Mzalendo 04.09.2005
Kikwete achanga sh. milioni 12 kusomesha wana-habari wanawake
Awapiku wanasiasa wenzake
Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete ameonyesha dhamira ya kuwasaidia wana-habari wanawake kwa kuwachangia sh. milioni 12, tofauti na wagombea wenzake, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) aliyetoa sh.400,000 na Freeman Mbowe (Chadema) sh.500,000.
Wagombea hao walitoa michango yao kwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA). Michango hiyo ilitangazwa kwenye halfa ya chakula cha jioni ya uzinduzi wa mfuko wa kusomesha wana-habari wanawake iliyofanyika juzi kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye. Viongozi wengine waliokuwepo ni aliyekuwa Spika wa Bunge, Pius Msekwa na mke wake Anna Abdallah, ambaye ni Waziri wa Afya.
Taarifa ya kwanza ya wachangiaji iliyosomwa kwa waalikwa ilionyesha Profesa Lipumba alichangia sh.100,000, Freeman Mbowe sh.500,000 na Kikwete sh. milioni mbili.
Mfuko ulipozinduliwa na waalikwa kuanza kutoa michango yao, Kikwete alimtuma mwakilishi wake aliyejitambulisha kuwa ni Mahmoud Kingwande na kutamka anatoa sh. milioni tano tofauti na sh. milioni mbili za awali na baadaye tena yeye (Kikwete) na marafiki wa Tamwa walitoa sh. milioni tano.
Profesa Lipumba baadaye ilielezwa alikuwa amepiga simu na ameongeza mchango wake kwa kutoa sh.300,000 zingine.
Waziri Mkuu Sumaye alichangia sh.milioni moja, Msekwa na mkewe sh. milioni moja na Mweka Hazina wa CCM, Salome Joseph Mbatia alichangia sh 200,000.
Ofisi ya Bunge ilichangia sh.500,000, mfanyabiashara na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Rostam Aziz sh.500,000 na Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, Edward Lowassa sh.500,000.
Wakati wa kuzindua mfuko huo, Sumaye alisema kuwa matatizo yanayolikumba bara la Afrika yanatokana na kuwaweka wanawake pembeni.
Alisema wanahabari wengi wanawake wana sifa za kwenda chuo kikuu, lakini hakuna wa kuwawezesha na kuongeza kwamba hafla hiyo ya kuchangia iwe chachu ya kuwawezesha wanahabari wanawake kupata elimu ya juu.
TAMWA mwaka huu imekusudia kukusanya sh. milioni 150 kuwawezesha wanahabari wanawake kupata elimu ya juu.
Kikwete: Nitakuwa rafiki wa wafanyabiashara wasiokwepa kodi
l Asisitiza sheria zifuatwe
Na Epson Luhwago, Mafinga
MGOMBEA wa urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete, amesema serikali yake itakuwa rafiki wa wafanyabiashara waaminifu na watu wasiokwepa kodi.
Alisema hayo jana mjini hapa alipokuwa anahutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Igowole, mjini hapa na kusisitiza uaminifu na kutowavumilia watakaokwepa kulipa kodi.
Kikwete aliwataka wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria za nchi, kwani, alisema, hiyo itakuwa na manufaa kwa wengi na wao wenyewe, serikali na wananchi kuweza kupata ajira zaidi.
Mojawapo ya vivutio katika mkutano huo kwenye uwanja wa Mashujaa, ni jinsi walemavu 20 walivyojiunga na CCM kwa mpigo, huku wakiweka bayana kwamba CCM ndicho chama pekee kinachoweza kuwakomboa.
Mgombea urais aliwaahidi walemavu hao wanaojihusisha na biashara ndogondogo, kuwa serikali ijayo ya CCM itahakiksha inawainua kiuchumi na wasijisike kwamba wanapungukiwa kiungo chochote.
Kupitia mikutano hiyo, Kikwete aliwatambulisha na kuwanadi kwa wananchi wagombea ubunge Joseph Mungai (Mufindi Kusini) na Benito Malangalila (Mufindi-Kaskazini). Katika kipindi kilichopita walikuwa wabunge.
Kwenye mkutano wa Mafinga, katibu wa NCCR Mageuzi jimbo la Mufindi Kusini, Boniface Mliga, alitangaza kujiunga na CCM na kuahidi 'kuwabeba' wafuasi wake wote waliobaki katika chama hicho.
Mliga aliishambulia kambi hiyo akieleza kwamba ni sawa na gari bovu, huku akitafsiri harakati za upinzani kwamba ni sawa na ndoto, kwani hazina mweleo wa kufanikiwa hivi karibuni.
Kwenye mkutano wa kampeni katika viwanja vya Igowole-Mafinga, wanachama 15 wa CUF walijiunga na CCM.
