wananchi.
13. Awe mtu
makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji wa
Viongozi/Watendaji na asiyevumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu/wajibu waliokabidhiwa ili kuinua Nidhamu ya Kazi, Tija na Ufanisi.