Kwa kuwa pamoja na wanaochochea vurugu Zanzibar, Marekani inazidi kulewa ubabe

Na Lucas Kisasa

ALHAMISI ya wiki iliyopita, ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa taarifa

 

nzito na kali kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, taarifa ambayo kimsingi imeweka wazi

 

kuwa serikali ya Marekani haiyatambui matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Oktoba

 

30, mwaka huu ambapo CCM imeibuka mshindi kwa Rais Amani Abeid Karume kutetea tena

 

nafasi yake.

Taarifa hiyo ya ubalozi wa Marekani kwa vyombo vya habari imeainisha mambo kadhaa

 

inayodai kuwa yalikiukwa katika mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar na kwamba

 

“inaiomba” serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kina na ulio wazi kuhusu

 

tuhuma za ukiukwaji huo.

Marekani inadai katika taarifa yake kuwa kulikuwepo na “vitendo kadhaa vya watu

 

kupiga kura zaidi ya mara moja, pamoja na hali iliyoashiria kwamba watu wa nje

 

waliruhusiwa kupiga kura kinyume na sheria. Vyombo vya usalama vilionekana

 

vikipiga kura, ingawa vidole vyao vilikuwa na alama ya wino usiofutika, hii

 

ikionyesha kuwa walikuwa tayari wamekwishapiga kura”.

Taarifa hiyo inaendelea kudai kuwa “daftari la kudumu la wapigakura halikutolewa

 

mpaka siku ya kupiga” na kwamba “hii ina maana kwamba Wazanzibari wengi hawakupata

 

fursa ya kuhakikisha kama majina yao yalikuwa kwenye orodha hiyo kabla ya siku ya

 

kupiga kura”.

Kutokana na madai hayo ya kinachoitwa ni ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi,

 

Marekani inaainisha katika taarifa hiyo kuwa ndiyo maana “Marekani bado inatiwa

 

wasiwasi na ukiukwaji huu na mwingine uliojitokeza, na inasita kutoa uamuzi kuhusu

 

uchaguzi huu kama ulikuwa huru na wa haki mpaka hapo athari zake juu ya matokeo

 

zimefafanuliwa. Kwa sababu hiyo Marekani haikuhudhuria sherehe ya kuapishwa Rais

 

iliyofanyika Zanzibar siku ya Jumatano”.

Kimsingi madai hayo ya Marekani, kupitia ubalozi wake wa hapa nchini, yanaoana na

 

madai ya chama cha upinzani cha CUF kilichoshindwa uchaguzi huo, na ambacho mara

 

tu baada ya upigaji huo wa kura kumalizika, na hata kabla ya Tume ya Uchaguzi ya

 

Zanzibar haijatoa matokeo, tayari kilijitangazia ushindi.

Kwamba Marekani, taifa kubwa pekee lililobaki duniani lenye nguvu kubwa za kijeshi

 

na kiuchumi, limetoa msimamo huo bila shaka hiyo imekuwa ni faraja kubwa kwa chama

 

cha CUF katika mikakati yake “ya kuifanya Tanzania nzima isikalike” kwa “kuleta

 

janga kubwa la kitaifa”.

Kwa ujumla wake ilichofanya Marekani kwa kutoa msimamo wa aina hiyo ni kuchochea

 

machafuko nchini, siyo kingine. Ilichofanya Marekani ni uchochezi.

Msimamo huo wa Marekani ndio ambao ulikuwa unaliliwa na CUF ili iwe ndiyo ngao ya

 

kufanya uasi nchini. Na wameanza uasi huo kwa kutoa “ultimatum” kwa Rais wa

 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba wanataka katika muda wa siku 45 zijazo

 

matokeo ya uchaguzi Zanzibar yafutwe na ikibidi, eti uchaguzi huo urudiwe.

Kwa wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa msimamo huo wa Marekani kuhusu

 

Zanzibar haushangazi kwani imekuwa ni hulka kwa taifa hili kubwa duniani kuingilia

 

mambo ya ndani ya nchi nyingine kinyume na taratibu na sheria za kimataifa.

