YALIYOJIRI KAMPENI ZA CCM RUVUMA
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete anaendelea na kampeni katika mikoa
mbalimbali kwa ajili ya kuwaomba wananchi kumchagua kushika wadhifa huo ifikapo Oktoba 30, mwaka huu.
Mwandishi Wetu EPSON LUHWAGO aliyefuatana na mgombea huyo katika mikoa ya kusini na Nyanda za Juu Kusini,
anaelezea yaliyojiri katika kampeni hizo mkoa wa Ruvuma.
BAADA ya kumaliza ziara katika mkoa wa Mtwara, Jakaya Kikwete aliingia mkoani Ruvuma kwa nia ya kuomba kura
kwa wananchi ili waichague CCM kwa maana ya Rais, Wabunge na Madiwani.
Kama ilivyokuwa mkoa wa Mtwara, Kikwete alizidi kuwachengua na kuwavuta wananchi wengi waliokuwa
wakijitokeza ama barabarani au kwenye viwanja vilikofanyika mikutano hiyo kwa nia ya kumwona au
kumsikiliza.
Mapokezi ya mgombea urais huyo wa CCM kuingia mkoani Ruvuma, yalifanyika eneo la Nakapanya wilayani
Tunduru. Alipokewa na Mwenyekiti wa Mkoa, Cornel Msuwa na Katibu wa CCM Mkoa, Sarah Uisso na viongozi wengine
wa Chama na Serikali.
Katika mapokezi hayo pia yalifanyika makabidhiano ya uongozi wa msafara kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake Tanzania (UWT), Anna Abdallah aliyeongoza Lindi na Mtwara kwenda kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya
CCM, Abdulrahman Kinana.
Baada ya makabidhiano hayo, msafara ulianza kupitia Mtonya, Namiungo, Majimaji, Muhuwesi, Chingulungulu,
hadi Tunduma mjini alikofanya mkutano mkubwa wa hadhara.
Maeneo yote aliyopita, Kikwete na msafara wake alikutana na vigingi vya watu waliojitokeza kwa wingi
kwa ajili ya kumlaki.
Kabla ya kuingia mkoani Ruvuma, Kikwete alipita vijiji mbalimbali vya wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara. Vijiji
hivyo ni Mkomaindo, Mtapika, Matawale, Mkapunda, Sulelu, Namatumbusi, Mikangaula, Nangamano, Nangomba,
Ndwika, Mwambani, Mangaka na Likokona.
MAELFU WAJITOKEZA
Watu walikuwa wakiziba njia kumtaka awasalimie na kuwaeleza mambo ambayo serikali ya awamu ya nne chini
ya CCM itafanya baada ya kuchaguliwa Oktoba 30, mwaka huu.
Dalili kwamba ‘masika ya watu’ ingekuwepo, ilijionyesha wazi katika vijiji vya wilaya ya Masasi
mkoani Mtwara ambako watu walijitokeza kwa wingi kwa minajili ya kumlaki na kumsikiliza.
Katika mapokezi, umati wa watu ulijitokeza kumlaki na baada ya kufanyika makabidhiano baina ya mikoa ya
Mtwara na Ruvuma, alihutubia wananchi hao na hatimaye kuendelea na safari.
Alipofika Majimaji, alikutana na umati wa watu ambao alishangazwa nao. Umati huo wa watu uliziba barabara
na hivyo kumfanya awape maneno kadhaa ambayo yalionekana dhahiri kuwazingua wananchi hao.
Hali hiyo ilijitokeza takriban vijiji vyote ambapo mamia ya wananchi, wake kwa waume, walijitokeza
kumlaki.
MKUTANO TUNDURU
Alipofika Tunduru, mambo yalikuwa mambo, kwani umati wa watu ulifurika uwanjani ambao ulipewa ‘maneno’
yenye msisimko juu ya sababu za CCM kuomba ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.
Kila alipokuwa akihutubia, wananchi walikuwa wakishangilia kuonyesha kuwa maneno aliyokuwa
akizungumza yalikuwa yakiwaingia barabara.
Kikwete mwenyewe alikuwa haishi kuwasifu wananchi waliokuwa katika mkutano huo kutokana na mapokezi.
Pamoja na shamrashamra za kumshangilia, mkutano huo uliiingia dosari baada ya Kikwete kuwaomba wananchi
kuchagua viongozi kwa mithili ya mafiga matatu.
Aliposema wachague Rais kutoka CCM wananchi walishangilia. Aliposema wachague madiwani wa CCM pia
walishangilia lakini aliposema wachague Mbunge wa CCM, umati uliibuka na kutamka: “Hatumtaki, hatumtaki”.
Hali hiyo ilidhihirisha kwamba kazi bado ni ngumu katika kinyang’anyiro cha Ubunge kwenye jimbo hilo
ambapo anayeshikilia wadhifa huo, Juma Akukweti, anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wana CCM
wenyewe na wapinzani.
Akukweti ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anagombea tena atahitaji
kufanya kazi ya ziada kurejea tena katika nafasi hiyo.
