Udalali wa visiwa vya Zanzibar sasa hadharani

WAKATI kampeni zikizidi kupamba moto, ahadi hewa na zisizotekelezeka zinazidi kutolewa na vyama vya upinzani. Kuna ahadi za asali na maziwa kutiririka Tanzania Bara na Visiwani, ahadi ambazo hata nchi zenye mafuta na rasilmali za kutisha zimeshindwa kuahidi au hata kujaribu kutekeleza. Makala hii iliyoandikwa na Mwandishi ALLY MWINYIKAI wa Idara ya Habari (MAELEZO) Zanzibar, inaeleza hatari ya kunadiwa  visiwa vya Zanzibar, endapo CUF itaruhusiwa kuingia madarakani na kutekeleza ahadi zake za kufikirika.

TAYARI harakati za kamapeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu zimeanza kwa vyama vya siasa kunadi ilani zao.

Vyama vinafanya hivyo kwa ajili ya kutangaza sera zao kwa wananchi ili wananchi nao wavutike kuwachagua wagombea waliosimamishwa na vyama hivyo katika nyadhifa mbali mbali.

Hapana shaka hiyo ni sehemu ya demokrasia na ni njia moja inayosaidia watu kuwafahamu vyema wanaogombea nafasi  za uongozi na uwezo wao.

Hivyo, katika kufikia lengo hilo wananchi wanapaswa kuzipima sera na Ilani za uchaguzi za kila chama, ili hatimaye wafikie uamuzi wa kuchagua nani anayefaa ufanyike kwa uhakika katika kupata viongozi bora.

Kwa kawaida kila mgombea awe wa nafasi ya Urais, Bunge, Baraza la Wawakilishi au Diwani hujiwekea matumaini ya kushinda na hujiona anao uwezo wa kuongoza katika nafasi aliyoiomba.

Pamoja na imani za aina hiyo walizo nazo wagombea hao, wananchi kwa upande wao nao wana nafasi kubwa ya kupima uwezo wa kila mmoja wao. Ndio maana kukawekwa utaratibu wa kampeni ili wananchi waweze kuamua nani anayewafaa.

Kwa kuwa muda uliosalia kabla ya kufikia siku ya uchaguzi ni mdogo, takriban wagombea wengi wameshaanza kujilabu na kutangaza ilani za vyama vyao. Katika kufanya hivyo, baadhi ya wagombea wamekuwa wakitoa ahadi ambazo hazina mwelekeo wa kuiendeleza nchi zaidi ya kuididimiza kiuchumi na ustawi wa jamii.

AHADI ZA UONGO

Katika kuvisikiliza vyama vya siasa wananchi wana wajibu wa kuwa makini katika kuzipima ahadi zitakazotolewa na wagombea wenyewe au vyama vyao, kwani dalili zimeanza kujitokeza za kutangazwa sera zenye mwelekeo wa kujaribu kuviuza visiwa vya Unguja na Pemba.

Mfano halisi wa ahadi hizo ni ule uliotolewa na Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha  CUF  Seif Sharif Hamad, wakati alipokuwa akizindua kampeni za chama hicho Septemba 8, mwaka huu kwenye uwanja wa Kibanda Maiti mjini Unguja.

Kilichoahidiwa na mgombea huyo ni kwamba chama chake kitakapoingia madarakani kitahakikisha kodi zote za bidhaa zinazoingizwa nchini hazizidi asilimia 10 ya bei ya ununuzi halisi wa bidhaa hizo.

Lengo la ahadi hizo limeelekezwa katika kuwavutia wananchi kuona kwamba bei ya bidhaa zitakuwa chini na hivyo kumpunguzia mwananchi wa kawaida ukali wa maisha katika kupata bidhaa muhimu kwa bei nafuu.

Wazo hili limepokewa na baadhi ya watu kwa furaha na matumaini makubwa kwa kufikiria kwamba huo utakuwa ukombozi wao katika kupambana na hali ya maisha. Lakini kilichokosekana ni juu ya athari za uendeshaji wa jambo hilo na ufanisi wake katika uendelezaji wa shughuli muhimu za kila siku za serikali.