Ubabe (wa Marekani) hivi sasa ndio unaotawala dunia. Marekani imelewa ubabe ambapo

 

hivi sasa taifa hili limekuwa sawa na “mwendawazimu aliyepewa rungu”.

Marekani kwa namna yoyote ile haina haki yoyote kuingilia mambo ya Tanzania. Wala

 

hakuna mtu aliyeialika Marekani itoe tamko kuhusu uchaguzi wa Zanzibar.

Yako makundi kadhaa ya kimataifa yaliyoshiriki katika uangalizi wa uchaguzi wa

 

Zanzibar yaliyotamka wazi kuwa ukiacha kasoro ndogo ndogo zilizokuwepo kwa ujumla

 

wake uchaguzi huo ulifanyika kwa uhuru na haki.

Miongoni mwa makundi yaliyotamka kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa huru na wa haki

 

ni Umoja wa Afrika (AU); Jumuia ya Madola; Jumuia ya Maendeleo ya nchi za Kusini

 

mwa Afrika (SADC) na kundi la waangalizi lililowakilisha makanisa.

Lakini kwa Marekani taarifa za makundi haya mengine zilikuwa ni za uongo isipokuwa

 

ile ya National Democratic Institute (NDI) na ambayo ripoti yake ndiyo iliyopewa

 

umuhimu na taifa hili. Kwamba Marekani imezingatia ripoti ya taasisi moja tu ni

 

jambo linaloshangaza mno na kimsingi ni kielelezo cha wazi kuwa taifa hilo lina

 

ajenda ya siri dhidi ya Tanzania.

Hoja zote zilizoainishwa na Marekani kuhusu uchaguzi wa Zanzibar zilishajibiwa na

 

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi huo ilipoanza

 

kwanza kwa kujibu madai ya CUF.

Kwa ufupi ni kwamba madai ya Marekani na CUF kuhusu kinachoitwa ukiukwaji wa

 

taratibu za uchaguzi hayana msingi, bali yamelenga katika kupotosha ukweli wa

 

kilichotokea Zanzibar wakati wa uchaguzi huo.

Marekani ina tabia moja mbaya nayo ni kwamba hutaka mataifa yote duniani yafuate

 

inachokitaka. Hujiita kuwa ni taifa la kidemokrasia, lakini ukweli ni kwamba

 

uongozi wa Marekani uko mbali na demokrasia kinyume kabisa na inavyohubiri.

 

Demokrasia ya Marekani ni ya ubabe na jeuri.

Bado tuna kumbukumbu ya kilichotokea huko Marekani katika uchaguzi wake mkuu wa

 

mwaka 2000 pale ukiukaji mkubwa wa taratibu ulipojitokeza ambapo watu wengi kwa

 

maelfu walinyimwa haki ya kupiga kura, huku pia kukiwepo na wapigakura

 

waliobainika kuwa walikuwa ni marehemu.

Kimsingi kulikuwa na wizi mkubwa wa kura katika uchaguzi huo wa mwaka 2000 mpaka

 

mahakama kuu ya taifa hilo duniani ikaamua kuingilia kati kwa kumtangaza George

 

Bush kuwa rais na kumtupa kando mpinzani wake kutoka chama cha Democrat, Al Gore.

Kama wizi huo wa kura wa mwaka 2000 haukutosha, tatizo hilo lilijitokeza tena

 

katika uchaguzi wa mwaka jana ambapo taratibu nyingi za uchaguzi zilikiukwa na

 

kuleta aibu kubwa kwa taifa hilo kubwa duniani.

Pamoja na ukiukwaji huo mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa Marekani kwa mwaka 2000

 

na 2004, hakuna kiongozi wa nchi nyingine duniani aliyeingilia kati suala hilo kwa

 

kutangaza kutoyatambua matokeo hayo. Viongozi wengi wa nchi nyingine hawakufanya

 

hivyo kwa kuwa walielewa kuwa kufanya hivyo ingekuwa ni kuingilia mambo ya nchi

 

nyingine.

