KWA NINI CCM IMEFANIKIWA

Kazi ya kujenga Umoja wa Taifa ili wananhci wajisikie wako huru na watu wa taifa moja, inafanyika kwa misingi ya sera. Ziko sera za vyama vya siasa na serikali ambazo husababisha kujengeka kwa umoja wa taifa huru na zipo sera ambazo hujenga mfarakano, chuki, uhasama au kutominiani katika nchi.

Sera za Chama Tawala (CCM) na kabla yake TANU na ASP , zimekuwa ni sera zinazojenga umoja , upendo , mshikamano, amani, utulivu na kuaminiana miongoni mwa wananchi wa Tanzania.

Sera kama hizo ni pamoja na sera ya msingi ya ujamaa na kujitegemea, ingawa wapo walio na mtazamo finyu ambao hawazingatii kanuni ya wakati na mahali katika kutafsiri sera hiyo katika mazingira ya sasa yanayotawaliwa na uchumi wa soko huru.

Katika mazingira ya sasa, upo umuhimu mkubwa kwa wana_CCM na viongozi wetu kuelewa vizuri dhana nzima ya kujenga ujamaa katika mazingira ya sasa, kwa sababu yapo mawazo kwamba CCM imeachana na falsafa ya ujamaa au ujamaa umekufa.

Chama Cha Mapinduzi kimekuwa na sera zinazounda mazingira ya amani na utulivu katika jamii na nchi. Sera hizo ni zile zinazopiga vita ukabila, udini, ubaguzi wa rangi (uzawa), jinsia na umajimbo.

Nyingine ni sera zinazojali na kuheshimu utawala wa sheria, sera zinazozingatia maslahi ya wanyonge na wavuja jasho katika jamii, sera zinazowashirikisha (ulinzi wa umma) wananchi wake katika kulinda nchi yao, sera zinazojenga mazingira ya ujirani mwema na sera ya demokrasia na uwazi na ukweli katika kuendesha shughuli za nchi na za taasisi kuanzia ngazi ya kitongoji au kijiji hadi Taifa.

Nchi nyingi za Afrika ambazo vyama na serikali zake zimekuwa na sera kinyume na sera hizi za CCM , zinashindwa hadi sasa kuwa nchi zenye umoja wa kitaifa. Wananchi katika nchi hizo bado wanakabiliwa na mfarakano ulioota mizizi katika misingi ya ukabila, udini, jinsia, ubaguzi wa rangi, umajimbo na kadhalika.

Kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya Upinzani hapa nchini na aina ya viongozi wenyewe wa vyama hivyo, ni ushahidi tosha kwamba hawana nia ya kuimarisha umoja wa taifa letu wala kuendeleza mazingira ya amani na utulivu nchini katika ajenda zao za kisiasa. Badala yake, kauli au matamshi yao na vitendo vyao vinaashiria utengano katika taifa, vurugu na uhasama.

MFUMO WA VYAMA VINGI

Kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi hapa nchini, hakukuwa na maana ya kuendeleza visasi baina ya chama na chama, kujenga chuki na uhasama, kutoa vitisho, kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini, kukashifu au kubeza kila kitu kinachofanywa na serikali zilioko madarakani, na kadhalika.

Lengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini yalikuwa :-

Vyama kushindana kwa sera au kushindanisha sera za chama na chama na wala si kuporomosha matusi, kutoa vitisho, kukashifu au kukejeli jitihada zinazofanywa na serikali kuwaondolea wananchi kero zinazowasibu.

Kupanua demokrasia ndani ya jamii ili kuwapa wananchi fursa kubwa zaidi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Kwa sababu ndani ya mfumo wa chama kimoja cha siasa wapo watu walioamini kwamba demokrasia ilikuwa finyu.

Kuchochea maendeleo kwa kuzikosoa serikali zilizoko madarakani kwa ustaarabu na wala sio kupinga kila kitu kinachofanywa na serikali. Tangu nchi yetu iingie katika mfumo wa vyama vingi vya siasa (Julai 1, 1992) na huu ukiwa ni takribani mwaka wa 13, mwelekeo wa sera za vyama vya upinzani haujabadilika hata kidogo.

Badala yake zimeendelea kuwa ni sera zinazojenga mfarakano (shari), sera zinazotoa vitisho vinavyoashiria kuvuruga amani na utulivu hapa nchini. Bila hata aibu baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wamefikia hata kutamka au kuutangazia umma wa Watanzania kwamba wasipotwaa madaraka ya kuongoza nchi Oktoba 2005 ati damu itamwagika, nchi itawaka moto au kutotowalika. Je, viongozi wa aina hiyo wanatutakia mema au balaa?

Aidha mwelekeo wa itikadi za baadhi ya vyama vya siasa ni kutumia udini, ukabila, ubaguzi wa rangi au umajimbo ama ukanda kama njia ya kuingia Ikulu. Je, nani hajui madhara ya sera za udini au ukabila?

Je, mateso wanayopata wananchi wa Burundi na Rwanda msingi wake ni nini kama si ukabila? Au mapambano ya muda mrefu ya wananchi wa kusini mwa Sudan na kaskazini ni nini kama si udini?

Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wanapopata fursa ya kuhutubia mikutano ya hadhara wanajazwa jazba, hasira kali huku wakiendelea kuporomosha matusi mazito na kuwaandama viongozi wa Chama Tawala kwa matusi ya nguoni na kashfa za kila aina.

Wapinzani wanapoandaa maandamano wananchi wanakosa amani. Kwa sababu maandamano yao mara nyingi hujaa vitimbi vya kila aina. Si mara chache hutakosa kuwasikia wakitamka mambo mazito kama vile jino kwa jino, ngangari, chechenia, ukanda wa gaza na kadhalika.

Mabango yao yakiwa yameandikwa kwa kauli mbiu zinazoashiria , vurugu na kejeli mbali mbali. Siku hizi umezuka mtindo wa viongozi wa vyama vya upinzani nchini kuyaona maandamano kama njia ya mkato ya kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi.

Wananchi badala ya kutumia muda wao kwa kazi za kujiletea maendeleo, wanapoteza muda mwingi kushiriki katika maandamano ya kwenda Ikulu.