Mzalendo Makala 04.09.2005 

Kwa nini Watanzania wanajiandaa kuipa CCM ushindi wa kishindo KAMPENI za uchaguzi mkuu mwaka huu zinaendelea nchini kote, Lakini mpaka sasa Idadi kubwa ya watanzania wamejiandaa kuwachagua wagombea wa Udiwani, Ubunge na Rais wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa nini wanaipenda CCM? 

Makala hii ya Mwandishi wetu LAUDEN MWAMBONA inajaribu kutoa majibu.

MSIMU wa vyama 18 vya siasa kujinadi kusaka ubingwa mbele ya Watanzania karibu milioni 30 ndio huu. Vyama vyote vinaomba ili wananchi wawachague madiwani, wabunge na Rais kupitia vyama husika. Baadhi ya vyama vinavyojaribu kufurukuta ni CUF, CHADEMA, TLP, NCCR-MAGEUZI, UDP, na NRA. Lakini, Chama tawala, CCM , ambacho watu mbalimbali wa ndani na nje wanatoa nafasi ya kupata ushindi mkubwa mwaka huu, kinaingia ulingoni kikiwa na sababu za kuomba tena kuendelea kutawala kutokana na kazi nzuri zilizofanyika kipindi cha miaka 10 tangu 1995 hadi sasa. Mafanikio ya wazi ya serikali ya CCM ndiyo yanayosababisha watu wengi kuwa na uhakika wa kuichagua CCM ili iendelee kuongoza Watanzania na kuboresha maisha yao. Kwa nini watu wanaichangamkia CCM na kuahidi kuichagua kwa kura nyingi mwaka huu? Baadhi ya vyama vya upinzani vimesikika vikitamka kwamba vitapata ushindi katika nafasi za udiwani, ubunge na nafasi kubwa ya Urais ili viongoze Watanzania. Lakini ukiviuliza sababu za kuamini hivyo hususani sababu za kuamini kwamba vitapata ushindi kwa mgombea wa Urais, vinashindwa kabisa kutoa sababu. Mara kadhaa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo vya upinzani, wameonekana wenyewe wakicheka wanapotamka suala la vyama vyao kupata nafasi ya Rais. Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba wagombea wa Urais kupitia vyama vya upinzani hawawezi kupata kwa sababu ya uwezo mdogo wa kuongoza. 'CCM iliwateua wagombea wa Urais, ubunge na madiwani wenye uwezo, uzoefu wa kufanya kazi,'_ alisema Mfanyabiashara mmoja wa Soko la Kariakoo aliyejitambulisha kwa jina la Juma Rashid. Watanzania wengi wanaamini kwamba wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani, watapatikana maeneo ambayo wanaCCM walitofautiana wakati wa kura za maoni kutokana na ubinafsi. Lakini uhakika wa CCM kushinda nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni wa asilimia 100 kwa Watanzania wote. MAFANIKIO YA CCM Kauli mbiu ya 'Kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya , Tanzania yenye neema tele inawezekana,'_ inachochea wananchi wazidi kuiamini na kujiweka tayari kuichagua siku ya Oktoba 30 mwaka huu. CCM imetoa ilani yenye ahadi chache za uhakika katika kuzitekeleza kipindi kijacho cha 2005-2010. Kwa mfano kuongeza ajira kwa watanzania, kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara vijiji sambamba na barabara kuu, kuongeza usimamizi katika kilimo, kujali wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi ni moja ya mambo ambayo Watanzania wote wanayahitaji. Watanzania wanakuwa na uhakika kwa CCM kwa sababu ni chama pekee ambacho kimeilea Tanzania tangu UHURU hadi leo hivyo ni chama chenye uchungu wa kweli kwa nchi na watu wake. Viongozi wake hawana uchu wa