Lakini Marekani haina aibu. Ni taifa linaloongozwa kwa misingi ya ukandamizaji, si

 

tu kwa mataifa mengine bali hata kwa watu wake. Haki za Wamarekani weusi zimeanza

 

kuwepo nchini mwao kuanzia miaka ya 1960 tu.

Kabla ya hapo Marekani ilikuwa sawa na Afrika Kusini katika suala la ubaguzi wa

 

rangi. Wamarekani weusi walikuwa ni raia daraja la mwisho katika nchi yao wenyewe.

 

Walikuwa wana shule zao; mabasi yao; baa zao; na kadhalika, huku wakiwa

 

hawaruhusiwi kugombea madaraka bali waendelee katika “taaluma” yao katika muziki

 

na michezo kama mbio, ngumi na mpira wa kikapu.

Kati ya mataifa yote, Marekani ndiyo inayonuka damu kwa kuua mamilioni ya watu

 

duniani wasio na hatia yoyote. Iliua maelfu ya watu huko Vietnam katika miaka ya

 

1960. Hivi sasa inaendelea kuua watu kwa maelfu Irak, huku wachambuzi wa masuala

 

ya kisiasa duniani wakiainisha kuwa mpaka sasa zaidi ya watu 150,000 wamekufa

 

katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.

Marekani ni taifa linalokataza nchi nyingine zisiwe na silaha za maangamizi

 

zikiwemo za nyuklia, lakini yenyewe imejilimbikizia silaha lukuki za maangamizi

 

ambapo zinaweza kuiangamiza dunia mara 20. Na si suala la kujilimbikizia silaha

 

tu, bali Marekani ndiyo nchi ya kwanza duniani kutumia silaha za nyuklia. Mabomu

 

ya Atomiki yaliyotupwa katika miji ya Hiroshima na Nagasaki huko Japan wakati wa

 

vita vya pili vya dunia, Agosti 1945, na kuua zaidi ya watu 200,000 ilikuwa kazi

 

ya Marekani.

Katika vita vya Vietnam, Marekani ilitumia silaha za maangamizi, yakiwemo mabomu

 

ya sumu ya ‘napalm’, kuwaua wananchi wa Vietnam na wengine bado wanaendelea kufa

 

pole pole kwa magonjwa kutokana na sumu hizo. Picha ya mtoto wa kike wa Vietnam

 

akiwa uchi wa mnyama na akikimbia, huku akiwa ameunguzwa vibaya na mabomu, bado

 

iko katika kumbukumbu za watu wengi duniani.

Marekani imekuwa ikisema kuwa inaendesha mapambano dhidi ya ugaidi duniani. Sawa,

 

lakini ugaidi uliopo duniani hivi sasa unazalishwa na nani? Unazalishwa na

 

Marekani yenyewe kwa kuendesha vitendo vya kibabe na uonevu kwa baadhi ya nchi

duniani.

Marekani ndiyo iliyoongoza majeshi ya kimataifa katika kuishambulia nchi iliyokuwa

ikiitwa Yugoslavia na hatimaye kumkamata Rais wa nchi hiyo, Slobodan Milosevic,

ambaye sasa anahukumiwa na kinachoitwa mahakama ya kimataifa.

Marekani hiyo hiyo ndiyo iliyoivamia Irak kwa kisingizio kuwa nchi hiyo ilikuwa na

silaha za maangamizi, jambo ambalo limekuja thibitika kuwa ni uongo. Aliyekuwa

Rais wa Irak, Saddam Hussein, alikamatwa na majeshi ya Marekani na sasa

anashitakiwa na kinachoitwa mahakama ambayo imeundwa na Marekani.

Jenerali Noriega wa Panama alikamatwa akiwa katika ikulu yake na hivi sasa yuko

jela Marekani. Ni Marekani ndiyo iliyoishambulia nchi ndogo ya Grenada na kuuondoa

uongozi wa nchi hiyo.

