Uchaguzi upi ulikuwa na kasoro nyingi:

SHUTUMA za ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kuhusu uchaguzi ulivyofanyika Zanzibar zinaweza kuwachanganya watu wasioifahamu  Marekani na unafiki wa nchi nyingi za magharibi.Kwa anayeijua atakwenda mbali zaidi na kuchunguza. Mwandishi wetu, ROBERT MOSHI, kwa utaratibu ule ule wa "Ondoa kwanza boriti" ndani ya jicho lako kabla ya kuona "kibanzi" kwa mwenzako, anaweka bayana katika makala hii, kasoro za kutisha zilizotokea kwenye uchaguzi wa Marekani mwaka 2000 na 2004 na kuhoji kama kweli nchi hiyo inapaswa kuwafundisha Watanzania demokrasia.

NENO ukandamizwaji wa wapigakura linaweza kuelezwa kama mbinu za kuwakatisha tamaa watu ambao walikuwa wapige kura. Nia ya kuwakandamiza watu hawa ni kuwafanya wasipige kura kwa kuhofia kwamba wakipiga, mgombea wa urais wa kambi fulani atashindwa.

Hii ni mbinu chafu inayotumiwa na chama pinzani chenye hofu ya kukosa kura kutoka kwa wapigakura wa eneo fulani. Mbinu hii ilitumiwa na Chama cha Republican cha Marekani, chama cha Rais wa sasa wa Marekani, George W. Bush.

Baada ya kuona kwamba kulikuwa na maeneo fulani Bush hatapewa kura, wapambe nuksi walibuni mbinu kuhakikisha  masanduku ya kupigia kura hayapo, vifaa mbalimbali, zikiwemo karatasi, vinakosekana na hivyo kituo kuhamishwa dakika za mwisho au mbinu za kuwakatisha tamaa wapigakura zilitumika ili waondoke.

 Kwa mfano mwakilishi wa jimbo la Ohio, Marekani, Dennis Kucinich, alieleza kukandamizwa kwa wapigakura wa jimbo lake kwenye uchaguzi wa mwaka jana.

 Alisema kulikuwa na mbinu chafu kwenye jimbo lake, ikiwemo kusambazwa kwa barua feki zilizoonyesha kwamba zimetoka bodi za uchaguzi, zilizokuwa zikiwaambia wapigakura kwamba waliojiandikisha kupitia vikundi vya wanaharakati wa Chama cha Democrat 'wameliwa'.

Kwamba hawataweza kupigakura.

Mbinu hizo chafu hazikuishia hapo. Barua ziliendelea kuwatahadharisha wapigakura, ambao ilionekana dhahiri kwamba wangelikipigia kura chama cha Democrat, kwamba vyama vya wanaharakati vya Democrat vilikuwa batili na kwamba watu waliotaka kumpigia kura mgombea wa urais wa tiketi ya Democrat, John Kerry, walipaswa kuripoti vituoni siku moja baada ya uchaguzi!

Mbinu nyingine chafu zilizotumika katika taifa hilo kubwa linalojitangaza lina demokrasia, ili mgombea wa Republican, George Bush ashinde, ilikuwa kupiga simu nyingi za uongo, kuwapa taarifa potofu wapigakura katika maeneo yaliyojidhihirisha wazi kwamba Bush hapendwi, hivyo hasingeambulia kitu.

Taarifa hizo potofu zilizokuwa zinasambazwa kwa simu, ziliwachanganya wapigakura wengi, wakashindwa kufuatilia maelekezo kwenye karatasi za kura na kura zao kuharibika.

HII NDIYO MAREKANI

Wakati wa uchaguzi, ni jambo la kawaida vyama vya siasa kuhimiza wapigakura wao kwenda kupiga kura. Hali haikuwa hivyo kwenye majimbo mengi nchini Marekani, hasa chama cha Republican kilipoona mgombea wake atashindwa.

Kwa mfano, mmoja wa wanasheria wa jimbo la Michigan, ambaye ni wa chama cha Republican, alikaririwa akisema mbinu chafu ni muhimu ili kuwamaliza wapigakura wasiokipenda chama hicho.

"Ikiwa hatutatumia mbinu chafu na kuvuruga  upigaji kura huko Detroit tutakuwa na wakati mgumu katika uchaguzi huu," alikaririwa akisema.