madaraka, hawako tayari kuona baadhi ya vyama vya siasa au vikundi vya kihuni vinafanya vurugu za kuumiza wananchi wake. Hivyo Watanzania wana imani kubwa na CCM pamoja na viongozi wao, kutokana na ukweli kwamba wamedhamiria kuondoa matatizo ya wananchi na kuonyesha nia ya wazi ya kuwasaidia wananchi kwa kutekeleza kwa vitendo kuondoa matatizo makubwa. Yapo matendo ambayo Mtanzania mmoja mmoja amesaidiwa na Serikali ya CCM na mengine yamegusa jamii au vikundi wakati mengine yamesaidia kuliboresha Taifa zima. Bila shaka Watanzania wengi wanaofuatilia kazi mbalimbali zilizofanywa na CCM walisoma au kusikia taarifa za serikali kupitia Wizara, Mikoa na baadhi ya wilaya zilizotangazwa na vyombo mbalimbali vya habari. Je, ni mambo gani ambayo yanawafanya Watanzania wajiandae kuipigia CCM kura nyingi? KUFUTA KODI, KARO Mambo ni mengi, lakini moja ya mambo ambayo wapiga kura wanaendelea kuikumbuka CCM ni suala la kufuta KODI YA KICHWA. Kodi hii ilikuwa kero kubwa kwa Watanzania wengi hususani wa vijijini. Kimsingi kodi hii iliwekwa kisheria kwa lengo la kutaka serikali ipate fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuendesha ofisi za serikali kutokana na uhaba wa maeneo ya kupata kodi kubwa. Wafanyakazi walikatwa kodi ya kichwa kila mwezi kupitia mishahara yao, lakini wakulima na wafugaji walikuwa na hali ngumu na kodi hii. Wakulima wengi walionekana wakikimbia nyumba zao na kushinda porini kwa hofu ya kukamatwa kwa tuhuma za kukwepa kodi. Wafugaji walifurahi kwani wakati wote walishinda kuchunga na walirudi na mifugo yao usiku. Hivyo mara baada ya serikali ya CCM kuona makusanyo ya kodi yanaongezeka kutoka bilioni 25 mwaka 1995 hadi bilioni 80 mwaka 1999 iliamua kuondoa kodi ya kichwa. Hatua hiyo ilitangazwa na Waziri wa Fedha Basil Mramba ambaye hivi sasa anawania ubunge jimbo la Rombo. Mramba alisema kufutwa kwa kodi kunafuatia ushauri uliotolewa na CCM kwamba inawakera Watanzania. Watanzania ambao ni walipa kodi walipokea tangazo la kufutwa kwa kodi hiyo kwa furaha na wengine waliandamana kuishukuru serikali. Jambo lingine litakalowafanya wapiga kura wafikirie kuichagua CCM ni suala la kufuta ushuru wa baiskeli na mazao ya wakulima. Ushuru huo ulifutwa baada ya kuona makusanyo yanazidi kuongezeka na pia kugundua kwamba ushuru huo ulikuwa ni kero kwa wakulima na watumiaji wa baiskeli ambao ni watu wa hali ya chini. Hivi sasa zaidi ya baiskeli milioni 18 zinasemekana zipo nchini zikitoa huduma bila kutozwa ushuru wowote sawasawa na mikokoteni yote. Kadri mapato ya serikali yalivyozidi kuongezeka , Serikali ya CCM ilizidi kuleta neema kwa Watanzania kwani iliweza pia kufuta karo ya wanafunzi wa shule za msingi nchini. Awali karo ilikuwa sh. 2,000 tu, lakini fedha hizo zilikuwa mzigo mkubwa kwa Watanzania wengi wenye kipato cha chini jambo ambalo CCM iligundua na kuitaka serikali yake iondoe karo hiyo kwa vile makusanyo ya kodi yalikuwa yakiongezeka vizuri. Kana kwamba haitoshi, serikali ya CCM pia ilipunguza ada ya wanafunzi wa Sekondari za kutwa kutoka sh. 40,000 kwa mwaka hadi sh. 20,000 ambazo zinalipwa hivi sasa. Tukio lingine ni la serikali ya CCM kuweka mazingira mazuri kwa