Kwa nini Watanzania wanajiandaa kuipa CCM ushindi wa
kishindo?
Sera zake za maendeleo zimejionyesha kwa yaliyotekelezwa, hata wapinzani
wanakiri
VYAMA vya upinzani vinaomba Urais
vitawale sawasawa na CCM inayoomba kuendelea na Utawala huo. Lakini mpaka
sasa wananchi wanatambua kwamba vyama vya Upinzani havichaguliki.
Makala hii ya Mwandishi wetu LAUDEN MWAMBONA inatoa ufafanuzi
zaidi ni kwa nini CCM
inaomba kuendelea kushirikiana na wananchi katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
WAGOMBEA tisa wa Urais kupitia Vyama vya upinzani
bado wanaendelea na kazi ya kuomba kura ili wapate nafasi hiyo. Pamoja na
kutokwa jasho jingi katika harakati hizo bado vyama hivyo vinajikongoja kusaka
Urais
Vyama vyenye wagombea ni SAU ambacho mgombea wake ni Paul Kyara,
NLD ambacho mgombea wake ni Emmanuel Makaidi,
DP chenye mgombea wake Christopher Mtikila na chama cha TLP ambacho kama
kawaida Mwenyekiti wake, Augustine Mrema anawania Urais kwa mara ya tatu.
Kiongozi mwingine wa chama cha upinzani anayewania kwa mara ya tatu tangu 1995
akisaka Urais ni Profesa Ibrahim
Lipumba wa CUF ambaye wanachama wake tayari wamempa somo kwamba akishindwa mara
ya tatu basi ashike lake.
Wengine ni Anna Senkoro wa chama
cha PPT Maendeleo, Freeman Mbowe wa CHADEMA, Sengondo Mvungi wa
NCCR-MAGEUZI na Profesa
Leonard Shayo wa chama cha Demokrasia
Makini.
KWA NINI WANAGOMBEA?
Watu wengi wanajiuliza sana swali hili na wanashindwa kupata jimbo. Baadhi ya
vyama vinavyoshiriki vinadai vinataka kuwasaidia wananchi. Wanasema vinataka
kuwapatia utajiri Watanzania na kuwaondoa kwenye umaskini. Lakini wanashindwa
kutoa mbinu za kutekeleza hayo.
Lakini maelezo wanayotoa kwenye
mikutano ya kampeni ni ya kukashifu na kuipinga CCM tu na wala siyo kueleza
watafanya nini.
Taarifa zinazopatikana kutoka kila mikutano yao wagombea wote wananukuliwa
kupinga CCM tu. Ni mara
chache Mgombea wa Urais wa TLP , Mrema alirukia pia kwa vyama vingine vya
upinzani akieleza kwamba havifai.
Mfano ni pale alipokuwa Shinyanga ambapo Mrema kwa kinywa chake aliwaambia
wakazi wa huko kwamba Profesa Lipumba wa CUF hafai kuwania Urais kwa vile
hajawahi kuwa hata katibu kata.
Mrema pia alinukuliwa akiwa Mwanza,
akisema, Lipumba hafai kwa vile aliwahi kuteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya
uchumi wa Rais Ali Hassan Mwinyi na
kusababisha uchumi kuporomoka kuliko kawaida.
Kipindi cha Lipumba serikali ilizembea kukusanya kodi, huduma
za jamii zilizorota, mishahara ya wafanyakazi wa serikali haikupatikana. Kwa
ujumla kipindi hicho wafanyakazi walidharauliwa. Na dhuluma ilijaa kwenye vyombo
vya dola na mahakama kutokana na vitendo vya rushwa kushamiri.
Lakini pia Mrema alivitaja vyama vya upinzani kuwa havina ushirikiano hata
kidogo na kufafanua kwamba CUF ilishindwa kutoa kura kwa vyama vya upinzani
mwaka 1996 huko Zanzibar badala yake kura zilipigwa kwa maruhani baada ya
wagombea wake kuenguliwa mahakamani.
Nasema ni Mrema pekee ambaye kidogo ameshambulia vyama vingine vya upinzani, kwa
vile ndiye aliyesikika, lakini ukweli ni kwamba vyama vingine vyote vinatembeza
magari yao kwa kuikashifu CCM bila kunadi sera.
Pamoja na CUF kuonyesha ilani yake
ya uchaguzi lakini mpaka sasa kinashindwa kuifafanua ilani hiyo ni kwa vipi
watatekeleza majukumu kwa vile
chama chenyewe hakijawahi kuwa na mipango ya maendeleo.
Kwa kawaida ilani , inaandaliwa kwa kuzingatia mipango ya maendeleo
iliyoandaliwa na serikali katika vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa, Wizara
na hatimaye Taifa jambo
ambalo halijafanywa na CUF.
Hivyo ni vigumu kwa wananchi kuelewa sababu za CUF na vyama vingine vya upinzani
kutaka vitawale Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
KWA NINI CCM INAOMBA KUENDELERA KUONGOZA
Sababu zipo nyingi, lakini kwa LEO nitaeleza mambo yatakayofanyika kwa sekta ya
afya ikiwa CCM itachaguliwa
Sekta ya afya ni muhimu kwa Watanzania wote. Watanzania wanahitaji kuona
hospitali zinatoa huduma safi za tiba na kinga kwa magonjwa. Pia lazima
mazingira yawe safi katika maeneo yote ya Hospitali, vituo vya Afya na
Zahanati.
Waziri wa Afya Anna Abdallah ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu
ya CCM alisema hivi karibuni kwamba mipango
ya maendeleo katika serikali ya CCM
inatarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 90.8
Fedha hizo zitatumika kwa kazi ya kuendeleza ukarabati wa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili iweze kutoa huduma bora na safi kwa
wagonjwa. Ukarabati huo utafanyika
katika wodi, maabara, chumba cha upasuaji na
kujenga wodi ya watoto wagonjwa Muhimbili.
