CCM na mikakati ya
ushindi Temeke
KATIKA kipindi hiki cha kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao, watu wasiojua
siasa za Temeke, 'wanaropoka' kwamba miongoni mwa majimbo yanayotajwa kuwa
huenda yakaangukia kwa wapinzani ni pamoja na lile la Temeke, mkoani Dar es
Salaam kwa madai kwamba limekuwa na historia
fupi ya kuongozwa na wapinzani. Hata hivyo wenye mwelekeo huo wanasahau kuwa
kuna nafasi kubwa ya jimbo hilo kwenda CCM kutokana na siri iliyofichika. Ni
siri gani hiyo? Mwandishi THOMAS MTINGE, anafafanua katika makala hii.
JIMBO la Uchaguzi la Temeke mkoani Dar es Salaam katika nafasi ya ubunge kabla
ya Uchaguzi Mkuu wa sasa lilikuwa chini ya CCM ambapo mbunge wake alikuwa
Khadija Kusaga.
Mgombea huyo wa CCM katika uchaguzi wa kura za maoni hakupata nafasi ya
kuteuliwa kutetea kiti chake na badala yake nafasi hiyo imechukuliwa na Abbas
Mtemvu ambaye anapeperusha bendera ya CCM katika kinyang'anyiro cha ubunge.
Wakati joto la kuwania nafasi hiyo likizidi kupanda kwa kuwa siku nazo
zinakaribia kuchagua viongozi, kumejitokeza baadhi ya wanaojiita watabiri wa
masuala ya siasa na watu wengine kwa ajili ya kutoa maoni mbalimbali huku
wakielezea kuwa jimbo hilo linaweza kuchukuliwa na upinzani na hasa chama cha
CUF.
'Watabiri' hao wanataja sababu nyingi mbalimbali lakini baadhi ni kuwa mgombea
wa CUF Tambwe Hizza ambaye amewania nafasi hiyo mara tatu sasa lakini bila
mafanikio, amepata ukomavu na uelewa mkubwa wa kisiasa hivyo kuwa rahisi
kushinda.
Wanasema kuwa kitendo cha Tambwe kupata nafasi hiyo tena, kinampa fursa ya
kuibuka na ushindi dhidi ya mgombea wa CCM.
Sababu nyingine inayotajwa ni kuwa wananchi wa jimbo hilo wameshawahi kuwapa
wapinzani ushindi kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa sasa wa TLP Augustine Mrema
ambaye alipata kuongoza jimbo hilo akiwa NCCR-Mageuzi.
Mrema alikuwa mbunge wa Temeke hadi alipotangaza kujiengua kutoka NCCR-Mageuzi
na kujiunga na Tanzania Labour ambapo kisheria alikuwa amepoteza wadhifa wake wa
ubunge.
Lakini jingine linalotajwa kuwa litachangia ushindi kwa CUF ni kuwa jimbo hilo
eti lina wanachama wengi wa CUF kuliko majimbo mengine katika jiji la Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, Wilaya ya Temeke ina majimbo mawili ya
Kigamboni na Temeke.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, katika mkoa mzima wa Dar es Salaam, jimbo
pekee lililochukuliwa na wapinzani ni lile la Kigamboni tu ambalo mbunge wake
alikuwa Frank Magoba. Kwa sasa Magoba amerejea CCM.
Majimbo mengine kama vile Kawe, alikuwa Ritha Mlaki ambaye amepata nafasi ya
kutetea kiti chake, Kinondoni alikuwa Peter Kabissa ambaye safari hii naye
hakuteliwa ambapo nafasi hiyo inatetewa na Iddi Azan, Ubungo alikuwa Charles
Keenja,anatetea kiti chake, Ukonga alikuwa Dk. Makongoro Mahanga, anatetea tena
kiti chake na Ilala alikuwa Idd Simba ambaye ameamua kupumzika na kuiacha
bendera ya CCM katika jimbo hilo ikipeperushwa na Mussa Azzan 'Zungu'.
UTABIRI HAUNA NGUVU
Lakini utabiri huo unaotolewa na baadhi ya watu katika jimbo hilo unatofautiana
kabisa na mtazamo wa kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM Kata ya 14, wilayani
Temeke Fard Bazar.
Akieleza mtazamo wake, Bazar
anasema utabiri huo kwa sasa hauna nafasi tena katika jimbo hilo kutokana na
jinsi CCM ilivyojiimarisha pande zote.