Kikwete mkutanoni hapo alizungumzia dhamira ya serikali ya CCM inayoomba ridhaa ya kuwekwa tena madarakani, kuwa tangu huko nyuma iliongoza vyema, tena kwa sera zinazokubalika.
Alisema serikali yake itaendeleza mapinduzi katika sekta ya ufugaji, na imenuia kuachana na 'uchungaji'.
Obetto Mwenyekiti mpya wa CCM Musoma Mjini
Na Didas Kaswamila, Musoma
MKUTANO Mkuu maalumu wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini umemchagua mfanyabiashara maarufu wa hapa Joseph Obetto kuwa mwenyekiti mpya wa Chama.
Uchaguzi huo uliitishwa ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha mwenyekiti wa zamani.
Uchaguzi huo uliofanyika mjini hapa juzi katika ukumbi wa mikutano wa CCM mkoani Mara ulifunguliwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Christopher Gachuma na kusimamiwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa mko Nimrod Lugoe ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katika Uchaguzi huo ambao ulilazimika kurudiwa baada ya kukosewa kwa idadi ya wajumbe waliohudhuria na kupiga kura mara ya kwanza, Obetto alichaguliwa baada ya kupata kura 279,ambapo wapinzani wake Charles Kayelle alipata kura 41 na Hafidh Waziri 33.
Awali Katibu Mwenezi wa CCM wilaya, God Kumira alikosea kujumlisha mahudhurio ya wajumbe na kudai waliohudhuria walikuwa 329 kati ya 444 wa mkutano huo lakini walipokwenda kuhesabu kura zilikutwa 403.
Baada ya ongezeko hilo la kura zilizopigwa, msimamizi wa mkutano huo aliitisha karatasi za mahudhurio ambazo wajumbe walijiorodhesha kila kata na kubaini kuwa wajumbe waliokuwa wamejiandikisha walikuwa 430 ndipo ilipokubaliwa na wagombea kuwa uchaguzi huo urudiwe bila kura kuhesabiwa.
Akiwashukuru wajumbe baada ya kuchaguliwa, Obetto alisema kazi ya kwanza atakayoifanya ni kuvunja makundi ndani ya Chama ambayo yamekuwepo kabla na baada ya kura za maoni.
"Kutokana na imani ambayo wajumbe mmeionyesha kwangu kwa kunichagua kwa kura nyingi, naahidi kuvunja makundi na kambi ambazo zimekuwepo wakati na baada ya kura za maoni ili tuweze kuunganisha nguvu zetu na kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu," alisema.
Akifungua mkutano huo, Gachuma aliwataka wanachama wa CCM katika wilaya hiyo kuhakikisha kila mmoja anapata wapiga kura watano watakaoipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu ili chama kipate ushindi wa kishindo.
Alisema wanachama ambao hawakuteuliwa kuwania udiwani au ubunge hawana budi kuvunja kambi zao na kuwaunga mkono walioteule na kuonya kuwa iwapo itabainika kuwa kuna ambao watakisaliti chama, hatua za kinidhamu zitachuliwa dhidi yao.
Gachuma aliongeza kuwa Chama kinahitaji kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo ili kiweze kushika uongozi wa dola na kuwa na sauti kubwa bungeni na kwamba kupata kura nyingi katika uchaguzi huo kitaifanya CCM kuwa na wabunge wengi wa Viti Maalum.
Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma mjini Lotrh Ole Meirut akieleza hatua zitakazochukuliwa na ofisi yake juu ya viongozi na wanachama ambao ni ndumilakuwili, alisema wilaya watajadili suala hilo.
Abdallah Mshindo achaguliwa Mwenyekiti CCM Kusini Pemba
Na Khatib Mjaja, Pemba.
MKUTANO Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, umemchagua kwa kura 101, Abdallah Mohammed Mshindo, kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM mkoa.
Hatua hiyo inafuatia kuachwa wazi kwa nafasi hiyo kutokana na kufariki kwa aliyekuwa Mwenyekiti wake Omar Msellem Haji.
Mkutano huo wa uchaguzi uliofanywa kwenye Ukumbi wa Mikutano Chachani, Chake Chake Pemba, ambapo Mshindo aliwashinda Sheha Mohammed Sheha aliyepata kura 36, na Fadhil Abassi aliyepata kura 22.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Dk Maua Daftari alisema uchaguzi huo umefanyika kwa njia ya kidemokrasia.
Dk. Maua ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasilano na Uchukuzi katika Serikali ya Muungano alisema jumla ya wapiga kura 164 walishiriki ambapo kura tatu ziliharibika.
Mapema akiufungua Mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa alisema wana CCM wanayo kila sababu ya kuvionyesha vyama vingine vya siasa nchini juu ya upeo wa demokrasia ndani ya Chama .
Naye Mwenyekiti mpya Mshindo ameahidi kutoa ushirikiano kwa wana CCM wote Tanzania katika kutetea Ilani na sera ya Chama.