Mikakati ya kuvuruga uchaguzi idhibitiwe,

·         Itaiingiza nchi kwenye matatizo makubwa

KATIKA kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 30, mwaka huu, kila chama cha siasa kimo katika mikakati na mbinu nzito katika kuhakikisha kinaibuka mshindi au hata kuambulia chochote katika uchaguzi ujao ambao utakuwa wa tatu katika mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu kuasisiwa mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Vyama vya siasa 18 vyenye usajili wa kudumu nchini vitashiriki uchaguzi mkuu huku vyama 10 vikiwa vimewasimamisha wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mapambano  ya kisiasa kwa vyama vyote kwa wakati huu yameelekezwa katika mbinu na mikakati ya kila chama katika kujihakikishia ushindi. Mikakati na mbinu za vyama hivi ziko katika namna mbili. Ziko mbinu na mikakati ya kistaarabu na kiungwana. Hii ni pamoja na wagombea wa vyama husika kueleza sera za vyama vyao kwenye majukwaa ya kisiasa lengo likiwa ni kuwavuta wapiga kura na wananchi kwa ujumla kuwapa kura siku itakapowadia.

Hata hivyo upo mkakati wa pili, usio wa kistaarabu au kiungwana, ambao unaonekana kutumika na baadhi ya vyama vya siasa, na hasa kwa upande wa upinzani. Katika mkakati huu, baadhi ya vyama vya siasa kwa upande wa upinzani vimeamua kutumia hadaa na vitisho kwa wananchi ili wavipigie kura vyama hivyo.

Lengo la mikakati hii ni kuwatia hofu wananchi kwamba wasipovichagua vyama hivyo basi wapiga kura hao watajikuta katika matatizo. Ni mbinu na mikakati gani hiyo iliyoandaliwa na baadhi ya vyama vya upinzani? Katika safu hii wiki iliyopita tulijaribu kuainisha baadhi ya mbinu chafu kwa upande wa upinzani.

Kutokana  na umuhimu na unyeti wa suala lenyewe tumeona ni vema tujaribu kuainisha na kuchambua tena mikakati hii michafu iliyoandaliwa na mingine kuanza kutekelezwa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa na hasa wale wa CUF na hata CHADEMA. Miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na wapinzani ni fujo kwa kuwaandama wafuasi wa chama tawala, CCM, kwa kuwapiga kwa mawe, fimbo na silaha nyingine wakati wa mikutano ya kampeni (wanapokwenda au kurejea kutoka katika mikutano hiyo) katika baadhi ya maeneo nchini.

Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuhusu matukio hayo ya uvunjifu wa amani wakati huu wa kampeni katika baadhi ya mikoa. Mfano ni matukio yaliyotokea huko Bukoba na Tarime siku chache zilizopita ambapo wafuasi wa CUF na hata wale wa CHADEMA walianzisha mapambano kwa kuwaandama wafuasi wa CCM na kuwapiga.

Hatusemi mkakati wa matusi wanayovurumishiwa wagombea wa CCM katika baadhi ya maeneo nchini kutoka kwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani. Iko mikakati mibaya zaidi ambayo imeandaliwa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani. Taarifa za uhakika kutoka katika baadhi ya mikoa nchini zinasema kuwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa wamepanga kufanya fujo kubwa kwenye vituo vya kupigia kura siku hiyo ya Oktoba 30 kwa lengo la kuvuruga uchaguzi.

Miongoni mwa mikakati na mbinu zinazotajwa kuwa zimeaandaliwa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa kwa upande wa upinzani ni kwa wafuasi wao kutoondoka kwenye vituo hivyo baada ya kupiga kura ili kuleta vurugu wakati wa kuhesabu kura na kuhakikisha kuwa "watu wao" wa upinzani "wanapita".

Pia inaelezwa kuwa baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani wamepanga hata "kupora" masanduku ya kura kwa lengo la kuvuruga upigaji kura na utangazaji wa matokeo. Hili la mkakati wa "kupora" masanduku ya kura ni la hatari. Lakini pengine msomaji wa safu hii atashitushwa zaidi kusikia kuwa zipo taarifa za mbinu zilizoandaliwa na baadhi ya wapinzani za kuwazuia njiani wapiga kura (wanaoonekana kuwa ni wana-CCM na hasa wazee na wanawake), katika baadhi ya vijiji, wasiweze kwenda vituoni kupiga kura.

Ikumbukwe kuwa huko vijijini upo uwezekano mkubwa kabisa kuwa baadhi ya vituo vya kupigia kura vitakuwa mbali na makazi ya watu ambapo inawezekana baadhi ya wapiga kura wakalazimika kuvifuata vituo vya kura zaidi ya hata kilomita 20.

Kama ndivyo, upo uwezekano wa baadhi ya wapiga kura, na hasa wazee na wanawake, kushindwa kupiga kura kwa kuzuiwa na wahuni wachache watakaokuwa wamejificha njiani. Kwa nini baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa waandae mbinu na mikakati hii michafu? Jibu la swali hili ni rahisi nalo ni kwamba vyama kadhaa vya siasa na hasa vile vya upande wa upinzani vimekata tamaa ya kushinda katika uchaguzi ujao kama utaendeshwa katika misingi ya amani, utulivu na haki.

Kwa hiyo vyama hivyo kwa upande wa upinzani vimeamua kutumia mbinu na mikakati ya kuwatia hofu wananchi ili idadi ya watakaoipigia kura CCM ipungue. Kinachoutia hofu upinzani katika uchaguzi mkuu mwaka huu ni uwezekano wa vyama vya upinzani kushindwa vibaya mno hali itakayoonyesha kuwa havina lolote wala maana katika siasa za Tanzania.

Kimsingi, uwezekano huo upo kwa vyama vya siasa kufa "kifo cha mende" kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 30. Kwenye uchaguzi wa viongozi wa vitongoji, vijiji na serikali za mitaa uliofanyika miezi michache iliyopita CCM imeweza kushinda kwa kishindo kwa kupata ushindi wa karibu asilimia 97 huku vyama vyote vya siasa vya upinzani, vikiwemo vile vikubwa vya CUF na CHADEMA, vikigawana asilimia tatu iliyobaki.

Zipo  dalili zinazoonyesha kuwa katika uchaguzi mkuu ujao wa oktoba 30 upinzani utaanguka zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2000 ambapo Rais Mkapa (CCM) alipata asilimia 72 ya kura zilizopigwa. Katika uchaguzi huo kwa upande wa ubunge, Tanzania Bara, upinzani uliweza kupata viti 14 tu. Katika uchaguzi mkuu ujao upo uwezekano mkubwa mgombea wa CCM kwa nafasi ya Urais, Jakaya Kikwete, akaweza kupata zaidi ya asilimia 85 ya kura zitakazopigwa.

Hii ikitokea litakuwa pigo kubwa kwa upinzani. Ili kuepukana na balaa hili la kushindwa vibaya ndipo baadhi ya wafuasi wa upinzani wanaona kuwa ni vema waanzishe mbinu na mikakati ya kuwatia hofu wananchi wasiweze kwenda kupiga kura.

Kimsingi mikakati na mbinu hizi chafu za baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani inabidi zipigwe vita kwani ni mbinu na mikakati ya kishenzi inayoweza kuitumbukiza Tanzania katika matatizo. Na hii ni kazi kwa vyombo vya dola vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha wote walioandaa mbinu na mikakati michafu ya uchaguzi wanashughulikiwa ipasavyo.

Simu: 0744-309858

E.mail: kisasa2000@yahoo.com