taasisi mbalimbali za fedha ambazo zimeweza kukopesha Watanzania wengi kuliko miaka ya 90 . Hivi sasa Watanzania wanapata mikopo kwenye mifuko maalum wa wanawake, vijana, Pride, mabenki na vikundi vya kuweka na kukopa vimeongezeka zaidi ya mara mbili. SHERIA ZAREKEBISHWA Mazinginra mazuri hayo pia yalipatikana baada ya kurekebisha zaidi ya sheria mbalimbali 270 katika kipindi cha miaka 10 ya mfumo wa vyama vingi ili kupata mafanikio . Mwanasheria mkuu wa serikali Andrew Chenge alifanya kazi ya ziada akishirikiana na mawaziri na maofisa wa serikali kuliomba bunge likubali kurekebisha sheria hizo ili kujenga mazingira mazuri ya kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo. Moja ya sheria zilizorekebishwa ni pamoja na sheria ya vyombo vya habari iliyotoa uhuru wa kuanzishwa vyombo mbalimbali binafsi vya habari. Kwa mfano mwaka 1995 kulikuwa na radio mbili tu, lakini sasa zipo karibu radio 32, televisheni 63 kutoka mbili wakati magazeti yapo 507. Kuongezeka kwa vyombo vya habari kumesababisha kuwepo kwa ajira ya zaidi ya wafanyakazi katika vyombo hivyo karibu 15,000. Sheria zingine ambazo zilirekebishwa na kusababisha unafuu kwa Watanzania ni pamoja na ubinafsishaji ambayo imewezesha baadhi ya kampuni zilizobinafsishwa kutoa ajira ya watu wengi mno. Kumbuka muuza bia kwenye baa amepata ajira hiyo baada ya uzalishaji wa bia za Kampuni ya bia nchini (TBL) kuongezeka . Taarifa za Waziri Ofisi ya Rais (Mipango na ubinafsishaji) Dk. Abdallah Kigoda aliyoitoa mwaka 2002 ilisema kuongezeka kwa uzalishaji wa TBL kumewezesha karibu watu 350,000 nchini kupata ajira ya kuuza bia TBL pekee na wote hao wana nafasi kubwa ya kutoa kura kwa CCM kutokana na uhakika huo wa ajira CCM kupitia serikali yake ilijali pia madeni ya Watanzania kwa serikali yao. ULIPAJI MADENI Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita , serikali ililipa mamilioni kwa walimu, watumishi wa afya na wadeni wengine waliokuwa wakizidai idara za serikali kwa masuala ya umeme, maji, na huduma zingine muhimu. Madeni hayo yalikuwa ya miaka ya 80 na 90. Wapo walioidai serikali kwa kipindi kirefu baada ya kutoa huduma kwenye vyombo vya dola kama kutoa vyakula kwa majeshi, shule na vyuo , lakini serikali ya CCM iliendelea kulipa madeni yote kadri fedha zilivyopatikana. Taarifa za mwaka 2002 zilionyesha kwamba zaidi ya bilioni 88 zilitumika kulipa madeni ya ndani sambamba na ulipaji wa madeni ya nje ulioendelea kama kawaida ili kujenga heshima ya nchi. Lakini jambo lingine muhimu kwa Watanzania ni kwamba CCM, kupitia serikali yake, wakati wote imehakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu mkubwa ili waweze kutekeleza kazi za maendeleo. Kwa nini wafanya biashara wanaipenda CCM? Wafanyabiashara wanatarajiwa kuipigia kura CCM kwa sababu nyingi, lakini moja ni ya kuondoa kero zilizokuwepo wakati wa kuanzisha biashara. Awali wafanyabiashara walikuwa wanazunguka ofisi nyingi kusaka leseni au kulipia kodi, lakini siku hizi imeondoa kero hizo. Jambo lingine zuri ni la serikali kutoa kodi kwa wafanyabiashara wadogo wanaoanzisha maduka ya mtaji mdogo. Hivi sasa biashara zote zenye mtaji wa chini ya sh.milioni