Inawezekana ni kweli Milosevic, Saddam Hussein na Jenerali Noriega walikuwa na

makosa yao, lakini pamoja na hayo Marekani haikuwa na haki kuzishambulia nchi hizo

na kuwakamata viongozi wake.

Hivi sasa Marekani na Uingereza zimemvalia njuga Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

kwa kumuita ni dikteta na king’ang’anizi wa madaraka. Kosa la Mugabe ni nini? Ni

uamuzi wake wa kuongoza mageuzi makubwa ya ardhi ya nchi hiyo kwa kuwanyang’anya

ardhi walowezi wa kizungu na ardhi hiyo kugawiwa kwa wananchi wazalendo waliokuwa

hawana ardhi katika nchi yao wenyewe.

Wakati Marekani inajidai kupinga ugaidi duniani, taifa hilo kubwa ndilo

linaloongoza kwa kuendesha ugaidi wa dola kwa kuzishambulia nchi nyingine na

kukamata viongozi wake.

Mwanamapinduzi na kiongozi wa Chile, Salvador Allende, aliuawa katika miaka ya

1970 kutokana na njama za Marekani. Tunafahamu kilichotokea huko Congo pale

mwanamapinduzi Patrice Lumumba alipouawa katika miaka ya 1960 kutokana na

kinachosadikiwa kuwa ni njama za Marekani na nchi nyingine za magharibi.

Watu kwa maelfu waliuawa nchini Angola kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe

ambavyo vilikuwa vinachochewa na Marekani kwa kumuunga mkono gaidi Jonas Savimbi.

Kwa hiyo ni dhahiri Marekani inanuka harufu ya damu, inanuka damu za maelfu ya

raia wasio na hatia wanaouawa katika nchi mbalimbali kutokana na njama za taifa

hilo kubwa.

Viongozi wa Marekani ndio kwa hakika wanaostahili kushitakiwa kwenye mahakama za

kimataifa kwa dhambi za serikali yao dhidi ya mataifa mengine duniani. Katika

kumshitaki Milosevic na Saddam kwenye mahakama zinazoitwa ni za kimataifa pengine

Rais George Bush naye alistahili kushitakiwa katika mahakama hizo kwa unyama wa

nchi yake dhidi ya nchi nyingine duniani.

Ubabe huu wa Marekani ndio unaowafanya Wamarekani wengi kuchukiwa katika nchi

mbalimbali duniani. Imefika wakati katika baadhi ya nchi duniani Wamarekani

huogopa na kushindwa kujitambulisha utaifa wao. Wanawindwa mithili ya panya

walioingia ndani ya nyumba.

Marekani haipendi nchi na viongozi wenye msimamo. Marekani ni nchi ambayo hupenda

kuleta uchochezi na yenyewe kunufaika kiuchumi kutokana na machafuko katika nchi

mbalimbali yaliyojitokeza kwa uchochezi wake.

Kwa msimamo wa kuiunga mkono CUF kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar ni dhahiri

Marekani inataka kuiona Tanzania ikiathirika na machafuko. Ni jambo linaloudhi

kuona kuwa Marekani inayojifanya kuwa ndiye kinara wa demokrasia duniani na

inayoendesha mapambano dhidi ya ugaidi ndiyo inakuwa na msimamo wa kukiunga mkono

chama cha siasa chenye mwelekeo wa ugaidi.

CUF wameshatangaza kuwa watahakikisha kuwa Tanzania inakumbwa na janga la kitaifa.

Wanachomaanisha hapa bila shaka ni kuhakikisha kuwa yanakuwepo machafuko nchini

yanayoandamana na umwagaji wa damu, ambayo kwa msimamo wa sasa, yatakuwa

yamebarikiwa na Marekani. Na hii ikitokea damu ya Watanzania watakaouawa kutokana

na vurugu zitakazotokea iwe pia mikononi mwa Wamarekani wa kizazi hiki na vizazi

vyao vyote vijavyo.

Simu: 0744-309858

E. mail: kisasa2000@yahoo.com