Kodi zinazotozwa katika nchi yoyote zinakuwa ni chanzo kikuu cha mapato ya Serikali. Nchi kama Zanzibar isiyokuwa na madini, mafuta wala viwanda vikubwa hutegemea sana mapato ya ukusanyaji wa kodi.

Ukusanyaji wa kodi ndio unaosaidia shughuli za kuendesha Serikali ikiwemo ulipaji wa mishahara ya wafanyakazi, kugharamia ujenzi wa shughuli za maendeleo kama vile barabara, maji, usambazaji wa umeme na huduma za afya.

Hivyo, kupunguza kiwango cha kodi kwa Zanzibar kuliko tangazwa na CUF ni sawa na kuipunguzia Serikali uwezo wake wa mapato. Linaloshangaza zaidi ni kwamba wakati chama hicho kimekusudia kuipunguzia Zanzibar uwezo wa mapato yake, hapo hapo kinatangaza kwamba kitapandisha mishahara ya wafanyakazi wa Serikali  kwa kiwango kikubwa zaidi.

Ahadi hiyo ya kupandisha kiwango cha mishahara ya wafanyakazi kimewekwa kuwa sh. 100,000 kwa kima cha chini cha msharara. Kiwango cha sasa ni sh. 50,000.

Kwa wataalamu wa uchumi ahadi hizo mbili zilizotolewa na mgombea huyo haziwezi kutekelezeka na ufanisi wa ukuaji wa kiuchumi ukapatikana. Kinachosababisha kushindwa kutekelezeka kwa ahadi hizo ni kwamba mambo hayo mawili yanalingana sana na yanakwenda sanjari. Hivyo, haiwezekani kimoja kupanda na kingine kushuka.

Kwa lugha nyepesi ni kwamba, ukusanyaji wa kodi unapokuwa mdogo maana yake uwezo wa Serikali katika kufanya shughuli zake unakuwa pia mdogo. Ndio maana hata nchi zilizoendelea zimekuwa zikisisitiza wananchi wake kulipa kodi.

Kitu kinachozikasirisha nchi wahisani hivi sasa ni kuona Serikali hasa za bara la Afrika, zimekuwa hazisimamii ipasavyo ukusanyaji wa kodi na badala yake zimekuwa zikitegemea kupata misaada inayotokana na makusanyo ya kodi kutoka kwa wananchi wa nchi hizo zilizoendelea.

 Sasa ilani iliyotangazwa na mgombea wa Urais kupitia CUF imezua maswali mengi yasiyoweza kupatiwa majibu na hasa katika kuangalia mustakabali ya nchi kiuchumi na ustawi wa jamii.

Hivi sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa  ikikusanya hadi sh bilioni 4 kwa mwezi. Makusanyo hayo ni kutokana na aina nne za kodi. Kodi ya uagiziaji asilimia 20, VAT ya uagiziaji asilimia 20, VAT ya biashara za ndani asilimia 20 na Kodi ya mauzo asilimia 10.

SERIKALI IMEJITAHIDI

Katika jitihada za kupunguza ukali wa maisha Serikali ya sasa inasamehe asilimia 50 ya kodi za bidhaa za chakula  zinazoingizwa nchini ikiwa ni pamoja na mchele, sukari na unga wa ngano. Aidha, imesamehe kodi ya mafuta kwa lengo la kuwapa unafuu wananchi na hivyo kufanya bei ya bidhaa hiyo kuwa chini ya kiwango cha bei ya kimataifa. 

Kutokana na mapato hayo chini ya kiwango cha sasa cha kima cha chini cha mshahara ambacho ni sh.50,000 Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya sh bilioni 4.2 kulipia mishahara ya wafanyakazi wake tu mbali ya shughuli nyingine za maendeleo.

Ili CUF iweze kutimiza malengo yaliyotangazwa na mgombea wake wa Urais ya kulipa mishahara kima cha chini sh 100,000 italazimika kuwa na zaidi sh. bilioni 9 kila mwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi waliopo hivi sasa tu mbali ya hao waliotangazwa kuajiriwa zaidi endapo chama hicho kitaingia madarakani.

