UHURU 07.09.2005
KIKWETE AITINGISHA MORO NA KUSEMA:CCM ndiyo mjenzi wa amani na utulivu
Kampeni zazidi kupamba moto, picha ya ushindi kwa CCM yazidi kung’ara
KIKWETE
AITINGISHA MORO NA KUSEMA:CCM ndiyo mjenzi wa amani na utulivu
Ndio
maana nchi imeendelea kuwa imara kwa awamu zote
Na
Bashir Nkoromo, Morogoro
CHAMA
Cha Mapinduzi kinajua kipi kinachojenga amani na utulivu, na ndiyo sababu nchi
imeendelea kuwa tulivu chini ya uongozi wake wa awamu zote.
Hayo yalisemwa jana mjini hapa na mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya
Kikwete katika mkutano wake mkubwa wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa
Jamhuri.
Alisema, kutokana na sababu hiyo, Watanzania hawana budi kuipa kura CCM ili
iendeleze kazi ya kujenga na kuimarisha amani na utulivu ambao alisema ndio
msingi wa kila kitu.
"Pasipo na amani hakuna chochote kinachoweza kufanyika. Hakuna maendeleo
yoyote yanayoweza
kufikiwa hata viongozi wakiwa mahodari kiasi gani kwa kuwa wananchi muda wote
wapo mguu nje mguu ndani
wakihofia usalama wao," alisema Kikwete huku akishangiliwa na umati wa
wananchi waliofurika katika
uwanja huo.
Alisema, CCM imeweza kujenga amani kwa sababu ya sera zake bora ikiwemo
kutoruhusu jamii kubaguana kwa misingi ya
rangi, kabila, utaifa, dini au jinsia.
Kikwete aliwasihi wananchi kuipa kura CCM na kumwezesha yeye kuwa rais wa nchi
kwa kuwa watakuwa na
uhakika wa nchi kupiga hatua ikiwa katika hali ya amani na utulivu badala ya
kuwachagua wapinzani.
Aliwatahadharisha wananchi kwamba viongozi wa vyama vya upinzani wapo tayari
kutumia ubaguzi wa kidini katika maeneo walikotoka ili mradi wapate uongozi,
hali ambayo alisema ni hatari kwa kuwa daraja hilo linalotumiwa na vyama ni
mauti ya binadamu.
Kuhusu elimu, Kikwete alisema, baada ya awamu ya tatu kuwezesha elimu nchini
kupiga hatua, hasa chini ya mpango wa MMEM, awamu yake itahakikisha walimu
wanaongezeka na kupatiwa nyumba katika maeneo ya shule.
Alisema pia kwamba azma ya serikali ya awamu ya nne katika nyanja ya elimu ni
kuboresha elimu ya sekondari na ya juu kwa kuwa eneo hilo ndio lenye mchango
mkubwa katika kutoa wataalamu wa nchi.
Kuhusu vijana, Kikwete alisema uongozi utahakikisha unawapatia ajira ile ya
ujira, na si kutegemea tu ya kuajiriwa serikalini, na kufafanua kwamba njia
mojawapo ni kuongeza vitega uchumi na wawekezaji nchini.
Aidha, alisema vijana watawezeshwa kupata mitaji kwa njia ya mikopo nafuu
kupitia utaratibu maalum, hasa ule wa kuzifanya rasilimali za wananchi wa hali
ya chini kuweza kuwa dhamana ya kuwapatia mikopo katika mabenki.
Kuhusu kinamama, mgombea huyo wa nafasi ya urais
alisema watawezeshwa kwa kupatiwa uwezo wa kuanzisha na kumiliki miradi
badala ya wengi wao kutegemea wanaume ambao baada ya fedha kupatikana ndio mara
nyingi huwa kipaumbele kupanga matumizi.
Kadhalika, Kikwete alisema serikali itahakikisha inatoa kipaumbele kwa watu
wenye ulemavu kama ilivyokuwa zamani kwa kuwawezesha na kuwa katika mazingira
bora ya kuweza kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea misaada kila wakati wote.
