Uhuru 06.09.2005

 

Karume asema SMZ kuendelea kujenga barabara za vijijini
Na Khatibu Suleiman, Chake Chake Pemba
RAIS wa Zanzibar Aman Abeid Karume amesema Serikali itaendelea na juhudi zake za ujenzi wa barabara za mjini na vijijini kwa kutumia fedha zake ili kuwaondolea wananchi tatizo la usafiri.
Akifungua barabara yenye urefu wa kilomita 12.8 ya Chokocho hadi Mtuhaliwa, Karume alisema Serikali yake imeonyesha mfano kuwa inaweza kuleta maendeleo bila kutegemea wahisani.
"Tunajigamba kuwa tunaweza kuleta maendeleo bila ya kutegemea wahisani," alisema Karume na kuongeza kuwa maendeleo ya kweli yanaletwa na wananchi wenyewe.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inaandaa mpango wa kumaliza barabara zote za Unguja na Pemba katika kiwango cha lami.
Karume alisema uwezo na nia ipo, hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono SMZ katika mikakati yake hiyo inayokwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Alisema CCM imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utekekezali wa Ilani yake na hivyo wananchi wana kila sababu ya kuwapa ridhaa ya kuongoza dola.
Mapema Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Brigedia Mstaafu Adam Mwakanjuki alisema wizara yake imefanikiwa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM kuhakikisha barabara za Unguja na Pemba hasa zinazokwenda vijijini zinajengwa kwa kiwango cha lami.
Mwakanjuki alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kurahisishia wananchi wa eneo hilo usafiri wao na mazao yao.

Serikali ya CCM imetekeleza miradi kibao Ukerewe
Na Florian Kaiza, Nansio
MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Ukerewe balozi Getrude Mongella, amesema mradi wa umeme kutoka gridi ya taifa kwenda visiwani humo kukamilika mwezi huu.
Balozi Getrude aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu zilizofanyika kijiji cha Hamkoko, kata ya Ngoma.
Alitaja miradi mingine ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali ya CCM kuwa ni pamoja na kuwapatia wananchi kivuko cha MV. Nyerere kinachofanya kazi kati ya kisiwa cha Ukerewe na Ukara.
Mwingine ni barabara iliyojengwa kwa kiwango cha changarawe maalum ya kuchanganywa na lami yenye urefu wa kilomita 5.5 kutoka mjini Nansio hadi kijiji cha Bulamba na hatimaye itafika Murutunguru.
Wakati huo huo, katika mkutano huo aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Mwanza na ambaye alikihama chama hicho na kuteuliwa na CCM kugombea udiwani kata ya Mukituntu, Isack Mungonge, alisema uzoefu wa CCM katika kuongoza harakati za maendeleo ya wananchi bado unahitajika.
Wanachama wapya 80 wa CCM walikabidhiwa kadi na balozi Mongela katika sherehe za uzinduzihuo.

Kuchagua wapinzani ni sawa na kukosea njia
Na Thomas Mtinge
KAMANDA wa Umoja wa Vijana wa CCM, Kata ya 14, Wilayani Temeke Farid Bazar amesema endapo wananchi wataamua kuchagua wagombea wa upinzani upinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao watakuwa wamejifunga kitanzi cha maisha katika kujiletea maendeleo.
Bazar aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanachama wa UVCCM kata hiyo kwa ajili ya kupanga mikakati ya kujiandaa na uchaguzi ujao.
Alisema kambi ya upinzani haijajiimarisha kisera hivyo haina uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi na kuwa wanachofanya ni kujaribu kujua wanakubalika kiasi gani.
Kamanda huyo aliwataka wana-CCM na wananchi kwa ujumla kutofanya makosa katika uchaguzi huo kwa kufanya majaribio ya kuwachagua wapinzani.
" Ilani za vyama zinatofautiana hivyo unapochagua Rais kutoka CCM na kisha ukachagua mbunge kutoka CUF, ujue hapo maendelo yake ni sawa na 'ziro' kwa sababu kila kiongozi atataka kutekeleza ilani yake," alisema Bazar.
Alisema kwa vyovyote, Kikwete atashinda katika uchaguzi ujao na kuwataka wananchi wamchagulie wabunge na madiwani kutoka CCM ili waweze kuchapa kazi na kuzungumza lugha moja ya kuwaletea maendeleo ya haraka.
Wakati huo huo, Bazar amewapongeza vijana hao kwa kuipigania CCM katika uchaguzi uliyopita wa serikali za mitaa na kupata ushindi wa asilimia mia moja katika mitaa yote ya kata hiyo.
Alisema ushindi huo ni kielelezo cha kukubalika kwa sera za CCM hivyo hawana budi kuipigania tena ili ishinde katika Uchaguzi Mkuu ujao.

