Lipumba: Mgombea urais wa CUF aliyejaa majisifu ya usomi

  • Lakini ‘mtupu’ katika kunadi sera mpya
  • Wengi walijitokeza kumwona anafananaje

KAMPENI kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu zimepamba moto. Vyombo mbalimbali vya habari haviko nyuma katika kufuatilia habari hizo za kampeni kama Mwandishi Wetu GODFREY MHANDO alifuatilia ziara ya siku kumi ya kampeni za urais za Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba katika Mikoa ya Kusini ya Ruvuma, Mtwara na Lindi kutokea Mbeya. Ifuatayo ni ripoti yake…

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba amemaliza awamu ya kwanza ya ziara ndefu iliyomchukua siku kumi katika mikoa ya Kusini, akifanya kampeni za kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Oktoba.

Juzi alilala Dar es Salaam na asubuhi yake jana aendelea na awamu nyingine ya  ziara hiyo katika mikoa ya Kati, akitokea Mkuranga mkoa wa Pwani na kuunganisha miji ya Manyoni na Singida.

Ziara hiyo ya mikoa ya Kusini, ambayo mimi niliifuatilia ‘nyuma nyuma’ kutokana na kunyimwa usafiri katika ‘kanvoi’ yake, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukosekana kwa nafasi ndani ya magari, niliungana nayo mkoani Mbeya na kwa muda wa siku kumi zilizofuata tulitembelea mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.

Nadhani nilinyimwa lifti katika magari ya ‘kanvoi’ ya Lipumba si kwa sababu hakukuwa na nafasi, bali bila shaka ni kwa sababu nilitokea katika magazeti ya ‘Uhuru’, magazeti ambayo yanaonekana kama ni chombo cha upinzani, na kwa imani yao haliwezi kuandika habari zozote nzuri za CUF.

Nilisafiri kwa kurukia mabasi kutoka basi moja na kuendelea na basi lingine katika msafara mzima kutoka Mbeya na katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi hadi kurejea Jijini.

Nini kilichojiri katika ziara hiyo?

Katika kampeni zo zote za kisiasa ili upate kura ni lazima unadi sera kwa kuwaeleza wananchi nini unachotarajia kufanya iwapo utachaguliwa katika nafasi unayoiomba.

Profesa Lipumba na wapambe wake katika kampeni yake kikubwa anachokinadi ni uwezo wa elimu yake kama mchumi… Lakini pia anasema kwamba CUF ikiingia madarakani itaboresha elimu na huduma za afya, mambo ambayo CCM pia imeyaainisha wazi katika sera zake za maendeleo ambazo si ngeni kwa wananchi na pia zimo katika utekelezaji.

Nchi hii ina wasomi wengi, wanaofaa kuwa viongozi, maprofesa wenye kisomo cha juu kama ama zaidi ya Lipumba, na kama ni suala la uongozi, digirii saba ama kumi si kigezo pekee cha uwezo wa mtu kustahili kuwa kiongozi.

‘Lipumba ana nne, Kikwete ana moja’ ndio wimbo mkubwa wa wapambe wa kiongozi huyo kila walipopita wakiomba kura, wakiwa na maana kwamba Lipumba ana digrii nne wakati Kikwete ana digrii moja, na kwa maana hiyo yeye ni msomi mwenye uwezo na kustahili kuwa rais.

Niliianza ziara na kikosi cha Lipumba chenye magari manne. Wakiwa ndani ya magari mimi niliwafuata nyuma nyuma hadi Songea, lakini katika maeneo mengi, licha ya kunyimwa ‘lifti’, nilikuwa wa kwanza kuwasili huko. Kitu hiki kiliwachanganya, kuwauma na kuwashangaza wapambe wake, hasa wakizingatia kwamba nilikuwa nikisafiri kwa basi, na wao wakienda kwa magari. Lakini kilichonisaidia ni kusoma ratiba yao iliyokuwa ikibadilika mara kwa mara na ambayo hawakuwa tayari kunipatia.

