Na Abihudi Saideya, Moshi, 04/10/2005 - Dk. Shein 
 
Vyama vya upinzani vinapungua nguvu Mkoani Kilimanjaro
kutokana na jitihada za Chama Cha Mapinduzi za
kurejesha majimbo manne ya Mkoa huo yaliyokuwa
yanashikiliwa na Wabunge wa upinzani.
 
Hali hiyo ilijidhihirisha leo 04/10/05 kwenye mikutano
miwili ya kampeni iliyohutubiwa na mgombea Mwenza wa
Rais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
katika Wilaya za Hai na Siha Mkoani Kilimanjaro.
 
Wakati wa mikutano hiyo wanachama 73 wa vyama vya
upinzani walirudisha kadi za vyama hivyo na kuhamia
Chama Cha Mapinduzi.
 
Mkutano wa kwanza ulifanyika kata ya Machame Kusini,
Kikavu Chini Wilayani Hai ambapo wanachama wote 31 wa
TLP tawi la Kijiji cha Mijongweni wakiongozwa na
Mwenyekiti wa tawi hilo Bw. Gaspery Mwangia
walirejesdha kadi na bendera ya Chama hicho.
 
Kiongozi mwingine,Katibu wa TLP wa Wilaya Bw.Gabriel
R. Mushi alitangaza kuhamia CCM kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kijiji cha Koboko, Kata ya Siha
Kaskazini,Wilaya ya Siha.
 
Bw.Mushi alisema ameamua kubwaga manyanga baada ya
kubaini vyama vya upinzani havina mipango makini kama
kilivyo Chama Cha Mapinduzi.
 
Wanachama wa upinzani waliorejesha kadi katika
mikutano hiyo walikuwa kutoka vyama vya TLP-35,CHADEMA
-33 na CUF watano.
 
Akizungumzia kuhama kwa wanachama hao Katibu wa CCM wa
Mkoa wa Kilimanjro Bw. Simon Nchimbi alisema hali hiyo
inaashiria dalili za kufanikisha azma ya kurejesha
majimbo na Halmashauri zinazoongwa na wapinzani.
 
Majimbo ya uchaguzi wa Bunge yaliyokuwa yanashilikiwa
na wapinzani katika kipindi kilichomalizika ni Moshi
Vijijini, Moshi Mjini, Vunjo na Hai.  
 
Bw. Nchimbi alisema CCM ina matumaini ya kushinda
Urais wa Jamhuri ya Muungano na majimbo yote tisa ya
uchaguzi wa Bunge yaliyoko Mkoani Kilimanjro. 
 
Pamoja na wimbi kubwa la wapinzani wanaohamia CCM,
alisema ushindi mkubwa wa CCM Mkoani Kilimanjro katika
uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2004 unadhirisha
CCM inakubalika zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
 
Akihutubia Mikutano hiyo Dk.Shein aliwaomba wananchi
wamchague Mgombea Urais wa CCM Bw.Jakaya
Kikwete,wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na
CCM kwa kuwa ndicho chenye sera madhubuti.
 
Dk. Shein alisema CCM ina rekodi ya kupigania ukombozi
wa kitaifa na ndicho chama chenye uwezo wa kuendeleza
udugu, umoja na maendeleo ya wananchi wote bila kujali
ubaguzi.
 
Aliviponda vyama vya upinzani vivyoeneza sera za
kugawa mali asili ya taifa kwa kuzingatia mikoa na
majimbo zilizopo mali hizo, akisema hizo sera ni za
kibaguzi.
 
Dk. Sheni alisisitiza kuwa Tanzania inaongozwa kwa
misingi ya katiba na sheria na kwamba CCM itawahudumia
Watanzania wote bila kubagua maeneo wanakotoka.
 
Katika ziara hiyo Dk. Shein alifuatana na Mwenyekiti
wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro Vicky Nsilo na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Grace Soka. Kesho
05/10/2005 Dk. Shein ataendelea na ziara ya Kampeni
Mkoani Tanga.
 
=mwisho=
ABIHUDI SAIDEYA - Mwandishi wa Habari - 0744-268961.