 

Serikali kuboresha barabara nchini
Na Prosper Kulita, Morogoro
SERIKALI ya Tanzania ipo katika mpango kabambe wa kuziboresha barabara mbalimbali nchini na kuziweka katika kiwango cha lami mpango ambao utatekelezwa na serikali ya CCM ya awamu ya nne.
Mojawapo ya barabara hizo ni ile ya Kilosa kupitia Mziha mpaka Handeni mkoani Tanga ambayo ipo katika wilaya ya Mvomero mkoani morogoro.
Mgombea ubunge wa jimbo la Mvomero aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi kilichopita, Suleiman Sadiq aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM wilayani humo katika viwanja vya soko la Mvomero.

Asema ataimarisha kilimo, ufugaji
Na Prosper Kulita, Morogoro
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Kilosa Kati kupitia CCM, Mustafa Mkulo ameahidi kusaidiana na wananchi kuboresha sekta ya kilimo na mifugo kwa asilimia kubwa katika jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza.
Akiongea katika mkutano wa hadhara katika eneo la Kimamba, Mkulo alisema atahakikisha kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza kuboresha sekta hizo kutokana na umuhimu wake kwa wananchi wa eneo hilo ambao hutegemea kilimo na mifugo.
Alisema kumekuwapo na matatizo mbalimbali katika kilimo, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo za kilimo sambamba na wataalam, hivyo kazi ya kwanza ni kuboeresha mfumo mzima wa kilimo.

 

Mwapachu awafananisha wagombea Urais upinzani na nguo za mitumba
: Asema hawapaswi kuchaguliwa kwani wamechakaa
Na Thobias Mwanakatwe, PST Tanga
MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Tanga Mjini Bakari Mwapachu amesema wagombea urais wa vyama vya upinzani ni sawa na nguo za mitumba ambazo zimevaliwa na kuchakaa kwa sababu vyama hivyo havina utaratibu wa kuchuja wagombea wapya wa urais kila mwaka.
Mwapachu ambaye anatetea nafasi yake katika Jimbo la Tanga alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Mwanzange wakati wa mkutano wa kampeni.
Alisema tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 1992, wagombea urais wa vyama vya upinzani wamekuwa wale wale kiasi kwamba wananchi wamewapachika majina na sasa wanawaita ni nguo za mitumba.
"Tukisema vyama vya upinzani havina mwelekeo ni kweli kabisa, wewe fikiria kila mwaka vinateua wagombea urais wale wale hivi ndiyo kusema kwamba havina wasomi au wanachama wengine wazuri wanaoweza kugombea nafasi hiyo," alihoji Mwapachu na kuwataka wananchi kumchagua mgombea urais wa CCM Jakaya Kikwete kwa kuwa yeye siyo mtumba kama wagombea wengine.
Alisema Ccm ina utaratibu mzuri wa kupata wagombea wake wapya na siyo kila uchaguzi wanakuwa wale wale na kwamba utaratibu huo ndiyo unakifanya kizidi kupendwa na wananchi kwa kuwa hakina ubabaishaji kutokana na kuwa na sera nzuri za kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwapachu alisema mara kadhaa viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani wamekuwa wakibeza serikali ya CCM kwamba haijaleta maendeleo yeyote wakati mambo yaliyofanywa na chama tawala na serikali yake yanaonekana wazi.
Alisema imefika wakati sasa kwa wapinzani kubadilika na kueleza ukweli katika mambo ya maendeleo yaliyofanywa na serikali ya CCM badala ya kuendelea kudai hakuna kitu kilichofanywa kwa lengo la kujenga uhalali kwa wananchi waweze kuwachagua.
Alisema Watanzania nao wanajua na wamekwishaona ni nini serikali ya CCM imekifanya tangu Tanganyika kupata Uhuru hadi sasa, hivyo kudai kwamba hakuna mabadiliko yeyote ya kimaendeleo yaliyofanywa siyo njia mwafaka itakayowashawishi wananchi waweze kuwachagua.
Aliongeza kuwa kila Mtanzania anatambua kuwa serikali ya CCM imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta ya elimu, kilimo, barabara na kwamba mambo mengine yaliyobakia kama utoaji wa ajira kwa vijana yanashughulikiwa kwa nguvu ili kuhakikisha wananchi wengi wanapata ajira.
0000

 