Akihitimisha hotuba yake, Kikwete pia alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea wa
udiwani na mbunge wa Morogoro Mjini na kuwataka wananchi wawape kura ili
kukamilisha utaratibu wake wa 'mafiga matatu'.
Mapema Kikwete alipokea wanachama wapya 300 kutoka
jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na wengine
zaidi ya 200 kutoka vyama mbalimbali vya upinzani.
Naye Aidan Libenanga anaripoti kuwa, mgombea
wa Urais kupitia CCM Jakaya Kikwete aliwasili jana mjini hapa na kulakiwa
na umati mkubwa wa watu waliofurika uwanja wa Jamhuri ili kumuona na kusikiliza
nasaha zake.
Idadi kubwa ya watu walijitokeza wakiwemo
wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi ambao ni dhahiri walitelekeza shughuli
zao na kufika eneo la mapokezi na mkutano wakiwa wamevalia fulana na mashati
yenye rangi ya kijani ambayo ni ya CCM.
Akihutubia umati huo kwenye uwanja wa Jamhuri uliofurika kuliko hata wakati wa
pambano la Yanga na Simba lililochezwa hivi karibuni mjini hapa, Kikwete
aliwasihi wakazi wa mkoa huo kumchangua yeye kwa tiketi ya CCM pamoja na wabunge
na madiwani wote wa CCM.
Wananchi Moshi Mjini waaswa kutodanganywa tena na upinzani
Zakia asema wapinzani wanaingia bungeni kufanikisha
biashara zao
Na Salome Kitomary, PST, Moshi
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Zakia Meghji amewataka wananchi
kutodanganywa na wapinzani kuwa watawaletea maendeleo, kwani wanawania nafasi
hizo kufanikisha biashara zao na si kuwaletea maendeleo wananchi.
Zakia ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema hayo mwishoni mwa
wiki wakati akizungumza na umati mkubwa wa wananchi katika viwanja vya Pasua
Sokoni, wakati wa uzinduzi wa kampeni na utambulisho wa wagombea wa nafasi
mbalimbali katika jimbo la Moshi Mjini.
Alisema kuwa amekaa bungeni kwa muda mrefu, lakini wabunge wengi wa upinzani
wamekuwa wakitoroka bungeni na kuendelea na shughuli zao za biashara badala ya
yale waliyotumwa na wananchi, huku wananchi wakiendelea kuteseka.
Zakia aliwataka wananchi hao kuhakikisha hawafanyi makosa tena kwa kuchagua
wapinzani katika nafasi mbalimbali za uongozi, bali CCM ambayo imejizatiti
katika nyanja mbalimbali zilizoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi.
Mjumbe huyo, akimnadi mgombea wa CCM wa jimbo hilo, Elizabeth Minde alisema
serikali ya CCM imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu, miundo mbinu na
kutokomeza umaskini kupitia Mpango wa Kutokomeza na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA).
Akizungumza na wananchi hao, Elizabeth alisema endapo atachaguliwa kuwa mbunge
wa jimbo hilo atahakikisha viwanda vyote katika Manispaa ya Moshi vinafufuliwa
ili vifanye kazi na kutoa ajira kwa vijana.
Alisema uchumi wa wananchi wa Moshi umeshuka, hali iliyosababishwa na wapinzania
kutokuwa na mikakati ya kuwaendeleza wananchi, ambao alidai kuwa wamekuwa
wakipitia mgongo wa CCM kujinadi kuwa wameleta maendeleo.
Elizabeth alisema atahakikisha anaboresha zaidi maisha ya wananchi wa jimbo hilo
ili waondokane na hali ya umaskini, pamoja na kuhakikisha kila kata inakuwa na
shule ya sekondari.
“Jamani naombeni kura za ndio, kwani mwaka 2000 nilikuja kwenu mkasema
hazitoshi sasa nimerudi tena, achananeni na huyo babu mwenye miaka 70
anayeng’ang’ania bungeni wakati kipindi chote mlichompa fursa ya kuwaongoza
hajafanya lolote,” alisema.
