ZIKIWA ZIMEBAKI TAKRIBAN WIKI MBILI KUFIKIA UCHAGUZI MKUU

"ALAMA za mtu mnafiki ni tatu, akizungumza husema uongo, akitoa ahadi hatimizi na akiaminiwa hufanya hiyana. unyago si Jang'ombe tu hata Zingwezingwe nako huchezwa".

Hayo yalikuwa maneno ya hekima ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ali Hassan Mwinyi, alipokuwa akiwahutubia wana CCM na wananchi wa Jimbo la Mpendae, Wilaya mjini Unguja hivi karibuni katika mkutano wa kampeni.

Kauli hiyo ni nzito ambayo wananchi wa Tanzania hasa Zanzibar,˙hawana budi kuitafakari kwa kina kabla ya kufanya maamuzi mazito ya kuwapigia kura viongozi wanaokuja kuomba ridhaa ya kuongoza nchini Tanzania na hasa Zanzibar.

Katika kipindi hiki, Tanzania iko katika hatua za lala salama za uchaguzi mkuu, utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu nchini kote.

Wakati hali ikiwa hivyo, kuna vyama na viongozi tele wanaopita na kufanya mikutano ya kampeni kuelezea mipango yao mingi na mingine isiyotekelezeka.

Kimtazamo maneno ya Mzee Mwinyi ni mafupi , lakini yana maana na hekima kubwa ndani yake, kwani yanafundisha kuwafahamu binadamu hasa katika kipindi cha hiki˙taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu.

Mwinyi kama alivyozoeleka kwa jina la 'Mzee Ruksa' ni mtu mzima tena kiongozi mpendwa wa Tanzania anayafahamu mambo mengi. Siyo kuyafahamu tu, ameyaona mengi, anayajua mengi na ameyasikia mengi katika dunia hii. Amewalea ˙viongozi wengi, wengine wanaitwa wapinzani hivi sasa.

Hivyo kutoa kauli kama hiyo ya kuwatahadharisha wananchi juu ya kuwataka kuwapima wagombea wote wanaoomba kura kwa kauli zao, vitendo vyao na tabia zao ni jambo la busara sana.

Ni jambo la busara sana, kwani Tanzania, imebakiwa na muda mfupi kufanyika uchaguzi mkuu nchini, kwa ajili ya kuwapata viongozi watakaoliongoza taifa.

Kwa mantiki hiyo, ni jukumu la wananchi kuwapima, kuwaaangalia tena kwa darubini kali viongozi na wagombea wa vyama vinavyojipitishapitisha kwa wananchi kuomba ridhaa ya kuwaongoza.

Ni lazima kuwafanyia uchunguzi wa kina historia yao, utumishi wao kwa taifa, uaminifu kwa umma, kauli zao kwa jamii, utendaji wao pamoja na ushirikiano wao kwa wananchi wa Tanzania, hasa Zanzibar.

Kiongozi anatakiwa awe mfano mzuri kwa anaowaongoza kwa kila jambo, kwani iwapo atakuwa kiongozi, lakini kauli na vitendo vyake vitakuwa havilingani na uongozi wake, taifa litayumba na kuwayumbisha wananchi.

Kwa Mzee Mwinyi, wagombea wengi wanaopitapita kwa wananchi kuomba kuchaguliwa, ili wawe viongozi amefanya nao kazi, anawajua kikamilifu, wengine wanafunzi wake, hivyo anaposema kuwa wapimme kwa kauli zao, vitendo vyao na tabia zao ni ushauri mzuri kwa taifa, hasa kwa vijana walio chini ya umri wa miaka thelathini.

Wengine hivi sasa wanapita kuomba kura kwa kutoa kauli zenye mvuto lakini historia yao kwa taifa hili hairidhishi tena kwa karne hii ya maendeleo.

Wengi watakumbuka˙kipindi cha machafuko ya hali ya hewa Tanzania. Chimbuko lake ni kwa baadhi ya viongozi kujihisi wanaonewa na Rais aliyekuwepo madarakani wakati huo na kusababisha kuanzisha makundi mabaya ndani ya serikali na CCM.

Hali hiyo ilisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi. Hiyo ilitokana na maneno ya Mzee Ruksa, ya alama za mtu mnafiki.