Wapinzani wanataka kuingia bungeni kufanikisha biashara zao

Na Salome Kitomary, PST, Moshi
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Zakia Meghji amewataka wananchi kutodanganywa na wapinzani kuwa watawaletea maendeleo, kwani wanahitaji nafasi wanazowania kwa ajili za kufanikisha biashara zao na si kuwaletea maendeleo wananchi.
Zakia ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na umati mkubwa wa wananchi katika viwanja vya Pasua Sokoni wakati wa uzinduzi wa kampeni na utambulisho wa wagombea wa nafasi mbalimbali katika jimbo la Moshi Mjini.
Alisema kuwa amekaa bungeni kwa muda mrefu, lakini wabunge wengi wa upinzani wamekuwa wakitoroka bungeni na kuendelea na shughuli zao za biashara badala ya kufanya kile walichotumwa na wananchi na badala yake wananchi wanaendelea kuteseka.
Zakia aliwataka wananchi hao kuhakikisha hawafanyi makosa tena ya kuwachagua wapinzani katika nafasi mbalimbali za uongozi, bali waichague CCM ambayo imejizatiti katika nyanja mbalimbali ambazo zimeainishwa katika Ilani yake ya Uchaguzi.
Mjumbe huyo, akimnadi mgombea wa CCM wa jimbo la Moshi Mjini Elizabeth Minde alisema serikali ya CCM imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu, miundombinu na umaskini kwa jumla kupitia Mpango wa Kutokomeza na Kupunguza Umaskini nchini (MKUKUTA).
Akizungumza na wananchi hao, Elizabeth alisema endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha viwanda vyote katika Manispaa ya Moshi vinafufuliwa ili vianze kufanza kazi na kutoa ajira kwa wingi kwa vijana.
“Nitahakikisha nashirikiana na serikali kuwahakikisha viwanda vyote vilivyofungwa vinaanza kufanya kazi ili kutoa ajira kwa vijana na makundi ya pembezoni,” alisema.
Mgombea huyo alisema kuwa uchumi wa mji wa Moshi umeshuka kwa muda mrefu na hiyo imesababishwa na wananchi kuchagua wapinzani, ambao alidai kuwa hawaleti maendeleo, bali wanataka kupitia mgongo wa CCM kujinadi kuwa wamefanya maendeleo.
Elizabeth alisema atahakikisha anaboresha zaidi maisha ya wananchi wa jimbo hilo na kuondokana na umaskini, kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari na pia ataendelea kutetea wanyonge.
"Jamani naombeni kura za ndio, kwani mwaka 2000 nilikuja kwenu mkasema hazitoshi sasa nimerudi tena, achananeni na huyo babu (Philemon Ndesamburo) anayeng'ang'ania bungeni na muda wote mliompa fursa ya kuwaongoza hajafanya lolote,” alisema.
Alisema serikali imekuwa ikikarabati hospitali ya Mawenzi na maendeleo mengine, kwa mfano, ujenzi wa barabara, lakini amekuwa akijinadi katika majukwaa kuwa ametoa misaada mbalimbali katika suala la maendeleo katika manispaa hiyo.
Alisema yeye fani yake ni ya sheria na amekuwa akitetea wanyonge kwa muda mrefu, hivyo ana uwezo mkubwa katika masuala mbalimbali ya kisheria na kazi ya bunge ni kutunga sheria, hivyo apewe nafasi ili ashirikiane na wabunge wengine wa CCM ili kuleta mabadiliko makubwa nchini.
0000

 

Hawa asema atadhibiti mapato jimboni mwake
Na Kennedy Kissula, PST, Mtwara
MGOMBEA ubunge Mtwara vijijini kwa tiketi ya CCM Hawa Ghasia amesema atasimamia vyanzo vya mapato vilivyopo jimboni kwake.
Alitaja baadhi ya vyanzo hivyo kuwa ni mazao ya biashara na mradi wa gesi wa Mnazi Bay unaozalisha umeme, ili wakazi wanufaike na pato litakalopatikana kuweza kuinua uchumi usiokuwa na utegemezi.
Hawa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na PST ofisini kwake ambapo alisema mradi wa gesi wa Mnazi Bay uliopo katika kijiji cha Msimbati, utakuwa unazalisha umeme na kusambazwa katika mikoa jirani na nje ya nchi.
Akizungumzia zao la korosho mgombea huyo alisema: “Unajuwa korosho zinaingiza fedha nyingi za kigeni na mwaka jana lilikuwa la kwanza kuingizia mapato… ni vyema likaimarishwa zaidi na kuongeza mazao mengine ya kibiashara,” alisema.
Mgombea huyo wa CCM alisema katika vipaumbele vyake, atahakikisha jimboni mwake vinafunguliwa viwanda vidogo vidogo vya kubangulia korosho, jambo ambalo litasaidia mkulima kuwa na mahali pa kuuzia na zingine zitaweza kupelekwa nje ya nchi.