Alisema serikali imekuwa ikikarabati hospitali ya Mawenzi na maendeleo mengine,
kwa mfano, ujenzi wa barabara, lakini mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo
amekuwa akijinadi kupitia majukwa kuwa ni yeye aliyetoa misaada ya maendeleo.
Hawa aahidi kusimamia vyanzo vyote vya mapato
Na Kennedy Kissula, PST, Mtwara
MGOMBEA ubunge Mtwara Vijijini kwa tiketi ya CCM Hawa Ghasia amesema atasimamia
kwa nguvu zote vyanzo vya mapato jimboni humo ili viweze kumnufaisha wananchi.
Alitaja baadhi ya vyanzo hivyo kuwa ni mazao ya biashara na mradi wa gesi wa
Mnazi Bay unaozalisha umeme, ili wakazi wanufaike na pato litakalopatikana
kuweza kuinua uchumi.
Hawa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na PST ofisini kwake ambapo alisema
mradi wa gesi wa Mnazi Bay uliopo katika kijiji cha Msimbati, utakuwa unazalisha
umeme, na kusambazwa katika mikoa jirani na nje ya nchi.
Akizungumzia korosho mgombea huyo alisema zao la korosho ambalo linalimwa kwa
kiasi kikubwa mkoani humo linaingiza fedha nyingi za kigeni na mwaka jana
lilikuwa la kwanza kuingizia mapato, hivyo ni vyema likaimarishwa zaidi.
Alisema atafanya juhudi kubwa kuhakikisha fedha zinazotokana na mauzo ya yao
hilo zinawanufaisha wakulima wa jimbo lake, sambamba na mkakati wa kuongeza
mazao mengine ya kibiashara.
Mgombea huyo wa CCM alisema mkakati wake wa kwanza ni kuhakikisha viwanda vidogo
vidogo vya kubangulia korosho vinafunguliwa, jambo ambalo litamsaidia mkulima
kuwa na mahali pa kuuzia korosho zake.
NEC yakubali rufani 12 na kutupa 168
Na Mwandishi
Wetu
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekubali jumla ya rufani 12 na kutupilia mbali
168 zilizowasilishwa na vikao vya chini, majimboni kuhusu uhalali wa wagombea
ubunge na udiwani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajabu Kiravu, aliwaambia waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, kuwa jumla ya rufani 180 ziliwasilishwa na zilizokubaliwa
ni sita za madiwani na wabunge.
Kwa mujibu wa Kiravu, sheria ya uchaguzi inawapa fursa wasioridhika
na maamuzi hayo kwenda mahakamani kutafuta haki zaidi, lakini ni baada ya
uchaguzi kufanyika Oktoba 30 mwaka
huu.
Alisema katika kikao chake cha Septemba 2, mwaka huu, Tume ilimvua madaraka
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Anthony Kalwani, wa kata moja iliyoko wilayani
Magu kwa kukiuka maadili ya kazi yake.
Kiravu, alisema uamuzi huo unatokana na kitendo cha msimamizi huyo kumdhamini
mgombea ubunge jimbo la Magu, Dk Festus Limbu (CCM). Nafasi ya Kalwani sasa
inachukuliwa na Jackson Nsabo.
Alisema, hata hivyo uamuzi huo hautaathiri uteuzi wa mgombea kwa kuwa alikuwa na
wadhamini wa ziada kulinganisha na idadi inayotakiwa.
Kwa mujibu wa NEC, majimbo ya ubunge yenye rufani zilizokubaliwa, wahusika,
pamoja na vyama vyao na maamuzi ya Tume katika mabano ni Sengo Kayalla wa Kahama
(mgombea-Chadema); Opulukwa Jeremiah wa jimbo la Meatu (mgombea- UDP); na Aboud
Mjuba wa jimbo Nkenge (Sio mgombea- CUF).
Wengine ni Martha Alfred wa Arusha Mjini (Mgombea- NLD); Kilango Robinson wa
Handeni (mgombea -Chausta), Makanyaga Simbili wa jimbo la Tunduru (mgombea
NCCR-Mageuzi) Mkama Mtaka Mkama wa Mwibara (mgombea - Chadema).