Mbunge na mgombea huyo hakuzomewa Tunduru mjini tu, bali hata maeneo mengine alikumbana na vikwazo hivyo.
Baada ya mkutano wa Tunduru, Kikwete aliendelea na safari ya kuomba kura ambapo alipita vijiji mbalimbali
njiani kabla ya kufika Namtumbo.
Akiwa katika safari, alikumbana na umati wa watu katika kijiji cha Nandembo uliozuia msafara wake na
hivyo kulazimika kusimama na hatimaye kuwasalimia na kuomba kuichagua CCM.
Mbali na Nandembo, alikutana na umati wa watu katika vijiji vya Ligunga, Matemanga na Namwinyu, vyote
hivyo katika wilaya ya Tunduru.
Kwa upande wa Namtumbo, kabla ya kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye uwanja wa Taifa, Namtumbo,
alipita vijiji vya Nchomolo na Masuguru ambako pia alikutana na vigingi vilivyomfanya aendelee kumwaga
sera za kuomba kura.
AWASILI NAMTUMBO
Baada ya kukumbana na vigingi vya watu njiani, Kikwete aliwasili Namtumbo saa 11.33 jioni kwa kupokewa na
wananchi lukuki waliokuwa na shauku ya kumwona kiongozi huyo, mpendwa wa Watanzania katika
kinyang’anyiro cha Urais.
Kutokana na muda kuwa mfupi, alikwenda moja kwa moja uwanjani na kuwahutubia wananchi waliokuwa wamefurika
uwanjani hapo.
Katika mkutano huo, mbali na kuwaomba wananchi kuendelea kuichagua CCM ili kuendelea kuongoza nchi,
alimnadi Vita Rashidi Kawawa ambaye ni mgombea ubunge jimbo la Namtumbo kupitia CCM. Vita ni mtoto wa
mwanasiasa mkongwe nchini na makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Rashidi Kawawa.
Baada ya kumnadi, uwanja ulilipuka kwa vifijo hali iliyoashiria kwamba ni kipenzi cha wananchi wa jimbo
la Namtumbo.
Kikwete alimaliza kuhutubia mkutano na kwenda Songea mjini kwa mapumziko kabla ya kuanza kampeni zake kwa
siku iliyofuata.
Hata hivyo, akiwa njiani alikutana na umati wa watu uliokuwa umejipanga barabarani kumlaki na wengine
kumwona. Hakuwaangusha wapiga kura hao kwani alikuwa akisimama na kuwaomba radhi kuwa kumekuchwa, hivyo
wamruhusu aende akapumzike.
SIKU YA PILI RUVUMA
Agosti 27, ilikuwa siku ya pili ya kampeni kwa Kikwete mkoani Ruvuma. Alianza safari ya Mbinga saa 2.30
asubuhi. Kama ilivyo ada, alizidi kuwavuta wananchi wengi waliojitokeza barabarani kwa nia ya kumwona.
Kituo cha kwanza kukutana na wapigakura kilikuwa Likuyufusi wilaya ya Songea Vijijini. Katika kituo
hicho wananchi walikuwa wamejipanga barabarani kumsubiri.
Alipofika alifungua gari upande wa juu na kuwasalimia na hatimaye kuwapa ‘maneno matamu’ ya kuwataka
wananchi waichague CCM katika nafasi za Rais, Wabunge na Madiwani.
Baada ya kuondoka Likuyufusi, aliendelea na safari hadi Kigonsera ambapo alikutana na wanafunzi
waliojipanga barabarani. Wanafunzi walisema walikuwa wameamka alfajiri na mapema kwa nia ya kutakakumwona.
Aliposimama aliwaeleza wanafunzi pamoja na wananchi waliokuwa mahali hapo kuwa CCM inaomba kura ili
kuendeleza mema yote iliyoyafanya kwa maslahi ya Watanzania.
MAKASISI NAO
Kikwete katika safari yake alisimama katika kanisa Kuu la Mtakatifu Kiliani, jimbo Katoliki la Mbinga na
kuwasabahi viongozi wa dini.
Alipokewa na Katibu wa Askofu, Kevin Haule kwa niaba ya Askofu Emmanuel Mapunda. Pia alipata fursa ya
kuzungumza na ujumbe wa kanisa Katoliki Jimbo la Wurzburg, Ujerumani- Jimbo ndugu na Mbinga katika
mambo ya kitume.
Katika hafla hiyo aliusifu ujumbe kutoka Ujerumani kwa kuonyesha nia ya kuwasaidia wakulima wa kahawa
wilayani Mbinga, jambo ambalo alisema wanaunga mkono hatua ya serikali ya awamu ya tatu na ijayo katika
kuwawezesha wananchi kiuchumi na ukuzaji wa uchumi, kilimo kikiwa ajenda kuu.
KIVUMBI MBINGA
Akiwa ameambatana na mkuu wa msafara, Kinana na wajumbe wa kampeni ambao ni waasisi wa TANU, Peter
Siyovelwa na Mustafa Songambele, Kikwete alipokewa kwa staili ya aina yake mjini Mbinga.
