Kauli za wapinzani ni za shari za kuigawa nchi

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Omar Ramadhan Mapuri, Oktoba 6, mwaka huu alihojiwa na Radio Uhuru juu ya mambo mbalimbali kuhusiana na Uchaguzi Mkuu pamoja na mwenendo wa kampeni unavyoendelea. Katika makala hii anabainisha kwa undani juu ya masuala hayo.

SWALI: Kwanza kabisa hali ya kampeni ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika hivi karibuni inaendeleaje?

JIBU: Kampeni za Chama Cha Mapinduzi kama wananchi wote wa Tanzania wanavyojua kama wanavyosikia kwenye redio, kuona kwenye televisheni na kusoma kwenye magazeti zinaendelea vizuri sana na zinaenda kama zilivyopangwa.

Wagombea wetu wa urais kwa Jamhuri ya Muungano, Zanzibar na mgombea mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wako kwenye msafara ya nchi nzima ili kuomba kura. Ratiba zimekuwa zikibadilika hapa na pale lakini kwa ujumla wake kampeni zinaendelea vizuri.

CCM tumetanda kila mahali nchini kwa ajili ya kampeni za kitaifa, za majimbo na kata kwa maana za wabunge, wawakilishi na madiwani. Tanzania nzima hivi sasa hivi imejaa rangi za njano na kijani kutokana na mabango ya Chama Cha Mapinduzi. Vifaa mbalimbali vya Chama Cha Mapinduzi kama vile fulana, kanga na mambo mengine kama hayo vimetanda nchi nzima.

SWALI: Tunajua kampeni bado zinaendelea lakini ni mambo gani ambayo yamejitokeza kama kero hadi sasa?

JIBU: Yapo mambo yanayotukera lakini zaidi tunayofanyiwa na wapinzani wetu hasa yanayoambatana na kutuvurugia mikutano. Kuna matukio mengi hasa Zanzibar lakini hata huku Bara kwa wapinzani kufanya jitihada za kutuvurugia mikutano yetu.

Kauli za uchochezi ambazo zimekuwa zikitoka kwa viongozi wa vyama vya upinzani nazo ni kero kubwa kwetu. Kauli za vitisho, matusi, kampeni za udini na sera za kuwagawanya wananchi kimajimbo zote nazo zimekuwa kero.

Lakini pia na jitihada ambazo tunasikia zinazofanywa na wapinzani kupunguza nguvu za CCM kwa kununua kadi za wapiga kura, nalo ni eneo ambalo linatukera. Zomea zomea nyingi ambazo tulipoanza kampeni tulisikia kwamba wana CCM wanawatangazia wagombea wa CCM wa ubunge kuwa hawafai lakini tumebaini kwamba sehemu nyingi yalikuwa yameandaliwa na wapinzani wetu.

Wapo waliojitahidi mpaka kupata sare za kampeni na kuzitumia kujionyesha kama wao ni wana CCM na kupanga watu kupiga kelele na wenyewe kupiga kelele kuashiria kwamba watu wanawakataa wagombea wetu.

Lakini pia kuna wakati mwingine mgombea urais wa CHADEMA kule Kilimanjaro mara moja alienda mahali ambapo ulikuwa umeandaliwa mkutano wa CCM wa Mbunge. Alipofika pale alikuta wananchi wamekwisha fika wanamsubiri mgombea wa CCM. Baada ya kufika na wafuasi wake wakaelekeza vipaza sauti vyao na kujenga mahema na kuanza kuhutubia. Sasa hii nayo ni kero.

Tumepata taarifa kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imelikemea kimaandishi hilo lakini ni aina ya mambo ambayo hatupendezewi nayo.

SWALI:: Inafahamika dhahiri kwamba wafuasi wa CUF wamekuwa wakivamia mikutano ya kampeni ya CCM na kusababisha vurugu katika maeneo kadhaa kama ulivyosema. Lakini wananchi wangependa kujua CCM imechukua hatua gani mpaka sasa?

JIBU: Hatua tumechukua za kulaani. Tumekuwa tukitoa matamko ya kulaani kila yalipotokea na yanayohusu hatua za kisheria wanachama wetu wamepeleka mbele vyombo vya kisheria ili yashughulikiwe na vyombo vya dola na taarifa tunazozipata wapo hata watu ambao wanashikiliwa kuhusiana na matukio mbalimbali ya aina hiyo.

