Waangalizi walikuja kuangalia, si kufundisha nini cha kufanya
Na Dunia Mzobora
ZIPO semi mbalimbali za Kiswahili zinazofundisha mambo kadha wa kadha kuhusiana na mwenendo wa maisha ya binadamu, katika sayari hii.
Semi hizi, mbali ya kuandikwa katika vitabu mbalimbali vitakatifu, pia huzungumzwa mara nyingi na wazungumzaji wa lugha, hususan Kiswahili.
Jambo moja la kuzingatia ni kwamba, japokuwa baadhi ya semi hizi zimeelekezwa kwa vitu, mimea na hata wanyama, lakini maudhui yake yanawalenga moja kwa moja binadamu.
Moja ya semi hizo ni ile isemayo: “Nyani haoni kundule”. Ukiiangalia kwa undani zaidi, usemi huo utadhani anayelengwa hapa ni nyani, mnyama mdogo aishiye porini, lakini kumbe anayezungumzwa hapa ni binadamu.
Kimsingi, binadamu ni kiumbe wa ajabu sana tofauti na viumbe vingine vya Mwenyezi Mungu. Siku zote binadamu huangalia ya mwenziwe tu, hata kama yeye amejaa mapungufu yasiyo na mfano.
Kwa hulka yake, binadamu ni kiumbe mwenye roho mbaya, kwani siku na muda wote humwombea mwenziwe mabaya, na endapo anayoyaomba yakimkuta, yeye husimama kando ‘akimsanifu’ na kuchekelea.
Tabia hiyo ilijidhihirisha hivi karibuni baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, mwaka huu, kumalizika kwa amani na utulivu, baadhi ya nchi zinazojifanya ‘vinara’ wa masuala ya ‘demokrasia’ zimeanza chokochoko.
Chokochoko hizi zinalenga kutaka kututia ‘kidole cha macho’ baada ya kushuhudia wananchi wa Zanzibar wakikataa kutumiwa kama daraja la kurejesha ‘ubwana’ katika visiwa hivyo.
Mabwana hawa wametaharuki baada ya wananchi wa visiwa hivyo vya Unguja na Pemba, kuwathibitishia kwamba “si kila ukitakacho utapewa, ila kwa mapenzi ya Mola”.
Kwanza, walitumia taasisi zilizokuja kwa ‘mgongo’ wa kutoa elimu ya demokrasia, huku vikipenyeza ‘sumu’ kali dhidi ya CCM na serikali zake, na kisha vyombo vya habari vilivyokesha na kutangaza kama visiwa hivyo ni sehemu ‘isiyokalika’, bado wananchi wamewaumbua!
Hata hivyo, baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa haikushangaza hata kidogo kuzisikia nchi kama Marekani na Uingereza zikija juu na madai kwamba uchaguzi katika visiwa hivyo haukuwa huru na haki!
Sasa hapa ndipo ule msemo wa ‘Nyani haoni kundule’ unapojiri na kusadifu. Hivi lini nchi hizo ambazo leo zinathubutu ‘kubwatuka’ kwamba uchaguzi Zanzibar haukuwa huru na haki, kwao ziliendesha uchaguzi huru?
Kwa kweli, leo sina sababu yoyote ya kuhangaika na nchi kama Marekani, ambayo huko kwao sina cha kujifunza kuhusiana na suala la uchaguzi huru na haki au msingi ya demokrasia ya kweli.
Hivi huko utajifunza nini, kama suala la uchaguzi wa 2000 na 2004 ni aibu tupu na mpaka leo hii bado lipo mahakamani? Kama si uungwana wa mabwana hawa Al Gore na John Kerry, sijui hali huko ingekuwaje leo hii?
Mwingine wenye kimbelembele ni hawa mabwana… Waingereza. Hawa tunawatambua kwa sababu wametawala hapa. Wamekaa kwa zaidi ya miaka 40, lakini hakuna lolote wala chochote walichofanya. Wao kazi yao ‘kuchonga’ tu! Watachonga sana, lakini wananchi hawana budi kuachana nao!