Kwa upande wa madiwani ni kutoka kata za halmashauri za manispaa za Ilala, kata
ya Kisutu (CUF) na Musoma katika kata ya Mwigombero (CUF).
Nyingine ni ya miji ya Ulanga katika kata ya Isongo (CCM),
Mahuta-Tandahimba (CUF), Mandwanga-Lindi (CCM) na Mchombe iliyoko
Kilombero (Chadema).
Kiravu alitaja sababu zilizokuwemo katika rufaa hizo, ni uraia wa wagombea,
kutodhaminiwa na wapiga kura walioandikishwa katika jimbo husika au kata,
kuchelewesha au kutowasilisha fomu na kutojaza fomu ipasavyo.
Sababu nyingine kwa mujibu taarifa hiyo ya Tume ya Uchaguzi, ni mgombea
kutokudhaminiwa na chama kilichosajiliwa au kutokuwa mkazi wa halmashauri husika.
CCM yaanza kampeni zake Unguja leo
L Ni baada ya kuzindua Pemba juzi kwa mafanikio
BAADA ya kuzindua kampeni zake kwa mafanikio makubwa kisiwani Pemba juzi, Chama
cha Mapinduzi leo kinaanza mikutano yake ya kampeni Unguja kwa mkutano mkubwa wa
aina yake utakaofanyika kiwanja cha Kibandamaiti mjini hapa.
Mkutano huo wa kwanza wa kampeni za mgombea urais wa Zanzibar, Amani Abeid
Karume, mjini hapa, utawapa nafasi wana CCM na wananchi wa Unguja kumsikiliza
mgombea huyo akiomba kura aendelee kutetea nafasi yake ya urais katika uchaguzi
mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu.
Karume katika mkutano huo atapewa ‘tafu’ na mgombea mwenza wa mgombea urais
wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Ali Mohammed Sheni, ambaye atamsaidia kuomba kura
kutoka kwa Wazanzibari kwenye uchaguzi huo.
Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar, katika mkutano huo unaotarajiwa kuwa na
mahudhurio makubwa kama wa uzinduzi wa kampeni huko Pemba juzi, atainadi Ilani
ya CCM ya mwaka 2005 hadi 2010, inayowaeleza wananchi nini CCM itafanya ikiwa
watairejesha kuongoza nchi katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa mambo ambayo ilani hiyo inawaahidi Wazanzibari ni kuimarisha
miundombinu, hasa ya barabara katika visiwa vya Unguja na Pemba, ili kuwawezesha
wananchi kuendesha shughuli zao za kilimo na kiuchumi kwa ufanisi mkubwa na kwa
kufanya hivyo kuondokana na umasikini.
Aidha, inasema kuwa katika miaka mitano ijayo itaendelea kuulinda Muungano wa
Tanzania na kulinda Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyowaondoa Wazanzibari katika
lindi la utumwa na madhila ya utawala wa kisultani.
Mkutano wa leo unafanyika kukiwa na kumbukumbu ya mafanikio makubwa ya mkutano
wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu uliyofanyika juzi kwenye
uwanja wa Gombani ya Kale, Chake Chake kisiwani Pemba, mkutano ambao
ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin Mkapa, mgombea urais wa
Muungano, Jakaya Kikwete.
Wengine ni mgombea mwenza Dk. Ali Mohammed Sheni, Mwenyekiti wa CCM mstaafu na
Rais mstaafu wa Muungano, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk.
Salmin Amour na waziri kiongozi mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Elizabeth Minde ahamasisha wananchi
wamchague yeye
Na Rodrick Makundi, Moshi
MGOMBEA ubunge wa Moshi Mjini, Elizaberth Minde (CCM), ameomba wanachama
waliompigia kura katika
uchaguzi wa mwaka 2000, kuhamasisha wanachama wengine zaidi kuipigia kura CCM
ili kufikia lengo la kupata
ushindi katika jimbo hilo kwenye uchaguzi wa Oktoba 30, mwaka huu.
Akiwahutubia wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kampeni za CCM jimbo la Moshi
Mjini juzi, Elizabeth alisema katika uchaguzi uliopita alifanikiwa kupata kura
l5,000 ambapo, pamoja na kushindwa alipata fursa ya kuweza kujikita zaidi katika
siasa na kutambua mambo mengi ya Chama na uongozi kwa jumla.