Mapuri: Wasilisheni sampuli za vifaa vyenu vinavyokampenia CCM
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi kimewataka wananchi wote wanaofanya biashara ya vifaa vya kampeni ya wagombea Urais wa CCM kuwasilisha sampuli za vifaa hivyo kwenye Ofisi za CCM Makao Makuu Dodoma, Ofisi Kuu Zanzibar au Ofisi Ndogo ya Makao Makuu Dar es Salaam ili viweze kukaguliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuidhinishwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Itikadi na uenezi), Omar Ramadhan Mapuri alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM jijini Dar es Salaam.
Mapuri alisema vifaa vya kampeni vinavyolenga kuwakampenia wabunge au madiwani wa CCM lazima viwasilishwe Ofisi za CCM Mikoa, Wilaya na Kata ili vichunguzwe kwanza na kupelekwa kwenye Ofisi za Tume.
Alisema CCM inatoa taarifa hiyo ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima kwa wafanyabiashara hiyo na kwamba lengo ni kuhakikisha vifaa hivyo havipingani na sheria ya Uchaguzi nchini.
Kwa mara ya kwanza CCM ilitoa taarifa ya aina hiyo Mei 31, mwaka huu ambapo iliwataka watu wote wanaotaka kutengeneza vifaa vya kampeni ya CCM kuwasilisha sampuli zao ili zichunguzwe kuona kama zinakidhi haja matakwa ya sheria ya uchaguzi.
Kufuatia agizo hilo, Mapuri alisema ni wafanyabiashara wachache waliofikisha sampuli zao na kwamba mpaka sasa imegundulika wafanyabiashara wengi wanauza vifaa vya kampeni za CCM bila ya CCM yenyewe kujua jambo ambalo siyo zuri.
“Kwa tangazo hili, napenda kusisitiza kwamba vifaa vya kampeni vinatawaliwa na sheria ya nchi. Ni lazima viwasilishwe Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kupatiwa vibali,” alisema na kuongeza kwamba kwa vifaa vya Kampeni za CCM, mwenye wajibu wa kuwasilisha vifaa hivyo Tume ya Taifa ya Uchafuzi ni CCM yenyewe.
Mapuri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi jana hiyo pia alifafanua zaidi juu ya suala la TOVUTI inayoitwa “www.kikwetesheini.com” kuwa ni ya vijana wawili ndugu.
Aliwataja wamiliki wa Tovuti hiyo kuwa ni Mike Mushi na Richard Mushi wakisaidiwa na baba yao Bill Mushi na kwamba Tovuti hiyo sasa imepata baraka za CCM, lakini maudhui yake siyo ya CCM moja kwa moja.
“Mambo rasmi ya CCM yanapatikana katika Tovuti yake ya “www.ccmtz.org” ambayo wakereketwa hao wameiwekea kiunganishi kwenye tovuti yao,” alisema.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliizuia CHADEMA kutumia mabango ya kampeni ya Urais yenye rangi ya bendera ya Taifa, lakini chama hicho nacho kilidai CCM nayo inatumia rangi ya bendera hiyo kwenye Tovuti yake jambo ambalo CCM ilikanusha tangu wiki iliyopita.
Mapuri alisema vijana hao waliondoa bendera ya Taifa kwenye Tovuti yao kwa vile waliiweka bila kibali cha Wizara yake na kwamba walirekebisha kosa hilo mara baada ya kusikia utaratibu unavyotaka.

 

Karume asema barabara zote Z'bar kujengwa ifikapo 2009
 - Awaomba kura wananchi ili akamilishe kazi hiyo
Na Mwadini Hassan, Pemba
Mgombea wa CCM kwa Urais wa Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume, amewahakikishia Wazanzibari kuwa ifikapo mwaka 2009 barabara zote za Zanzibar zitakuwa zimejengwa.
Rais Karume alitoa ahadi hiyo hapa jana kwenye viwanja vya Gombani ya Kale, wakati wa uzinduzi wa kampeni zake kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu.
Karume ambaye anatetea nafasi yake hiyo katika uchaguzi huo, alisema barabara zote za Unguja na Pemba zitakuwa zimekamilika.
"Mtandao wa barabara utakuwa umekamilika," aliuambia umati wa wana CCM na wananchi waliyohudhuria uzinduzi huo wa kampeni za Zanzibar, ambao walilipuka kwa shangwe na hoi hoi.
Alisema barabara za kilomita 156 Unguja na kilomita 110 za Pemba zitajengwa katika kukamilisha ujenzi huo wa barabara.
Alizitaja barabara zitakazojengwa kwa unguja kuwa ni Mazizini/Fumba, Mfenesini/Bumbwini, Welezo/Dunga, Tunguu/Kinyasini, Makunduchi/Jambiani/Paje, Mkwajuni/Nungwi, Pongwe/Matemwe, Paje/Pingwe, Donge/Mkokotoni.
Pemba barabara zitakazojengwa ni Kengeja/Mtambile, Kenya/Chambani, Mizingani/Wambaa, Tundaua/Pujini, Mtambile/Kangani, Chake Chake/Wete, Wete/Konde, Wete/Gando, Mkoani/Makombeni na Mgagadu/Kiwani.
Alisema mbali ya barabara CCM ikirudishwa madarakani na wananchi kupitia uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, serikali zake zitaendelea kuimarisha elimu ya msingi na sekondari, na kukamilisha kazi ya kuimarisha miundo mbinu.
Rais Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliwataka Wazanzibari kuendelea kuichaguzi CCM iongoze dola pamoja wagombea wake wote wa urais, ubunge, uwakilishi na madiwani.
Alisema wananchi wasibahatishe katika kuchaguzi rais kwa sababu urais ni kushika maisha ya wananchi wote, hivyo kumkabidhi kiongozi asiye na uhakika nafasi hiyo ni kuyaweka rehani maisha ya wananchi.
Aliwataka Wazanzibari kuchagua viongozi wenye imani wa nchi na wananchi wake ili nchi ipate mafanikio na kupiga hatua ya maendeleo.
Uzinduzi huo wa kampeni pia ulihudhuriwa na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi wa Muungano na wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, ambao wote walipowasalimia wana CCM na wananchi kwenye mkutano huo waliwaomba kumpa kura zote Rais Amani Abeid Karume, ili akamilishe kazi ya kuleta maendeleo aliyoianza mwaka 2000.
Kivutio kikubwa kilikuwa Rais mstaafu Mwinyi ambaye alisema mwaka 2000 alipokuja Pemba kumnadi kwa mara ya kwanza Rais Karume, aliwaambia wananchi kuwa ameleta mwari.
"Napenda safari hii kuwaambieni kuwa yule mwari wetu amekua, sasa amekuwa kungwi. Hakuniaibisha," alisema huku akishangiliwa na kuwataka wananchi wamuongeze kipindi kingine cha miaka mitano akamilishe kazi ya kuleta maendeleo.
Alinukuu usemi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati wa vita vya pili vya dunia, Hayati Winston Churchill, ambaye aliwaambia Waingereza wakati wa vita hivyo wampe vifaa ili akamilishe kazi ya kupambana na Wajerumani.
"Nami nanukuu maneno ya kiongozi wa Uingereza, Churchill, tupeni vifaa tukamilishe kazi. Vifaa ni kura zenu zote ziende kwa Amani Karume akamilishe kazi," alifafanua Mzee Mwinyi.