Wapinzani, alisema
hawana nafasi tena ya kulitawala jimbo hilo kwa sababu walichezea bahati
waliyoipata katika uchaguzi wa mwaka 1995 ambapo Mrema alichaguliwa kuwa mbunge.
Pamoja na wananchi kutupa karata yao katika kambi ya upinzani wakitarajia kupata
mabadiliko ya maendeleo, bado ikaonekana kama ndoto kwao baada ya Mrema
kuwatelekeza kwa kujiuzulu ghafla bila kutoa sababu za msingi.
Kitendo cha Mrema kujiuzulu wadhifa huo bila sababu za msingi, kimewachukiza
wananchi na kuwafanya wasiwe na imani tena na kambi hiyo, anasema Bazar.
Akifafanua,alisema kuwa kutokana na
imani hiyo iliyojengeka kwa wananchi, kambi ya upinzani sasa imekuwa haiaminiki
tena.
" Samaki mmoja akioza wote wameoza'. Hivyo kitendo alichokifanya Mrema
kinaweza kufanywa pia na wagombea wengine kutoka kambi ya upinzani endapo
watapewa ridhaa ya wananchi kushika nafasi za uongozi."
Kutokana na kulitambua hilo, ndio maana ulipofanyika uchaguzi mdogo wa kujaza
nafasi iliyoachwa wazi na Mrema, wananchi wakaamua kuichagua CCM.
Kamanda Bazar anasema wameamua kuichagua CCM si
kwa kubahatisha, bali wakiwa
na matumaini kwamba ni Chama chenye sera nzuri na kinachoweza kuwaletea
maendeleo.
Kwa mujibu wa Bazar, katika uchaguzi huo mdogo ambapo CCM ilimsimamisha John
Kibaso kuwa mgombea wake, iliibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya wapinzani.
Ushindi huo wa CCM, ndio ikawa mwanzo wa kuzika ndoto za wapinzani kuliongoza
tena jimbo hilo.
Kwa kuthibitisha hilo, wapinzani
walisambaratishwa tena katika Uchaguzi Mkuu uliyofanyika mwaka 2000.
.CCM haiwezi kubishana na vyama ambavyo havina sera wala mwelekeo ambavyo hata
wananchi tayari wameonyesha hali ya kutovikubali.
" kama ni mchezo wa mpira wa miguu basi naweza kusema kwa sasa CCM ndio
timu ya Simba na wapinzani ni Yanga.kwahiyo hawa ni wateja wetu na wataendelea
kuwa wateja wetu hadi hapo tukapoamua vinginevyo," anasema kamanda Bazar.
Litakuwa ni jambo la ajabu kwa wananchi wa jimbo hilo kuthubutu kurudia makosa
waliyoyafanya mwaka 1995 kwa kuchagua mgombea kutoka kambi ya upinzani.
Endapo wananchi wataamua kuchagua wagombea waliosimamishwa na vyama vya upinzani
katika uchaguzi mkuu ujao, watakuwa wamejifunga kitanzi cha kujiletea maendeleo
katika maeneo yao husika.
Hii ni kwa sababu kambi hiyo haijajiimarisha kisera na hivyo haina uwezo wa
kuwaletea maendeleo wananchi.
UONGOZI SI MAJARIBIO
Wanachokifanya sasa kuhusu kushiriki kwao katika uchaguzi huo, Bazar anasema
ni kutaka kujaribu kama wanakubalika kiasi gani.
Anashauri wana-CCM na wananchi kwa ujumla wao kutofanya makosa ya majaribio ya
uongozi kwa kuwachagua wapinzani.
"Uongozi kamwe haujaribiwi hata siku moja kwani kufanya hivyo ni sawa na
kuchezea shilingi katika tundu la choo ambapo ikidumbukia haitapatikana tena.
" Kuwapa uongozi wapinzani kwa majaribio ni sawa na kumpa panga mwenda
wazimu ambaye anaweza kulitumia vibaya wakati wote na baadaye ukajutia uamizu
wako uliyoufanya," anasema.
CCM, anasema imejiandaa vema
kukabiliana na hali ya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao. "Tuko
imara kukabiliana na hali yoyote ile kwani tuna silaha za kutosha za kupambana
nao na lazima CCM itashinda tu na si vinginevyo.