Hospitali kuu za jiji nazo zitakarabatiwa ikiwa ni pamoja na kukarabati wodi za
wagonjwa hospitali ya Ocean Road,
kujenga maabara ya kudhibiti ubora na kununua vifaa vya maabara Dar es salaam na
Mwanza.
CCM inaomba kura kwa sababu inataka
serikali yake ikarabati na kuboresha vituo vya utafiti wa magonjwa ya binadamu
huko Amani, Gonja, Mwanza, Tukuyu,
na ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Afya.
Vyuo vyote 35 vya afya navyo
vitakarabatiwa na kununua vifaa zaidi vya hospitali za rufani za Mbeya, Mirembe,
Buhando na KCMC. Hospitali za mikoa, wilaya na hospitali teule nazo kuangaliwa
kwa karibu zaidi.
Jambo lingine ambalo CCM inaomba kura kwa wananchi ili serikali yake ifanye kazi
ni kuendeleza mipango ya kudhibiti malaria, kifua kikuu na ukoma,
na kusimamia kikamilifu mpango wa kudhibiti ukimwi ili waathirika wengi
zaidi wapate dawa za kurefusha maisha bila ya malipo
CCM inasema wajawazito na watoto
wataendelea kupata huduma za tiba bila malipo. Na kwamba huduma za chanjo za
kinga zitaimarishwa zaidi.
Suala la kupatikana dawa kwenye vituo vya afya na zahanati ni jambo ambalo
limeahidiwa kuimarishwa zaidi
katika mipango ya maendeleo ya serikali ya CCM.
CCM ilitaja Zahanati
zitakazoongezwa katika kupata dawa kuanzia mwaka huu wa fedha baada ya
kuchaguliwa kuwa ni Olkerieni , Ngyani,Terrati na Kipendenkovele zote za
halmashauri ya Arumeru wakati kituo
cha afya cha Themi manispaa ya Arusha nacho kitapata dawa za kutosha .
Zahanati na vituo vingine vitakavyopata dawa kwa mkoa wa Arusha Matale, Meserani,
Aya-labe, Lambo, Oldeani, Esere, Oloipiri na Magaiduru
wakati kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam zahanati zitakazopata
dawa ni Ukonga, Msewe,
Mlalakuwa na Makongo juu.
Zahanati za mkoa wa Dodoma
zinazoongezwa katika mpango safi wa kupata dawa
ni Ntuba, Zuzu, Chahwa, Michese, Ntyuka, Gawaye, Ndembwe, Mpamatwa,
Chinyangutu, Tambi, Matonya, Chitemo, Ikuyu, Kiboriani, Kimagai, Mtamba, Kidenge,
Ndurungumi Ihanda, Chiwe, Chamkoroma, Pigalame, na Lenjulu.
CCM inasema serikali yake itapeleka dawa zahanati mbalimbali za mkoa wa Iringa
zikiwemo za Masisiswe, Ndegenda, Ngongwa, Ibanda,
Ilungu, Ukange, Kipagalo, Muhinga, Igombavanu, Kilolo, Mhula na vituo vya afya
vya Makoka, Sadani, Mgololo na Kimande.
Huko Kagera dawa zitakwenda zahanati za Bulembo, Kibirizi, Buzi, Nyakato na
Bulembo wakati huko Kigoma zahanati
zitakazopata ni Kanazi, Mugera, Kajana, Nyamugali, Risaba, na Kituo cha afya cha
Janga.
Ahadi kama hizo pia zinatolewa mkoa
wa Kilimanjaro ambako zahanati zitakazoingizwa kwenye mpango wa kupata dawa za
kutosha ni Mdawi, Mahoma, Kindi, Kimangara, Marangu Kiraracha, Mdawi, Karamba, Bwambo na Mhezi.
Huko mkoa wa Lindi , dawa zitaongezeka katika
Zahanati za Namalongo, Kihuwe, Nkaloji na Kituo cha Afya Marando.
Zahanati za mkoa wa Manyara zitakazoongezwa kwenye orodha ya zahanati zinazopata
dawa nyingi ni Endasaki, Manyara,
Simbai, Gahandu, Ngorat, Hasama, Tsawa, Onyomat, Dohoni, Dabir, Mayoka, Minjingu,
Lemukuna, Chokaa, Narakau, na vituo
vya afya vya Gallapo na Mererani.
Mkoa wa Mara utaongezewa dawa kwenye
zahanati za Kunzungu, Wariku, Mirwa, Bwitegi, Ochuna, Kibuyu wakati mkoa wa
Mbeya utaongezewa dawa kwenye zahanati za Saza, Mbogani, Soweto, Ifuko, Maoga,
Nsalanga, Iwambi, Iwowo, Kapele, Namwanga, Mpapa Itumbi wakati vituo vya afya
vitakavyofaidika ni Mwakaleli.
Huko Morogoro , CCM imeahidi kwamba
serikali yake itaongeza dawa kwenye zahanati za Mabula, Majawanga, Mzaganza, Masenge, Dakawa na
Kituo cha Afya cha Kidete.
Ahadi kama hizo pia zimetolewa kwa zahanati kadhaa za mikoa ya Mtwara, Mwanza,
Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.
Kwa hali hiyo, CCM inayo sababu kubwa ya kuomba wananchi waichague ili itekeleze
kazi hiyo kwa sekta ya Afya kwani wagombea wengine hawajui hali halisi ya huduma
zitolewazo kwenye zahanati hizo.