Mchango wa sekta ya madini kwa mauzo ya nje umeongezeka maradufu
KIPINDI cha miaka kumi iliyopita cha Serikali ya awamu ya tatu kimeshuhudia kufufuka na kukua kwa kasi kwa uzalishaji viwandani, ikiwemo migodi. Makala hii inafafanua mafanikio hayo yaliyochangiwa zaidi na utekelezaji wa sera ya taifa ya ubinafsishaji, na vilevile ufunguaji wa milango kwa mitaji kutoka nje ya nchi.
Katika kipindi kilichopita, Serikali imetekeleza kwa dhati sera ya ubinafsishaji. Pia iliandaa Sera Endelevu ya Viwanda, Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na Sera ya Utekelezaji ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi. Sera zote hizo zilisaidia sana kuimarisha viwanda. Vilevile, yalianzishwa maeneo maalum ya uzalishaji kwa ajili ya kuuza bidhaa nje (EPZ). Viwanda vingi vimepata wawekezaji wapya wenye uwezo wa kuingiza teknolojia mpya na uzoefu wa kuendesha viwanda kisasa.
Matokeo ya hatua hizo za ubinafsishaji wa viwanda ni pamoja na :-
Kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa viwandani na hivyo kukidhi mahitaji ya wananchi. Kwa mfano, uzalishaji wa nguo uliongezeka kutoka mita za mraba milioni 73.6 mwaka 2000 hadi mita za mraba milioni 109.8 mwaka 2004; usagishaji wa ngano kutoka tani 162,634 mwaka 2000 hadi 333,789 mwaka 2004 ; uzalishaji wa chuma kutoka tani 11,181 mwaka 2000 hadi tani 46,559 mwaka 2004. Ongezeko kubwa, la uzalishaji lilipatikana pia katika bia, sigara, mabati, saruji, biskuti na tambi, utengenezaji wa kamba za katani, uuzaji nje wa samaki wa kusindikwa n.k.
Kuongezeka kwa ukuaji wa sekta ya viwanda kutoka asilimia 4.8 mwaka 2000 hadi asilimia 9 mwaka 2003.
Kuongezeka kwa thamani ya miradi iliyoidhinishwa kutoka sh. bilioni 123.8 mwaka 2000 hadi sh. bilioni 239.6 mwaka 2004, ongezeko la asilimia 93.5.
Kuongezeka kwa ajira viwandani kutoka 153,938 mwaka 2000 hadi 207,571 mwaka 2003, ongezeko la asilimia 34.8.
Madini
Serikali katika kutekeleza Ilani ya CCM ya 2000 katika sekta ya madini iliongozwa na Sera ya Madini ya mwaka 1997 ; Sheria ya madini ya mwaka 1998 na kanuni za mwaka 1999. Sera hiyo ililenga kuvutia wawekezaji binafsi. Azma ya kuwavutia wawekezaji imefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Utafiti wa madini uliongezeka na migodi mikubwa ilifunguliwa. Ushiriki wa sekta binafsi katika utafutaji na uchimbaji wa madini umewezesha kuwepo kwa migodi yenye hadhi ya kimataifa kama Geita Gold Mine, Kahama Mining, Buhemba Gold Mine (Musoma), Afrika Mashariki Gold Mine (Tarime) na Tulawaka Gold Mine (Biharamulo).
Kwa upande wa wachimbaji wadogo wadogo, wamekuwa wakipatiwa mafunzo katika nyanja mbali mbali kama uchimbaji salama wa madini, utunzaji wa mazingira, utafutaji wa madini, biashara ya madini, masuala ya afya n.k. Pia, wachimbaji wadogo wadogo walifundishwa namna ya kupata mikopo kutoka SIDO na taasisi nyingine zinazotoa mikopo. Kutokana na hatua hizo, sekta ya madini imeweza kupata mafanikio yafuatayo katika kipindi cha 2000-2005:-
Tanzania kwa sasa inazalisha takriban tani 50 za dhahabu kwa mwaka na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uzalishaji wa dhahabu Barani Afrika.
Sekta ya Madini imekuwa kati ya sekta zenye kasi kubwa ya ukuaji. Ukuaji uliongezeka kutoka asilimia 13.9 mwaka 2000 hadi asilimia 14.1 mwaka 2004, ikiwa imefikia kilele cha asilimia 17 mwaka 2003.
Mchango wa sekta ya madini katika mauzo ya nje uliongezeka kutoka asilimia 26.9 mwaka 2000 hadi asilimia 51.4 mwaka 2004, na hivyo kuongoza katika muzo ya nje ikilinganishwa na mauzo ya bidhaa nyingine.