Lakini tunawanasihi wafuasi wetu wa CCM na wanachama wasijibu chochote kwa sababu tunauona huu ni mtego unaowekwa na wapinzani waliokata tamaa ambao wanajua kwamba hawana nafasi ya kushinda.

Wameweka mtego huo kwa makusudi kabisa ili uchaguzi uvurugike. Sasa tumekuwa tukiwanasihi na tunaendelea kuwanasihi wanachama wetu waubaini mtego huo. Kama watajibu ina maana kwamba tutapoteza hivyo tumechukua tahadhari kwani wapinzani hawana cha kupoteza.

SWALI: Inadaiwa kwamba wagombea urais Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, Augustine Mrema wa TLP na Freeman Mbowe wa CHADEMA wamekuwa wakijinadi kwa kuahidi kutoa bure elimu na afya na mambo kadhaa iwapo watachaguliwa katika nafasi ya urais. CCM mnazionaje ahadi hizo?

JIBU: Unaweza kutoa ahadi hiyo ikiwa una uhakika wa msingi wa uchumi wako. Kama wanatoa ahadi hizo pengine ni kutokana imani yao kwamba msingi wa uchumi wetu ambao tumekwishauweka hivi sasa utawawezesha kuhimili utekelezaji wa ahadi hizo.

Kama kweli wanaamini hivyo kwanza waisifu na kuishukuru CCM kwamba imejenga msingi mzuri wa uchumi ambao utaweza kuhimili hali ya kufanya hivyo. Lakini inashangaza kuona kwamba wanasema hivyo wakati wamekuwa wakisikika wakisema uchumi ni mbovu. Sasa watatekelezaje hayo bila kuwa na uchumi imara.

Lakini kwa uzoefu wetu tunataka tuwe waangalifu na tumekuwa waangalifu katika kutoa ahadi. Tunaelekeza nguvu zetu katika kuzidi kuimarisha uchumi kwanza, tukijua kwamba hayo mengine ya huduma mbalimbali kutolewa bure. Elimu, afya na mengine ni matokeo kila hali nzuri ya inaporuhusu.

Nadhani Watanzania wote ni mashahidi kwamba mwaka 2003 tuliondoa ada ya shule za msingi baada ya kuongezeka kwa mapato ya serikali kutokana na kuimarisha kwa uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo kwanza wanapozungumzia kutoa elimu bure nadhani hilo tumekwishalitekeleza. Kama wanaahidi hivyo sijui wanaahidi kitu gani kwa sababu hiyo kwa elimu ya msingi tayari na tulipoana hali imeruhusu tukapunguza ada ya elimu ya sekondari kwa asilimia 50.

Sasa tutaendelea kuimarisha uchumi wetu na kadri ambavyo uchumi unaimarika, mapato ya serikali yanaongezeka na ndivyo hivyo ambavyo wananchi tutakuwa tunawapunguzia mzigo. Lakini wakati huo huo tunaendelea kuamini kwamba ushirikiano baina ya serikali na wananchi ndiyo njia ya uhakika ya kupata huduma endelevu, nzuri na za kumridhisha kila mtu.

Huko nyuma tuliwahi kutangaza na kutoa elimu bure, matibabu bure lakini haikuwa endelevu kutokana na msingi wa uchumi haukuwa imara. Kwa hivyo hatuwezi tukaelekea kutoa ahadi zisizokuwa na matumaini bila ya kuwa na uhakika wa msingi wa uchumi.

Tunasisitiza kwamba tunaendelea kukuza msingi wa uchumi wetu ili uendelee kuhimili huduma hizi ambazo tunazitoa katika kipindi hiki. Tunaendelea kushirikiana na wananchi hadi hapo ambako kila mtu ataona kwamba hizo zitatolewa bure.

SWALI: Profesa Lipumba amewahi kusikika akiahidi kwamba kama CUF itaingia madarakani serikali yake itapandisha mrabaha wa madini kutoka asilimia tatu hadi 30 ili kuongeza mapato ya serikali kwa lengo la kuwezesha kupatikana kwa ajira mpya milioni 2.5. Nini maoni yako kuhusu ahadi hizi?

JIBU: Ni kweli na mimi nimesikia akisema kuwa atapandisha mrabaha toka asilimia tatu hadi 30. Lakini niliposoma ilani yao ya uchaguzi nikakuta wamesema maneno tofauti kidogo. Mle wanasema watapandisha kiwango cha mapato ya serikali kutokana na madini kutoka asilimia tatu hadi 30. Sasa hizi ni dhana mbili tofauti sasa sijui Profesa Lipumba alikusudia kipi katika hayo kama alikuwa ananukuu ilani ya chama chake au alikuwa anatoa yake menyewe.

