KAMPENI ZA MGOMBEA URAIS  WA TANZANIA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE MKOA WA DAR ES SALAAM

 

 

Mgombea Urais wa  Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi yaCCM Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ahutubia uwanja wa Burahati na kusema Ubora wa Kiongozi lazima awe anahubiri Amani, Umoja, na Utulivu. Sio kuwa na Kiongozi ambaye kutwa nzima anahubiri Ukabila, Udini na Ukanda wa kuangalia maeneo anakotoka

 

Akihutubia mkutano huoMhe. Kikwete aliwahakikishia  wananchi kuwa pindi akiingia madarakani atahakikisha kuwa anayaenzi na kuyadumisha mafanikio yote yaliyo patikana toka serikali za awamu zote tatu na kupambana na tatizo la umasikini kwa Watanzania. Nitajivunia sana pindi napomaliza muda wangu nikawa nimemaliza  au kupunguza hili tatizo la ajira kwa vijanaMhe. Kikwete alisema.

 

Kuhusu matatizo ya maji, alisema atatumia uzoefu wake alioupata kama Waziri wa Maji kuhakikisha anatatua suala hilo, pia nafasi yake kama Waziri wa Fedha kuhakikisha anapata fedha na tena kutumia uzoefu wake kama Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje kuhakikisha anatafuta wafadhili ili kupatikane kwa maji hata kama italazimu kutoa mto Rufiji yupo tayari kufanya hivyo. Ili mradi kupunguza au kumaliza tatizo la maji katika Jijini la Dar es Salaam.

 

Pia alielezea kuendeleza uboreshaji wa miundombinu na kuahidi pindi akichaguliwa kuwa Rais wa awamu ya nne atahakikisha anaendelea kuziboresha barabara za mijini kwa kiwango cha lami. Alisema ifikapo Desemba 2006 kutakuwa na barabara ya lami kutoka Mtwara hadi Mwanza.

 

Mhe. Kikwete alipokea wanachama wapya wa CCM 18 na wanachama 10 toka vyama vya upinzani. Kati yao watatu ni wagombea udiwani kwa tiketi ya CHADEMA – Mgeni Mwarami, Athumani Issa Katunzi na Amina Said Salum, wakati Sospita Kanuti yeye ni Katibu wa Mkoa wa Iringa wa Chama Cha Demokrasia Makini.

 

Leo alhamisi Mhe. Kikwete anaendelea na ratiba ya kampeni katika Mkoa wa Pwani katika Wilaya ya Bagamoyo.