Karume: Chaguo la wananchi lisilo na shaka

MIAKA mitano si muda mrefu, lakini mtu anaweza kujipatia sifa kwa kipindi hicho kifupi kwa mazuri aliyoyafanya kwa jamii yake. Makala hii ya Mwandishi Omar Said Ameir inaeleza kwa kinagaubaga mambo mengi yaliyofanywa na Rais Amani Abeid Karume na hivyo kuonyesha uhalali wananchi kumchagua tena kuendelea kuongoza Zanzibar.

RAIS Amani Abeid Karume, tangu alipochaguliwa miaka mitano mwaka 2000, amefanya mambo makubwa kwa Zanzibar katika kipindi hicho cha miaka mitano.

Hivi sasa anaomba tena ridhaa kwa wananchi kwa ajili ya kuwatumikia katika kipindi kingine cha miaka mitano.

Rais Karume siyo tu kwamba anaomba kuendelea kuongoza bali hatua hiyo, inakuja baada ya kuwa kiongozi bora kwa kuleta maendeleo ya nchi kwa muda mfupi na kwamba wananchi wakimpa ridhaa ya kuendelea zaidi bila shaka Zanzibar itakuwa imekamilisha hatua yake kubwa ya kuimarisha miundombinu na huduma za jamii.

Kiongozi huyo ambaye ni mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ana uzoefu na ni mfano wa kuigwa.

Katika siasa na uongozi wake, ameonyesha dira kwa kuiweka nchi katika ramani ya dunia kwa huduma za jamii kama afya , elimu, umeme na miundo mbinu ya barabara.

Pamoja na makubwa hayo yote aliyoyafanya, Rais Karume ambaye kimaumbile ni mrefu, mwenye kuongea kwa upole, mnyenyekevu, msikivu, mvumilivu na ni mtu ambaye hana tabia ya kukurupuka baada ya kusikia jambo.

Hutumia bisara busara na hatawaliwi na pupa. Lakini kubwa zaidi ni kiongozi asiye na majigambo hata afanyapo jambo kubwa.

AMANI NA UTAWALA BORA

Sifa kubwa ambayo ni ya kipekee na ya kujivunia mgombea huyo katika kipindi hicho kifupi ni kuiweka Zanzibar katika nafasi ya juu kimaendeleo.

Aliikuta nchi ikiwa katika matatizo ya kiuchumi kutokana na kususiwa na wahisani baada ya uchaguzi wa mwaka 1995.

Kufuatia hali hiyo nchi ilikuwa katika hali mbaya kiuchumi, kiuhusiano na mataifa ya nje, mashirika ya kimataifa pamoja na jumuia ya kimataifa.

Baada ya kuingia madarakani, Karume aliweza kuwawishi wahisani kuja tena Zanzibar na kutoa misaada ya maendeleo kufuatia muafaka baina ya CCM na CUF mwaka uliotiwa saini mwaka 2001.

Hatua hiyo ikaifanya Zanzibar kuwa na amani na utulivu na kutawalika kwa njia ya utawala bora aliouanzisha na hadi sasa mambo kadhaa yameshafanyika .

Mambo hayo ni pamoja na kuundwa kwa tume huru ya Uchaguzi, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Tume Maalum ya Muafaka ambayo imeshamaliza muda wake lakini ilifanya kazi nzuri ya kuwaelimisha wananchi juu ya dhamira ya Muafaka huo wa kisiasa.

Rais mstaafu wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi, amelithibitishia taifa kuwa kwa kusema kuwa Rais Karume ameonesha uwezo mkubwa wa kujenga uchumi na maendeleo ya Zanzibar kwa jumla.

Michango na misaada kutoka kwa washirika wa Maendeleo tangu kuwepo madarakani imeimarika na hali kadhalika mitaji ya uwekezaji imeongezeka visiwani Zanzibar.

Hatua hiyo inaonekana kuwa ni kukubalika kwa Rais Karume na washirika wa maendeleo na hivyo kuna kila sababu ya kumrudisha tena madarakani.

SERA YA KUPUNGUZA UMASIKINI

Rais Karume ni mtu anayekerwa na hali mbaya ya umasikini katika jamii. Kutikana na kuchukia kwake huko, alianzisha Mpango Mkuu wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUKUZA), ambao umeshirikisha wahusika kadhaa lengo likiwa wananchi angalau waishi kwa matarajio mapya ya kupunguza hali hiyo katika nchi.

Mpango huo aliouanzaisha ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020 , ambayo inahimiza kupunguza janga la umaskini miongoni mwa wananchi.

Juhudi mbalimbali zimefanyika katika kipindi cha miaka mitano ya awali aliyoongoza.Baadhi ya juhudi hizo ni kuimarisha miundo mbinu ya barabara kwa kuondosha umasikini wa kipato ikiwa ni nyenzo ya kuwafanya wananchi kwenda huku na kule kwa harakati za kibiashara.

Mikopo ya fedha kwa vikundi vya vijana, wanawake na wazee imetolewa ikiwa ni moja ya hatua ya kuunguza umaskini.

Wananchi wanaoishi kando ya bahari pia wamepatiwa nyenzo za kilimo cha mwani ikiwa ni kukabiliana na umasikini. Wengine wamepatiwa boti za uvuvi na zana zake Unguja na Pemba ili kuwasaidia wananchi kupambana na umasikini. Vifaa hivyo vina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 377.

Chini ya uongozi wa Rais Karume, mikopo kutoka katika benki na taasisi za fedha imeongezeka na benki zingine kufungua matawi Zanzibar kama vile Barclays na Benki ya Posta.