tano hazilipiwi kodi yoyote. Vijana, wanawake na watu wote makini wanafungua vibanda vya kuuza soda, bia au vyombo vya nyumbani bila bughudha. Bila hata soni, kila Mtanzania sasa anatambua kwamba Tanzania inakwenda sambamba na dunia kwa masuala mbalimbali yakiwemo ya mawasiliano na nchi nyingine duniani. Simu za mikononi zimechukua nafasi kubwa kwani karibu watu milioni tatu wanatumia simu za aina hiyo. Mpango huo ulitekelezwa vizuri kupitia Wizara ya Mawasiliano na uchukuzi inayoongozwa na Profesa Mark Mwandosya ambaye tayari ameupata ubunge bila kupingwa jimbo la Rungwe Mashariki. CCM imeondoa kero za Serikali za mitaa kwa kuanzisha mradi wa kuboresha serikali za mitaa ulioanza baada ya uchaguzi wa mwaka 1995. Baadhi ya wilaya 38 za kwanza kutekeleza mpango huo zilionyesha mafanikio makubwa katika kuboresha utendaji kazi. Ofisi za serikali zilikarabatiwa, watumishi walipangwa vizuri na vitendea kazi viliongezeka. Kazi hiyo ilisimamiwa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ikiongozwa na Brigedia jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi ambaye sasa anawania ubunge jimbo la Mlalo. Nayo serikali kuu ya CCM kupitia Ofisi ya Rais (Menejimenti ya utumishi wa umma), ikiongozwa na Dk. Mary Nagu anayewania Ubunge jimbo la Hanang ilijirekebisha kwa kadri ya uwezo wake ili kuhakikisha kazi za umma zinafanyika kwa ufanisi. Watanzania wataichagua CCM kwa sababu imeonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya maji kupitia mamlaka zinazotoa huduma za maji safi na taka katika miji mbalimbali ikiwemo ya Mbeya, Dodoma, Arusha, Moshi, Mwanza, Shinyanga na Tabora. Pia wataichagua CCM kwa sababu wameshuhudia ujenzi wa barabara za lami uliokamilika na unaoendelea sehemu mbalimbali nchini ili CCM iweze kukamilisha miradi hiyo. CCM itachaguliwa kwa sababu kimsingi dawa zimejaa katika maduka mbalimbali nchini na pia zipo katika hospitali, vituo vya afya na zahanati ingawa zinauzwa walau kwa bei nafuu. Hivyo wapinzani wanaodai kwamba watashinda , wanaonekana vichekesho kwa vile mpaka sasa hawajaonyesha utawala bora ndani ya vyama vyao, na pia bado havijatoa ushirikiano wa dhati kwa wananchi wakati wa kipindi chote kisicho cha kampeni. Viongozi wa vyama vya upinzani , mara nyingi wamevunja rekodi kwa kutumia ukumbi wa Idara ya habari (MAELEZO) kutoa sera kwa waandishi bila kwenda kwa wananchi vijijini ili kuvitambulisha vyama vyao. Wengine akiwemo Mwenyekiti wa DP Christopher Mtikila wanatumia ujanja wa kutangaza habari zao kwa kuwaita waandishi wa habari ofisini kwao kila Jumapili. Kibaya zaidi baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani akiwemo Profesa Ibrahimu Lipumba wamekuwa mabingwa wa kuitisha maandamano kila wiki kuanzia Ofisi zao hadi wanakojua wenyewe. Mambo hayo hayajasaidia sana kuwafanya Watanzania wawe na imani na vyama hivyo kiasi cha kuwapatia kura. Bila shaka viongozi wenyewe wa vyama vya upinzani wanajua suala hilo na wanachofanya ni kuhakikisha wanatekeleza wajibu wa kuwepo kwao katika mfumo wa vyama vingi. Hivyo ipo haja kwa Profesa Lipumba wa CUF na Mbowe wa CHADEMA kujiweka tayari kushindwa badala ya kuwa na ndoto za ushindi.