Maoni ya Mhariri wa Uhuru
Wana-CCM wawabaini na kuwapuuza wenye njama za kutaka kupandikiza mpasuko
bandia miongoni mwa wanachama
UPO mwelekeo wa kuweko vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani wanaotaka ionekane kwamba kuna mpasuko katika Chama cha Mapinduzi, hasa katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi wa wabunge.
Kuwepo vya vitendo vya aina hiyo kulijionyesha mwishoni mwa wiki iliyopita katika matukio mawili, moja mjini Mtwara, na lingine mjini Morogoro.
Katika tukio na mjini Mtwara, mbunge wa zamani wa jimbo la Newala, Hasnein Murji, alisema wapo wafuasi wa kambi ya upinzani wanaotumia jina lake kuhujumu kampeni za CCM, jimbo la Mtwara mjini, wakidai kuwa anawaunga mkono.
Murji alisema wapinzani wenye kueneza madai hayo wanajenga hoja zao kwa kutumia kuenguliwa kwake katika uteuzi wa kugombea ubunge wa jimbo hilo mwezi uliopita, baada ya kuwa ameongoza kura za maoni.
Lakini Murji amesisitiza kuwa, mbali na kwamba alishavunja kambi yake ya kuwania ubunge, atabakia kuwa mwana-CCM mwaminifu, na atatoa ushirikiano mkubwa kwa kampeni za Chama Cha Mapinduzi popote atakapohitajika kuhakikisha ushindi unakuwa wa kishindo.
Kwa upande mwingine, habari kuhusu tukio la mjini Morogoro ni za aina yake. Imeelezwa kwamba wapo wanachama wa kambi ya upinzani ambao wamenunua sare za kampeni za CCM ambazo wamepanga kuzivaa wakijifanya ni wana-CCM na kuhudhuria mkutano wa hadhara wa kampeni utakaohutubiwa leo na mgombea wa urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete.
Lengo lao, kwa mujibu wa taarifa hizo, ni kupiga kelele mkutanoni kuashiria kwamba uteuzi wa Dk. Omary Mzeru kuwania ubunge, jimbo la Morogoro Mjini, hauungwi mkono na wana-CCM, atakapokuwa anadiwa na Kikwete.
Kwa hujuma hizo zilizokusudiwa kufanywa kwa mgombea wa jimbo la Morogoro Mjini, CCM imeeleza kwamba imeshazibaini na kuahidi kuchukua hatua kukabiliana na wenye malengo hayo.
Ni muhimu ikaeleweka kwamba vitendo kama hivyo vyenye kufanywa kwa kupandikiza baadhi ya wafuasi wa vyama katika mikutano ya kampeni za vyama vingine ni ukiukaji wa maadili yanayoongoza kampeni za kistaarabu za uchaguzi. Na kwa jumla tafsiri pekee ya vitendo hivyo ni uchochezi wenye kulenga katika kuanzisha fujo.
Kwa CCM, kinachohamika ni kwamba kwa jumla kambi zilizokuwepo wakati wa mchakato wa kuwania uteuzi wa Chama kwa ngazi mbalimbali zimeshavunjwa na ari ya wana-CCM sasa ni kushikamana ili kuhakikisha wanakiletea chama chao ushindi.
Kuweko kwa kinachoonekana ni vikundi cha kupinga baadhi ya wagombea, kama ilivyokwishabainika, ni mbinu tu za kambi ya upinzani kutaka kujenga mpasuko bandia ndani ya CCM. Muhimu kwa wana-CCM ni kuzikataa na kuzipuuza mbinu hizo na kukamia kuendelea kufanya kampeni za kistaarabu, na hivyo kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu.