CUF ondoeni mkosi, safari ijayo msimpe nafasi Seif Sharif Hamad kugombea urais

 

 

SEIF Sharif Hamad baada ya kushindwa uchaguzi uliopita huko Zanzibar, anasema

kwamba uchaguzi ujao 2010 atagombea tena. Inashangaza sana kusikia hivyo. Hivi

Seif anaona Zanzibar hakuna watu wengine wenye uwezo wa kugombea urais kwa tiketi

ya CUF zaidi yake, au haoni aibu kwamba sasa awape nafasi na wenzake wengine ili

nao wajaribu bahati yao ?

Kama ni urais angekuwa amekwisha kaa miaka 15, muda ambao ni zaidi ya ule wa

miaka kumi ya kikatiba. Lakini kapitisha miaka mitano, hivi katika vyama

tuendelee kuruhusu tu ? Mtu kashindwa safari ya kwanza, safari ya pili na safari

ya tatu. Bado waendelee tu kumpa nafasi kugombea kana kwamba katika CUF hakuna

watu wengine wa kuweza kugombea nafasi hiyo na kukipa CUF

ushindi ?

Inafurahisha sana kuona kwamba sasa Seif anabadili kauli, kwa kudai kwamba

amemshinda Karume kwa asilimia 50.7 badala ya madai yake ya awali kwamba

ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 57.

Anadai kwamba ana uhuru wa kufanya hivyo. Sawa, kwa vipindi vitatu mfululizo

uchaguzi baada ya uchaguzi anagombea, na anashindwa. Hivi wana CUF kweli

wanamhitaji tena, kwamba kila uchaguzi anashindwa, na bado wanampa nafasi

kuendelea kugombea ? Si ingekuwa bora wakaondoa mkosi kwa kuchagua mwanachama

mwingine akagombea nafasi hiyo labda huenda kikafanikiwa kuondoa mkosi na kupata

urais katika

uchaguzi ujao ?

Kwa kutokubali kushindwa Seif anazidi kuthibitisha udhaifu wa wanasiasa wa Afrika

kwa kutokubali matokeo ya kura halali, kwani hata katika uchaguzi wa Liberia

George Weah kama Seif Sharif Hamad, alidai kuchezewa rafu katika uchaguzi huo kwa

madai kwamba alishindwa kutokana na wizi wa kura, akidhani kwamba umaarufu wake

katika soka, kwa kupigiwa kelele mitaani ndio kungempa ushindi wa urais Liberia.

Hebu atuambie uchaguzi halali ni upi na unakuwa kuwaje ? Anataka sasa uchaguzi

urudiwe na kusimamiwa na taasisi za nje. Daftari la kuandikisha wapiga kura

halikufaa ?

Suala la daftari la kuandikisha wapiga kura lilikuwa agenda kubwa sana kwa CUF,

na waliishikilia hadi kukubalika katika muafaka. Sasa inakuwaje tena wanageuka na

kuliponda hilo daftari na kudai uchaguzi mwingine, na usimamiwe na taasisi za

nje?

Taasisi za nje kama zitasimamia uchaguzi ndio wataweza kubadili utashi wa

wananchi wa Zanzibar ili CUF ishinde ?

Seif Sharif si mjinga kiasi hicho, cha kutoweza kutambua kwamba uchaguzi uliopita

Zanzibar ulikuwa halali, na matokeo yanatoa sura sahihi ya matakwa ya wananchi

wapiga kura wa visiwa hivyo.

Hebu tuanze na kuangalia madai ya wizi wa kura. Inawezekana kweli katika uchaguzi

uliopita Zanzibar, kulikuwa na uwezekano wo wote wa kura kuibwa kwa kuzingatia

jinsi wafuasi wa CUF walivyokuwa macho na makini kuhakikisha kwamba wapiga kura

katika maeneo yote walikuwa wapiga kura halali ?

Kitu kingine ni kwamba, wapiga kura wote walikuwa watu walioandikishwa kihalali

kwenye daftari la wapiga kura, na kura zote zilihesabiwa vituoni. Nani kamwibia

kura mwenzake ? Jibu ni kwamba hakuna chama cho chote kilichoiba kura, na matokeo

ya upigaji kura yalikuwa ni utashi wa wapiga kura wa Zanzibar, na kila mtu

analazimika kukubali kwamba hayo ndiyo matokeo halali.

Napenda kukiri kwamba Zanzibar kulikuwa na ushindani mkubwa kati ya Rais amani

Abeid Karume wa CCM na Seif Sharif Hamad wa CUF. Ushindani huo pia imejitokeza

kati ya wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani na hivyo kujitokeza kwa changamoto

kubwa miongoni mwa wapiga kura. Baada ya kupiga kura wananchi walikuwa na shauku

kubwa kuyapata matokeo.

Matokeo yalipoanza kutangazwa hadi mwishoni ilionekana dhahiri kwamba huko Pemba

CUF ndiyo yenye nguvu, na Zanzibar CCM ndiyo imeshika hatamu, na baada ya

kujumuishwa na kuhesabiwa kura zote CCM ndiyo iliyojitokeza mshindi.

Kwa matokeo hayo, na kama kungekuwa na wizi wa kura basi CCM ingeshinda kura huko

pemba ambako CUF ndiyo ina nguvu, au kama CUF ingeiba kura basi ingeshinda

Zanzibar ambako CCM ndiyo yenye nguvu. Sasa kwa matokeo hayo nani amemwibia

mwenzake kura ? Jibu la mwenye akili timamu ni kwamba hakuna aliyemwibia mwenzake

kura matokeo ya kura yameonyesha nguvu ya kila chama katika eneo lake…

Kwa upande mwingine matokeo hayo ni funzo kwa vyama vya CUF na CCM kwamba upigaji

kura ulio huru na kama ulivyojitokeza Zanzibar ni kigezo sahihi kinachoonyesha

nguvu za kweli za kila chama huko visiwani, na kama ndiyo hivyo, ni bora kuanzia

sasa kwa kila chama, kama kinataka kukamata dola mwaka 2010 ni lazima kuanzia

sasa kuweka mikakati ya kuimarisha nguvu ya vyama vyao tayari kwa uchaguzi wa

2010.

Haitasaidia chochote kwa sasa kulalamikia matokeo ya uchaguzi halali, kwani

matokeo hayo ndiyo matakwa ya wananchi. Kushindwa kwa wingi wowote wa kura ni

ushindi unaokubalika katika taratibu zote za kidemokrasia, hivyo aliyeshindwa

anapaswa kukubali. Vinginevyo asiyekubali kushindwa si mshindani.

simu: 0744 - 464279

e-mail: mhando3@hotmail.com