Kwa ufupi kauli aliyoitoa Profesa Lipumba si ya kuaminika sana na pengine tunaweza kushangaa itolewe na mtu ambaye ni Profesa. Tunaambiwa ni Profesa wa uchumi lakini hakuna hata nchi moja duniani inayotoza mrabaha wa asilimia 30 ya madini ya aina yoyote. Bostwana nimeitolea mfano inatoza mrabaha wa asilimia kumi kwa madini yaliyo adimu sana yale ya thamani kubwa na kwa madini ya kawaida kama dhahabu ni kati ya asilimia tatu na tano.

Tumefanya utafiti na kubaini hakuna nchi inayotoa mrabaha wa zaidi ya asilimia 10 na kauli hiyo itakuwa ya kuwatisha wawekezaji wanaokuja. Huwezi kumwambia atoe asilimia 30 wakati hajaanza hata kuchimba madini na kupata faida.

Kwa kauli hiyo, kama CUF wataingia madarakani ina maana kwamba wawekezaji watakimbia. Walioko hapa nchini wataondoka na wale wanaokusudia kuja ndiyo kabisa hawatakuja. Sasa kama hali itafikia hapo kutakuwa na maendeleo yoyote?

SWALI: Mbowe amekuwa akiahidi kwamba akiingia madarakani ataondoa mikoa na badala yake ataweka kanda kwa maana majimbo ambayo wakuu wake watachaguliwa. Sambamba hilo amekuwa akiahidi kwamba kila eneo la nchi litaachiwa kutumia pekee mapato ambayo yatakuwa yakitokana na rasilimali za nchi. CCM mna maoni gani kuhusiana na sera hizi?

JIBU: Kwanza tungependa wananchi wabaini unafiki uliopo kwenye hizi kauli. Mbowe amekuwa akijinasibu kwa uzalendo na kwamba yeye atajenga serikali yake kwa msingi wa urithi wa Baba wa Taifa kwamba ataendeleza yale ya Baba wa Taifa. Sera za Baba wa Taifa zinafahamika kwamba ametujengea misingi ya taifa moja lenye umoja na mshikamano kwa watu wake.

Sasa kama mtu unataka kuendeleza urithi huo tulioachiwa na Baba wa Taifa wa umoja wa kitaifa na wa taifa moja lililo imara, lenye watu wenye mshikamano wa hali ya juu huwezi sasa ukaja na sera ambazo zina mwelekeo wa kuwatenganisha na mwelekeo wa kuumomonyoa huo umoja ambao umekwishajengwa.

Kwanza anaposema ataondoa mikoa na kanda hizo zitakuwa na serikali zake ambazo zitachaguliwa, sasa hapo unaweza kujikuta unajenga vitaifa ndani ya taifa. Hivi sasa kuna taifa moja lakini ukianza kuweka hizi kanda ambazo aghalabu zitakuwa za ukabila zitachukua sura za kiukabila na hapo hatakuwa anafuata misingi tuliyoachiwa na Baba wa Taifa bali atakuwa anaivunja. Matokeo yake tutajikuta tunafarakana katika majimbo.

Vile vile ukisema unaondoa mikoa 21 tuliyo nayo kwa Tanzania Bara au 26 kwa Tanzania nzima uweke majimbo kama manane ina maana kwamba unaondoa utawala kutoka kwa wananchi. Jitihada zote tumekuwa tukifanya kusogeza huduma za utawala kwa wananchi ndio maana mikoa imekuwa ikiongezwa.

Rais Mkapa ameongeza mkoa wa 21 kwa hoja hiyo ya kusogeza huduma kwa wananchi na hivi karibuni ameongeza wilaya alipokuwa akivunja Bunge kwa hoja hiyo hiyo ya kusogeza huduma za utawala kwa wananchi. Sasa tumekwishafika huko anakuja Mbowe na sera yake sasa ya kuzikimbiza hizo huduma kwa wananchi ili sasa wananchi badala ya kumtafuta mkuu wa mkoa labda umemkuta pale kwa kumfuata kilomita 100 tu au kilomita 200 sasa utalazimika kumtafuta kwa zaidi ya kilomota 400 hadi 500. Sidhani kama hizo sera zitakuwa ni za manufaa kwa wananchi.