Mchango wa sekta ya madini kwa mapato ya fedha za kigeni umekua kutoka dola za Marekani milioni 178.2 mwaka 2000 hadi dola milioni 543 mwaka 2004. Hili ni ongezeko la asilimia 204.8.
Watafutaji na wachimbaji madini wakubwa na wadogo hulipa ada za leseni na mrabaha kwa madini wanayouza. Tangu mwaka 2000, maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa na Wizara yaliongezeka kutoka sh. bilioni 7.441 mwaka 2000/01 hadi sh. bilioni 22.786 mwaka 2003/04, likiwa ni ongezeko la asilimia 206.2
Migodi mikubwa imekuwa ikisaidia katika utekelezaji wa miradi ya jamii kama vile afya, elimu, maji na barabara. Huduma hizo huvinufaisha vijiji vinavyozunguka migodi hiyo. Baada ya uchimbaji madini kufikia kikomo, majengo ya migodi hiyo yatatumika kwa huduma za jamii kama kuanzisha shule au huduma nyingine kulingana na vipaumbele vya wanajamii katika eneo husika.
Ajira rasmi katika migodi mikubwa imeongezeka kutoka 1,781 mwaka 1997 hadi 7,082 mwaka 2003, likiwa ni ongezeko la asilimia 297.6. Pia, mwaka 2003 inakadiriwa kuwa zilizalishwa nafasi 42,000 za ajira nje ya migodi kutokana na kuwapo kwa migodi hiyo. Kwa upande wa kujiajiri, inakadiriwa walikuwapo wachimbaji wadogo zaidi ya 500,000 waliokuwa wamejiajiri.
Biashara
Biashara ni muhimu sana katika jitihada za kuongeza pato la wananchi na kuendeleza uchumi. Dunia ya sasa ya utandawazi imeegemea sana kwenye biashara ya kimataifa. Kwa kutambua hilo, Serikali imeweka msukumo wa pekee katika kukuza mauzo ya bidhaa zetu nje na kuongeza wingi na ubora wa bidhaa katika soko la ndani. Kutokana na msukumo huo, hatua zifuatazo zilichukuliwa katika kipindi kilichopita :-
Kuondoa kero ya ulipaji wa kodi ya makisio kabla ya hata kuanza biashara yenyewe. Serikali iliweka wazi masharti ya kuanzisha biashara, viwango vya ada kwa aina mbali mbali za biashara na hivyo kupunguza vishawishi vya rushwa.
Kushiriki katika majadiliano kuhusu mfumo wa biashara kimataifa. Julai, 2001, Tanzania iliandaa mkutano wa mawaziri wa biashara kutoka nchi maskini sana uliofanyika Zanzibar. Tamko Rasmi la Zanzibar liliweka msimamo wa pamoja katika mikutano ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO) ya Doha, Qatar, Novemba, 2001 na Cancun, Mexico, Septemba 2003. Ushirikiano huo ulizuia upitishaji wa ajenda ambazo zingeendeleza na kuimarisha maslahi ya nchi kubwa dhidi ya nchi changa. Mchango wa Tanzania katika kujenga nguvu hii ulikuwa mkubwa.
Ili kukuza maendeleo ya kiuchumi, na hasa viwanda na biashara, Serikali iliendelea kushirikiana na nchi jirani, hasa za Afrika Mashariki kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kutunga Sheria ya kudhibiti uingizaji holela wa bidhaa kutoka nje ili kulinda nchi yetu isigeuzwe kuwa dampo la bidhaa hafifu kutoka nje.
Kuanzisha maeneo huru ya biashara
Kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo katika taaluma za ujasiriamali, namna ya kupata mikopo kutoka mifuko mbali mbali na benki, na kurahisisha taratibu za kupata mikopo chini ya Mkakati wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.
Kupunguza mlolongo wa leseni kabla ya kuanzisha biashara.
Kutungwa sera na mikakati ifuatayo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kuwezesha ukuaji wa biashara kubwa na ndogo:-
(i) Sera ya Utekelezaji ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.
(ii) MKUKUTA
(iii) MKURABITA
Kutokana na hatua hizo na nyinginezo, mafanikio makubwa yamepatikana yakiwemo yafuatayo:
Ukuaji wa sekta ya biashara uliongezeka kutoka asilimia 6.5 mwaka 2000 hadi asilimia 7.4 mwaka 2004.
Mauzo ya nje yaliongezeka kutoka dola milioni 663.3 mwaka 2000 hadi dola milioni 1,142 mwaka 2003, likiwa ni ongezeko la asilimia 72.2
Biashara imechangamka zaidi nchini.