Na Abihudi Saideya, Mbulu, 01/10/2005  = Dk.SHEIN
 
Mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. Ali Mohamed Shein jana (30/09/2005)
alipokelewa na mamia ya wananchi alipowasili Mbulu,
Mkoani Manyara kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu. 
 
Kabla hajawasili mjini Mbulu Dk. Shein alilakiwa na
viongozi wa CCM,wanachama, wakereketwa na wananchi
katika kata ya Daudi, mpakani mwa Wilaya za Karatu na
Mbulu.
 
Alipoingia Mbulu Mjini alikaribishwa na halaiki kubwa
ya watu waliojipanga barabarani wakiimba nyimbo kwa
staili ya Kimbulu, baadhi yao wakiwa wamevalia shanga
za rangi mbalimbali.
 
Dk.Shein akiwa amefuatana na Wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM ya Taifa (NEC),Dk. Mary Nagu na Mama Grace
Soka aliwapungia mkono huku gari lake likipita kwa
mwendo wa pole.
 
Kabla ya kuhutubia wananchi hao kwenye Mkutano wa
hadhara uliofanyika Mbulu Mjini, Dk. Shein alifungua
Shina la Wakereketwa wa CCM liitwalo "Nguvu Kazi",
Kata ya Gehandu.
 
Shina la Wakereketwa wa CCM la "Nguvu Kazi" lina
wanachama 100 wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na
michezo.
 
Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara Dk. Shein
alivikwa skafu na Chipukizi wa CCM na kukagua vikundi
vya sanaa vya kata mbalimbali za Wilaya hiyo ambayo
vilikuwa vikitoa burudani mithili ya mashindano.
 
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Dk. Shein, Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Mkoa wa Manyara
Dk. Nagu alisema kujitokeza kwa wananachi wengi katika
mkutano huo ni ishara ya kukubalika kwa CCM na
wagombea wake.
 
Alisema Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Bw.Jakaya 
Kikwete ni kiongozi mzoefu ambaye ameonyesha uadilifu
katika utumishi wake ndani ya Chama na Serikali.
 
"Amekuwa waziri kwa miaka 17 na ni mwanadiplomasia
anayekubalika ndani na nje ya nchi," alisema na
kuwaomba wananchi wasichague viongozi ambao hawana
uzoefu na masuala ya uongozi wa taifa.
 
Kuhusu Mgombea Mwenza wa Rais kupitia CCM, Dk. Ali
Mohamed Shein, Dk. Nagu alisema ni mwanasiasa makini
asiyetiliwa mashaka.
 
Dk. Nagu aliwaomba wananchi kuwachagua wagombea wote 
wa CCM wakiwemo Wabunge na Madiwani ili kuweka timu
imara itakayosimamia maendeleo na uongozi wa taifa.
 
Akihutubia hadhara kubwa iliyojitokeza kwenye mkutano
huo, Dk. Shein aliwashukuru wananchi Mbulu kwa
mapokezi mazuri na akafafanua kwa kirefu mafanikio ya
serikali ya CCM na mipango ya maendeleo iliyopo kwenye
ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 hadi 2010.
 
Alisema kwa kiasi kikubwa Serikali ya CCM imefanikiwa
kuendeleza huduma za jamii na miundo mbinu Wilayani
Mbulu na sehemu nyingine nchini.
 
Dk. Shein alisema kwa kuwa Wilaya hiyo imeshapatiwa
umeme, sekta nyingine za maendeleo zitapanuliwa kwa
haraka zaidi na akaadi kuwa Serikali itajenga Chuo cha
Ufundi(VETA)Wilayani ili kuwawezesha wananchi kupata
ujuzi wa kuendesha miradi ya maendeleo.
 
Akizungumzia masuala ya utawala bora, Dk. Shein
alisema serikali ya CCM ya awamu ya nne ikiingia
madarakani itaimarisha mfumo wa siasa ya vyama vingi
kwa kuimarisha utoaji wa elimu ya uraia.
 
Alisema serikali itavitaka vyama vya siasa kujiendesha
kwa kuzingatia misingi ya demokrasia kuanzia ndani ya
vyama vyenyewe.
 
Dk.Shein alisema nia ya Serikali ni kuepusha vitendo
vya uenezi wa siasa za chuki, fujo na uchochezi. 
 
Alimtambulisha mgombea Ubunge wa jimbo la Mbulu
kupitia CCM Bw.Philip Marmo na wagombea udiwani wa
kata zote za Wilaya hiyo na kuwaomba wananchi
wawapigie kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka
huu.
 
Kesho kutwa ( 03/10/2005) Dk. Shein ataendelea na
ziara ya kampeni za uchaguzi Mkoni Kilimanjaro.
 
(Mwisho)
 
*ABIHUDI SAIDEYA ni  Mwandishi wa Habari - Contact:
 Cellphone: 0744-268961 au 0787-052221.