Na Abihudi Saideya, Musoma,14/10/2005 =Dk. SHEIN
 
Serikali ya awamu ya nne ya Chama Cha Mapinduzi
ikiingia madarakani itaweka utaratibu utakaowezesha
wananchi wanaoishi karibu na migodi kufaidika na
madini yanayopatikana sehemu hizo.
 
Hayo yalisemwa jana (13/10/2005) na Mgombea Mwenza wa
Rais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni
za uchaguzi katika Kata ya Buhemba, Wilaya ya Musoma
Vijijini Mkoa wa Mara.
 
Dk. Shein alisema lengo la mpango huo ambao umeingizwa
kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 ni
kuchochea maendeleo katika sehemu hizo na kurekebisha
athari za kijamii na kimazingira zinazotokana na
uchimbaji madini. 
 
Pia alisema serikali itaboresha utaratibu wa kulipa
fidia na ujenzi wa makazi mapya kwa wananchi
wanaohamishwa au mashamba yao kuchukuliwa kupisha
uanzishaji wa shughuli za migodi.
 
Dk. Shein aliongeza kuwa serikali itapitia upya sera
ya madini ili kuangalia namna ya kuboresha mahusiano
mazuri baina ya wawekezaji na wananchi wanaoishi
jirani na maeneo ya migodi kwa nia ya kuepusha
migogoro. 
 
Kata ya Buhemba ni moja ya maeneo yenye migodi ya
dhahabu ambayo ilianzishwa baada ya serikali kupanua
uwekezaji katika sekta ya madini.
 
Ili kuendeleza sekta ya madini Dk.Shein alisema
Serikali itaongeza vivutio kwa wawekezaji hususan kwa
miradi ya kuongeza thamani ya madini ikiwemo ukataji
wa madini na utengenezaji wa vito.
 
Serikali itahakikisha inaongeza kiwango cha madini
kinachosafirishwa kikiwa kimeongezwa thamani kutoka
asilimia 0.3 hivi sasa, hadi 3.0 mwaka 2010, alisema.
 
Halikadhalika alisema serikali itatoa elimu ya
uchimbaji madini na mikopo kwa wachimbaji wadogo
pamoja na kujenga mahusiano mazuri kati ya wachimbaji
hao na wakubwa.
 
Alisema serikali ya CCM ya awamu ya nne itaendeleza
uchumi na kukuza huduma za jamii kwa ari mpya, nguvu
mpya na kasi mpya chini ya uongozi imara wa Bw. Jakaya
Kikwete.
 
Dk. Shein aliwaomba wananchi wamchague Kikwete
kuchukua nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano na
Wagombea Ubunge na Udiwani kupitia Chama Chama Cha
Mapinduzi.
 
Aliwataka wananchi wasichague wagombea wa upinzani kwa
kuwa vyama hivyo vinaendeshwa kwa jazba, hali ambayo
alisema inaweza kuchochea vurugu na machafuko nchini.
 
Dk.Shein alihutubia mkutano mwingine wa kampeni Kata
ya Murangi, Musoma Vijijini  ambako aliupokea msafara
wa Vijana wa CCM (UVCCM)wapanda pikipiki Mkoani Mara
waliozunguka Mkoa mzima kuwaombea kura wagombea wa
Chama Cha Mapinduzi.
 
Katika ziara yake ya kampeni Mkoani Mara iliyomalizika
leo Dk. Shein alifuatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM Taifa wa Mkoa wa Mara Bw. Christopher
Gachuma,Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Joseph Warioba na
viongozi mbambali wa Chama Mkoani.
(mwisho)
*ABIHUDI SAIDEYA ni Mwandishi wa Habari-
Contact:0744-268961 au 0787-052221.