Mgombea huyo alisema kuwa anaamini kuwa idadi ya wanachama waliompigia kura
mwaka 2000 inaweza
ikaipatia CCM ushindi iwapo kila mwanachama ataweza kuhamasisha wanachama watatu
kila mmoja kuichagua CCM.
“Hii sio mara ya kwanza kusimama mbele yenu kuomba Kura, kwani mwaka 2000,
nilikuja mbele yenu kuomba kura
mkaona ngoja muwape wapinzani, mkidai mnataka kujaribu kuona maendeleo
watakayoleta sasa mwaka huu naomba
kura zenu zikipe Chama cha Mapinduzi ushindi,” alisema.
Aliongeza: “Wakati huo wanachama 15,000 walisema mama Minde anafaa wengine
wakasema hebu tuwape wapinzani
ili kuona nini watakifanya sasa naamini katika wanachama hao walionipigia kura
uchaguzi uliopita
watawahamasisha wengine kuichagua CCM katika uchaguzi wa mwaka huu,” alisema.
Aliwaambia wananchi na wanachama wa CCM kwamba huu ni wakati wa mabadiliko ya
kimaendeleo na chanzo kikuu cha maendeleo kwa wananchi ni kuhakikisha CCM
inashinda kwa kishindo.
Salma Kikwete ahimiza kinamama kuchagua CCM
L Asema wao ndio injini itakayoipatia ushindi
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi kinaamini kuwa wanawake ndiyo nguzo na injini itakayokipatia
ushindi katika uchaguzi mkuu ujao uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.
Akizungumza na viongozi wa Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT) wakati wa ziara
yake mkoani Dar es Salaam iliyoanza jana, mke wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete kwa tiketi ya CCM, mama Salma Kikwete
alisema ushindi wa CCM unaanzia kwa wanawake kutokana na
kuridhishwa kwao na juhudi zilizoonyeshwa na viongozi wake katika
kuwatumika.
“Ushindi unaanzia hapa kwa wanawake ambao ndio muhimili imara kwa CCM,”
alisema na kuongeza kuwa kinachobakia kwa sasa ni kuwakumbusha tu ili waweze
kufanikisha kwa ufanisi zaidi jukumu lao hilo itakapofika wakati wa kupiga kura.
Akimaanisha kuwachagua wagombea urais, ubunge na madiwani wa CCM.
Alisema anaamini wanawake wataendelea kuipa ushindi CCM ili waendele kufaidika
na matunda yanayotokana na serikali
zake ambayo ni pamoja na kuwaendeleza kiuchumi, sambamba na kubakia kuishi kwa
amani na utulivu.
Mama Salma alisema kutokana na mafanikio hayo, hakuna haja ya kukubali
kurubuniwa na kuwapiga kura madalali na wachuuzi wachache wa kisiasa ambao lengo lao ni kuleta
machafuko.
Huku akishangiliwa kwa shangwe na vifijo na hivyo kulazimika kukatisha hotuba
yake, Mama Salma alisema kuwachagua wapinzani ni hatari kwa wanawake, kwani
amani ikivurugika, wao ndio watakaohangaika na watoto wao kutafuta hifadhi.
“Msikubali kurubuniwa na kuvuruga amani na badala yake itunzeni, kwani
imejengwa kwa gharama kubwa na endapo tutaruhusu ivurugwe, kuirejesha ni ghali
mno,” alisisitiza.
Katika kudhibiti hali hiyo, alisema njia pekee ni kuichagua CCM na ili
kufanikisha lengo hilo aliwaagiza wanawake kuhamasishana kuanzia nyumba kwa
nyumba na hatimaye kitanda hadi kitanda.
Katika hatua nyingine, Mama Salma aliahidi kuwa serikali ijayo ya awamu ya nne
kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM itawaendeleza wanawake siyo tu kiuchumi, bali
hata kwa kuwapatia nafasi zaidi za uongozi.