Kwa matamshi mengine ni kwamba Serikali hiyo inayofikiriwa na CUF kuundwa italazimika kupata ziada ya karibu mara tano ya mapato yatakayokusanya ya sh. bilioni 2.1 kutokana na kodi hiyo ya CUF ambayo haitopindukia asilinia 10. Ziada hiyo ya mara tano itakuwa kwa ajili ya kulipia mishahara tu mbali na ahadi nyingine zilizotangazwa na Maalim Seif kwa kuimarisha sekta ya elimu, afya na kadhalika.

Ili kufikia kiwango cha sasa cha ukusanyaji wa kodi kulingana na kiwango kitakachowekwa na CUF, kutahitajika kuongezeka kiwango kikubwa cha bidhaa zaidi ya mara sita ya bidhaa zinazoingizwa sasa hivi.

Kuongezeka kwa kiwango hicho kutahitaji pia kupanuka kwa soko ambalo litalazimika kuongezeka ambalo lazima nalo liwe nje ya Zanzibar ambayo hivi sasa ina wakazi wapatao milioni moja tu.

CUF ITAKAVYOKWAMA

Tamko la mgombea Urais wa CUF mbali ya kukosa muhimili ya kiuchumi lakini litakabiliwa pia na kikwazo cha kisiasa kwani mwelekeo wake ni wa kujitenga kutoka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Hiyo ni kutokana na juhudi za hivi sasa zinazochukuliwa za kutaka kuweka viwango vya kodi kwa nchi za Afrika ya Mashariki kuwa vya aina moja.

Kwa kuwepo Jumuiya hiyo kwa kiasi kikubwa Zanzibar itapoteza fursa ya kuwa na soko kubwa nje ya visiwa hivyo na kwamba mipango yoyote itakayowekwa Serikali hiyo ya CUF itakwama. Mgogoro wa katiba utaibuka na njia za Zanzibar kujikwamua zitagonga ukuta.

Kujiengua katika Jumuiya hiyo maana yake ni kutoka katika Muungano wa Tanzania na hivyo Zanzibar kuwa na kila kitu chake ikiwemo sarafu yake. Hapa ndipo linapojitokeza tatizo jingine kuwa kubwa katika ugumu wa kutimiza malengo yaliyotangazwa na CUF.

Ugumu huo utajitokeza kwa kuiangalia Zanzibar itakayokuwa na sarafu yake na viwango vyake vidogo vya ukusanyaji wa kodi ambavyo havitaweza hata kulipia robo ya mishahara ya wafanyakazi wake.

Kutokana na mtazamo huo ni kwamba kiwango cha chini cha mshahara wa sh 100,000 kitakachotolewa kitakuwa na ulinganisho wa kiasi gani cha dola ya Marekani. Mizania za uchumi zinaonyesha kwamba kiwango hicho kitakuwa chini ya dola 10 sawa na sh 10,000 za sasa.

Hiyo itatokana na kuwa sarafu hiyo ya Zanzibar kutokuwa na nguvu zozote kwani Zanzibar itakuwa haina rasilimali za kutosha kama vile dhahabu, mafuta na kodi ya kuweza kuudhibiti uchumi wake usididimie na kuyumba. Itakapofikia kiwango hicho na mpango wa Zanzibar kuwekwa zabuni utakuwa umekamilika.

Kwa mantiki hiyo, Zanzibar itakuwa ni nchi ya kwanza ya kupigiwa mfano itakayokuwa na wananchi waliotopea katika ufukara na umasikini wa kupindukia.

Nadharia hiyo itakuwa imeipotezea nchi uwezo uliopo sasa wa kujikwamua katika maeneo ya uchumi na ustawi wa jamii na hivyo ahadi zilizotolewa na CUF za kuboresha elimu, huduma za afya, mawasiliano na huduma nyingine za jamii kama vile maji na umeme itakuwa ni njozi tupu.