Alipokewa na vikundi vya kwaya, ngoma za asili za Lindeku, Chioda, Mganda wa Kimanda, Mganda wa
Kimatengo na Lizombe. Burudani hizo zilihanikiza mapokezi hayo na kuonekana ya aina ya kipekee tofauti
na maeneo mengine.
Mara baada ya kupanda jukwaani, alivalishwa mgolole ikiwa heshima ya kutawazwa kuwa Chifu wa Wamatengo na
hatimaye kuketishwa kwenye kigoda. Pia alipewa silaha ya jadi maarufu kwa jina la kinjenje ikiwa ishara ya
kiongozi shupavu.
Mke wa mgombea, Mama Salma Kikwete naye hakusahauliwa kwani kina mama wa Mbinga walimzawadia chombo maalum
cha kuhifadhia vyombo, kwa kimatengo maarufu kama ‘jamanda’. Jamanda ni kikapu maalum chenye mfuniko
kilichosukwa kwa utaalam wa hali ya juu na kutiwa rangi mbalimbali.
SONGEA YATAPIKA
Baada ya kumaliza mkutano wa Mbinga, alirejea Songea mjini ammbako alihutubia mkutano mkubwa wa kampeni
kwenye Uwanja wa Majimaji.
Katika mkutano huo, uwanja ulijaa na kutapika jambo ambalo wananchi waliokuwepo walieleza kuwa haujapata
kutokea mkutano mkubwa namna hiyo.
Kujaa huko pomoni kwa uwanja, kulimfanya Kikwete kufurahi kupita kiasi na hata alipofika jukwaani akawa
anacheza kwa madoido, hivyo kuwafanya watu kuchenguka zaidi na minjonjo yake ya uchezaji wa nyimbo
zilizokuwa zikitumbuiza.
Katika mkutano huo alimnadi mgombea ubunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Siku iliyuofuata, alianza safari saa 1.45 asubuhi kwenda Madaba, jimbo la Peramiho, ambako alifanya
mkutano wa mwisho wa kampeni katika mkoa wa Ruvuma.
Katika mkutano wa Madaba, Kikwete alimnadi mgombea Ubunge Jenista Mhagama na kumwagia sifa mbunge
anayemaliza muda wake, Profesa Simon Mbilinyi.
“Profesa Mbilinyi namfahamu tangu nilipokuwa nasoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alikuwa mwalimu wangu wa
uchumi kwa miaka yote.
“Pia ameonyesha kuwa mkomavu wa kisiasa kwa kukubali matokeo jambo ambalo ni nadra kwa wanasiasa wengine
kufanya hivyo. Na kubwa zaidi ameahidi kuisaidia CCM kuibuka na ushindi wa kimbunga,” alisema.
Alipomaliza mkutano huo, msafara wake uliondoka kupitia Igawisenga hadi Kifanya, Njombe mkoani Iringa
yalikofanyika makabidhiano baina ya viongozi wa mkoa wa Iringa na Ruvuma.
MAMBO MUHIMU
Katika mikutano yote, Kikwete alieleza azma ya serikali katika ukuzaji uchumi, kilimo ikiwa ajenda
namba moja katika kufikia malengo.
Alisema katika kukuza uchumi, serikali ya awamu ya nne chini ya CCM itahakikisha kilimo kinafanyiwa mageuzi
makubwa na ya kisayansi kwa kuwawezesha wakulima kuondokana na zana za kale na kutumia zana bora na za
kisasa.
Kikwete alisema serikali ijayo pia itahakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati unaotakiwa
na kwa bei ya chini ili kuwawezesha wakulima kuzipata kwa wingi na kwa urahisi.
Pia suala la masoko ya mazao ya wakulima lilizungumzwa kwa undani. Alisema serikali ijayo itaweka mazingira
mazuri ya masoko ya mazao ili kuepusha hali ya sasa ya kutokutabirika kwa bei kumfanya mkulima kupata
hasara kila uchao.
Kuhusu ajira kwa vijana, Kikwete alifafanua kwamba zitapatikana kwa njia mbili; uwekezaji wa ndani na
nje, na kujiajiri kutakakotokana na vijana wenyewe kuanzisha miradi baada ya kupata mikopo.
Pia masuala ya barabara za Songea hadi Masasi na Songea hadi Mbinga, umeme, huduma za maji, elimu ya
sekondari na elimu ya juu zilipewa mkazo wa aina yake kwenye mikutano yake mkoani Ruvuma.
Vile vile Kikwete aliwataka wananchi kuepukana na watu wanaotaka uongozi kwa kutumia udini na ukabila kwa
madai kuwa watu hao ni hatari na wanataka kuipeleka nchi ‘kuzimu’.
Kwa jumla, mikutano yote ya mkoa wa Ruvuma ilikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na umati wa watu uliokuwa
ukijitokeza.
Hali hiyo inaashiria kwamba upinzani mkoani Ruvuma hauna nafasi katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani.
Mbali na vitongoji vichache vya Songea Mjini na wilaya ya Tunduru, maeneo mengi ya Ruvuma yalionekana
kushamiri bendera na mabango ya CCM na wagombea wake.
___________________________________________________________
Ho