Alitoa mfano ambapo alisema wakati katika bunge lililopita uwakilishi wao
ulikuwa asilimia 30, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 50 ifikapo
mwaka 2010.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar es Salaam, Janet Kahama
alimshukuru Mama Salma kwa kuanza ziara yake mkoani humo na kueleza kuwa hali
hiyo inadhihirisha mapenzi yake makubwa kwao.
Mama Salma na ujumbe wake unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT
Taifa, Zakia Meghj, leo anaendelea
na ziara yake hiyo ya kuzungumza na wanawake wilayani Ilala.
Kampeni zazidi kupamba moto, picha ya
ushindi kwa CCM yazidi kung’ara
Na Lucas Kisasa
KADRI siku zinavyozidi kusonga mbele katika kipindi hiki cha kampeni kwa
wagombea na vyama vyao vya siasa, ndivyo
mwelekeo wa kisiasa unavyoanza kujionyesha kuhusu ni nani wataibuka washindi
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30 mwaka huu.
Ni kweli inawezekana ni mapema mno kwa sasa kuweza kusema lolote la uhakika
kuhusu kile kitakachotokea siku ya kupiga kura.
Lakini pamoja na hayo kwa upande
wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wazi
mgombea wa CCM wa nafasi hiyo, Jakaya Mrisho Kikwete, ndiye kwa kila hali
anayeonekana ataibuka mshindi kwa kupata ushindi wa kishindo au wa tsunami kama
ambavyo wana-CCM na viongozi wao wamekuwa wakijinadi.
Ushindi wa Kikwete kwa nafasi ya Urais unaonekana ni dhahiri kutokana na mapokezi makubwa ambayo
amekuwa akipata kila anakopita mikoani katika ziara yake ya kampeni.
Kila anakokwenda Kikwete amekuwa akipokewa na maelfu kwa maelfu ya
wananchi na kuleta mtikisiko mkubwa wa kisiasa nchini.
Ni kweli kwa mgombea kuvuta umati mkubwa wa watu siyo kigezo cha kudhani kuwa
wote hao watampigia kura kwani
wengine wanaweza kuwa wasikilizaji tu.
Lakini umati wa Kikwete ni tofauti.
Ni umati ambao umekuwa ukionekana kuhamasika na kuwa na msisimko wa
kipekee.
Ni dhahiri kabisa wananchi wengi watampigia kura Kikwete.
Hii ni kutokana na tathmini kuhusu kauli za wananchi katika maeneo
mbalimbali nchini kwa sasa. Upo uwezekano mkubwa Kikwete akajipatia ushindi wa
zaidi ya asilimia 85 kwa nafasi hiyo ya Urais.
Wagombea wengine wanaoweza kumfuatia Kikwete kwa mbali ni Profesa Ibrahim
Lipumba wa CUF; Freeman Mbowe wa CHADEMA; na Augustine Mrema wa TLP.
Wagombea wote hawa inawezekana kabisa wakagawana hiyo asilimia iliyobaki
ambayo inaweza kabisa isizidi 15.
Lakini wako wagombea wengine pia waliojitokeza kuwania nafasi
ya urais na kufanya idadi ya wagombea kwa nafasi hii ya juu kabisa nchini
katika uchaguzi mkuu ujao kuwa kumi. Wagombea
hawa wengine ni Dk. Sengondo Mvungi (NCCR-Mageuzi); Profesa Leonard Shayo (DEMOKRASIA
MAKINI); Emmanuel Makaidi (NLD); Christopher Mtikila (DP); Paul Kyara (SAU); na
mgombea mwanamke pekee, Anna Senkoro (PPT).
Wagombea hawa katika kundi hili la
mwisho hawatarajii kupata asilimia kubwa ya kura.
Watakachofanya ni kumega asilimia iliyobaki ya akina Lipumba, Mbowe na
Mrema na hivyo kufifisha zaidi
kiwango cha kura watakachopata kila
mmoja wa wagombea wa upinzani wa
nafasi ya urais.