Silaha hizo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo
Bazar anasema imetekelezeka kwa asilimia kubwa katika serikali ya awamu tatu.
Lengo la CCM, ni kupata tena ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu ujao, ili
kuendeleza mafanikio iliyoyafanya na kuongeza mengine zaidi ili kuondoa kero
zinazowakabili wananchi wake.
CCM ina uwezo wa kutekeleza ahadi zake inazozitoa kwa wananchi
hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu tofauti na sera za wapinzani
ambazo hazitekelezeki hata kidogo.
Ushindi huo kwa CCM, Bazar anakiri hauwezi kupatikana hivi hivi bali utapatikana
kwa kunadi mafanikio yaliyopatikana kupitia ilani yake ya uchaguzi kwa wananchi.
Akiwa kama kamanda wa UVCCM, alisema atahakikisha kwamba
vijana wake wanashiriki kikamilifu katika kunadi sera za CCM kwa wanchi.
Bazar anasema kushiriki kikamilifu kwa vijana katika kunadi sera za CCM ni
sehemu ya wajibu wao lakini pia kutawafanya wananchi walio wengi kutambua nini
ilichokifanya CCM.
Alifafanuwa kwamba kumekuwa na
taarifa za upotoshaji zinazosambazwa na wapinzani mitaani eti CCM katika kipindi
cha utawala wake haijafanya kitu chochote huku wakitembelea barabara nzuri,
kupata maji safi, afya, elimu na maendeleo mengine mengi.
"Vijana ndio nguzo ya CCM hivyo lazima washiriki kikamilifu katika uchaguzi
huo kwa kuwaelimisha wananchi waachane na vyama 'uchwara' ambavyo havina sera
madhubuti na badala yake waichague CCM iendelee kuleta maendeleo," anasema.
Katika kipindi hiki cha uchaguzi, Bazar alisema
atahakikisha kwamba kauli ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Benjamin
William Mkapa ya kuwataka makamanda wa UVCCM washirikiane na vijana badala ya
kuvaa majoho tu inatekelezwa ipasavyo kwa kuipatia ushindi CCM katika jimbo hilo.
Akielezea alivyoawaandaa vijana, alisema tayari
amekaa na vijana kupanga nao mikakati ya kuipatia CCM ushindi ukiacha ile ya
kujiletea maendeleo endelevu ambayo pia ishakamilika.
Kwa mujibu wa Bazar, anakusudia
kukutana na makamanda wenzake wa UVCCM waliomo katika jimbo la Temeke ili
kujenga nguvu na mawazo ya pamoja ya jinsi ya kuwahimiza vijana ili wajitokeze
kwa wingi wakati wa kupigakura kuchagua viongozi na waichague CCM.
Kuna haja ya makusudi kabisa kila mwana-CCM kuunga mkono kauli ya mgombea wa CCM
wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ya kuweka
serikali yenye mafiga matatu, alibainisha.
Kauli hiyo, aliongeza imejaa ukweli
tupu kwamba wananchi hawawezi kupata maendeleo safi endapo serikali ijayo
itakuwa na upungufu wa mafiga matatu kama alivyosema Kikwete kwa maana ya kwamba
rais, wabunge na madiwani lazima watokane na CCM.
" Ilani za vyama zinatofautiana hivyo unapochagua Rais kutoka CCM na kisha
ukachagua mbunge kutoka CUF, ujuwe wazi kwamba hapo maendelo yake ni sawa na 'ziro'
kwa sababu kila kiongozi atataka kutekeleza sera ya ilani yake," anasema
kamanda Bazar.
Kwa vyovyote vile, aliongeza Kikwete
atashinda katika uchaguzi ujao na kuwataka wananchi wamchagulie wabunge na
madiwani kutoka CCM ili waweze kuchapa kazi na kuzungumza lugha moja ya
kuwaletea maendeleo ya haraka.
Kamanda Bazar anaongeza kuwa serikali ijayo ya CCM inauhakika wa kuongoza nchi
kwa kipindi cha miaka kumi ijao kutokana na ukweli kwamba sera zake zinakubalika
na wananchi.
"Ari mpya, nguvu mpya. Kasi mpya 2015," anasema Bazar akimaanisha kwamba CCM itaendelea
na kasi hiyo kwa kipindi chote hicho.