Na Abihudi Saideya, Morogoro, 22/09/2005
Wanasiasa ambao wamekuwa wakilidhalilisha taifa na kuomba jumuiya ya kimataifa isitishe misaada ya maendeleo hawafai kupewa uongozi, amesema Mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Akihutubia mikutano ya kampeni kwa nyakati tofauti jana (21/09/05) katika Wilaya ya Morogoro Vijijini Dk. Shein alisema kuna wagombea ambao wamekuwa wakiharibu sifa nzuri ya Tanzania kila wanaposhindwa uchaguzi. Akitoa mfano bila kutaja majina , Dk. Shein alisema baada ya uchaguzi Mkuu wa 1995 na 2000 mgombea mmoja alizunguka sehemu mbalimbali akiomba Zanzibar izuiliwe misaada. “ Kuomba Watanzania wazuiliwe misaada hata ya chanjo , ni kutolitakia mema taifa,” alisema na kuwaomba wananchi wasiwachague viongozi wa aina hiyo. Dk. Shein alisema ushindani wa kidemokarasia hauna maana ya kudharau na kupinga kila kitu kinachofanywa na serikali na akaongeza kuwa hata katika mataifa yaliyobobea kwa demokrasia huwezi kuona wanasiasa wakikebehi na kudhalilisha taifa lao nje ya nchi. Licha ya kuwa hakutaja majina, lakini inafahamika Mgombea wa Urais wa CUF Zanzibar, Bw. Seif Sharif Hamad amekuwa akilalamikia matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na hivi sasa amekwishaanza kampeni ya kuomba mataifa ya nje yafuatilie uchaguzi Mkuu wa mwaka huu akidai hana imani na vyombo vinavyosimamia uchaguzi. Dk. Shein alisema upinzani unatakiwa kuwa katika hoja na akaongeza kuwa vitendo vya kuliponda taifa na kukana mafanikio yake ni mambo ya kujidhalilisha mbele ya jumuiya ya kimataifa. Akizungumza huku akikatizwa kwa vibwagizo vya kushangilia kutoka kwa waketeketwa na wapenzi wa CCM, Dk. Shein alitamba: “ CCM itaendelea kuwabwaga wapinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa ina sera nzuri na inakubalika kwa wananachi wengi”. “ Wapinzani hawana watu, nimetembea karibu nchi nzima wapinzani wachache sana, wakishindwa wanasema wanaibiwa kura, “ alisema na kutaja mfano wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana ambao CCM ilipata ushindi wa asilimia 96.8 ya nafasi zote za uongozi. Aliwaambia wananchi kuwa vitendo vya kuiba kura vinaweza kufanywa na vyama visivyokubalika na akasisitiza CCM haiwezi kufanya hivyo. Dk. Shein ambaye alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Morogoro Bw. Peter Kingu na viongozi wengine wa CCM alihutubia mikutano mikubwa ya kampeni katika Kata ya Kisemu, jimbo la Morogoro Kusini na Kata ya Mbuyuni jimbo la Morogoro Kuisni Masharaiki. Dk. Shein alisema mafanikio yaliyopatika katika kuendeleza huduma za jamaii, ujenzi wa barabara, mawasiliano ya simu na kuimarishwa kwa uchumi chini ya uongozi wa CCM, yanadhirisha uwezo wake katika uongozi na akawaomba wananchi wamchague Mgombea Urais Bw. Jakaya Kikwete, wagombea Ubunge na Udiwani waliosimamishwa na Chama Cha Mapinduzi. Alisema mwaka huu CCM inatarajia kupata ushindi mkubwa zaidi na kama vyama vyama vya upinzani vitakufa itakuwa uamuzi wao wenyewe, “serikali haitafuta mfumo wa vyama vingi” alisisitiza. Katika mikutano hiyo miwili iliyofanyika Wilaya ya Morogoro Vijijini Dk. Shein aliwapokea wanachahama 193 wa vyama vya upinzani waliovikimbia vyama hivyo na kujinga Chama Cha Mapinduzi. Wachama hao walikuwa ni wa vyama vya CUF - 133, UDP - 53, TLP - 3, NCCR – 3 na TADEA mmoja. Miongoni mwa wanachama wa upinzani walioamua kuachia ngazi ni Katibu Kata wa TLP Bw. Amos Lubacha , jimbo la Morogoro Kusini na Katibu Mwenezi wa UDP Kata ya Kiloka, jimbo la Morogoro Kusini Mshariki Bw. Mkasi Said.