Rais Mkapa: Ahadi za upinzani ni miujiza

Na Mwadini Hassan, Pemba
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Rais Benjamin Mkapa, amesema vyama vya upinzani nchini havichaguliki kutokana na kuwahadaa wananchi kwa ahadi za miujiza.
“Wapinzani wanaahidi kutoa dawa bure, lakini hawaelezi watazitoa wapi, wanasema watajenga barabara nchi nzima, lakini hawaelezi kilomita moja inagharimu kiasi gani na fedha watazipata wapi,” alisema Rais Mkapa jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwa mgombea urais wa Zanzibar.
Alisema Watanzania wasifanye makosa kuchagua wapinzani kuongoza nchi kwa sababu ni mabingwa tu wa kulalamika na kulaumu. Hawana sera mbadala zitakazobadilisha maisha ya Watanzania na nchi yao.
Uzinduzi huo wa kampeni ulifanyika kwenye uwanja wa Gombani ya Kale, nje kidogo ya mji wa Chake Chake na ulihudhuriwa na maelfu ya wana CCM na wananchi.
Alisema vyama vya upinzani vinawapa Watanzania ahadi za miujiza zisizotekelezeka na kuwataka wananchi kuichagua CCM na serikali zake kwa sababu zimeshaonyesha uwezo na mafanikio katika kuleta maendeleo ya nchi.
Rais Mkapa ambaye alipanda jukwaani huku akicheza kufuatia muziki uliyopigwa na bendi ya Chipukizi wa CCM na kuwa kivutio kikubwa, alisema CCM ina sababu za kuchaguliwa kwa sababu ndiyo muasisi wa Mapinduzi, muhimili mkubwa wa Muungano, na inayoongoza maendeleo ya taifa na watu wake.
“Wazanzibari msicheze karata katika kuchagua viongozi wa nchi, chagua CCM iendelee kuongoza,” alisisitiza.
Aliwakumbusha Watanzania kuwa wako watu wanaodhani ukifanyika uchaguzi mabadiliko ni lazima, na mabadiliko kwao maana yake ni kuondosha chama na serikali iliyopo madarakani.
“Hiyo ni dhana potofu. Tanzania hakuna haja ya kufanya mabadiliko ya serikali. Hiyo ndio rai yangu,” alieleza Mwenyekiti wa CCM, Rais Mkapa huku akishangiliwa na umati uliohudhuria mkutano huo uliyonakishiwa kwa rangi za kijani na njano kutokana na kanga, fulana, kofia, na skafu. Rangi hizo ndizo rangi rasmi za CCM.
Alisema wapinzani wamekuwa wakiwahadaa Watanzania kuwa mabadiliko ndiyo maendeleo, ‘ni waongo wakubwa’.
“Watakuja wahisani na waangalizi ambao watasema bila kuiondoa CCM madarakani hakutakuwa na mabadiliko. Ni waongo na wababaishaji wakubwa,” alisema Rais Mkapa na kusisitiza kauli yake kuwa Watanzania wasikabidhi uongozi wa nchi kwa mtu wasiye na uhakika naye.
Alisema Tanzania hakuna mbadala wa CCM anayefaa kukabidhiwa nchi, kwa sababu CCM ina ilani na sera za wazi, za ukweli ambazo zinafafanua kwa wananchi ilichofanya katika kipindi kinachomalizika na kueleza malengo kwa kipindi kijacho na yatatekelezwa vipi.
Mwenyekiti alisema maendeleo ya nchi yanatokana na juhudi za wananchi wenyewe kwanza, ndipo wahisani wanapovutika na kujitokeza kusaidia juhudi hizo.
Alisema wapo wapinzani wanaodai kuwa kuendelea kuichagua CCM wananchi wanajitafutia balaa, na kueleza kuwa watakuwa wanafanya makosa makubwa ikiwa watawachagua wapinzani kwa misingi ya hadaa zao wanazozieleza katika kampeni zao na kuziamini ni ‘kujitafutia balaa zaidi’.
Aliwataka wananchi kuendelea kuichagua CCM na wagombea wake wote wa urais wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar, wabunge na madiwani ili Chama cha Mapinduzi kiendelee kukamilisha kazi ya kuleta maendeleo nchini ambayo imeshaianza.
Katika mkutano huo Rais Mkapa aliwapokea wanachama wapya wa CCM 600 waliyojiunga na chama.