Hivi sasa wananchi wanakopa katika benki hizo kwa kufanya biashara na wengine kujenga nyumba za kuishi hasa kwa wafanyakazi wa serikali na huku PBZ ikiwa inaongoza kwa kutoa mikopo hiyo kwa wafanyakazi.

KODI NA UWEKEZAJI

Chini ya uongozi Rais Karume, suala la ulipaji wa kodi limeimarika sana na hivi sasa serikali inakusanya fedha nyingi.

Mapato ya serikali yameongezeka kutoka shilingi bilioni 38.60 mwaka 2000 hadi kufikia shilingi bilioni 50.70 mwaka 2004. Hali ya uwekezaji rasilmali nao umekuwa mara dufu kutoka thamani ya shilingi bilioni 24.40, mwaka 2000, kufikia bilioni 56.60 mwaka jana.

Hii inaonesha dhahiri kuwa chini ya uongozi wa Rais Karume mambo mengi yamefanyika yenye maslahi ya kwa wananchi kwa kutumia fedha za walipakodi .

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuimarisha huduma za maji mijini na vijijini , afya na barabara kadhaa zilizojengwa na serikali pekee na pia ujenzi wa nyumba za Michenzani ambazo ziliachwa kwa muda mrefu.

KILIMO

Rais Karume hakuacha suala la kilimo, kwani anaelewa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa Zanzibar na ndiyo njia pekee ya kujitosheleza kwa chakula.

Kwa mujibu wa takwimu, chini ya uongozi wake kilimo kimechangia wastani wa asilimia 23 katika pato la taifa. Pia katika utawala wake, serikali imetenga kiasic ha hekta 8,000 kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji kujitosheleza kwa mchele nchini na tayari Japan imeonyesha nia ya kuasaidia.

Nchi rafiki pia kama China na Korea nazo zimeshasaidia zana kilimo kama matrekta na vifaa vyengine kwa lengo la kukuza kilimo na kupunguza umasikini.

Rais Karume katika juhudi zake za kuiweka Zanzibar katika utalii wa daraja la juu kwa kuinua uchumi wa nchi, amelenga kuwepo kwa hoteli za kisasa ambazo tayari zimeanza kujengwa kama vile Ocean Paradise na zingine.

BARABARA

Katika kipindi cha miaka mitano, Rais Karume ameimaririsha miundo mbinu ya barabara kuliko awmua nyengine tano zilizotangulia.

Ameweza kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 127.7 kwa Unguja na Pemba na katika kiwango cha lami. Kati ya kilomita hizo 75.1 zimejengwa Unguja na zilizobaki Pemba .

Katika kuhakikisha kwamba barabara zinazojengwa zinakuwa na utunzaji mzuri pamoja na uimara madhubuti, ameanzisha mfuko wa barabara ambao tayari umekusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.43.Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.19, zimetumika katika sekta hiyo muhimu.

UMEME

Bila shaka hakuna asiyefahamu kuwa nishati ya umeme ni muhimu sana kwa maendeleo ya mwanadamu na pia katika kujikwamua kimaisha kwa kutumia nishati hiyo.

Huduma ya umeme imekuwa na mabadiliko makubwa ya maendeleo. Tayari vinu vitatu vya vya kuzalishia umeme kisiwani Pemba vimefanyiwa matengenezo makubwa kwa msaada wa NORAD na serikali na hivi sasa tatizo la mgawo limeondoka.

Aidha juhudi za kumaliza tatizo la umeme Pemba, zinaendelea kuchukuliwa kwa kutafuta uwezekano wa kupeleka umeme kisiwani humo kutoka Tanga kwa njia ya bahari .

Hivi sasa kisiwani Pemba katria mradi unaofadhiliwa na NORAD wa kusambaza umeme vijijini, kiasi cha vijiji 61, vyenye wananchi zaidi ya 30,000 vinatarajiwa kufaidika na huduma hiyo kazi.

Mradi wa TASAF ambao umekuja wakati wa awamu ya kwanza ya Rais Karume, nao umesaidia sana katika kuimairsha huduma jamii kwa wananchi .

Mfuko huo Zanzibar ilipatiwa jumla ya shilingi bilioni 3.00, kutoka Benki ya Dunia, ambapo zimegawiwa sawa Unguja na Pemba.

Jumla ya miradi 75 ya maendeleo ya kijamii imekamilika na kati ya hiyo 40 imetekelezwa Unguja na iliyobaki Pemba na hivi sasa wananchi wanafaidi matunda yake.

ELIMU NA AFYA

Kwa sekta ya elimu tayari Rais Karume amelivusha taifa katika mkataba wa kimataifa juu ya sekta hiyo.

Zanzibar imeweza kufikia lengo la Maendeleo ya Milenia kuwapatia elimu ya msingi watoto wote wanaopaswa kupatiwa elimu hiyo kabla ya mwaka 2015.

Aidha idadi ya skuli zimeongezeka kutoka 331 hadi kufikia 521 na sasa kuna vyuo vikuu vitatu nchini.

Hali ya huduma ya afya kumekuwa maendeleo makubwa chini ya uongozi wa Rais Karume. hadi kipindi sasa kuna vituo 141 kwa Unguja na Pemba na hivi sasa hakuna anayetembea zaidi ya kilomita tano bila ya kupata huduma ya afya Zanzibar.

Vituo vya maji safi na salama katika kipindi chake cha miaka mitano vimeongezeka kutoka 58 vilivyokuwa vinatoa lita milioni 62 hadi vituo 122 ambavyo vinatoa jumla ya lita 103 kwa Zanzibar nzima.