Kutoana ngeu si njia ya kumaliza tofauti zetu

WAKATI tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, hali ya usalama kwa wafuasi na wapenzi wa vyama mbalimbali vya siasa inazidi kuwa hatarini, kwani baadhi ya viongozi hawana ustaarabu hata kidogo. Wanajiona kama madume wawili wanaogombea 'mchumba' mmoja, na hivyo kujengeana uhasama ambao wanadhani namna ya kuumaliza ni 'kummaliza' mpinzani wako.

Ustaarabu na 'kuchezeana rafu' katika mapambano ya kisiasa ni mambo ya kawaida kwa watu wa kambi tofauti, isipokuwa kutukanana na kupigana. Kinachotamba katika kampeni ni nguvu ya hoja na wala si kutunishiana misuli, na mwamuzi wa mwisho ni wananchi siku ya kupiga kura.

Katika siku hizi za kampeni, kila siku kuna habari za mapambano kati ya wafuasi wa vyama tofauti. Hivi mbona hatujasikia viongozi wa juu wa vyama hivi wakitoana ngeu - bali baadhi yao wamekuwa mabingwa wa kuwachochea wafuasi wao watwangane, wakati wao na familia zao wako sehemu fulani salama salimini? Huu ni ustaarabu gani ?

Ustaarabu wa kupigana ni utamaduni mgeni kabisa katika siasa nchini mwetu. Ni utamaduni wa kuiga kutoka vyama na makundi ya kisiasa ya nchi za nje ambako hulka ya kupigana ndiyo jadi yao. Suluhu kwao haipatikani kwa namna yoyote zaidi ya umwagaji wa damu na kutoana roho.

Kwa nini baadhi ya vyama vya siasa vinaamua kufanya vurugu na mapigano na vikundi vingine? Mtu ambaye hajiamini mara nyingi anakuwa na tabia ya uchokozi. Mtu asiyejiamini akishindwa yuko tayari kupigana kwa madai kwamba ameonewa na hakushindwa kihalali.

Chunguza tabia ya mtoto mchokozi mtaani. Mtoto huyu huwa na tabia ya kutoridhishwa na kila kitu, na hivyo huziba upungufu wake kwa kupiga wenzake na hata kama atatokea mtoto mwenzake atakayeweza kumdhibiti, bado ataendelea na tabia ya kupiga wenzake kila anapopata nafasi.

Katika siasa ni vyama dhaifu na visivyokuwa na hoja pekee ndivyo chimbuko la uvunjaji wa amani kila wakati, kwa sababu vinatambua hatma yake mbele ya umma, na hivyo huona njia pekee ni kufanya vurugu ili vionekane kwamba vipo, ni hai na vinakubalika.

Suala la demokrasia limekuwa ndilo kinga ya vurugu zote za kisiasa. Lakini kwa nini hatuko tayari kujifunza kutoka baadhi ya nchi ambako demokrasia na ustaraabu wa kisiasa umejengeka, na kule ambako uhasama wa kisiasa umesababisha kumwagika damu na utulivu wa kisiasa haupo kabisa ? Tuna haja kweli kukumbushana Burundi, Kongo, Liberia kwa kutaja nchi chache katika Afrika na kwingineko, ambako maisha ya watu yameangamia kutokana na uhasama wa kisiasa ?

Vyama vya kisiasa vinapaswa kutambua kwamba demokrasia siyo kuruhusu vitendo vya kuvunja sheria, na unapozuia vitendo hivyo wala si ukandamizaji. Sheria hizi hizi zilizopo sasa, mpe serikali kiongozi yeyote aliyepo atatawala kwa kuzifuata hizo, na wengine waliopo nje ya serikali watadai kwamba sheria hizo ni za ukandamizaji.

Hulka ya vyama vingi vya siasa vya upinzani katika nchi zinazoendelea kama yetu ni kupinga serikali bila hoja ya msingi kwa lengo la kutaka kuiondoa serikali madarakani, wakati katika nchi za wenzetu hoja, pamoja na kwamba ni kutaka kuleta mabadiliko wanayoona ni ya msingi kwa kuiondoa serikali madarakani kwa njia ya kura, lakini siyo kweli kwamba wakati wote viko katika mapambano na chama cha serikali iliyoko madarakani kwa kuanzisha vikundi vya vijana wenye silaha na kuzusha mapigano na umwagaji damu na wapinzani wao.

Kwa taratibu za kistaarabu hakuna haja ya watu kupigana kutokana na tofauti za kisiasa. Inapofikia kupigana magumi na mateke tunakaribisha nguvu za dola kuingilia, kwani hali hiyo haikubaliki na wala hairuhusiwi, na kitakachofuata hapo ni kuilaumu dola kwa ukandamizaji, hata kama walioanzisha fujo ni wapinzani ambao kama wasingedhibitiwa na dola wangesababisha maafa makubwa.

Vitendo vya kupigana ni kuvunja sheria za nchi na kuhatarisha usalama wa raia, na wanaodhurika ni waliomo na wasiokuwemo, na kunapotokea vurugu mlengwa na asiyelengwa wote wanapata madhara. Je hivi ndivyo tunavyotaka iwe ?

Simu: 0744-464279

e-mail: mhando3@hotmail.com