Kuchagua chama tofauti Z’bar ni kuweka rehani Muungano - Kikwete
- Abainisha iwapo Wazanzibari wanapenda Muungano waipende CCM
Na Mwadini Hassan, Pemba
MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, amesema kuchagua vyama tofauti kuongoza serikali za Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar ni kuuweka rehani Muungano.
Alitoa kauli hiyo jana uwanja wa Gombani ya Kale, Chake Chake hapa, alipohutubia mkutano wa kuzindua kampeni za urais wa Zanzibar, jana.
Alisema ana rai za kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao alisema zipo kasoro ndogo ndogo zinazoukabili zinazoweza kurekebishwa ili kuuboresha, lakini ili kufanya hivyo ni lazima pawepo maridhiano kati ya serikali zote mbili.
“Lakini kama wananchi watachagua serikali za vyama tofauti kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano sioni maridhiano kati ya CCM na CUF,” alifafanua.
Alisema kuchagua vyama tofauti kuongoza serikali mbili tofauti nchini Tanzania ni kuuweka shakani Muungano.
Aliuambia umati uliyohudhuria uzinduzi huo wa kampeni za urais wa Zanzibar, Mtanzania yeyote anayeupenda Muungano, aipende na kuichagua CCM kuongoza serikali zote mbili, kwani ni CCM iliyoasisi Muungano kupitia vyama vya ASP na TANU na ndicho chenye uwezo wa kuulinda na kuudumisha.
Kikwete alisema karibu vyama vyote vya upinzani haviyazungumzii Mapinduzi ya Zanzibar katika ‘vitabu’ vyao (Ilani), na kusisitiza kuwa hiyo peke yake inaonyesha namna gani vyama hivyo visivyoyajali Mapinduzi yaliyowakomboa wanyonge wa Zanzibar.
Aliwataka wananchi kutofanya makosa ya kukabidhi ‘unahodha’ wa nchi kwa mtu wasiye na uhakika naye ila wafanya hivyo kwa kumkabidhi nchi nahodha makini na mwenye uhakika ambaye ni Rais Amani Abeid Karume.

 

Tume ya Uchaguzi yatupilia mbali rufani ya Kasaka
Na Mwandishi Wetu
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetupilia mbali rufani ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Lupa, Njelu Kasaka (CCM), kutaka aidhinishwe kuwania kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya CUF.
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Lewis Makame, alisema jana maamuzi hayo ni kwa mujibu wa kikao cha Kamati ya Maadili ya Tume, ambacho kimeridhia uamuzi wa msimamizi wa jimbo hilo, kumzuia Kasaka kugombea.
“Kwa maana hiyo, Kasaka si mgombea tena wa ubunge,” alisema Jaji Makame huku akibainisha kuwa kikao hicho cha kamati ya maadili, kilikuwa chini ya mwenyekiti ni Omar Makungu, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa NEC.
Baada ya kutumikia ubunge kwa vipindi vingi, mwaka huu alienguliwa katika kura ya maoni za CCM na baadaye katika dakika za mwisho aliibukia CUF kutetea nafasi yake. CCM ilimuwekea pingamizi na vikao vya NEC jimboni viliridhia hoja zake.
Hata hivyo, Jaji Makame alikataa kufafanua juu ya vigezo vilivyotumika kufikia maamuzi hayo akisema: “Kesho (leo) kutakuwa na mkutano wa waandishi wa habari na Mkurugenzi (Rajabu Kiravu) atawafafanulia yote hayo.”
Rufani hiyo kwa mujibu wa Jaji Makame ni kati ya rufani 180 za udiwani na ubunge zilizosikilizwa na NEC. Kati ya hizo, 65 ni za ubunge na 115 za madiwani kote nchini, ambazo Kiravu ambaye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi anatarajiwa kuzitolea ufafanuzi leo.
Maamuzi ya awali ya vikao vya Tume jimboni Lupa, yaliridhia hoja kuwa mgombea huyo aliyewasilisha fomu zikiwa zimebaki dakika 36 muda husika uishe kuwa hakufuata taratibu kama inavyotakiwa na sheria za uchaguzi.
Alipotakiwa kufafanua ni kwa nini imechukua muda mrefu maamuzi hayo kufanyika, Jaji Makame alisema: “Pamoja na watu wengine kusema tunachelewa, tumekuwa tukifanya kazi kutwa nzima, siku nyingine hadi saa moja usiku, Jumapili na Jumamosi tuko ofisini.”
Wakati huo huo, jana wawakilishi wa walemavu walikuwa na kikaa kirefu na Mkurugenzi wa NEC, Kiravu, katika kupitia vifaa vya kupigia kura vitakavyotumiwa na wahusika hao, hasa wasioona.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walemavu (CHAWATA) Palema Rwejahura, alisema kazi hiyo ilifanywa kwa kuchambuzi vifaa vya mfano kama vinafaa na hatua itakayofuata ni kurudishia kwa mtengenezaji.
Rwejahura alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na visanduku na makaratasi maalum ya kupigia kura kwa matumizi ya walemavu kama itakavyokubalika na pande hizo mbili. Hadi jana alasiri kikao hicho kilikuwa kinaendelea.
“Kwenye mwezi Oktoba mwanzoni, watakuja walemavu na kufanyia mazoezi vifaa hivyo kama vinafaa,” aliyetimisha Rwejahura.