Lakini pia katika hili suala la kugawa rasilimali anaposema kila wananchi katika maeneo yao watumie rasilimali zao- Wachagga watumie mlima Kilimanjaro, Mbeya na Nyanda za Juu Kusini watumie madini yao ya chuma na makaa ya mawe. Sasa hizi ni sera za kufitinisha watu.

Kwanza hutaweza kujenga taifa maana serikali kuu itapata wapi mapato yake ikiwa kila mtu aambulie chake. Ile mikoa ambayo haina kitu watafanya nini? Watajisikia Watanzania au utawaambia nini watu kama hao? Lakini zaidi ya yote ikiwa atakuja na hoja hiyo karibu asilimia 80 ya mapato ya serikali yanakusanywa katika mkoa wa Dar es salaam. Kwa hali hiyo unaweza kuwadanganya watu kwamba hapa mna Mlima wa Kilimanjaro, utalii mwingi lakini katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato asilimia themanini yanakusanywa katika mkoa wa Dar es Salaam.

Naamini hizi sera kama ni za ubaguzi. Mimi sijaona Ilani ya CHADEMA naisikia tu na kama zipo sera kama hizi nadhani hazikufanyiwa utafiti wa kina kujua madhara yake na yanayoweza kulipata taifa. Madhara hayo yatasababisha kutuletea fitina na watu wataoneana wivu.

Lakini pili tutakuza tofauti za kiuchumi baina ya maendeleo ya nchi yetu. Hivi sasa jitihada ni kuzipunguza hizo tofauti lakini zikija sera kama hizi zitazidi kuzipanua. Kwa maoni yangu sera hizi ni za hatari za kutenganisha za kuvunja misingi ya taifa letu ambayo ni umoja na mshikamano na za kuleta kuongeza tofauti baina ya watu wetu na kufitinisha watu wetu. Tunaomba Watanzania wazikatae sera hizo.

SWALI: Umezipokeaje mbwembwe za Mbowe kuanza kutumia helikopta katika kampeni zake?

JIBU: Nadhani umetumia neno zuri mbwembwe! Lakini nadhani Watanzania hawataki mbwembwe wanataka umakini wa sera, sera za kuleta matumaini na siyo kupita ukiwakoga na wakati mwingine helikopta inaporuka inawarushia vumbi tu watu.

Mimi naona pana unafiki tu hapa sababu ni watu hawa hawa walikuwa wkaipinga ununuzi wa ndege ya serikali ambapo serikali ilijenga hoja kwamba inarahisisha usafiri wa mkuu wa nchi ndani na nje ya nchi kwa sababu mkuu wa nchi kazi zake ni za ndani na nje.

Watanzania ni mashahidi kwamba jitihada hizi alizozifanya Rais zimeleta matunda mazuri katika kipindi chake cha awamu ya tatu cha miaka kumi. Sehemu kubwa ilitokana na safari zake za nje ambapo amekwenda kuonana na viongozi wenziwe kujenga hoja mpaka tukafikia mahala pa kufutiwa madeni, tukajenga imani kwa marafiki na wahisani wetu wakajenga imani iliyokuwa imewatoka hata ya kutukopesha na kuturudishia ambayo ilikuwa imezuiwa. Yote haya yamewezekana kutokana na kusafiri nje.

Kwa hivyo sisi tulijenga hoja hiyo kwamba ipo haja ya kurahisisha usafiri lakini wakawa wa kwanza kuipinga. Sasa kimekuja kipindi cha kampeni tu wanatumia helikopta.

Sisi katika CCM tulilijua kwa sababu CHADEMA walisema zamani kwamba watatumia helikopta. Siku zile walisema watanunua na sisi tukaulizana tukatafakari ndani ya chama busara ya kutumia helikopta zetu. Lakini tukaamua kwa makusudi tu kwamba hatutatumia helikopta tutatumia magari, tutatumia baiskeli, tutatumia pikipiki tutakwenda kwa wananchi kwa miguu ili tuwe karibu nao tunapozungumza nao tunajua na shida zao, shida za usafiri za usafiri zinazowakabili wananchi walioko mbali au popote pale walipo utaijua kwa kwenda na kwa kuhisi tatizo lenyewe. Kama kuna matatizo ya maji, shule utayaona kwa kwenda kwa usafiri wa magari, pikipiki, baiskeli na hata miguu si kwa helikopta.

