Uhuru 05.09.2005
Sheikh Yahya apongeza Magezi kufichua kampeni misikitini
Ni kauli yake kuhusu Shura ya Maimamu
Na Robert Moshi
MNAJIMU maarufu Afrika Mashariki na Kati Sheikh Yahya Hussein amempongeza Sheikh Magezi Shaaban kwa kusema ukweli kuhusu yale aliyokuwa akifanya wakati akiwa Shura ya Maimamu kwamba shura hiyo ilianzishwa ili kukidhi malengo ya kisiasa.
Sheikh Yahya alitoa pongezi hizo wakati wa kipindi chake cha Nyota kinachoendeshwa kila Jumamosi usiku kwenye kituo cha televisheni cha Channel Ten cha mjini Dar es Salaam. Kipindi hicho kilirushwa juzi usiku.
Alisema kutokana na kauli zake kwamba Chama cha CUF ndiyo mbia mkubwa wa Shura ya Maimamu, Sheikh Magezi hapaswi kushutumiwa na chama hicho na wala CCM haipaswi kumpongeza kwa kauli zake hizo, kwani sasa hazina nguvu.
Akifafanua, Sheikh Yahya alisema Sheikh Magezi amekuwa mkweli kueleza yale aliyokuwa anayafanya wakati akiwa kwenye Shura hiyo.
Hivi karibuni, Sheikh Magezi aliwaambia Waandishi wa habari kwamba Shura ya Maimamu ilianzishwa ili kutumbukiza masuala ya kisiasa ndani na kwamba chama cha CUF kilikuwa mbia kwenye Shura hiyo.
Wakati huo huo, Sheikh Yahya amesema Wilaya ya Kinondoni inang'ara kinyota mwaka huu baada ya kumtoa Mshindi wa urembo Miss Tanzania 2005.
Alisema kwenye kipindi chake juzi usiku, wakati akijibu swali kwamba jina la Nancy Sumari, aliyeshinda tuzo hilo mwishoni mwa wiki, herufi zake zikijumuishwa zinatimia 11 ambazo kinyota ni K na K ni Kinondoni.
Alisema K ina nguvu sana kinyota mwaka huu na ndio maana hata mshindi wa pili Natalie Noel anatoka huko huko Kinondoni.
Aliwataka watu wasiojua nyota, hasa waandishi wa habari na wamiliki wa majarida kuacha kutabiri au kuwapigia 'debe' warembo ambao wao (wenye majarida) wanawaona ni wazuri, lakini kinyota hawatashinda. Alisema ni vizuri watu wasiojua mambo ya utabiri, wakawaachia watabiri kazi yao.
"Mwaka jana waliniuliza mshindi, nikawaambia Faraja Kota. Mwaka huu hawakuniuliza, lakini wamekurupuka kuwapigia debe watu ambao hawana mvuto kinyota kushinda, matokeo yake wameshindwa, mambo ya nyota tuachieni sisi," alisema.
Kinondoni, aliongeza Sheikh Yahya, imemtoa pia mgombea Urais ambaye jina lake ni K dalili kwamba K inatamba na itaendelea kutamba mwaka huu.
"Wakristo wameshasema hawataki ubaguzi, wametoa zawadi kwa kiongozi wa Kiislamu ambaye wameona atashinda. Wanajua, huwezi kutoa zawadi kwa mtu ambaye unajua atashindwa," alisema.
CCM yazindua kampeni za Urais wa Zanzibar leo
Karume,Kikwete kunguruma Pemba
Wamo pia Mkapa, marais wastaafu
Na Mwadini Hassan, Zanzibar
MBIO za kuwania urais wa Zanzibar, zinaanza rasmi leo ambapo Chama cha Mapinduzi kinazindua kampeni
zake. Kampeni za CCM zitazinduliwa kwenye viwanja vya Gombani, kisiwani Pemba.
Katika uzinduzi huo wagombea wote wawili wa urais, wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete na wa Zanzibar, Amani Abeid
Karume, watakuwepo ambapo atakayeongoza uzinduzi huo ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin
Mkapa.
Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Mkapa atakuwa wa kwanza kupanda jukwaani kuzungumza kwenye mkutano huo wa kwanza wa kampeni Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka
huu. Atafuatiwa na mgombea mwenza wa Muungano, Dk. Ali Mohammed Sheni na mgombea
urais, Jakaya Kikwete.
Rais Karume, ambaye ndiye anayeingia dimbani kwa mara ya kwanza mwaka huu kuanza kampeni za kutetea kiti
chake, atakuwa wa mwisho kuzungumza kwenye mkutano huo.
Ratiba ya sherehe hizo za uzinduzi wa kampeni za CCM kwa urais wa Zanzibar iliyotolewa mjini hapa
jana, imeonyesha kuwa marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi na Dk. Salmin Amour pia watakuwepo kwenye uzinduzi
huo.
Uzinduzi huo wa kampeni za Chama cha Mapinduzi unafanyika siku tatu tu baada ya wagombea urais wa Zanzibar kurejesha fomu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
(ZEC), ambayo imewapitisha wagombea sita kuwania kiti hicho.
Wagombea waliyopitishwa ni Amani Abeid Karume (CCM), Seif Shariff Hamad (CUF), ambao ndiyo wanaochuana vikali kutokana na uimara wa vyama vyao katika siasa za Zanzibar.
Kabla ya uzinduzi huo wa kampeni utakaoanza saa saba mchana, Rais Karume atazindua barabara mpya ya kilomita 8.8 ya
Mtuhaliwa/Chokocho ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami.
Barabara hiyo kwa jumla ina urefu wa kilomita 12.8 na kilomita nne zilizosalia ambazo ni kati ya
Bogowa/Michenzani na Mkanyageni/Shidi zimeshajengwa kwa matayarisho ya mwanzo na kazi ya kuzitia lami inatarajiwa kuanza
karibuni. Gharama za ujenzi wa barabara hiyo zimeshafikia sh. 893,902,840.
Mgombea CUF mbaroni kwa kufanya fujo
Na Latifa Ganzel, Matombo
MGOMBEA udiwani wa CUF katika Kata ya Kismu, Frank Kando (28) amekamatwa na polisi kwa tuhuma ya kwenda ofisi ya Kata ya CCM kufanya fujo na kuchana picha ya mgombea urais wa CCM Jakaya Kikwete. Mwenyekiti wa CCM wa Kata hiyo James Mg'ong'o alisema Kando alifika ofisini Ijumaa saa tatu na inadaiwa alifanya fujo na kuchana picha ya Kikwete. Mg'ong'o alisema kuwa walitoa taarifa polisi na mtuhumiwa alijipeleka polisi na kuwekwa ndani ambapo anatarajia kufikishwa mahakani leo. Polisi walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kikwete aahidi vyuo vikuu zaidi nchini
Ataka kuona vijana zaidi wanapata elimu hiyo
Na Epson Luhwago, Iringa
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema serikali ijayo itahakikisha idadi ya vyuo vikuu vinaongezeka ili kuongeza idadi ya wanafunzi wenye sifa za kujiunga na elimu ya
juu.
Akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa kampeni kwenye uwanjawa Kumbukumbu ya
Samora, mjini hapa, mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete alisema kazi hiyo itapewa kipaumbele iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa awamu ya
nne.
"Elimu ni rasilmali muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote duniani. Hata mataifa yaliyoendelea bado yanatilia umuhimu suala la
elimu. Licha ya kupiga hatua mbele katika elimu, Chama cha Labour cha Uingereza kiliweka suala hili kama agenda kuu kwenye
kampeni.
"Ni wazi kwamba taifa likiwa na wasomi wengi litajikwamua katika matatizo kwa sababu litawatumia katika kutatua matatizo yanayolikabili kwenye njanja
mbalimbali," alisema.
Alisema idadi ya wanafunzi wanaofaulu kiwango cha daraja la kwanza imekuwa ikiongezeka mwaka hadi
mwaka, lakini kati yao ni wastani wa wanafunzi 32,000 tu wanaochaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa masomo ya shahada na stashahada ya
juu.