Kinyang’anyiro cha nafasi ya urais kwa Zanzibar inaelekea kitakuwa cha vuta
nikuvute kutokana na maandalizi makubwa yaliyokwisha fanywa na vyama viwili
vyenye mvutano mkubwa wa kisiasa vya CCM na CUF visiwani humo.
Maalim Seif wa CUF anawania nafasi hiyo kwa mara ya tatu sasa katika mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Anapambana
na Rais wa sasa wa Zanzibar Amani Abeid Karume
wa CCM.
Ikiwa msemo wa Kiswahili kwamba ‘dalili ya mvua ni mawingu’ ni sahihi basi
kuna uwezekano mkubwa kuwa
Amani Karume, kwa maana ya CCM, ataibuka
tena kuwa mshindi kwenye kiti cha urais huko Zanzibar. Kwanini
iwe hivyo. Kwa kuwa CUF wameonyesha dalili za kushindwa hata kabla ya
upigaji wa kura.
CUF wamekuwa wakipiga kelele kuwa wanaonewa.
Viongozi kadhaa wa CUF na hasa wale waandamizi
wamekuwa wakitamka hadharani
kuwa watakataa matokeo ya uchaguzi ikiwa daftari la wapiga kura halitaweza
kuhakikiwa.
Kelele hizi za CUF ni dalili kuwa wana hofu na uchaguzi.
Katika uchaguzi huu itakuwa vigumu kweli kweli kwa watu wasiohusika huko
Zanzibar kuweza kupiga kura kwani sasa watakaopiga kura ni wale tu waliomo
kwenye daftari la wapiga kura. Wapiga
kura mamluki kutoka Tanga, Dar es Salaam na kwingineko nje ya Zanzibar
hawataweza kupiga kura huko visiwani.
Hata katika nafasi ya Ubunge kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inaelekea CCM itafanya vizuri pengine kuliko chaguzi mbili zilizopita katika
mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Wako baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa, vikiwemo vyombo vya habari, ambao wamekuwa wakisema kuwa upo uwezekano mkubwa kwamba CCM
ikapoteza majimbo mengi kwenye kinyang’anyiro cha ubunge katika uchaguzi huu
ujao.
Kigezo cha wachambuzi hao wa masuala ya kisiasa ni kwamba inaelekea wako
wananchi waliowachoka baadhi ya wagombea wa nafasi ya ubunge waliopitishwa na
CCM hali inayojidhihirisha na kile kinachodaiwa ni kuzomewa kwa baadhi ya
wagombea hao (wa ubunge) wakati wa ziara ya kampeni katika baadhi ya maeneo
nchini ya mgombea wa urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete.
Ni maoni yetu kwamba kuzomewa kwa wagombea hao na baadhi ya wapiga kura
haimananishi kuwa huo ndio mwisho wa wagombea hao wa CCM.
Ni kweli inawezekana baadhi ya wagombea hao wa CCM kwa nafasi ya ubunge
wamekuwa wakizomewa na baadhi ya wapiga kura.
Lakini ni kweli pia kuwa wako wapiga kura wengi ambao hawakuwazomea
wagombea hao na kwamba wataonyesha hisia zao kwenye sanduku la kura kwa kuwapa
kura nyingi wagombea hao waliozomewa.
Hivyo basi kwa hali yoyote ile CCM
inaelekea itavuna viti vingi mno vya ubunge pengine kuliko uchaguzi mwingine
uliopita katika mfumo huu wa vyama vingi vya siasa.
Falsafa ya Kikwete ya ‘mafiga matatu’ ambayo mgombea huyu wa urais amekuwa
akiinadi kila anakopita katika kampeni (kwamba wapiga kura wachague wagombea wa
CCM kwenye nafasi ya Urais, ubunge na udiwani) ndiyo ambayo inaonekana itawateka
wapiga kura na kuwapa kura nyingi wagombea wa CCM.
Kwa hiyo wako wagombea wa CCM kwa nafasi ya ubunge na udiwani watakaonufaika
vilivyo na mvuto wa Kikwete na
kuifanya CCM ishinde kwa kishindo katika kila nafasi itakayoshindaniwa kwenye
uchaguzi huu.
Simu: 0744-309858
E.mail: kisasa2000@yahoo.com