Hilo tuliliacha kwa kujua kabisa kwamba tutakuwa karibu na wananchi na tutaelewa vizuri matatizo yao ikiwa tutawaendea kwa njia ya ardhini kuliko kwa njia za angani. Kutokana na hali hiyo tuliamua kununua magari kwa viongozi wetu wa chama katika ngazi ya mkoa, wilaya na pikipiki na baiskeli kwa viongozi wa matawi ili wawafikie wananchi kwa urahisi.

Hali hiyo imewezesha mtandao kuwa wa uhakika zaidi sio wa mbwembwe bali kwa umakini wa kujua shida za watu ili kuja kuwashughulikia ipasavyo.

SWALI: Wananchi wengi wamekuwa wakijiuliza kwa maana kwamba nchi yetu ni moja ya nchi zenye sifa ambazo sifa ya amani na utulivu. Sasa kwa kuangalia chama cha CUF ukiangalia bendera yao ina mchirizi mwekundu. Unalielezeaje hilo?

JIBU: Bendera ya CUF ni wao wenyewe wameamua rangi zao lakini kama mtu wa Zanzibar kule najua wakati wa ukoloni kulikuwa na sera ya Sultani tukiita pesa ya shaba. Ile ilikuwa na mizani sasa tulipoona wenzetu wameweka mizani tukaona ni kumbukumbu ya usultani ndio maana tukaitazama kwa shaka.

Bendera nyekundu nayo ni urithi kwa sababu nayo bendera ya Sultani ilikuwa nyekundu. Nadhani kila mmoja ana sababu zake za kuziweka hizo rangi lakini kubwa ambalo ningeweza kusema hapa kama Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi ni kwamba huu mwelekeo wa vurugu ambao haidhuru wakati mwingine na vyama vingine vinafanya lakini zaidi chama cha CUF mara nyingi. Vitendo vya vurugu ambavyo vimetokea utakuta ni baina ya CCM na CUF lakini aghalabu CUF ndio wanakuwa wameanza.

Sasa huu siyo mwekeleo mwema na eneo ambalo nadhani hata katika muafaka baina ya vyama vyetu malengo yake yalikuwa kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi ulio uhuru na wa haki na uchaguzi ulio huru na wa haki ni ule ambao utakuwa wa salama na amani.

Sasa ikiwa tunaanza kuvuruga amani tunavunja ile misingi ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki. Katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa sasa wenzetu wamekwishabainisha kwamba wanashindwa wakubali tu wasitafute njia za kuvuruga ili tukose wote. Lakini hatuwezi tukakosa wote na hakika Chama Cha Mapinduzi kitashinda kama ambavyo kimekuwa kikishinda.

SWALI: Kwa kumalizia, nini maoni yako kuhusiana na uchaguzi wa mwaka huu ambao utatufungulia ukurasa wa nne wa uongozi?

JIBU: Wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura. Kwanza wasikubali hivi vitisho vinavyofanywa na wapinzani. Vitisho hivyo vina lengo la kuwazuia kwenda kupiga kura kwa hivyo wasiwape faida hiyo wapinzani, isiwe mtu akifanya vurugu anapata lake hatutajenga Tanzania ambayo tunakusudia. Tunawaomba wajitokeze tu kwa wingi siku ya kupiga kura.

Pili kuna dhana ambayo imeanza kujitokeza mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete ameishachaguliwa. Sasa hii inatia wasiwasi kidogo kwamba isije ikajengeka hiyo dhana kwamba hakuna haja ya kwenda kupiga kura. Kikwete atachaguliwa kuwa Rais kutokana na kura ambazo Watanzania wote watampigia na kura hizo zitapigwa kwenye vituo kwa hivyo wananchi itabidi watoke kwenda kwenye vituo kumpigia kura.

Kwa kufanya hivyo tutakuwa na uhakika wa asilimia 100 kwamba tumemchagua Kikwete . Kwa hivyo natoa mwito kwa wananchi wote tuhimizane na tuelimishane katika hilo maana ipo hatari kama tusipoelemishana wengine watasema tayari amekwisha kuwa Rais.

Wote tujitokeze tuelimishane, tuhimizane siku ya uchaguzi ili wote kwa umoja wetu watanzania kwa nguvu zetu zote twende tukampigie kura Kikwete ili tufaidike na ile kauli mbiu ya Ari Mpya Nguvu Mpya na Kasi Mpya katika ujenzi wa Tanzania yetu.