Kutokana na tatizo hilo, alisema serikali imeshaanza kuchukua juhudi za makusudi katika kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuanzisha vyuo vikuu sehemu mbalimbali
nchini.
Alivitaja baadhi ya vyuo vikuu hivyo kuwa ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa
(zamani shule ya sekondari Mkwawa) na Mbeya ambacho kwa sasa ni chuo cha ufundi.
Mbali na kuanzishwa kwa vyuo vikuu vipya, pia alisema serikali inafikiria kuongeza nafasi zaidi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zilizopo sasa ili watu wenye sifa waweze kupata
nafasi.
Licha ya elimu ya juu, Kikwete alisema serikali ijayo chini ya CCM itahakikisha katika miaka mitano ijayo inakamilisha ujenzi wa barabara kati ya Minjingumkoani Arusha kupitia
Babati, Dodoma hadi Iringa kwa kiwango cha lami.
"Kazi hiyo itaanza kwa ujjenzi kutoka Minjingu hadi Dodoma na baadaye hadi Iringa ili mtu aweze kusafiri kwa gari kutoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri kwa kutumia barabara hii maarufu kama 'great north road',"
alisema.
Barabara hiyo kutoka Capetown hadi Cairo ni ya lami isipokuwa kipande cha Iringa hadi Minjingu ambacho hakina
lami.
Vile vile, alisema barabara zingine kuu zitajengwa kwa kiwango cha lami ili kusaidia kukuza uchumi na kasi ya kupunguza umaskini kwa
wananchi.
Kikwete pia alisema serikali ya awamu ya nne ya CCM, katika kipindi cha miaka mitano ijayo itahakikisha miji yote mikuu ya wilaya nchini inapata
umeme. Kwa upande wa Iringa alisema miji mikuu ya Kilolo, Makete na Ludewa itapatiwa huduma hiyo kwa haraka
zaidi.
Kwa upande wa hifadhi ya mazingira, mgombea urais wa CCM aliwaomba wananchi wa mkoa wa Iringa kutunza vyanzo vya maji ili kunusuru hali ya ukame na ukosefu wa
maji.
Alisema Iringa ina vyanzo vingi vya maji ambavyo hutumia kuzalishia umeme kama vile
Ruhuji, Rumakali, Mpanga na Kihansi lakini vimeanza kupungua kwa sababu ya uharibifu wa
mazingira.
Kutokana na hali hiyo, aliwahimiza wananchi kutunza mazingira na kuiga mfano wa Kilolo katika upandaji wa miti na utunzajiwavyanzo vya maji.
Kikwete alihitimisha awamu ya kwanza ya kampeni iliyojumuisha mikoa ya kusini na nyanda za juu.
Alifanya hivyo kwa kuhutubia mikutano miwili ya kampeni katika kijiji cha Boma la Ng'ombe wilayani Kilolo na Samora mjini Iringa.
Awamu ya pili ya kampeni hizo itaanza kesho kwa mkoa wa Morogoro katika wilaya na Kilombero. Mikoa mingine atakayofanya kampeni kwaawamu ya pili ni Dodoma, Singida na Manyara.
Mambo si shwari kwa Dk. Kabourou Kigoma
Azidi kukimbiwa na wanachama CHADEMA
MAMBO ni magumu kwa mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma mjini kwa tiketi ya
CHADEMA, Dk. Walid Kabourou kufutia moja ya ngome yake muhimu jimboni humo kusambaratika na wanachama wa ngome hiyo kujiunga na
CCM.
Hayo yalibainika katika mikutano ya kampeni ya mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya
CCM, Peter Selukamba katika kata za Gungu na Buhanda ambapo wanachama hao wa CHADEMA zaidi ya 100 wamerudi
CCM.