Nilijaribu kuwahoji wapambe wake kila nilipopata nafasi waniambie nini kilikuwa kinafuata. Kwa mfano, niliuliza baada ya mkutano huu mwenyekiti anaelekea wapi? “Hatuna hakika, tutakuwa na kikao jioni saa mbili… baada ya hapo ndipo tutajua mwelekeo. Wewe usiwe na wasiwasi, tutakupigia simu kukuarifu”, ndio majibu ambayo kila wakati nilikuwa nikipatiwa, bila shaka kwa nia ya kunikwepa na kunipotezea dira na mwelekeo wa msafara.

Hata mimi pia sikuamini maelezo yao, hivyo wakati nikisubiri kupigiwa simu, jambo ambalo halikutokea hata siku moja, pia nilipanga mikakati ya msafara wangu. Walikuja tahamaki kunikuta nimekwisha wasili pale wanapokwenda.

Tulitoka Mbeya kuelekea Songea mkoa wa Ruvuma, kutoka hapo msafara ulielekea Tunduru, Masasi, Mtwara na Lindi. Katika maeneo hayo alivuruga na maeneo ya vijijini ambako kote alifanya mikutano iliyokuwa na hotuba zenye mwelekeo wa kueleza uwezo wake kama msomi mahiri na profesa mwenye hadhi ya ‘Fulbright Fellow’ ambao hawazidi hata kumi katika Afrika, mshauri wa mambo ya kiuchumi wa nchi zilizoendelea, mwenye digrii nne za uchumi na ambaye ndiye anayefaa kuwa Rais wa Tanzania.

Lakini hoja ya usomi, uprofesa, na kuwa na digrii nyingi ndiyo vigezo pekee au sifa ya kumfanya mtu aweze kuwa rais wa nchi? Kama hiyo ni hoja ya msingi, Tanzania kuna wasomi wangapi. Wasomi ni kweli wanahitajika, lakini wasomi si wote wenye uwezo wa kuwa marais. Wengi wanastahili kushika chaki na kufundisha darasani, na ukimleta kwenye uwanja wa siasa hauziki.

Kilichonichosha katika ziara ya Lipumba ni kwamba maneno anayozungumza ni yale yale mkutano baada ya mkutano. Hakuna kipya.

Mkutano utaanza kwa mmoja wa wapambe wake kupanda jukwaani na kutoa wasifu wa Lipumba, vyuo alivyosoma hapa nchini, Marekani na shahada alizopata. Baada ya hapo atapanda Lipumba na kuanza kwa kuponda sera za CCM katika maeneo ya uchumi na elimu, na kisha ataeleza kile atakachofanya.

Ukienda ndani ya analosema utakuta anarejea kauli za CCM na sera zake katika kukuza uchumi, huduma bora za afya, ajira ya vijana na kupanua elimu ya msingi – Sasa ni kipi kipya Lipumba anachojaribu kuwaeleza Watanzania?

Pengine kutoa chakula cha mchana anachodai kwamba CUF ikiingia madarakani itahakikisha kinatolewa kwa wanafunzi katika shule zote za msingi, kitu ambacho hakuna hata serikali moja duniani iliyofanikiwa kufanya kwa ukamilifu.

Katika maeneo mengine nilikopata nafasi ya kuzungumza na kuwahoji wananchi, wengi walionekana kuwa na hamu ya kumuona Lipumba anafananaje, kuliko kuvutiwa na sera zake. Wengi, na hasa kinamama, walifika kwenye mikutano yake kwa nia ya kutaka kumwona Lipumba ni nani, na baada ya hapo kubeba watoto wao na kuelekea majumbani kwao.

Lakini hata wanaume nao waliofika mikutanoni na niliopata nafasi ya kuhojiana nao, wengi walisema walitarajia kusikia kitu kipya, lakini  waligundua hakuna jipya zaidi ya majigambo ya Lipumba na kurejea sera za CCM.