Mbinu chafu kama hizo zilisababisha kesi kufunguliwa mahakamani na vyama vikuu vya Republican na Democrat vikajikuta kwenye kesi za uchaguzi. Chama cha Green cha            Ohio pia kilijikuta katika mkumbo wa kesi, kila chama kikilaumu kingine kwa kutumia mbinu chafu kuwapotosha wapigakura wa chama kingine.

Kwa mfano, huko Wisconsin, kijana wa kiume wa mbunge wa chama cha  Democrat na watu wengine wanne wa  kujitolea,  waliokuwa kwenye kambi ya kampeni ya   Kerry/Edwards, walitoboa matairi yote kwenye magari 25 yaliyokodishwa na chama cha Republican kwa ajili ya kampeni.

Vijana hawa watano walitiwa mbaroni na kufunguliwa mashitaka.

Kwa Wamarekani hizo si vurugu, huo si uhalifu, bali uhalifu ni pale askari wa FFU nchini Tanzania wanapowafyatulia mabomu ya gesi kutolea machozi wafuasi wa CUF wanaowarushia mawe baada ya kuhamasishwa na viongozi wao.

Mwaka  2004 suala la kuweko misururu mirefu ya wapigakura kwenye maeneo mengi na ushindi ukaonekana dhahiri ni wa Democrat kulizua mjadala.

Kuweko kwa idadi kubwa ya wapigakura wa Democrat, wakati mashine za kupigia kura zilikuwa chache, ni mbinu iliyokuwa inatumika kuchelewesha wahusika ili muda wa kupigakura uishe na baadaye vifaa viondolewe. Kuna wapigakura ambao huamua kususa na kuondoka baada ya kusubiri mno.

UBAGUZI WA RANGI

Ubaguzi wa rangi nchini Marekani, hata kama utajificha, wakati wa uchaguzi huibuka kwa kasi. Tume ya kutetea haki za kiraia imekadiria kwamba mwaka 2000 jimboni  Florida, asilimia  54 ya masanduku ya kura yaliyokuwa na maandishi "YAMEHARIBIKA" yalikuwa yametumiwa na Wamarekani wenye asili ya Afrika, ambao walikuwa hawampendi Bush.

Mwaka  2004 uchaguzi wa Marekani ulizidi kutoa picha kwamba Wamarekani weusi wangeendelea kukipigia kura chama cha Democrat. Matokeo yake maeneo mengi ya watu weusi yaliandaliwa kasoro za makusudi ili wasipige kura kwa wingi.

Greg Palast, mwanamapinduzi mweusi alisema kwamba kama uchaguzi ungeendeshwa kistaarabu, bila kasoro kubwa na za kutisha, basi John Kerry angeshinda.

Mchungaji Jesse Jackson, mwanaharakati mweusi wa Marekani ambaye pia ni mwanzilishi wa Muungano wa Rainbow, alilalamika sana siku ya uchaguzi kutokana na ubaguzi wa wazi kwenye maeneo ya Wamarekani weusi. Kwa mfano, maeneo mengi  vifaa havikuwepo; kama vilikuwepo vilikuwa vichache au walipelekewa mashine ambazo hazijawahi kutumika kabisa na wala wapigakura hawakuelimishwa jinsi ya kuzitumia.

 

Mapema Agosti 2004, viongozi kadhaa wa kutetea haki za Wamarekani wenye asili ya Afrika, walisema chama cha  Republican kilikuwa kinaendesha kampeni kuwazuia Wamarekani weusi na wapigakura wengine kutoka kwenye jamii za Wamarekani wachache wasifike kwenye vituo vya kupigia kura, Novemba.

Maofisa kutoka idara ya kukazia sheria ya Florida ambayo huwajibika kwa gavana wa jimbo hilo, Jeb Bush (mdogo wake Rais wa sasa) walipelekwa kwenda kuchunguza udanganyifu kwenye uchaguzi wa meya wa mji wa Orlando.

WAANGALIZI

Wakati makundi makubwa na mengi ya waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi huletwa kwenye nchi za Kiafrika na nyinginezo zinazoendelea, hali ni tofauti kwa Marekani.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka jana, kikundi kidogo cha Taasisi ya Usalama na Ushirikiano ya Ulaya (OSCE)ndicho kilichoalikwa kuangalia uchaguzi wa Marekani.

Waangalizi wa kikundi hicho waliruhusiwa kutembelea vituo vichache sana katika majimbo machache, na wakati mwingine wilaya chache tu za jimbo.

Licha ya kubanwa ili wasione mengi machafu kwenye majimbo na wilaya hizo chache, lakini waliandaa ripoti yao.

Katika ripoti yao, walishutumu upendeleo uliokuwa dhahiri wa maofisa wa tume ya uchaguzi (ambayo kwayo ni 'Tume huru') na misururu mirefu kwenye vituo vya kupigia kura.

UKIMYA WA WANAHABARI

Waandishi wa habari wa Tanzania wasiokuwa na uzalendo, au hata utaifa, waone vyombo vya habari vya Marekani vilivyo na utaifa inapotokea aibu ya kuisuta nchi yao.

Tangu zianze kutolewa taarifa za udanganyifu katika uchaguzi mkuu nchini Marekani uliofanyika mwaka jana, hasa mkanganyiko kwenye matokeo ya urais na wizi wa kura, vyombo vikuu vya habari vya nchi hiyo vilikaa kimya, havikugusia kabisa hali hiyo.

Vyombo vya habari vinavyotukuka nchini Marekani ambavyo ni rahisi sana "kuimba" udhaifu wa mambo kama hayo yanapotokea katika nchi nyingine, havikuandika au kutangaza kabisa habari hizo; havikuuelimisha umma na badala yake wananchi walilazimika kugeukia kwenye vyombo vya kawaida, vingine vidogo sana ambavyo walau viliandika.

Vitendo vya udanganyifu kwenye vituo vya kupigia kura vilikithiri kwenye uchaguzi wa mwaka 2000 na wa mwaka jana nchini Marekani. Kwa mfano, katika jimbo la Florida ambako wizi wa kura, ukandamizaji wa wapigakura na udanganyifu vilishamiri ili chama cha Republican kishinde ni mambo yaliyokuwa wazi.

Katika maeneo kadhaa wapigakura wengi kura zao hazikuhesabiwa.

Kwa mfano, zaidi ya kura 90,000 zilizopigwa Florida mwaka 2000 hazikuhesabiwa kwa madai kwamba mashine zilizotumika ni tofauti na zilizokuwa zimeandaliwa na kudaiwa kuwa ni kura bandia. Baadhi ya maeneo kuliwekwa majina ya wapigakura ambao wameshakufa.

BUNGE LAJADILI

Uozo uliokithiri kwenye udanganyifu katika jimbo la Florida mwaka 2000, ulijirudia tena mwaka jana, lakini jimbo la Ohio safari hii likiwa limerithishwa maovu yote ya Florida ya mwaka 2000.

Kutokana na uozo huo, kamati ya sheria ya Bunge ililazimika kufanya vikao kadhaa kujadili aibu hiyo katika mfumo mzima wa uchaguzi kuanzia uandikishaji, vifaa vya kupigia kura, vitisho, wizi wa kura, udanganyifu wa kutisha na kura bandia.

Wakala wa serikali anayehusika na masuala ya uchaguzi (GAO) alilazimika kumwita msimamizi mkuu wa uchaguzi wa jimbo la Ohio, Kenneth Blackwell, kujieleza mbele ya kamati ya sheria ya bunge kutokana na mapungufu makubwa yaliyojitokeza.

Kamati hiyo ilikutana Desemba 8 na 13, 2004 na miongoni mwa washiriki wengine waliokuwepo kupinga ubadhirifu huo na kuhoji wizi wa kura ni Mchugaji Jesse Jackson, Cliff Arnebeck, David Cobb, Bob Fitrakis na Steve Freeman.

Ripoti yenye kurasa  100 iliandaliwa  na kutolewa Januari 5, mwaka huu, siku moja kabla ya vikao vya pamoja vya bunge la Marekani kwa ajili ya kupokea taarifa ya uchaguzi na hali ya upigaji kura.

Taasisi ya serikali inayowajibika na masuala ya kura ilisema baada ya kuipitia ripoti hiyo, kwamba ingelifanya uchunguzi wa kina kutokana na maswali mengi yaliyokuwa yanaulizwa kuhusu udanganyifu na kasoro zilizojitokeza kwenye majimbo mengi, hasa Ohio na Florida.

Mapungufu ya ziada ni pamoja na mashine za kuhesabia kura kushindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu ya kuchokonolewa makusudi na baadhi ya wataalamu walioonekana kuandaliwa.

Udanganyifu mwingine ni kupelekwa kwa watu wasiohusika na upigaji kura katika eneo moja na wahusika (halali) kukatazwa kupiga kura kwa madai kwamba mashine na kompyuta za uchaguzi hazikuwa na kumbukumbu za majina yao kama waandikishwa wa eneo husika.

UCHUNGUZI

Hata hivyo, wakala wa bunge aliyepewa mamlaka ya kuchunguza udanganyifu huo kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani alisema haruhusiwi kuchukua hatua yoyote dhidi ya watu waliohusika na udanganyifu, hata kama kasoro zilikuwa zinajidhihirisha wazi.

Moja ya udanganyifu uliomnyima kura mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Democrat, John  Kerry, ni kompyuta zenye vioo vipana ambavyo wapigakura walisema zilirekodi majina ya wagombea ambao wao hawakuwa wamewachagua.

Mijadala bado inaendelea kutaka mabadiliko yafanywe kwenye mfumo mzima wa uchaguzi wa Marekani, na tayari miswada kadhaa yenye madhumuni ya kuondoa baadhi ya dosari zilizojitokeza imeshawasilishwa bungeni.

Wananchi wengi Marekani wanajadili mapungufu yaliyojitokeza kwenye uchaguzi wa mwaka 2000, ambao ulitia fora kwa kuwa na udanganyifu mwingi na wizi wa kura, na wa mwaka jana.

Mijadala hiyo kwenye majimbo mengi ya Marekani inaendelea katika nyanja zote za jamii na inatarajiwa kuleta mabadiliko kadhaa katika utaratibu mzima wa kupiga kura.

Tathmini iliyofanywa na wasomi na watafiti imeonyesha kwamba kuna dosari kubwa katika mfumo mzima wa uchaguzi wa Marekani kuanzia uandikishaji, uingizaji wa majina kwenye kompyuta na mashine nyingine za kuhifadhi kumbukumbu, mpangilio mzima wa kupiga kura na mbinu chafu za kuwazuia wapigakura halisi kupiga kura.

 Tathmini inaonyesha kwamba baadhi ya wasomi wamefungua kesi ya madai dhidi ya  jimbo la  Louisiana, ambako maofisa waliosimamia uchaguzi walidai kwamba watu wenye kipato cha chini na cha kati, walinyimwa haki yao ya kupiga kura kwa sababu vituo vingi vya kupigia kura havikufunguliwa, baadhi vilichelewa sana kufunguliwa na vingi havikuwa na vifaa vilivyohitajika kupigia kura, yakiwemo masanduku na karatasi.

Mtandao wa kulinda haki za uchaguzi ulifungua kesi mahakamani na zilianza kusikilizwa Novemba 13 na 15, 2004 kwenye mji wa Columbus, Ohio. Kwenye kesi hizo, wananchi waliwasilisha malalamiko yao kuhusu walivyonyimwa haki za kupiga kura na udanganyifu mwingine uliofanyika.

DEMOCRAT YAPINGA

Wabunge 34 wa Chama cha Democrat, akiwemo Seneta mmoja, walipinga taratibu nzima za kuhesabu kura katika jimbo la Ohio. Walitoa pingamizi hiyo Januari 6, mwaka huu.

Hata hivyo, kupinga kwao hakukufanikiwa kwani wabunge wengi wa upande wa serikali waliwazidi  kura baada ya mjadala uliodumu kwa saa nne mfululizo.

Sehemu ya ushahidi uliotolewa kwa ajili ya mijadala  bungeni, ulitoka kwa wajumbe wa kamati ya sheria ya Bunge ya chama cha Democrat iliyoandaa taarifa yenye kurasa 101 na kichwa cha maneno "Kilichoharibika Ohio".