Kufuati hali hiyo Chama Cha Mapinduzi, kikaona basi kama kweli wanaonewa wapeni nafasi za uongozi, ili hayo wanayotaka kuyafanya kwa maslahi ya wananchi wayafanye umma uyaone,lakini wapi?

Hakuna kitu kilichofanywa badala yake kuanzisha makundi ya Ubara, Unguja na Upemba kwa maslahi yao binafsi, hivyo huo ndiyo uongozi unaohitajika sasa?

Wapigakura wote wa Bara na Zanzibar hawana budi kuwapima wagombea kwa kauli zao, vitendo vyao na historia yao kwa taifa, ili wasiiingie katika mtego wa kuwapa nafasi za uongozi na baada ya muda mfupi kujikuta wakiingia kwenye majuto.

Hadi sasa kwa wagombea wanaopitapita kuomba kura kutoka vyama vya upinzani hawana sifa zinazoweza kuwafanya wananchi waamini kuwa ni bora kama wale wa CCM.

Wagombea wa CCM ni safi kutokana na utekelezaji wao makini wa Sera na Ilani ya chama chao. Wameonesha wana nia njema ya kuwatumikia wananchi na kubwa wanaguswa na shida na matatizo yao.

Kwa upande wa Zanzibar, mgombea urais wa CCM , Amani Amani Abeid Karume, ameonyesha uwezo, ujasiri, uvumilivu na ustamilivu na kubwa kuyachambua matatizo ya wanyonge wa Visiwa vya Unguja na Pemba bila ubaguzi.

Katika kipindi cha miaka mitano akiwa Rais wa Zanzibar, Karume ameuonesha ulimwengu kuwa pamoja na umasikini wa Zanzibar, bado mambo ya maendeleo kwa wananchi yanawezekana tena kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe.

Karume katika kipindi hicho ameilinda, ameitetea na ameitekeleza Katiba ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nguvu zote bila kutetereka. Huo ni ujasiri mkubwa kwani wengine walishindwa tena walikuwa wasaidizi wa Rais tu.

Wapinzani walikuwa wakidai eti Zanzibar, haina bendera yake, Karume ameweza kuleta bendera na sasa inapepea kila penye ofisi ya serikali hapa Zanzibar. Hata kwa Sheha wa Shehia ya Mtambwe ipo. Kama siyo mafanikio ni nini basi?

Si hivyo tu, Karume ameanzisha Muafaka wa Vyama vya CCM na CUF, ili kusikiliza madai ya wapinzani hao wana nini wanachodai mbele ya mataifa ya nje.

Lakini licha ya kuanzishwa kwa muafaka huo, imebainika hakuna kitu cha msingi wanachodai bali walichokuwa wakidai ni maslahi binafsi ya kupatiwa mshahara kila mwezi kutokana na kwamba wamelimitukia taifa kwenye nyadhifa kuwa za wasaidizi wa Rais.

Muafaka huo ndiyo leo ulioanzisha Kamati ya Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa vilivyopata Usajili wa kudumu nchini Tanzania.

Nani kama Karume? Jibu hakuna ni jukumu la wananchi wa Zanzibar, kumpa tena ridhaa Rais Karume, ili azidi kuwaletea maendeleo, wananchi wa Visiwani, tena bila ubaguzi wowote.

Kwa maneno ya Mzee Mwinyi, ni dhahiri kwamba wapinzani anawajua kikamilifu na tahadhari aliyoitoa juu ya wananchi kufanya uchunguzi wa wagombea ni jambo la busara.

Huwezi kumpa mtu nchi ambaye anatiliwa shaka na kufanya hivyo ni kuwajengea misingi mibovu wananchi wake kufuatia kukabidhiwa taifa mtu ambaye historia yake na matendo yake huko nyuma hayakulijengea heshima taifa la Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Aliongeza kuwa kuwachagua wapinzani ni wananchi kupoteza kura zao jambo ambalo litakuwa si kutumia vyema demokrasia yako , kwani demokrasia nzuri ni pamoja na kuwachagua viongozi wenye uhakika katika kuongoza.

Alikumbusha kwamba wapinzani hawana uzoefu wa kuongoza nchi na kinachostahili ni Chama Cha Mapinduzi, hususan Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia mgombea Urais kupitia

CCM, Amani Abeid Karume, pekee ndiye anayeweza kuwavusha wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa amani na utulivu .

Hata kwa wagombea wengine wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani ni vyema wakapigiwa kura wagombea wa CCM ili waweze kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.