Miongoni mwa ngome hizo ni ile ya kata ya Gungu yenye wapiga kura 17,000 ambayo ilikuwa ndiyo kitovu cha kampeni za Dk. Kabourou katika kampeni za mwaka 2000 ambapo mkurugenzi wa kampeni wa kata hiyo Alua aliongoza kundi la watu 35 kurudi
CCM.
Mwanachama mwingine wa CHADEMA ambaye naye aliongoza kundi la chama hicho kuhama ni meneja wa kampeni kitengo cha wanawake wa Dk. Kabourou katika uchaguzi wa mwaka 2000, Zubeda Kwigizi ambaye pamoja na kukihama chama hicho amemtuhumu mbunge huyo kwa
ubinafsi.
Zubeda alidai kuwa pamoja na kushinda usiku kucha na Dk.Kabourou makaburini katika uchaguzi wa mwaka 2000 wakifukiza dawa zilizomsaidia
kushinda, mbunge huyo ameshindwa kuwathamini kwa kazi kubwa waliyoifanya dhidi
yake.
Mwanachama huyo alisema kuwa kwa kipindi chote cha miaka mitano ambayo Dk. Kabourou alikuwa mbunge ameshindwa kufanya chochote kuwasaidia wananchi wa jimbo la Kigoma Mjini na badala yake amekuwa akijinufaisha binafsi kwa kutumia nafasi
hiyo.
Mwanachama mwingine aliyejiengua kutoka CHADEMA, Iddi Kafurunzi alisema kuwa katika ahadi nyingi ambazo Mbunge huyo ameahidi hakuna hata moja ambayo aliyoitekeleza
Akihutubia katika mikutano hiyo mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Selukamba aliahidi kulishughulikia tatizo la maji linalowakabili wananchi wa kata ya
Buhanda-Businde.
Aidha, mgombea huyo alisema kuwa kwa muda wa miaka 10 ambayo Dk. Kabourou ambayo amekuwa mbunge ameshindwa kutumia elimu yake kuwakomboa wananchi wa jimbo la Kigoma Mjini na kuwaondolea matatizo
yao.
Selukamba alisema kuwaondolea matatizo wananchi kunahitaji kiongozi shupavu na mchapakazi kama yeye ambaye anagombea kwa ajili ya kuwatumikia watu badala ya kujinufaisha binafsi kama alivyofanya mbunge
aliyemtangulia.
Changamoto yatolewa vyombo vya habari kuandika habari za wagombea
wanawake
Na Mwandishi Wetu
VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kutoa kipaumbele kwa habari zinazowahusu wagombea wanawake katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu ili kuupa umma nafasi nzuri ya kuchagua viongozi hasa wanawake kulingana na sifa
zao.
Wito huo, ulitolewa juzi na Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), mkoa wa Dar es Salaam, Sauda
Mpambalyoto, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali katika hafla ya chakula cha mchana iliyofanyika katika hoteli ya Peacock mjini Dar es Salaam.
Sauda alisema iwapo wanawake watapewa fursa sawa kwa habari zao kutangazwa ni wazi jamii itakuwa katika nafasi nzuri ya kufikia maamuzi ya kutoa kura zao kwa kundi hilo lenye umuhimu wa pekee katika
jamii.
Alisema wanawake wengi waliojitokeza kuingia kwenye kinyang'anyiro katika uchaguzi mkuu wana sifa zinazokubalika ndani na nje ya
nchi, hivyo jamii haina budi kuwatambua na kuwapa kura kutokana na sifa zao.
Kwa mujibu wa Sauda, hilo litasaidia kwa kiwango kikubwa katika kumuwezesha rais ajaye kutimiza azma yake ya kuhakikisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linafikisha asiliamia 30 ya wabunge wanawake na hivyo kuliwezesha kundi hilo kuwa na uwakilishi wa kutosha
bungeni.
"Kama tutachagua vizuri wanawake, naamini rais ajaye atapata nafasi nzuri ya kuwachagua wanawake katika nafasi za
uongozi," alisema Sauda na kuitaka jamii kutopiga kura kwa misingi ya jinsia na badala yake kuangalia sifa za
wagombea.
Akifafanua, Sauda alisema wanawake wengi na hasa waliopitishwa na CCM kwenye tanuru katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wana sifa za kutosha na hivyo wanapaswa kuungwa mkono na jamii kwa kupewa
kura.
Sauda alitoa mfano wa mafanikio na uwezo ulioonyeshwa na baadhi ya viongozi wanawake nchini akiwemo Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Asha Rose Migiro na aliyekuwa mbunge wa Ukerewe ambaye pia ni Rais wa Bunge la
Afrika, Getrude Mongela.
Alisema nafasi zilizofikiwa na viongozi hao kitaifa na kimataifa ni kubwa, hivyo wanastahili kupewa ushirikiano katika kuhakikisha taifa linaendelea kuwa idadi kubwa ya viongozi
wanawake.
Pia, katibu huyo aliwapongeza wanawake wote waliojitokeza katika kuomba kuteuliwa kugombea nafasi mbalimbali ambao
hawakupita, kukubali matokeo na kuahidi kushirikiana na UWT na CCM kwa jumla katika kufanikisha uchaguzi
mkuu.
'Sijatuma watu watumie jina langu kuihujumu CCM'
Ni Murji ambaye alishinda kura za maoni akaenguliwa
Na Rashid Mussa, Mtwara
MBUNGE wa zamani wa jimbo la Newala, Hasnein Murji amewaonya wapinzani wanaotumia jina lake kuhujumu kampeni za Chama jimbo la Mtwara Mjini kwa madai kuwa anawaunga
mkono.
Kauli hiyo ya Murji ambaye aliongoza katika kura za maoni katika jimbo hili, lakini
akaachwa, aliitoa mwishoni mwa wiki katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama ya wilaya ya Mtwara Mjini ambapo aliahidi kutoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha CCM inashinda kwa
kishindo.
Alikana kambi yake kufanya kampeni chafu dhidi ya mgombea wa CCM, Mohamed Sinani aliyeteuliwa na Chama ya kuwaambia watu wapigie upinzani kutokana na hasira ya kuachwa
kwake.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na viongozi wa Chama mkoa, alisema kuwa wanaofanya hivyo wanafanya kwa matakwa yao na wala hakuwatuma ama kuwafadhili kwa njia
yoyote.
Alisema yeye ni mwana CCM na atabakia kuwa mwana CCM, na kwamba atatoa ushirikiano mkubwa kwa kampeni ya Chama popote atapohitajika kuhakikisha kinapata ushindi wa
kishindo.
Kauli hiyo ya Murji anayeonekana kuwa kipenzi cha wapiga kura wengi katika jimbo hili imewalaza mlango wazi kambi ya upinzani ambao walikuwa na mategemeo makubwa sana ya kuiweka CCM mahali pagumu katika uchaguzi jimbo
hili.
Matarajio ya upinzani ambayo kwa msimamo huu wa Murji utakuwa umeyayeyusha
kabisa, yalitokana na habari ambazo zilikuwa zikivuma mjini hapa kuwa mwana CCM huyo kwa hasira ya kuachwa amekuwa akisaidia upinzani kupitia kambi yake ambayo ilikuwa bado
kuvunjwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii mara baada ya kikao hicho Murji alisema upinzani utakuwa unafanya makosa sana kufikiria kuwa yeye angewasaidia kwa njia yoyote ile kuihujumu CCM katika uchaguzi huu eti kwa sababu ya
kuenguliwa.
Alisema yeye amekulia CCM na kwamba huu siyo mwisho wa uhunzi na kwamba amekubali matokeo na siyo lazima awe
mbunge, kwani uana-CCM wake haukuwa wa mkataba wa kuwa mbunge.
Hata hivyo, Murji aliwashauri wapenzi wa pande mbili hizi yake na ya Sinani kuacha kutambiana kwa kejeli kipindi hiki cha kampeni na badala yake kuungana na kushirikiana ukiwa kitu kimoja ili kuhakikisha CCM inaibuka na ushindi katika ngazi zote hadi
Urais.