Taarifa hiyo iliwasilishwa bungeni Januari 6 mwaka huu. Wabunge wengi wa Democrat, ambao wako kwenye kamati ya sheria ya bunge, wameshaiandikia Taasisi  ya Serikali inayoshughulikia masuala ya  uchaguzi (GAO)

wakitaka uchunguzi rasmi ufanywe.

 Barua yao ya kwanza iliandikwa siku tatu baada ya uchaguzi Novemba  5, na kufuatiwa na ya pili Novemba 8, mwaka jana. Uchunguzi unaofanywa na GAO unaendelea.

Vyama mbalimbali vya siasa, kikiwemo cha Green, vimetaka uchunguzi ufanywe kuhusu uozo uliojitokeza Ohio katika mfumo mzima wa uchaguzi mwaka 2004.

Kadhalika, wanataka uchunguzi ufanywe kuhusu kura zilivyopigwa na kuhesabiwa katika jimbo la Nevada. Hata hivyo, ombi la kutaka uchunguzi ufanywe Nevada, liliondolewa na walalamikaji kutokana na wingi wa gharama za kuushughulikia.

TULIWAPASHA

Mwishoni mwa Julai, 2003 wahariri na waandishi wa habari waandamizi wanane kutoka Tanzania, walikuwa Marekani kwa mafunzo ya kikazi. Miongoni mwa majimbo waliyotembelea ni Orlando Florida, jimbo ambalo gavana wake ni Jeb Bush.

Kulifanyika mdahalo mkali kwenye televisheni ya Wesh iliyowajumuisha wanahabari kutoka Tanzania na baadhi wa wabunge, wabunge wastaafu wa Marekani, wanasiasa, wanasheria na mabingwa wa masuala ya vita na silaha.

Mjadala uliokuwa mkali sana ulikuwa ni kuhusu udanganyifu katika kupiga kura, na uchaguzi mzima wa mwaka 2000, hasa katika jimbo la Florida. Uchaguzi huu ndio uliomweka George Walker Bush madarakani baada ya mwezi mzima wa aibu ya wizi wa kura na kigugumizi cha kutangaza matokeo.

Miongoni mwa watu mahiri waliokuwa kwenye mdahalo huu ni  aliyekuwa mbunge wa chama cha Republican, Loui Frey, kwa jimbo la Florida. Huyo ni mmoja wa wanasiasa wakongwe na msomi wa kutukuka aliyeandika machapisho mengi.

Wengine ni Naibu Meya wa mji wa Orlando, Robert S. Miller, Rais wa kituo cha televisheni cha WESH 2 Channel William Bauman,  mwandishi mwandamzi wa gazeti la Orlando, Sentiel Debbie Salamone na magwiji wengine.

Baada ya mjadala mkali na wenye mantiki,  mkongwe Frey, mwenye shahada na sifa lukuki, na jopo la Wamarekani wenzake walikiri udhaifu kwenye mfumo wa uchaguzi, hasa Florida mwaka 2000.

Pia alilalamikia mashine mbovu za kuhesabu kura, mikataba na wamiliki wa mashine hizo na kutohesabiwa kwa kura katika baadhi ya maeneo wanamoishi Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Mjadala huo uliibua aibu kubwa kwa teknolojia duni ya mashine  za kupigia kura zilizotumika  Florida, kwa nchi kama Marekani ambayo iko mbele miaka mingi katika teknolojia ikilinganishwa na nchi zinazoendelea. Nchi zinazoendelea zinaitwa mataifa ya juzi zinapolinganishwa na Marekani ambayo ilipata uhuru wake zaidi ya miaka 200 iliyopita.

Loui Frey amejipatia sifa nyingi bungeni na katika vyuo vinavyotukuka Marekani, lakini pengine sifa ambayo imemwinua sana ni mchango wake wa machapisho ya masuala kama ya elimu, siasa,  elimu ya uraia na uchumi.

Ni mbunge huyo aliyeandika: "Brief History of the Electoral College." Hilo ni chapisho linaloelezea historia ya namna makamu wa rais wa Marekani wanavyochaguliwa. Kwa "ustaarabu wa demokrasia"  za Marekani si kila Mmarekani ana haki ya kumchagua makamu wa rais. Uchaguzi wa makamu wa rais hufanywa na "wateule" wachache, wengine wanaishia kupiga kofi tu!