 

Kikwete aiteka Njombe
BAADA kumaliza ziara ya kampeni katika mkoa wa Ruvuma, mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete aliendelea na ziara yake mkoani Mbeya. Kabla ya kuingia mkoani humo, alipita wilaya ya Njombe mkoani Iringa ambako alipokewa kwa aina yake kama anavyosimulia Mwandishi Wetu EPSON LUHWAGO aliyekuwa katika ziara hiyo kwa mikoa ya kusini na Nyanda
MIKUTANO ya kampeni za mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa wilaya ya Njombe mkoani Iringa, ilitia fora kiasi cha kuwachanganya hata wapinzani.
Kikwete alifanya ziara katika wilaya hiyo alipokuwa akipita kwenda Mbeya kwa ajili ya kampeni kuomba wananchi wamchague kuwa Rais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.
MAPOKEZI MAKUBWA
Mgombea urais wa CCM alipokewa na viongozi wa mkoa wa Iringa kutoka kwa viongozi wa Chama mkoa wa Ruvuma saa 5.10 katika eneo la Kifanya.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Tasil Mgoda, alipokea jahazi la msafara wa Kikwete kutoka kwa Cornel Msuwa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma.
Viongozi waliokuwepo katika mapokezi hayo ni Katibu wa Mkoa Constantine Malyagili, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Anne Makinda ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kusini na wenyeviti na makatibu wote wa CCM wilaya za Iringa.
Wengine ni Wabunge Jackson Makwetta (Njombe Kaskazini), Thomas Nyimbo (Njombe Magharibi), William Lukuvi (Ismani), Monica Mbega (Iringa Mjini) na wagombea Ubunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla na Stanley Kevella wa Njombe Magharibi.
Alivalishwa skafu na vijana wa chipukizi wa wilaya ya Njombe na hatimaye kupita kwenye njia iliyopambwa kwa majani ya miti ya 'cyprus' yaliyokoleza kijani na kufanya alama halisi ya CCM.
Wakati wa mapokezi hayo, mgombea urais alipokewa kwa burudani za aina mbalimbali za kwaya na ngoma huku mabango yenye ujumbe mbalimbali yakipambiza.
Baadhi ya mabango hayo yalisomeka 'SACCOS KIFANYA
MKOMBOZI WA WANYONGE', 'WANAWAKE NA MAENDELEO', na
'SERA YA CHAMA NI KUONDOA UMASKINI.'
Baada ya mapokezi hayo, Kikwete alikwenda katika viwanja vya makao makuu ya tarafa ya Kifanya ambako alifanya mkutano wa hadhara.
Kwenye mkutano wa hadhara, alisifu mapokezi na kuwaomba wananchi waliofika kuichagua CCM katika nafasi zote zinazogombewa- urais, ubunge na udiwani.
Aliwataka Watanzania kutokuchezewa amani iliyopo nchini ambayo imedumu kwa muda mrefu.
"Amani na utulivu tulio nao ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya nchi. Ni rahisi sana kuiondosha lakini ni gharama kubwa saba kuirejesha na pindi itakapotoweka itasababisha nchi kutumba.
"Viongozi wetu waliotangulia walibaini umuhimu wa amani na sisi tunaendelea kuidumisha, hivyo tusiichezee kwani itasababisha maafa kwetu," alisema.
Kiongozi huyo aliendelea kuwahamasisha wananchi kwamba waichague CCM ili iweze kuendeleza mema yote iliyoyafanya na kuanza harakati endelevu za kukuza uchumi wa nchi, kilimo kikiwa ajenda namba moja.
NJOMBE YACHANUA
Baada ya kuhutubia mkutano wa Kifanya, safari ya kwenda Njombe Mjini ilianza huku kukiwa na magari 44, pikipiki na baiskeli za 'kumwaga'.
Alipoingia Njombe mjini alishangazwa na umati wa watu uliokuwa umejipanga kuanzia uwanja wa ndege hadi ofisi za CCM Wilaya.
Umati huo uliashiria kwamba Njombe kumekucha tayari kwa mapokezi ya kiongozi huyo ambaye amekuwa akivuta hisia za watu tangu kuanza kwa mchakato wa kuwania urais ndani ya Chama na kampeni zenyewe.
Wingi wa watu waliojipanga ilikuwa sawa na rasharasha kwani alipofika uwanja wa Sabasaba alikofanya mkutano mkubwa wa hadhara wa kampeni, aliduwaa zaidi baada ya kukuta uwanja umefurika.