Lakini kwa wachambuzi wa siasa, hususan za Zanzibar, kamwe hawawezi kuwashangaa hawa. Wanachotaka kuionyesha dunia ni kutaka kufuta aibu na machungu yaliyowafika mwaka 1964 kutokana na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Nani hajui kuhusu njama za kuinyima ushindi ASP katika uchaguzi mara tatu kulikofanywa na Mfalme wa visiwa hivyo, akisaidiwa na Mwingereza? Kwa Zanzibar, Mwingereza ana ajenda maalum, na suala la kusema uchaguzi haukuwa huru na haki ni njama za kutaka kurudi kuendeleza hujuma zake dhidi ya Wazanzibari, hatua ambayo haina nafasi katika karne hii.
Hivi ingekuwaje kama mabwana hawa wangekuwa wametia mkono mfukoni na kutoa japo fedha kidogo kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo? Nadhani wangelala pale Ikulu ya Zanzibar, huku wakiikoromea serikali juu ya madai yao ambayo hayana msingi hata kidogo!
Ukweli ni kuwa uchaguzi wa Zanzibar umeendeshwa kwa fedha ya ndani kwa asilimia 100, na kamwe asitokee mtu akajinadi kwa hili au lile… kwani penye ukweli uongo hujitenga na Wazanzibari wamethibitisha hilo.
Kuhusu hili la demokrasia ya kweli, ambayo wenzetu hawa Waingereza wanadai kuwa wao ndio vinara. Hebu tuwaulize: “Hivi Malkia anachaguliwa na nani?” Sasa demokrasia ya kweli mnayodai kuwa nayo na kwamba nyie ndiyo wenyewe iko wapi?
Ningewashauri mawaziri Jack Straw na mwenzake Ian Pearson badala ya kuhangaika na hili la Zanzibar, washughulikie kwanza masuala ya ndani kwao, hasa hili lililoanza kujitokeza kwa Waingereza kuhoji juu ya uhalali wa Malkia, na hasa matumizi yaliyokithiri yanayotokana na fedha za walipa kodi.
Vinginevyo, kwanini tusiamini kwamba hizo ni mbinu za Marekani na Uingereza za kutaka kujipenyeza katika nchi changa kama Tanzania na nyingine kwa mlango wa nyuma kwa kisingizio cha kuimarisha demokrasia, ambayo kwao imewashinda?
Hivi shauku ya nchi hizo ilikuwa kutaka kuiona Tanzania na Watanzania wanapigana wenyewe kwa wenyewe? Hivi hii taasisi ya National Democratic Insitute (NDI) ya Marekani ina mamlaka gani katika kuzungumzia uchaguzi wa moja ya nchi za Afrika kuliko Umoja wa Afrika (AU)?
Kwa Afrika, taarifa ya AU iliyothibitisha uchaguzi wa Zanzibar kwamba ulikuwa huru na haki, ina maana zaidi kuliko ya NDI ya Marekani, ambayo haielewi lolote wala chochote kuhusu mazingira ya Afrika na Waafrika wenyewe.
Lakini, kama alivyosema Rais Benjamin Mkapa wakati akiwakaribisha waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa walipokuwa wanakuja nchini, kwamba waangalizi waje kuangalia tu na siyo kuwafundisha Watanzania nini cha kufanya.
Uchaguzi Zanzibar umekwisha, Marekani na Uingereza wawaache Watanzania wamalize ngwe nyingine ya uchaguzi hapo Desemba 14, kisha wananchi waendelee na ujenzi wa taifa lao changa katika kupambana na maadui watatu, yaani ujinga, maradhi na umasikini.
Watanzania hawangependa kila kukicha ajenda iwe ni uchaguzi, uchaguzi, uchaguzi kwa mwaka mzima. Wanayo mengi ya kufanya kujiletea maendeleo yao, na uchaguzi ni moja tu ya mambo hayo.
duham64@yahoo.com
O744-696895