 Kadhalika ameandika majarida mengi kuhusu utangazaji, tathmini ya siasa za Orlando, Florida jimbo aliloliwakilisha bungeni kwa zaidi ya miaka 10, na mfumo mzima wa televisheni. Ameshiriki kubuni na kuendeleza uandishi wa safu mbalimbali kwenye magazeti ya Florida na redio za jimbo hili.

Loui Frey, kama walivyo Wamarekani wengi, alishiriki kwenye mafunzo ya kijeshi kuanzia  1955-1958, hasa katika kikosi cha wanamaji ambako alikuwa nahodha wa meli ya kivita ya Marekani, USNR.

Mjadala mwingine mkali uligusia ushiriki wa Marekani katika vita mbalimbali duniani na nchi ilizovamia. Mjadala kuhusu  Osama Bin Laden na Saddam Hussein ulichangamsha mdahalo kwa jinsi Watanzania walivyokuwa na takwimu sahihi kuhusu Marekani ilivyowagharamia na kuwajenga watu hao wawili, ambao leo inawaita magaidi.

HITIMISHO

Baada ya kuona kasoro zilizotokea kwenye taifa hilo kubwa, lenye zana za kisasa na fedha nyingi za kuendeshea uchaguzi, ingetarajiwa kwamba katika kutoa kauli yake kuhusu uchaguzi wa wiki moja iliyopita visiwani Zanzibar, Marekani ingezingatia lugha ya kutumia, ili udhaifu huo uliotokea Marekani, uweze kuendelea kujificha kwa sababu vyombo vikuu vya habari vya huko havikuugusa kabisa.

 Pia, ilitarajiwa ingelichunguza kwa kina mwenendo wa chama cha CUF kujua ukweli kabla ya kuanza kutoa matamshi hadharani. Ziko taratibu za kidiplomasia za kuelezea namna nchi fulani isivyoridhika na jambo fulani.

Ndiyo maana mabalozi walioko Washington hawakulaani mara moja (au hawakulaani kabisa) udanganyifu wa kutisha uliofanywa Florida,  na maeneo mengine kiasi cha kuchelewesha matokeo ya urais mwaka 2000 kwa zaidi ya mwezi mmoja. Udanganyifu huu ndio uliomweka Bush madarakani.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inashutumiwa kwamba si tume huru.  Sasa kwa mtaji kama tulivyoona kwa Marekani ni nani anayetenda haki? Jeb Bush (mdogo wake Rais Bush na gavana wa Florida) aliyesuka udanganyifu wote hadi kaka yake "akaula" au ZEC ambayo Watanzania waliichagua na hata CUF wanaolalamika waliiafiki?

Mdogo wake Rais Amani Abeid Karume angekuwa ZEC, dunia ingesemaje? Ingekaa kimya kama ilivyokaa kutokana na "ushuzi" huu wa Florida? Au "ushuzi" huu wa Florida ni manukato?

Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani, Condoleezza Rice, anakifahamu sana chama cha CUF. Amemfundisha mmoja wa viongozi wake - Au wanadhani sisi hatujui? Hivi  kwa uelewa huu, bado Marekani inaweza kweli kuitetea CUF?

Sikatai kukitokea udhaifu na kasoro, mkubwa na mdogo hurekebishana, lakini kasoro ni nyingi wapi: katika uchaguzi wa Zanzibar ambao matokeo yake yalitangazwa kama yalivyotarajiwa na wakati uliopangwa, au ya Marekani yaliyokuwa na kigugumizi cha mwezi mzima?

Kwa uoza huu wa Florida na Ohio mwaka 2000 na 2004 kweli Marekani inaweza kukurupuka haraka hivyo katika uchaguzi unaofanyika Tanzania na kutoa taarifa ya kushutumu, tena kwa kukariri taasisi moja tu ya National Democratic Institute (NDI)?

Ni busara kuikumbusha Marekani kwamba kesi za kupinga uwepo wa Bush madarakani bado ziko mahakamani na mijadala haiishi bungeni. Ni vema basi ikaanza kundoa "boriti" la mti wa mninga lililoko jichoni mwake kabla ya kuona "kibanzi" cha muwa kilichoko Zanzibar.