Katika mkutano huo Kikwete alizidi kumwaga sera zenye matumaini kwa kila rika la watu waliofika kwa kuashiria kwamba kuichagua CCM ni kuendelea kutoa matumaini ya maisha bora kwa wananchi wote.
Alimaliza mkutano huo kwa kuwanadi wagombea ubunge wote wa majimbo matatu ya Njombe ambayo ni Njombe Kusini, Njombe Magharibi na Njombe Kaskazini pamoja na wagombea udiwani.
Kikwete, katika kuwanadi wagombea hao, alisema kuwachagua viongozi wa ngazi hizo pamoja na Rais kutoka CCM kutahitimisha staili ya mafiga matatu.
"Kuchagua kwa mithili ya mafiga haya matatu ni kukamilisha kazi muhimu ya kuunda timu ya maendeleo ya wananchi. Ukiweka kitu kingine hapa katikati unatia giza," alisema.
KIKWAZO MTWANGO
Baada ya mkutano huo, mgombea na msafara wake waliendelea kuambaa katika barabara ya Songea Makambako na hatimaye kukutana na 'msitu wa watu' katika mji mdogo wa Mtwango.
Watu waliofurika mahali hapo, walizuia msafara kwa kukatisha barabara jambo lililomfanya mgombea kusimama na kuwahutubia kwa takriban dakika sita.
Mkusanyiko huo wa watu ulisababisha baadhi yao kusukumana kwa minajili ya kumwona mgombea. Baadhi yao, katika kutimiza azma hiyo, walisimama kwenye mapaa ya nyumba na juu ya miti pamoja na kwenye magari.
"Baada ya kuwaeleza haya ndugu zangu, naomba mturuhusu tupite kwani wenzenu wa Makambako wanasubiri," alisema na wananchi kumwitikia: "sawa".
MAKAMBAKO YAPAGAWA
Kikwete alikutana na umati mkubwa katika mji wa Makambako ambao dhahiri ulizidi umati wa Songea Mjini kwenye uwanja wa Majimaji, siku iliyopita.
"Haijapata kutokea," yalikuwa maneno ya Kikwete kushangaa umati wa watu uliokuwa umefurika kwenye viwanja vya polisi Makambako.
Licha ya umati huo, watu walijitokeza kwa wingi na kujipanga barabarani kumpokea kwa umbali takriban
kilomita tatu kutoka uwanjani hapo.
Kama kawaida alimwaga sera maridhawa za kuomba wananchi kuichagua CCM ili iendelee kuongoza na kuleta maendeleo yaliyopatikana katika serikali za awamu zote tatu zilizopita.
Suala la ajira kwa vijana liliteka umati huo, hali iliyoonyesha kwamba neema kwa vijana imewadia na hivyo kuondokana na umaskini na ukosefu wa ajira ambao
Kikwete mwenyewe amekuwa akifananisha na bomu la kutega ambalo linaweza kulipuka wakati wowote.
Pamoja na shamrashamra za mkutano huo, Mbunge wa Njombe Kaskazini na mwanasiasa mkongwe, Jackson
Makwetta alipata wakati mgumu baada ya baadhi ya wananchi kumkataa waziwazi kuwa hawamtaki.
Wananchi hao walisema wameridhika na maendeleo yaliyopatikana wakati wa uongozi wake kwa miaka 30 lakini walisema amechoka, wanahitaji mtu mwingine.
Wananchi hao walimkataa waziwazi hata kiongozi wa msafara wa Kikwete kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Mkoa wa Ruvuma, Abdulrahman Kinana aliposimama na kumnadi.
Hata Makwetta mwenyewe alishindwa kuzungumza baada ya kutakiwa awasalimie wananchi. Aliishia kusema: "Nashukuru sana".
Hali hiyo iliashiria wazi kwamba inatakiwa kazi ya ziada kwa Chama kuhakikisha mkongwe huyo anapita katika uchaguzi. Si hivyo tu, bali kulinusuru jimbo kuchukuliwa na upinzani.
Kikwete aliendelea na safari hiyo kwa kuhutubia mkutano mwingine kwenye mji mdogo wa Wanging'ombe jimbo la Njombe Magharibi kwa kumnadi Stanley Kevella anayegombea ubunge jimbo hilo.
Mkutano huo wa Wanging'ombe ulikuwa wa mwisho kwa wilaya ya Njombe kabla ya kwenda Mkoani Mbeya ambako aliendelea na mikutano ya namna hiyo.
Pamoja na kuonyesha upinzani kwa Makwetta, baadhi ya viongozi wa CCM mkoa akiwemo Mwenyekiti Tasil Mgoda walieleza kuwa Iringa itaibuka kwa ushindi wa kishindo na hata kuwashangaza watu wanaodhani kuna upinzani.
"Hizi tunazichukulia kama changamoto kukaza uzi kuelekea ushindi. Lakini kelele hizi hazitutishi sana kwani waliofanya vile ni vijana wa hapa Makambako tu, kwingine mambo shwari kabisa," alisema Mgoda.